FANYA HAYA HISIA ZA MAPENZI ZIENDELEE


TUNAISHI kwenye ulimwengu unaoenda kasi sana kiasi kwamba usipokuwa makini, unaweza kujikuta ukimpoteza mtu uliyempenda sana maishani kwa sababu tu ya kujua namna ya kwenda naye sawa wakati ukiendelea na mchakamchaka wa kukimbizana na maisha!
Inafahamika kwamba mapenzi ni hisia lakini ni wachache wanaoweza kueleza jinsi ya kufanya hisia za mapenzi ziendelee kuwa hai. Siku hizi ndoa nyingi zinaendelea kuwepo kwa sababu ya kudra tu, unakuta mume na mke wanaishi kwa sababu ya mazoea tu lakini si kwa sababu ya mapenzi!

Wengine wanakwambia kabisa, ‘mapenzi yalikuwa wakati tunaanzana’! Wanaishi tu ilimradi siku zinaenda, ilimradi wanawalea watoto lakini si kwa sababu ya upendo kati yao.
Wengine wanafikia hatua hata ya kulala mzungu wa nne au kutengana vyumba kabisa! Kwa nje mnawaona kama wanapendana lakini kumbe ndani kuna ufa mkubwa kati yao, hakuna tena mapenzi kati yao.
Cha ajabu, utakuta watu hawahawa ambao leo wanaishi kimazoea, wakati wanaanzana walikuwa wakioneshana mapenzi motomoto! Walikuwa wakigandana kama ruba, walikuwa wakioneshana kila aina ya bashasha za kimapenzi.
Ukiuliza nini kimetokea? Hakuna mwenye majibu, maudhi ya mara kwa mara yamekuwa kitu cha kawaida kwao, usaliti, kutoheshimiana na kujibizana hovyo kumewafikisha hapo walipo, hakuna tena mapenzi, Wazungu wanasema No More Love!
Hata pale inapotokea maelewano yakapatikana, mnapokutana faragha, hakuna tena msisimko kama zamani, kwa wanaume wanaanza kupatwa na tatizo lingine la kupungukiwa na nguvu za kiume wakati wanawake wao wanapoteza kabisa hamu ya tendo.
Utafiti wa kisayansi, unaonesha kwamba mwanaume anapokosa hisia, dalili zinazoonekana kwa haraka ni ukosefu wa nguvu za kiume! Lakini cha kushangaza, mwanaume huyu ambaye mkewe anamlalamikia kwamba hamtoshelezi kwenye tendo, ikitokea amepata mchepuko, huko nje ‘anapafomu’ kwa kiwango cha juu kabisa, akirudi ndani mambo ni yaleyale.

Mwanamke pia anayepoteza hamu ya tendo kwa mumewe, ambaye
hafurahii tena kuwa faragha na mumewe, ikitokea amekutana na mchepuko huko nje, utashangaa analifurahia mno tendo na pengine ‘akafika’ kwa urahisi kabisa, akirudi ndani mambo ni yaleyale.
Kwa maelezo haya, ni dhahiri kwamba unaona umuhimu wa hisia katika mapenzi! Ili mapenzi yawe matamu, ili uhusiano udumu, ni lazima kila mmoja awe na hisia na mwenzake. Hata hivyo, hisia haziji tu zenyewe, zinajengwa!
Hisia za mapenzi ni kama bustani ya maua, haiwezi kustawi wala maua hayawezi kuchanua na kutoa harufu nzuri kama huitunzi bustani yako KILA SIKU! Hisia za mapenzi siyo kitu cha kuja na kupita, unatakiwa ushughulike na hisia za mwenzi wako kila siku.
Hatua ya kwanza kabisa unayotakiwa kuifanya, unapoona unaishi kwenye maisha ambayo hisia za mapenzi kati yako na mwenzi wako hazipo tena, ni kuanza kujiweka karibu na mwenzi wako.

Kama hukuwa na mazoea ya kuwahi kurudi nyumbani, au ukiwa nyumbani unakuwa bize na mambo mengine, badilisha utaratibu, anza kutenga muda wa kutosha wa kukaa naye karibu na kuwa mnyenyekevu kwake!
Siyo unawahi kurudi nyumbani halafu muda wote mna kazi ya kubishana na kulumbana! Jifanye mjinga, jishushe na muoneshe kwamba unampenda! Hata kama alikuwa na dukuduku lake moyoni, litaanza kupungua, ataanza kuzungumza na wewe, ataanza kukuchangamkia na hapo utakuwa umefanikiwa kuanza safari ya kuziamsha upya hisia zake.

Tafuta muda wa kutoka naye ‘out’, mpeleke maeneo mliyozoea kwenda kipindi mapenzi yenu yalipokuwa motomoto, taratibu hisia zitakuwa zinaendelea kuongezeka kidogokidogo.


No comments: