Hatua 12 za kufuata katika malezi ya mtoto
Watu wengi wanatamani kuwa na watoto, lakini wengine hukumbana na changamoto katika malezi ya mtoto au watoto walionao, na kuna wakati wanashindwa kuwawekea watoto mazingira ya kuzifikia ndoto zao.
Katika Makala ya leo, tutazungumza kwa kifupi masuala 12 ya msingi ya kuzingaika katika malezi ya mtoto:
Tambu kwamba mtoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, na ni Baraka kubwa kuzizidi zote. Usimlee katika njia ambayo itamfanya afanane na wewe, baba yake, baba yako au jirani yako au mtu mwingine yeyote. Kila mtoto ana upekee wake, hivyo aruhusiwe kuwa yeye, na sio kushurutishwa kuwa kitu ambacho sio.
Usimvunje moyo mtoto pale anaposhindwa. Na kamwe usimlinganishe na wenzake ambao wamemzidi uwezo.
Tambua kwamba, hasira na chuki ni hisia za asili, msaidie mwanao kupata majarida ya muhimu ya kumsaidia juu ya hisia hizi, vinginevyo zikiendelea kukaa ndani mwake zitatoka nje katika kama matatizo ya kimwili na kiakili.
Muadhibu mwanao kwa kiwango kinachotakiwa, usiruhusu hasira zako zikufanye ushindwe kujizuia wakati wa kumuadhibu. Endapo atatambua kwamba huwa unatenda haki hata kwenye kumuadhibu, kamwe hutokosa heshima na upendo kutoka kwake. Ni muhimu sana kuhakikisha kuwa adhabu na kosa vinauwiana, kwani hata kama ni mtoto mdogo, huwa na hisia za kuona kama ametendewa haki au ameonewa.
Elewa kuwa kila mtoto anahitaji wazazi wawili. Kamwe usifungamane na mwanao dhidi ya mzazi mwenzako, kwani jambo hili litatengeneza mgongano wa kimaslahi wa kimawazo katika akili ya mwanao nay a kwako pia. Pia inaweza kupelekea hisia za kujiona mkosefu na mwenye kutokujiamini.
Kamwe usimpe mwanao kila kitu ambacho moyo wake unataka. Mpe nafasi atambue thamani ya kupata kitu kwa jitihada zake na furaha ya kufanikiwa katika jambo.
Usijifanye kuwa wewe ndio kipimo cha usahihi, kwani hili litakuwia vigumu kulitekeleza muda wote. Itakuwia rahisi kuwasiliana na mwanao endapo utamuonesha kuwa baba na mama wakati mwingine pia huwa wanakosea.
Usitoe vitisho unapokuwa na hasira au ahadi pale unapokuwa mwenye furaha sana. Vitisho au ahadi unazotoa zinatakiwa zile tu unazoweza kuzitekeleza. Kwa mtoto, maneno ya mzazi ni kila kitu. Mtoto ambaye hana imani juu ya wazazi wake, huwa ni mgumu sana kuamini kitu chochote.
Usimdekeze mwanao kwa kumuonesha upendo wa bandia, upendo ambao ni wa kidhahania. Upendo wa kweli utaonekana kadiri mnavyohusiana kila siku, jambo ambalo huzaa kujiamini na uhuru.
Wafundishe wanao kuwa kuna utu katika kujituma/ kufanya kazi, bila kujali kazi hiyo unatumia nyenzo gani, ziwe za kisasa au kienyeji. Mfahamishe kuwa kuwa maisha yenye tija ni yale yenye baraka, na kuwa hatoambulia kitu kwa kusaka urahisi na anasa kwenye maisha.
Usijaribu kuwakinga wanao dhidi ya kila jambo ambalo linaonekana kuwarudisha nyuma au kuwa kwamisha kwenye mipango yao. Kupitia changamoto hizo, au kwa kukumbana na mazingira tofauti wataweza kujifunza vitu vingi zaidi.
Mfunze mwanao kumpenda Mungu na kuwapenda wenzake. Usimwache aende peke yake katika nyumba za ibada, bali ambatana naye huko. Watoto hujifunza zaidi kupitia mifano, kumwambia kitu sio kumfunza. Unapompa mwanao mafundisho mema ya dini yatamsaidia sana pale ambapo mambo mengine yote yatakuwa yamekwamba.
No comments: