Kutoa mimba kumenisababishia ugumba



MSEMO wa wahenga ‘Majuto ni mjukuu, huja baada ya kitendo’ unaweza kufupisha masahibu aliyopitia, Rebeca Samuel (siyo jina lake halisi) na kumfanya sasa aishi akijuta maisha yake yote yaliyobaki.


Halikadhalika usemi kwamba ‘Ujana ni maji ya moto’ unamhusu pia mwanamke huyu ambaye sasa anaelekea utu uzima kama utasoma makala haya hadi mwisho.

MKASA WA REBECA

Mwanamke huyu mrembo, msomi mwenye shahada ya Mawasiliano ya Umma, anakiri kwamba kutotulia kwake alipokuwa msichana anayetikisa wanaume kila anakopita kulimfanya ajiingize katika matukio ambayo yamempa ugumba na sasa anajuta.

Anauguza kidonda alichojisababishia miaka 16 iliyopita na sasa ameamua kutoa mkasa wake hadharani ili pengine ukasaidia wasichana wadogo yasije yakawakuta yaliyomkuta.

Anaamini masahibu yake yalichangiwa na wazazi kutompa taarifa mapema kuhusu madhara ya kujiingiza katika mapenzi kabla ya muda sambamba na ushauri mbaya wa marafiki zake alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) kilichoko jijini Mwanza.

Kwa kifupi anasema ‘wapambe nuksi’ walimshauri kutoa mimba ya miezi mitatu kienyeji, hatua ambayo licha ya kukaribia kumtoa roho ilisababisha kizazi chake kuharibika na hivyo madaktari kukiondoa ili kunusuru maisha yake lakini ikawa chanzo cha kuandamwa na machozi yasiyokoma. Ni hatua hiyo iliyosababisha ndoa zake mbili muhimu sana kwake kuvunjika na kumwachia ukiwa.

“Ninatamani niwe kwenye ndoa kama wengine lakini imeshindikana. Nikiona watoto wa wenzangu na kugundua kwamba kwangu haiwezekani tena kuzaa wakati nilipata mimba kadhaa nikawa ninazinyofoa, nalia sana,” anasema Rebeca katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya jijini Mwanza

Anaongeza: “Nilipokuwa chuoni nilitoa mimba kadhaa, lakini mimba ya mwisho ndio ilitaka kuchukua uhai wangu. Niliharibika kizazi, na nilipopelekwa hospitali huku nikiwa nimeshaanza kuoza madaktari walishauri kutoa kizazi ili kuokoa maisha yangu.”

Rebeca, mwanamke mwenye wajihi mrefu, mweupe na mwenye umbo namba nane kama wengi wanavyopenda kuwaita wasichana wa aina hii na mwenye miguu iliyojazia au miguu ya bia kama wengine wanavyoita, anasema:

“Uzuri wangu uliniponza, nikawa limbukeni… Lakini tamaa ya pesa kutoka kwa wanaume pia imenifikisha hapa.”

Anapoulizwa kufafanua kuhusu tamaa ya pesa, Rebeca anasema ingawa anatokea katika familia yenye kipato cha kati, alipokuwa chuoni alitamani kuishi maisha ya juu kama baadhi ya wasichana wenzake wanaotoka familia tajiri.

“Nilitamani kumiliki vitu vya gharama ikiwemo gari na fedha lakini ili kuvipata nilijikuta natumbukia kwenye mahusiano na wanaume tofauti tofauti hadi waume za watu,” anasema Rebecca ambaye mwaka huu ametimiza umri wa miaka 42 lakini angekuwa na uwezo anatamani kalenda ingebadilika arudie ujana, arudi chuoni halafu aishi maisha ya kutoendekeza tamaa na ghiliba za wanaume. Oh! Haiwezekani.

MIMBA ILIYOTAKA KUMUUA

Anasimulia kwamba alipokuwa mwaka wa pili chuoni hapo, alianzisha urafiki na mume wa mtu ambaye alikuwa akimpa pesa ya ‘kutakata’. Licha ya kutotaka kuzaa kabla ya kuolewa, jambo ambalo limengewaudhi pia wazazi wake, ‘buzi’ lake hilo pia lilikuwa halitaki kusikia habari ya mtoto.

“Nilipogundua nina mimba, tena ya mume wa mtu nilijua kwanza angeikataa na kuwa hata chanzo cha kuachana na mimi. Lakini pia nilihofia kuchekwa na wanafunzi wenzangu hususani wanaume niliokuwa ninawadengulia. Kwa kifupi sikuwa tayari kuzaa. Nikaamua kuitoa,” anasema.

Anafafanua kwamba hata wazazi wake aliamini wangelimwona malaya na kufikiria kusitisha kumlipia masomo ya chuo kama mimba hiyo ingedhihirika. Anasema marafiki zake wa karibu pia walimshauri kutoa na kuna huyu aliyemhimiza kuchemsha Coca-Cola na kunywa ili kuitoa hiyo mimba. Mbadala wa hilo marafiki hao walimshauri kutumia kijiti cha muhogo chenye utomvu.

“Niliona rahisi ni kuchemsha soda. Nilinunua chupa mbili za Coca Cola na kuchemsha, kisha nikanywa. Baada ya saa mbili nikaanza kuona damu zinatoka nyingi, mabonge kwa mabonge. Rafiki yangu mwingine akanipa dawa iliyonisaidia kukata damu,” anasema.

Hata hivyo, anasema hali yake ilianza kubadilika siku hadi siku wakati huo akiwa hosteli na ilipofika siku ya tano baada ya tukio lile la kutoa mimba alianza kuumwa tumbo sana.

“Tumbo lilikuwa linabana na kuachia, baadae nikaanza kutoa harufu mbaya. Hali ilipokuwa mbaya nikalazimika kurejea nyumbani ili kupelekwa hospitali ambako ndipo wazazi wakagundua kwamba nilikuwa nimetoa mimba,” anasema.

Anasema awali alidhani anapelekwa chumba cha upasuaji ili asafishwe lakini habari mbaya ambayo hataisahau maishani mwake ni kuelezwa kwamba kizazi kilikuwa kimeharibika na ili kunusuru maisha yake ni lazima kitolewe.

“Ile sauti kwamba kizazi changu kimeharibika, huwa inajirudia hadi leo masikioni mwangu, ninaishi na donda hilo la moyo ambalo limegoma kuondoka,” anasema.

MAISHA YA NDOA

Ingawa aliaibika kwa wazazi wake baada ya kugundua alitoa mimba huku yule mwanamume aliyechangia kutoa mimba naye akimkimbia, maisha yaliendelea.

Akafanikiwa kuhitimu chuo. Rebeca anasema aliajiriwa na kampuni moja kama ofisa mawasiliano na kisha akapata mchumba, wakafunga ndoa kubwa mwaka 2005 ambayo ilitikisa jiji la Mwanza, lakini bila kuthubutu kumwambia mumewe kwamba alishatolewa kizazi.

“Kuanzia siku ya ndoa nilikuwa ninajiuliza sana maswali itakuwaje mume wangu atakapotaka mtoto na mimi nilidhamiria nisimwambie kitu,” anasema.

Anasema katika kipindi cha miaka saba walichoishi na mumewe huyo ambaye Rebeca anasema alimpenda sana, aliwajengea wazazi wake nyumba na kumfungulia yeye biashara ya uhakika anayoendelea nayo hata sasa.

Anasema kuna siku mumewe alitaka wakapime ili kujua tatizo ni kwa nini mtoto hapatikani. Akawasiliana na yule daktari aliyemtoa kizazi akimpanga kwamba atakapokuja na mumewe basi amsaidie kuonesha kwamba hana tatizo lolote labda ni Mungu hajapenda apate mtoto.

“Licha ya kumwahidi fedha, yule daktari aligoma kabisa. Akasema hawezi kushiriki katika dhambi hiyo na kwamba taaluma na maadili yake ya kazi hayamruhusu kutoa majibu wa vipimo vya uongo. Ikabidi nizue dharura za uongo tusiende kupima,” anasema na kuongeza kwamba tangu siku hiyo akawa anaendelea kuzua dharura za uongo kila wanapopanga kwenda kupima.

MBIO ZA SAKAFUNI

Anasema baada ya kupiga chenga kwa muda mrefu, anahisi mumewe alipata taarifa kwa ‘wapambe nuksi’ kwamba kuna shida kubwa kwa mkewe na hivyo siku moja akamlazimisha kwamba ni lazima waende hospitali kupima, akawa hana tena namna ya kukwepa mithili ya mbio za sakafuni ambazo hazifiki mbali.

“Aliniambia huwezi kila siku ukadai una shughuli nyingi kwa jambo linalotunyima furaha katika ndoa yetu,” anasema na kuongeza kwamba walipokwenda kupima, licha ya kujaribu kutaka ‘kumpanga’ daktari aliyehusika kumpima bila mafanikio, ikabainika dhahiri kwamba alishatolewa kizazi muda mrefu na hivyo hawezi kuzaa.

Anasema daktari alimwambia mumewe asisumbuke kumaliza fedha zake kusaka matibabu nje ya nchi kwani yeye hana tatizo na una uwezo wa kumpatia mwanamke mimba isipokuwa tatizo liko kwa mkewe kwa sababu inaonekana alishaondolewa kizazi.

“Jamani sitaki kuikumbuka hii siku, ilikuwa siku ya Alhamisi, naichukia siku hii, ni kipindi kirefu kimeshapita lakini ni tukio lilioacha maumivu makubwa ndani ya moyo wangu. Nilitamani ardhi ipasuke niingie, nguvu ziliniisha, jasho likanitoka, mume wangu akanishika mkono na kunipeleka kwenye gari, tukarudi nyumbani. Njiani hakuna aliyeongea na mwenzake, machozi yalikuwa yananimwagika kama bomba.

KUKIMBIWA NA MUMEWE

“Siku nzima baada ya kutoka hospitali hatukuongea na mume wangu. Kwa siku mbili alikaa kimya kama hakuna kilichotokea lakini siku hiyo ya tatu alirudi usiku akiwa kalewa na ndipo akataka nimweleze ukweli kuhusu kilichotokea hadi nikatolewa kizazi,” anasema.

Anasema alipokosa majibu huku akibaki kumwomba radhi, alimwona mumewe akibeba nguo na vitu vyake muhimu akaondoka, akamwachia gari moja alilomnunulia na nyumba ambayo ndio anaishi hadi sasa.

“Yeye alienda kujenga nyumba nyingine na ndiko anakoishi. Ameshaoa na ana watoto wawili sasa,” anasema.

KUOLEWA TENA

Mwaka 2016 alikutana na baba mwingine wa makamo aliyekuwa kafiwa na mkewe kwa ugonjwa wa saratani na kumwachia watoto wawili.

“Huyu sikumficha alipotaka tufunge ndoa, nikamweleza ukweli kwamba sina uwezo wa kuzaa na yeye akasema watoto wawili alio nao wanamtosha.

“Hata mwaka haikuisha, maneno maneno ya ndugu zake yakawa mengi na yeye akaanza kunibana nimwambie kwa nini nilitolewa kizazi. Kwa kweli nilisimangwa sana hadi yakanishinda,” anasema Rebeca ambaye sasa hafikirii kuolewa tena.

MAJUTO MJUKUU

“Nimeachika kwa mume wangu mpenzi, mume aliyenipenda kwa moyo wake wote, alinidekeza, alinithamini na hakutaka nipate shida, alinipa kila nilichokihitaji, biashara hii unayoiona (duka la nguo) alinifungulia yeye, si hii tu nina biashara nyingine ya vitu vya elektroniki, amewajengea wazazi wangu nyumba lakini nilishindwa kumzalia mtoto aliyekuwa akimhitaji sana.

“Pesa na mali si kitu, furaha ya ndoa ni watoto, kuna muda roho inaniuma sana nikikumbuka watoto niliowatoa nikiwa chuo,” anasema.

Anatoa mwito kwa wazazi kuwa makini na watoto wao na kuwaeleza madhara ya kujiingiza katika mahusiano kabla ya muda na pia kuwahimiza kutumia kinga ikitokea wakajiingiza katika masuala ya mapenzi.

Anasema kama angebahatika kupata mtoto hivi sasa, kitu ambacho angefanya ni kuzungumza naye, kumtaka asijiingize katika masuala ya mapenzi na ikitokea akapata tatizo kama alilopata yeye asithubutu kutoa mimba vichochoroni kwani kuna hatari nyingi, ikiwemo kifo.

TAKWIMU ZA KUTISHA

Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa vifo vya wajawazito vilikuwa 556 kati ya vizazi hai 100,000. Katika utafiti wawakilishi wa kwanza kitaifa kuhusu matukio ya utoaji mimba na huduma baada ya kuharibika kwa mimba nchini, iligundulika kwamba utoaji mimba kwa siri hutokea mara nyingi na huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye vifo vya wajawazito.

Utafiti huo, uliofanywa na watafiti kutoka taasisi ya Guttmacher iliyoko Marekani kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHANS).

Katika utafiti huo iligundulika kwamba takribani mimba 405,000 zilitolewa nchini ndani ya mwaka 2013, nyingi zikitolewa kwa taratibu ambazo si salama na kuhatarisha maisha ya wanawake.

Katika utafiti huo uliofanyikia kwenye vituo vya afya na kufanya mapitio ya taarifa za idadi ya watu na uzazi, iligundulika kwamba takribani wanawake 66,600 walipewa huduma baada ya kuharibika kwa mimba kwenye vituo vya afya kutokana na matatizo yaliyotokana na utoaji mimba usio salama ndani ya mwaka 2013.

Hata hivyo, utafiti ulionesha kwamba karibu wanawake 100,000 ambao walipata matatizo ya aina hiyo hawakupata matibabu sahihi waliyoyahitaji.

Hata hivyo, kwa kutambua kuwa utoaji mimba usiokuwa salama ni chanzo kikuu cha vifo vya wajawazito, Serikali imepanua wigo wa upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa mimba katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita.

Takwimu zilizopo pia zinaonesha kwamba kiwango cha kitaifa cha utoaji mimba nchini Tanzania ni wanawake 36 kwa kila wanawake 1,000 walio kwenye umri wa uzazi na kinafanana na viwango vya nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Hata hivyo, viwango vya utoaji mimba vinatofautiana kwa kanda ambapo viwango vya juu ya utoaji mimba vipo katika Kanda ya Ziwa ambapo ni wanawake 51 kwa kila wanawake 1,000 na Nyanda za Juu Kusini yenye wanawake 47 wanaotoa mimba kwa kila wanawake 1,000.

Kiwango cha chini kiko Zanzibar ambapo ni wanawake 11 kwa kila wanawake 1,000.

Viwango hivyo tofauti vya utoaji mimba huhusishwa kimsingi na utofauti katika viwango vya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na mimba zisizotarajiwa sambamba na uwezekano wa wanawake kuamua kutoa mimba baada ya kupata mimba zisizotarajiwa.

“Mbali na huduma baada ya kuharibika kwa mimba, wanawake wa Kitanzania wanahitaji upatikanaji bora na kamilifu wa huduma mbalimbali za njia za uzazi wa mpango na ushauri kuhusu uzazi wa mpango ili waweze kufanya uamuzi sahihi,” anasema Godfather Kimaro, mtafiti kutoka NIMRI. “Ndani ya mwaka 2013, wanawake wa Kitanzania walipata mimba zisizotarajiwa zaidi ya milioni moja, ambazo kati yake asilimia 39 ziliishia kwenye kutolewa,” anasema.

Anasema kukabiliana na mahitaji yasiyokidhiwa ya uzazi wa mpango kutapunguza kiwango cha mimba zisizotarajiwa na hivyo kupunguza uhitaji wa kutoa mimba na vifo na majeruhi ambayo mara nyingi hutokea baada ya taratibu zisizo salama.

Anahimiza umuhimu wa kujumuisha utoaji wa huduma za uzazi wa mpango kama sehemu ya huduma baada ya kuharibika kwa mimba na kushauri kila mwanamke anayetibiwa kutokana na matatizo yanayohusiana na kutoka kwa mimba apewe ushauri wa kina na nyenzo za uzazi wa mpango.

Naye daktari wa magonjwa ya wanawake kutoka kliniki ya serikali ya mama na mtoto iliyopo Makongoro mkoani Mwanza, John Chacha, anasema vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 30, wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari na vyuo ndio wanaokumbwa zaidi na tatizo la utoaji mimba usio salama.

Anasema wengi wanatumia njia za kienyeji ikiwemo dawa za kuzuia damu wakati wa kujifungua aina ya misoprostol bila kufuata taratibu na kuishia kupata maambukizi kwenye kizazi.

“Wengine wanakuja hapa wameshatoa mimba huko kwa njia wanazozijua wenyewe, kwa sababu kimsingi ni kosa kisheria kutoa mimba kwa sababu ambazo si za kiafya. Wanapofika hospitalini jukumu letu la kwanza ni kuokoa maisha yao. Tatizo wengi huja wakati mambo yameshaharibika sana. Wengine huja tayari damu imeshabadilika na kuwa usaha.

“Hatua kama hii ni mbaya kwa sababu kizazi kinakuwa kimeshaoza na mtu anakuwa anatoa harufu… Janga hili ni kubwa ingawa halionekani sana machoni pa wengi. Kuna vitu vya ajabu vinafanyika, watu wanafundishana namna ya kujitibu lakini hawajui kila mtu na mwili wake na mazingira yake pia,” anasema.

Daktari bingwa kutoka In gender Health ambaye pia ni mwanachama wa chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake (Agota), Anna Temba anahimiza familia kujitahidi kutoa elimu kwa watoto wao kuhusu madhara ya kujihusisha katika mapenzi yasiyo salama.

“Ukiachilia mbali sababu nyingine kama umasikini, kushindwa kujitetea (kubakwa), sababu kubwa inayoongoza kusababisha utoaji mimba usio salama ni upungufu wa habari za afya ya uzazi, uhaba wa elimu katika jamii inayowazunguka ikiwamo wanafamilia kutotoa elimu kwa watoto,” anasema Temba.

Mganga Mkuu mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa anasema madhara ya utoaji mimba kwa njia za kienyeji ni pamoja na kuipatia serikali hasara ya kumtibu mhusika kwa sababu wengi huwa katika hali mbaya ambapo huhitaji huduma ya dharura, ikiwemo kuongezewa damu.

Madhara mengine anasema ni kupata ugumba na wakati mwingine vifo kutokana na utoaji mimba ambapo bakteria kuingia sehemu wasiyohusika na kusababisha madhara mengi yanayosababisha kizazi au eneo kubwa la tumbo kuoza.

“Wengi huishia kutolewa kizazi na baadhi yao hufa kabisa kwa sababu wakifanya mambo hayo huona aibu kusema mapema na matokeo yake kizazi huzidi kuathirika au kuathiri mfumo mzima wa tumbo,” anasema.

Anasema Mwanza ni miongoni mwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ina idadi kubwa ya vifo vya wajawazito na vingi vinatokea kwa wajawazito wanaotumia mitishamba kuharakisha uchungu wakati wa kujifungua, ikiwemo utoaji mimba kwa kutumia mitishamba ambao usio salama abadani.





No comments: