Unatamani Uishi katika Mahusiano ya namna gani fanya hivi upate unachokitaka
AMANI na furaha ni sababu ya kwanza ya watu kuingia katika mahusiano. Lakini jiulize, umejiandaa kuitengeneza? Kama ilivyo kwa vitu vingine, furaha katika mahusiano pia ina misingi yake. Unaijua na uko tayari kuifuata? Wengi ukiwauliza hilo swali wataitikia ila hawatojitolea kwa vitendo na kauli kwa ajili ya misingi ya furaha katika mahusiano yao.
Moja ya kanuni muhimu ya kupata furaha na amani katika mahusiano yako ni kuwa na mtu unayempenda na yeye ukakupenda. Uko tayari kwa ajili ya kuwa makini na kuepuka pupa ili kupata mtu utakayependana naye? Walio tayari kwa hili ni wachache sana, ila wengi wao tamaa ya miili, mali na mkumbo imekuwa sababu kubwa ya kutafuta wapenzi katika maisha.
Wanawake wanampima mume bora kwa sababu ya kipato ama umaarufu wake. Namna anavyompenda na kumjali sio muhimu sana. Wako baadhi ya wanawake wako radhi hata kuolewa na yule mtu ambaye anavuma kwa tabia mbaya kisa ana uwezo wa kumuhakikishia maisha ya kisasa.
Thamani ya kuangalia upendo na tabia ya mtu imemezwa na tamaa ya mali na usasa. Baadaye mwanamke anayeoolewa katokana na sababu za mauza uza kama hizi, akikosa furaha katika mahusiano yake anasema ana mikosi. Unajiuliza ni mikosi gani wakati ulishindwa kufuata misingi na kanuni za kutafuta furaha ndani ya mahusiano yako?
Mwanaume mwingine anataka kutafutiwa mke aoe. Hili linaweza kuwa si tatizo. Ila je, unajua kuwa kila binadamu ana tabia tofauti? Je, umejiuliza kuwa baada ya kumuoa na hujajiandaa kwa tabia zake hali yako ya ndoa itakuaje?
Sisemi watu wakae kinyumba ndipo baadaye waoane. Ninachomaanisha watu wanatakiwa kujuana kitabia na misimamo kabla ya kuingia katika ndoa au mahusiano makini. Furaha yako ya kesho inategemea na msingi utakaojenga leo.
Na furaha ya mahusiano haiwezi kutokea ikiwa mmoja baina yetu hatokuwa na furaha. Furaha yako inategemea na mwenzako alivyo na furaha na furaha yake pia inategemea na wewe namna utakavyokuwa na furaha. Umejiandaa vipi katika mahusiano yako?
Ili mwenzako awe na furaha ni lazima awe na mtu anayempenda, una hakika wewe ni chaguo lake halisi? Au amelazimika kuwa na wewe kutokana na hali mbaya ya uchumi iliyopo nyumbani kwao na kuvutwa na hali njema ya nyumbani kwako?
Mapenzi yanayojengwa katika mtindo wa kusaidiana ama wa kulipana fadhila hata siku moja hayawezi kuleta matokeo tarajiwa. Ukiwa na mtu unayependana naye kwa dhati kila kitu kizuri kitakuwa cha kweli na cha milele.
Kumbuka furaha yako ya ndoa haijengwi kutokana na utajiri wake wala umbile lake la kibantu. Kumbuka mapenzi halisi ndiyo chanzo cha kila kitu cha heri katika mahusiano yako. Bila kujidanganya, jiulize ni kweli huyo unayetaka kuingia naye katika mahusiano mnapendana kwa dhati? Kipimo chako cha kuamini mnapendana kwa dhati ni nini?
Mwanaume kukupa pesa haina maana kuwa anakupenda. Kama anazo nyingi anashindwa vipi kukupa ili atimize lengo lake kwako? Mwanamke kumvulia nguo mwanaume na kumruhusu afanye lolote ajisikialo si kipimo cha mapenzi.
Huenda mwanamke husika ana mihemko ya kingono, sasa kivipi kwake iwe ngumu kufanya mapenzi na wewe? Kufanya ngono ni starehe, labda kaamua tu kustarehe na wewe, kivipi hiki kiwe kipimo cha mapenzi? Fikiri zaidi ya hapo. Hata makahaba na wanaoitwa Malaya wanagawa ngono, hiki hakiwezi kuwa kipimo cha mapenz halisi.
Unataka mpenzi wako awe vipi? Kabla ya kukimbilia kuanzisha mahusiano na mtu hakikisha kwanza kati yenu mnaunganishwa na mapenzi. Ni mapenzi pekee ndiyo yatakayoleta furaha na faraja katika maisha yenu. siku njema!
Instagram: g.masenga
Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia ( Psychoanalyst)
@@@@@
No comments: