MAPENZI MATAMU NI KUSIKILIZANA NA KUSHAURIANA KWA PAMOJA










KILA kunapokucha ni vyema ukamshukuru Mungu kwa maana bila yeye, mimi na wewe tusingeweza kukutana katika safu yetu . Tumepata nafasi ya upendeleo hivyo tushukuru na tuitumie vyema nafasi hii.
Wiki hii nakukumbusha kuhusu wewe mwanaume au mwanamke ambaye umekuwa ni msiri kupitiliza wa hata mambo muhimu ya familia, hutaki kumshirikisha mwenza wako. Tabia hii inasemekana wanayo hasa wanaume.
Achana na mambo yale ya kipindi cha nyuma ya wewe mwanaume au mwanamke kushindwa kumpa nafasi mwenza wako katika kumshirikisha mambo mbalimbali ya kifamilia.
Mapenzi mazuri kwa mwaka 2018 ni yale ya kushirikishana na kushauriana kwa kila jambo ambalo unalohisi linakutatiza, usikubali kuumia mwenyewe moyoni mwako kwa jambo lolote hata kama ni gumu vipi bila kumshirikisha mwenza wako.
Kwa nini unamchukulia poa mwenza wako? Si ajabu jambo linalokutatiza, yeye ana ufumbuzi wake au ana mtu wake wa karibu ambaye anaweza kukusaidia kulitatua. Achana na mambo ya umimi ambayo miaka mingine ulikuwa nayo. Wapenzi wengi wanafeli kwa sababu ya kutokuwaamini na kuwapa nafasi wapenzi wao hasa wa kike. Baadhi ya wanaume wanawachukulia wanawake kama watu wa kuambiwa na kutekeleza kila jambo. Wakati mwingine kuna mambo unaweza ukawa unakosea, lakini kwa sababu ya ubabe, umimi na mfumo dume wako kwa mwenza wako, basi mpenzi wako anashindwa kukushauri, ingawa anakuwa anatamani na mwisho wa siku jambo ambalo ulilifanya bila kumshirikisha linaharibika. Kama ni biashara, basi unafilisika.
Jitahidi kumpa nafasi mwenza wako kwenye mambo muhimu ya maendeleo ya penzi au familia yenu. Labda kama mwanamke au mwanaume uliyenaye huna imani naye, huna uhakika kama ndiye mwenza wako, lakini kama una
uhakika na pengine mnaishi kwenye ndoa kwa muda mrefu, basi peaneni nafasi ya kushirikishana na kushauriana kwa kila jambo kwa afya ya uhusiano wenu.
Mambo yako yanaweza kuwa yanafeli kwa sababu humpi nafasi mkeo. Hupati baraka kutoka kwa mkeo, unategemea nini kitafuatia kama siyo kula za uso?
Mwaka 2018, kaa chini na mwenza wako na mshirikishane, achaneni na mambo ya ubinafsi ambayo ndiyo hasa yanachangia ninyi kushindwa kufikia malengo ya juu.
Kubali kubadilika mwaka huu, kama kweli mwenza wako ulimchagua na kumpenda kwa dhati, basi mpe nafasi katika uamuzi na awe mshauri wako. Inawezekana wewe ni mzuri wa kutafuta fedha, lakini hujui kupanga bajeti, lakini mkeo ambaye humuamini kiasili ni mtalaam wa bajeti na maendeleo.
Tabia ya kutokumshirikisha mwenza wako katika ndoa imewakosti wanaume wengi sana. Kuna waliofariki dunia na kuacha familia zao zikiteseka mtaani na kazini akiwa na pesa nyingi sana ambazo anazidai.
Kuna wanaume wengine wameacha majumba na mali zao nyingi kwa sababu hawakutaka wenza wao wajue, leo amefariki dunia, mali zinawasaidia watu baki huku familia ikigeuka ombaomba na kuishi maisha ya kutangatanga.
Wapo wanaume wengine ambao kabla ya kuoa walipata watoto wa ujanani, hata hilo nalo wamewaficha wenza wao. Kama mtoto ni wa ujanani, muweke wazi mwenza wako ajue kuliko aje kujua mwenyewe, atakuona si mwaminifu wala mkweli na ndiyo maana ukamficha.


No comments: