KWENYE MAPENZI PESA NI MBWEMBWE TU
Katika maisha ya kindoa na uhusiano wa kimapenzi, siku hizi kumekuwa na misemo mingi inayomaanisha kuwa fedha ni kitu cha msingi sana unapozungumzia kuhusu msichana kuishi kinyumba na mvulana.
‘Hapendwi mtu hapa pochi tu’, Mapenzi Bongo?, Acha maneno hata kwenye kanga yapo na mengine kadha wa kadha. Ni misemo ya watoto wa mjini inayoonyesha jinsi gani watu wanatanguliza fedha kwanza katika suala la maisha ya uhusiano wa kimapenzi au ndoa.
‘Hapendwi mtu hapa pochi tu’, Mapenzi Bongo?, Acha maneno hata kwenye kanga yapo na mengine kadha wa kadha. Ni misemo ya watoto wa mjini inayoonyesha jinsi gani watu wanatanguliza fedha kwanza katika suala la maisha ya uhusiano wa kimapenzi au ndoa.
Hii siyo mara yangu ya kwanza kuzungumzia suala hili. Nimesema mara nyingi kwamba ni kweli, katika maisha ya sasa, ni vigumu sana kutoihusisha fedha katika mapenzi, kwamba uwepo wake, unasaidia kwa kiwango kikubwa kuimarika kwa penzi lenyewe.
Ukitembea na kuzungumza na vijana wengi wa sasa wanakuambia ukiwa na pesa ‘utang’oa’ demu wa aina yeyote, kwa sababu huwa hawana ujanja panapo mapesa. Na hili linadhihirishwa na wengi wanapobadili wanawake kwa sababu ya uwezo wao wa kifedha.
Na hata wanawake wenyewe nao wanaonekana kuhamasika sana kukutana na mvulana mwenye fedha, kama ambavyo hata vijana wa kiume nao siku hizi hupenda wadada wenye nazo.
Lakini ninataka kusema jambo moja ili kila mmoja limkae akilini mwake, kwamba pamoja na ukweli huu wa fedha kuchagiza sana mapenzi, lakini mapenzi ya kweli yapo na yana nguvu kubwa kuliko kawaida.
Uthibitisho wa hili, chunguza au jichunguze mwenyewe unapofuatilia penzi la pesa. Kwa wavulana, wana pesa, wana mke nyumbani (wanayempenda) utawasikia wanatamka maneno kama haya “leo nataka mlupo wa maana nikapumzike nao”
Na akina dada nao, wanaoishi na waume wawapendao unaweza kuwasikia wakisema “Sijui nimpate wapi zoba ajiingize nipate hela ya saluni.”Maana ya kauli ya wawili hawa ni kuwa wako tayari kutumia au kutumiwa na fedha ili kukidhi matamanio yao ya kimwili na kimahitaji. Mvulana atataka aifurahishe nafsi yake kwa kumpata msichana kwa fedha, wakati mdada atahitaji fedha kwa kuutumia mwili wake ili mradi tu apate kutimiza mahitaji yake.
Lakini jambo tunaloweza kujifunza ni kwamba wote wana wenza wao ambao hawahitaji fedha ili kufurahi nao. Wanaume wenye wapenzi wao, huogopa kuwapa fedha zenye mlengo wa kuhonga.
Pesa hutajwa kwenye maendeleo baina ya wawili na siyo mtaji wa kumalizana kiu ya kimahaba. Unaweza kumkuta msichana mrembo anatoka na mtu mwenye fedha, lakini ukimchunguza undani wake, unakuta kuwa huko anakotoka, anaye mpenzi wake wa dhati kabisa, ambaye wakati mwingine huwa anaelewa uhusiano wa mpenziwe huyo na kibopa.
Ninachotaka wote kuamini ni kuwa hakuna kiwango cha fedha kinachoweza kununua mapenzi, isipokuwa mapenzi ya dhati yanaweza kukusanya kiasi chote cha fedha kilichopo na kukileta ndani.
Pesa ni mbwembwe tu, lakini hazina ubavu wowote wa kudhibiti penzi. Ndiyo maana unawaona wanawake walioolewa na matajiri wanatoka nje, tena na magari yenye vioo vya giza, wanaenda kuupa moyo burudani huko kusiko na fedha.
Msichana atakimbia ndoa ya kijana wa bilionea, atafurahia kuishi na mwenza wake hohehahe, ili mradi tu, nafsi yake inapata burudani iliyokusudiwa.Hujaona watoto wa kike wakijinyonga kwa kukataa ndoa za lazima? Hii ni kwa sababu wazazi wameshachukua ng’ombe na hela, lakini upendo wa binti uko kwa mtu mwingine kabisa, ambaye wakubwa hawamtaki kwa vile hawezi kutoa mahari kubwa!
No comments: