DONDOO ZA KUMDATISHA MPENZI WAKO

UZUNGUMZAJI WAKO
Unavyozungumza na mpenzi wako ni tofauti kabisa na unavyozungumza na watu wengine. Ni hatari sana kutumia lugha ya ukali ama isiyo ya kiungwana kwa mpenzi wako.
Unatakiwa kufahamu kwamba, mpenzi wako ni mtu muhimu sana katika maisha yako hivyo unatakiwa kuwa makini pindi unapozungumza naye.
Kuonesha kwamba wapo wasiojua mapenzi ni nini, unamkuta mtu anamwita mpenzi wake majina kama vile mshamba, demu, shembe na mengine mengine kama hayo. Mpenzi wako kweli umuite demu? Na wale wengine kule mtaani utawaita nani?
Huo si ustaarabu na kamwe mapenzi yenu hayawezi kushamiri kwa mtindo huo. Kuna wengine matusi hayawaishi midomoni mwao. Kwa kufanya hivyo jua tu kwamba unamboa laazizi wako.
Aidha mapozi katika uzungumzaji wako ni miongoni mwa vitu vinavyoweza kumdatisha mpenzi wako. Ukiwa na mpenzi wako usiongee kama chiriku au kama unagombana na mtu. Ongea kwa mapozi na hilo litamfanya akutofautishe wewe na watu wengine.
Kuna ambao wanapozungumza na wapenzi wao hawapitishi sentensi bila kutaja neno Dear ama Sweet. Hakika inavutia na ni mbolea tosha katika penzi la watu hao.
Lakini pia kuna baadhi ya maneno ambayo ukiyafanya kuwa sehemu ya maisha yako yanaweza kumvutia mpenzi wako. Kwa mfano neno NAKUPENDA!
Hakuna asiyefurahia kupendwa hata kama ni mtoto mdogo, anafurahi sana kusikia neno ‘Nakupenda’ kutoka kwa watu wake wa karibu. Lakini linapokuja suala la mahusiano ya kimapenzi, neno hilo linachukua nafasi kubwa sana.
Ili kulifanya neno hilo kuwa na uzito wengine hulitamka kwa lugha ya kigeni yaani ‘I love you Dear au sweet’, ni sawa tu kwani maana ni ile ile. Huo ni mfano wa maneno ambayo ni chachu katika mapenzi.
Pia unatakiwa kuwa mwepesi wa kushukuru. Wengine hata wapenzi wao wajitahidi kuwafanyia mambo mazuri vipi, lakini ni wagumu sana kutamka neno ASANTE.
Hata wanapowakosea wapenzi wao ni wagumu sana kuomba samahani. Kwa taarifa yako kama wewe ni mmoja wa wenye tabia hiyo elewa kwamba unamboa sana mpenzi wako.
Pia mnapokuwa faragha na mpenzi mkistarehe,baada ya kukufanyia kile ambacho roho yako imefurahi, mwambie asante kwa kukupeleka kwenye sayari mpya ya mahaba.
TABIA ZAKO
Huu ndio msingi imara wa uhusiano wa kimapenzi. Wapo wanawake ambao ni wazuri na wenye kila sifa ya kuwa na wapenzi bora, lakini kutokanana tabia zao chafu wamekuwa wakiachwa kila wanapoingia katika uhusiano.
Nani atakupenda na kudiriki kuendelea kuwa katika uhusiano na wewe kama tabia zako si nzuri? Wengi wetu tunapenda kupata sifa ya kuwapata wapenzi ama wachumba wenye tabia nzuri ili tuweze kusifiwa na marafiki zetu pamoja na wazazi.
Kwa maana hiyo basi, kuwa makini sana na tabia ambazo unajua haziwezi kumvutia mpenzi wako ama jamii inayowazunguka kama vile WIVU uliopitiliza kiasi cha kuwa kero, kutaka makuu pamoja na tamaa zisizo na msingi.
Nimeweka wivu juu kutokana na ukweli kwamba, kuna wanawake hata wakiwakuta wapenzi wamesimama ama kupigiwa simu na mtu wa jinsia tofauti bila kujua ukweli wa mambo wanaanzisha vurumai, huu ni ulimbukeni.
JINSI UNAVYOMRIDHISHA
Yote hayo hapo juu ni tisa, lakini kumi ni jinsi unavyoweza kumridhisha mpenzi wako hasa mnapokuwa faragha mkipeana raha za dunia.
Hata kama una tabia nzuri na umbile la kumvutia kiasi gani, kama huna utaalam na ujuzi wa kutosha katika kumpa raha mpenzi wako hasa linapokuja suala la tendo la ndoa, lazima penzi ama ndoa yako itakuwa na walakini.
Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba, tunapozungumzia mapenzi hatumaanishi ngono. Ngono ama tendo la ndoa ni sehemu tu ya mapenzi ambayo haichukui nafasi kubwa sana kama baadhi yetu tunavyochukulia.
Lakini kitu ambacho kimekuwa kikiwavutia walio wengi waume kwa wanawake ni utundu na ubunifu wakati mnapokuwa faragha. Kinachotakiwa ni kupeana kile roho inataka ili suala la kusalitiana lisiwepo.


No comments: