FAIDA NA HASARA ZA MAJIBIZANO KWENYE MAPENZI

Sidhani kama kuna ambaye hajawahi kujikuta kwenye majibizano na mpenzi wake, ziko hata nyakati mnaingia katika mlipuko wa majibizano hata mnashindwa kujua sababu ya kujibizana kwenu. Vitu kama vile mmoja kuchelewa kurudi nyumbani, kushindwa kuwasiliana sawa na mwingine alivyotarajia, kushindwa kutoa msaada pale ulipohitajika, hisia za kuwepo kwa mahusiano pembeni, tabia zisizoeleweka baina ya mmoja na simu yake ya mkononi, au ndugu zenu kuingilia mahusiano yenu kwa namna yeyote ile. 

Haya ni baadhi tu ya maeneo ambayo wengi wetu tumejikuta tunapishana kimaneno na wapenzi wetu. Mara nyingine inatokea mmepanga kwenda kula au kunywa nje ya nyumbani “outing” mnafika tu sehemu husika mkiwa mnasubiria chakula au mmeshaanza kula mara mmoja wenu anatoa neno moja linaloamsha majibizano makali sana ghafla ile raha ya kuendelea kuketi na kula pale inaisha, mnaamua kukiacha chakula na kuamua kuondoka, tena ikiwezekana kila mmoja kwa njia yake. 

Najua kama ingekuwa tuko darasani nikasema wanyooshe mikono wale ambao hali kama hizi au zinazo fanana na hizi zimewahi kuwatokea wengi wangenyoosha mikono. 

Inabidi kuwa makini sana kwasababu kutofautiana katika maneno kunaweza kuwa na muendelezo bila hata ya nyie kugundua na baadae kuwapeleka pabaya. Kwamfano, wapenzi hawa wawili wanaanza taratibu katika maongezi yao “leo tunakula nini” mmoja anauliza, mara anajibiwa “kwanza kila ukimaliza kula unaacha vyombo mezani badala ya kunisaidia hata kuvisogeza wakati unajua tuko wawili tu?”Baada ya muda kupita na majibizano kama haya kuendelea, mmoja anaanza kuchoka na kumwambia mwenzake “mimi naona tunatofauti kubwa sana kwenye mambo ya majukumu ya hapa ndani na kwa jinsi hii sioni kama tutawezana bora kila mtu afuate ya kwake”. 

Hapa uaona kuwa majibizano yaliwahi kuanza muda mrefu huko nyuma ila yalikuwa na muendelezo hata pasipo wapenzi hawa kugundua na hivyo kuwapelekea kutengana. 

Kutofautiana katika maneno na mpenzi wako kunauma na unaweza ukatamani kufungua mlango wa gari likiwa katika mwendo utoke ili tu uondokane na kinywa chake. Hali hii inapozidi unaweza kujikuta unayatilia shaka mahusiano yenu na kuanza kuwa na hisia za kuyasitisha. Lakini hatuwezi kuukwepa ukweli kwamba majibizano na kutofautiana ni kitu cha asili kwenye mahusiano yeyote, jambo hili limetiliwa mkazo na wataalamu wengi wa mahusiano akiwemo mshauri Beth Fitzpatrick. 

Tafiti zinaonyesha kwamba wapenzi wengi wanaohudhuria huduma za ushauri wamekiri kwamba matatizo kama vile mawasiliano mabovu, kushindwa kusikiliza, kutojali, kupinga kila kinachosemwa au kutendwa, na kutumia lugha za matusi yamekuwa yakudumu katika mahusiano yao. Yamkini hali hii ipo pia katika mahusiano yako. 

Kama nilivyokwisha kusema awali, kwa kule kupitia katika majibizano hakumaanishi kwamba mahusiano yenu yanamatatizo, kinyume chake ni kwamba mahusiano yeyote yasiyopitia majibizano na kutofautiana yanaweza kukosa ubora unaotakiwa kimahusiano au kindoa. Maranyingine wapenzi wanaosema hawajawahi kutofautiana au kugombana wana madhaifu mengi tofauti na vile wanavyoonekana mbele za watu. 

Kule kukosa mazingira ya kutofautiana katika mahusiano yenu kunaweza kuwa na madhara makubwa kuliko kuwa na mazingira ya kutofautiana, wale wenye kukosa kutofautiana kimaneno wanaweza kuwa na tabia kama vile ukatili wa kimya kimya, kunyamaziana, kuziriana, kununiana, kunyimana tendo la ndoa na pia kukwepana. Tabia hizi zina madhara makubwa katika mahusiano. Kama mazingira ya kutofautiana yapo na ni dhahiri, kwanini msitofautiane ? Cha muhimu ni kuchagua kutofautiana kwa namna inayojenga na sio inayobomoa





No comments: