KWA VITU KONKI VYA CHUMBANI KWENYE NDOA ZINGATIA HAYA

MAISHA yana changamoto nyingi sana ambazo unatakiwa uzitatue kabla hazijayaathiri maisha yako. Huna sababu ya kuchanganyikiwa eti kwa kuwa mke au mume kakuacha, huna haja ya kulia eti kwa sababu unayempenda, yeye hakupendi. Pambana kuikabili hali hiyo na kisha uyaache maisha yako yaendelee.  
Mpenzi msomaji wangu, ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba ndoa ni jambo la msingi sana katika maisha ya kila binadamu na ndio maana wapo wanaofikia hatua ya kusema, matukio muhimu katika maisha ya binadamu ni kuzaliwa, kuoa ama kuolewa na kufa.
Hata hivyo kuoa ama kuolewa ni heshima katika jamii na ndio maana leo hii wapo wanaofanya kadiri wawezavyo kuhakikisha wanapata watu wa kuwa nao kama mwili mmoja pale wanapofikia umri wa kufanya hivyo. Ikumbukwe kufunga ndoa kuna wakati wake, sio kwamba pale unapojisikia kufanya hivyo basi ufanye hata kama mazingira, umri na hali yako kimaisha havikuruhusu.
Lakini sasa, kibaya ambacho nimekuwa nikikishuhudia katika jamii yetu kila siku ni kwamba wapo ambao huchukulia kuoa ama kuolewa kama fasheni, hali ambayo huwasababishia kuingia katika matatizo ambayo hawakuyatarajia. Ieleweke kwamba hadi kufikia hatua ya kutamka kwamba unataka kufunga ndoa ni lazima uwe umefanya uchunguzi wa hali ya juu na kuhakikisha kwamba unaingia katika maisha ambayo hutayajutia.
Suala la kuoana si la kukurupuka, ni lazima kwanza uangalie, je ni kweli unastahili kuoa ama kuolewa kwa wakati huo? Hili ni swali la msingi kujiuliza na kama jibu litakuja akilini mwako kwamba muda bado basi unatakiwa kusubiri. Suala la kuoa ama kuolewa ni la heri na halitakiwi kuharakishwa eti kwa kufuata mkumbo. Waswahili wanasema; mambo mazuri hayataki haraka.
Kwako wewe mwanamke, unapodhani umefikia umri wa kuolewa kwanza unatakiwa kuangalia mwanaume sahihi, mwanaume ambaye hata utakapoingia kwenye maisha hayo ya ndoa, utadumu na haitakuwa ndoa ndoano. Epuka sana wanaume walaghai, matapeli wa mapenzi ambao mara nyingi hutumia gia za kuoa ili wakubaliwe kimapenzi.
Anapokutokea mwanaume na kukuambia anakupenda na angependa kuwa wako wa maisha, mchunguze kwa muda mrefu kabla hujafanya uamuzi wa kumkubalia. Usimkubalie haraka ili nawe uitwe mke wa mtu kama ilivyo kwa rafiki au ndugu yako aliyeolewa hivi karibuni.
Kwa ujumla ni kwamba kabla ya kumtamkia yule ambaye ungependa umuite mke na yeye akuite mume ni lazima kwanza mtaanza kuwa wapenzi wa kawaida kisha baada ya kuona kwamba, mmependezana kitabia ndipo suala la ndoa litaingia. Kama mtaafikiana katika hilo mnaweza kuingia katika hatua.


No comments: