NANI ANASTAHILI KUHONGWA,MWANAMKE AU MWANAUME?

Related imageKaribuni katika mada yetu mpya ya leo. Kwa mujibu wa vitabu vya dini hususan Biblia, vinatufundisha kwamba kiasili mwanaume ndiye kichwa cha familia. Ndiye anayepaswa kusimamia maamuzi yote ya familia sambamba na suala la fedha. 

Mwanaume ndiye anayetoa fedha kwa watoto, ndiye anayempa mkewe fedha kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Huo ni utaratibu tu uliozoeleka, leo nataka nikujuze kwamba si mzuri sana. 

Kwa kutumia falsafa hiyo, wanawake wengi wamekuwa wakiwategemea wanaume kwa kila kitu. Wanabweteka. Wao wanategemea kila kitu kupewa. 

Utasikia ‘baba fulani nataka niende saluni naomba hela, baba nanii naomba hela kwa ajili ya mchezo au nipatie fedha za kununulia nguo za mtoto’. 

Kautaratibu haka kamewakaa hata wanaume. Wengi wao huwa hawana kipingamizi waombwapo matumizi ya kila kitu, wanatoa hata bila ya kuhoji mkewe anafanya kazi ambayo inamuingizia kipato au la. 

Mbali na kwa wanandoa, dhana hii imejengeka hadi kwa wachumba. Mabinti wengi wanaoingia kwenye uchumba kwa kizazi cha sasa wanaamini katika falsafa ya kuhongwa.  

Wanataka kila kitu kutoka kwa mwanaume hata kama na yeye ana kazi yake. Hiyo haimhusu mumewe, ‘cha mumewe ni cha kwao, cha kwake ni cha kwake’. 

Wanaomba fedha za vocha, wanaomba fedha za matumizi ya nyumbani na hata zile za kuendea saluni pia. Anahakikisha mchumba wake anakuwa ndiyo ‘injini’ ya kutoa kila kitu. 

Na endapo ikitokea siku ameomba fedha za kitu fulani akanyimwa basi ni tatizo. Ugomvi ndiyo unaanzia hapo. 

Atakasirika na kuanza kumuondoa thamani mpenzi wake. Ni rahisi kwenda mbali na kufikia hatua ya kusema ‘huyu mwanaume hana sifa za kuwa na mimi. Mwanaume gani anashindwa kunilipia hela ya saluni. Mwanaume suruali.’ 

Ugomvi utakuwa mkubwa na suluhu yake huwa ni kuhamia kwa mwanaume mwingine ambaye atakuwa hazisikilizii fedha zake. 

Tabia huwa ni kama ngozi, huwezi kuibadili. Utakutana na mwanaume mwingine ambaye naye ana fedha, lakini pale atakapoyumba kiuchumi tu, naye utamuacha na kutafuta mwingine. 

Staili ya maisha yako itakuwa ni ya kutanga tanga. Leo kwa huyu kesho kwa mwingine. 

Tatizo hili pia lipo hata kwa wanaume. Wapo ambao nao wanaamini katika falsafa ya kuhongwa na wanawake. 

Hawataki kujishughulisha, wanataka kuhongwa. Mwanamke asipomhonga naye hamtaki, anatafuta mwingine ambaye ataweza kumtimizia mahitaji yake yote. Kama ana kazi yeye mshahara wake unakuwa na matumizi yake ambayo anayajua mwenyewe. 
Ndugu zangu lazima tukubaliane kwamba katika ulimwengu wa wapendanao fedha zinachangia kurahisisha maisha lakini zinageuka kuwa tatizo pale mnapozipa kipaumbele kwenye uhusiano wenu. Kwamba fedha ikitoweka na uhusiano umekufa. 

Maisha ya uchumba na hata ya ndoa yanapaswa kukubaliana na hali halisi mliyonayo. Kama mumeo ana kazi na wewe huna kazi, kwa kizazi cha sasa kinakupasa na wewe kubuni vimiradi vidogovidogo ambavyo vitampunguzia makali ya maisha mumeo. 

Itakusaidia kuondoa tatizo la utegemezi katika kila kitu. Maisha ni kusaidiana, ondokana na tafsiri ya kusema mwanaume ndiyo kichwa basi umtegemee kwa kila kitu. Vingine unapaswa ujiongeze wewe mwenyewe, hiki si kizazi cha mwanandoa kuwa golikipa. 

Wanaume ambao pia wana kamchezo haka wanatakiwa kubadilika. Huwezi kumtegemea mwanamke awe anakupa wewe fedha kila siku. Jengeni utaratibu wa kusaidiana lakini si kila siku mmoja tu ndiye awe anaumia.

No comments: