UKIYAONA HAYA JUA UPO KWENYE MAPENZI HATARISHI,KIMBIA

Matukio ya wanandoa kuwaua wenzi wao au kuwafanyia ukatili wa kutisha, yanazidi kuongezeka. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya mume kumuua mke, mke kumuua mume au kusababishiana vilema vya kudumu.
Lakini si kwa waliopo kwenye ndoa pekee, hata wale waliopo kwenye uhusiano wa kawaida wa kimapenzi au wachumba nao wapo kwenye mkumbo huu wa kufanyiana ukatili wa kutisha.
Kiasili mapenzi yanapaswa kuwa na amani, huwezi kufurahia mapenzi kama una hofu juu ya mwenzi wako, kila siku mnatukanana, mnapigana au hata kutishiana maisha.
Kwa bahati mbaya, watu wengi wapo kwenye aina hii ya mapenzi, mapenzi hatarishi au kwa Kiingereza Violent Love na hawajui nini cha kufanya, huku wengine wakichukulia kuwa ni kitu cha kawaida.
Kutofautiana katika mapenzi ni jambo la kawaida, lakini kwa nini mfikie hatua ya kutishiana maisha, kupigana, kutukanana au hata kuuana? Wengi wanaopoteza maisha yao au kupata vilema, ni kwa sababu walishindwa kuchukua hatua mapema, waliliona tatizo lakini hawakuwa wanajua kama ni kubwa kiasi hicho au hawakuwa na mbinu za kujitoa.
Unapoona upo kwenye uhusiano uliojaa vurugu, hutakiwi kupuuzia. Unatakiwa kuchukua hatua haraka kwa sababu maisha lazima yaendelee, unaweza kuendelea kufurahia maisha hata bila ya uwepo wake. Sasa utajuaje kama upo kwenye penzi hatarishi?
Hebu jiulize maswali yafuatayo: Huwa unapatwa na hofu ndani ya moyo wako unapokuwa karibu na mwenzi wako? Huwa unaogopa kukosea hata yale makosa ya kibinadamu ukiwa karibu na mwenzi wako? Unajihisi kama muda wote wewe ndiye unayefanya makosa? Haupo huru hata katika mazungumzo ya kawaida ukihofia kumkasirisha umpendaye?
Bila shaka kila mmoja atakuwa na majibu yake. Kadiri majibu yako yanavyokuwa ‘ndiyo’, basi ndivyo dalili kwamba upo kwenye uhusiano hatarishi zinavyoongezeka.
Hebu jiulize tena maswali mengine yafuatayo: Mwenzi wako ana kawaida ya kukufokea au kukutolea lugha chafu? Ana kukosoa mara kwa mara hata pale unapoamini kwamba upo sahihi? Anathamini zaidi pesa zako au anakutumia kama chombo cha starehe? Anakulazimisha kufanya tendo la ndoa au anakulazimisha kumtimizia mahitaji ambayo huna uwezo nayo? Anapandwa na jazba hata kwa vitu vidogo?
Majibu utakuwa nayo mwenyewe na kama ilivyokuwa hapo juu, ukipata majibu ya ndiyo mengi, basi jua upo kwenye hatari. Watu wengi huwa wanaamini mapenzi hatarishi ni yale tu ambayo mwenzi wako anakupiga au anatishia kukuua.
Ni kweli kupigana au kutoleana vitisho ni jambo la hatari, lakini huwa ni dalili za mwisho za hatari. Dalili za awali ndiyo mbaya zaidi na usipozichukulia hatua, zitawafikisha pabaya.
Wengi wanaamini kwamba wanaume ndiyo pekee wanaofanya ukatili, lakini utafiti unaonesha kwamba mara nyingi wanawake ndiyo huanza kwa kuonesha dalili hizo za awali niliozitaja hapo juu, mwisho mwanaume anashindwa uvumilivu na kuchukua maamuzi yanayomshangaza kila mtu.
Katika matukio yote ya kikatili wanayofanyiana wanandoa unayoyasikia, yalianza kwa dalili za awali na wahusika kushindwa kuchukua hatua, mwisho yakatokea ya kutokea. Hakuna mtu anayependa kufanyiwa ukatili na mwenzi wake, si mwanaume wala si mwanamke.
Hakuna anayependa kusikia ndugu yake, rafiki yake, mwanaye au mtu wake wa karibu amefanyiwa ukatili na mtu ambaye awali walikuwa wakipendana. Kama ni hivyo, basi ni jukumu la kila mmoja, kumsaidia mtu aliyepo kwenye uhusiano hatarishi.
Narudia tena kusema kwamba mapenzi ni kitu cha hiyari na yanapaswa kuwa ya furaha, upendo na amani. Kukoseana ni kitu cha kawaida lakini inapotokea kwamba wanandoa au wapenzi wameanza kufanyiana ukatili, basi hapo hakuna mapenzi tena na hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa.
Jambo la msingi ambalo kila mmoja anapaswa kulitambua ni kwamba yule anayefanyiwa ukatili ndiyo anayetakiwa kuchukua hatua. Usije kuwa unafanyiwa mambo ya kutisha ndani ya nyumba yako halafu ukategemea kwamba majirani au ndugu wanaweza kuja kuingilia.
Wewe ndiyo unapaswa kuwa wa kwanza kupaza sauti na kukataa kabisa kuendelea kuhatarisha maisha yako kwa sababu tu ya mapenzi. Anapokufanyia vitendo kama kukupiga na kukuumiza vibaya, kukutolea maneno ya vitisho au kutishia kukuua, usikae kimya.
Matukio ya wanandoa kuuana yanazidi kuongezeka kila kukicha, ukiuliza kisa utasikia ‘wivu wa mapenzi’, mwanamke anauawa, mume anakamatwa na kwenda kufungwa kifungo kirefu gerezani, wanaoteseka ni watoto ambao sasa wanabaki bila kuwa na baba wala mama.
Ni hapo ndipo uzito wa suala hili unapoonekana, iweje mambo yenu yaje kusababisha watoto wasio na hatia wakateseka? Ni bora mtengane kwa amani kwa sababu hata kama hamtakuwa na nafasi ya kuwalea watoto pamoja, lakini bado watakuwa chini ya uangalizi unaoeleweka, kuliko kusubiri mpaka maafa yatokee kisha watoto wabaki wakiwa wanateseka bila hatia.
Wakati mwingine, watu wanaowazunguka wanandoa wa aina hii, wanapaswa kuwa msaada pia, kwa sababu itakuwa na maana gani kama unawasikia watu fulani wakipigana kila siku, halafu baadaye unakuja kusikia mmoja kamuua mwenzake kwa sababu ya migogoro ya kimapenzi?
Kama nafasi ya kusaidia unayo, fanya hivyo mapema. Mshauri yule anayefanyiwa ukatili, wengi huwa wanakuwa wagumu kupokea ushauri lakini ni vyema ukatimiza wajibu wako ili hata likitokea la kutokea, uwe ulishafanya kila kinachowezekana ndani ya uwezo wako.


No comments: