CHANGAMOTO ZA KUCHANGANYA MAPENZI NA KAZI




















Jambo la msingi unalopaswa kulitambua, siku zote mapenzi na kazi ni vitu ambavyo havitakiwi kuchanganywa, kama unafanya kazi na mwenzi wako, basi mkiwa kazini ni mfanyakazi mwenzako kama walivyo wengine wote na mkiwa nje ya kazi, hapo ndipo muendelee na mambo yenu.

Hii inawahusu hata wale ambao hawafanyi kazi na wenzi wao, lakini wanachanganya sana mapenzi na kazi, yaani muda wa kazi, badala ya kuelekeza nguvu kwenye kazi, unawaza mapenzi, iwe ni kwa uzuri au kwa ubaya.

Badala ya kuzingatia kazi, unatoka muda wa kazi na kwenda kuonana na mpenzi wako, hilo ni kosa kubwa. Kwa wanaofanya kazi sehemu moja, jambo la muhimu, ni kuwekeana mipaka, kila mmoja atambue nafasi yake, hii itapunguza sana migogoro na changamoto zinazoweza kutokea.

Kama wewe ni mwanaume, ukitaka uishi vizuri na mwenzi wako, mnapokuwa kwenye mazingira ya kazi, muachie uhuru wake. Yaani kichwani jenga mtazamo kwamba huyo ni mfanyakazi mwenzako, achana na mambo ya wivu au amri kwake kwa sababu wanawake hawapendi kabisa kunyimwa uhuru.

Mpe uhuru, kama ana marafiki zake, muache ajumuike nao, wakati mwingine hata baada ya kazi. Hata kama marafiki zake wengine ni wanaume, ondoa ile hofu ya kusalitiwa, muache awe huru na hapo utamjenga kujiamini na kujichunga mwenyewe. Yapo matukio ya wanaume ambao wanawazuia wapenzi wao kuwa na mazoea na wafanyakazi wenzao wa kiume, hataki wazungumze au hata kucheka pamoja.

Matokeo yake, utakuwa unajiumiza moyo kwa sababu muda wote utakuwa unahisi utasalitiwa wakati ukweli ni kwamba, mazoea ya kazini hayana uhusiano wowote na uhusiano wa kimapenzi. Huwezi kumchunga mwenzi wako, kama angekuwa anafanya kazi ofisi nyingine ungepata wapi muda wa kujua kwamba muda huu anazungumza au anacheka na nani? Jiamini, itakusaidia sana.

Kwa wanawake pia, kama unafanya kazi na mwenzi wako ofisi moja, hebu acha kujishtukia. Usiishi maisha ya kuigiza kwa sababu unahisi atakufikiria vibaya au atahisi una mambo mengi. Kama unajiheshimu, wasiwasi wa nini?

Ishi maisha yako ya kawaida na kama nilivyosema, mchukulie kama mfanyakazi mwenzako. Ukiishi kwa kujishtukia, matokeo yake ni kwamba hata ufanisi wako wa kazi utashuka. Utaogopa kushirikiana na wenzako ukihofia kumkwaza, muda wote utakuwa unawaza mapenzi badala ya kazi, jambo ambalo ni hatari sana.

Pia na wewe unapaswa kumpa uhuru mwanaume wako, muache azungumze na marafiki zake, hata kama ni wa jinsia tofauti. Amini kwamba hawezi kukufanyia jambo baya mbele ya macho yako na hapo roho yako itakuwa na amani. Jambo la muhimu kwa wote wawili, ni kujiheshimu na kutanguliza busara kwa kila jambo.

Mtu anayejiheshimu, hawezi kuwa na mazoea ya kuvuka mipaka kwa watu wa jinsia tofauti, kwamba mnacheka mpaka mnakumbatiana hadharani, au mtu wa jinsia tofauti anakufanyia masihara ya kimapenzi mbele ya macho ya watu.


No comments: