YATIMA: Baba Nisamehe ,Mama bora ungebaki Tasa



“BABA naomba unisamehe… ni ujinga wangu na upumbavu wangu wa kukutaka uje kwenye ‘gradu’ (graduation- mahafali),” ni maneno ya kuchoma moyo ya mtoto Anna Zambi baada ya kufika kwenye makaburi ya wazazi na wadogo zake.


Mtoto huyo alifika nyumbani kwao Goba jijini Dar es Salaam jana saa 10 alfajiri, baada ya kumaliza mitihani ya kidato cha nne na kuanza safari kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mother Theresa of Calcutta ya Same mkoani Kilimanjaro bila kufahamu juu ya vifo vya ndugu zake.

Baba yake, Lingston Zambi, mama yake, Winfrida Lyimo pamoja na wadogo zake, Lulu, Andrew na Grace walikufa katika ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda kwenye mahafali yake kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwezi uliopita wilayani Handeni mkoani Tanga.

Alivyosafirishwa hadi Dar Baada ya kumaliza mtihani, bibi mzaa mama na nduguze wanaoishi mkoani Kilimanjaro, walitumia mbinu ya kwenda na keki hadi shuleni kwa Anna, wakampongeza kwa kumaliza mitihani kabla ya kuanza safari ya kurejea Dar es Salaam.

Binti huyo akiwa na furaha ya kurudi nyumbani, ilikatishwa na taarifa alizopokea hiyo alfajiri ya jana umbali mdogo kabla ya kufika nyumbani. Baada ya kukaribia nyumbani, watu wanne ambao ni waumini wenzake na marehemu wazazi wake, ndiyo walikwenda kumpa taarifa ndani ya gari. Mtoto huyo alilipuka kwa kilio, ikabidi asaidiwe kufikishwa nyumbani akiwa amebebwa.

Akiomboleza, mtoto huyo alisema licha ya kufichwa taarifa za msiba, alipata ishara kwani alikuwa hajisikii vizuri kiafya wakati wa kipindi chote cha mtihani.

Kilio ibadani, makaburini Wakati ibada ikiendelea, mtoto alikuwa akilia na kuomboleza kwa sauti hali iliyosababisha watu wengi kushindwa kujizuia kulia.

Mtoto huyo alisikika akisema: “umeniachia msiba… familia yetu sita nimebaki mmoja!” Vilio viliendelea kutawala miongoni mwa waombolezaji baada ya mtoto kupelekwa makaburini, umbali mdogo kutoka nyumbani na kushuhudia makaburi matano ya wazazi na wadogo zake.

Akiwa amekaa pembeni mwa kaburi la baba yake, Anna alilia akimuomba baba yake amsamehe kwa kile alichosema ni ‘ujinga’ wake wa kumshawishi aende kwenye mahafali yake.

“Baba naomba unisamehe…ni ujinga wangu na upumbavu wangu wa kukutaka uje kwenye ‘gradu’ ( graduationmahafali),” alisema.

Akiwa kwenye kaburi la mama yake, Anna alisema, “mama bora ungebaki tasa… tumekulipa zawadi ya makaburi”. Vile vile akiwa kwenye kaburi la mdogo wake Lulu, alilia akimshukuru kwa zawadi ya matokeo mazuri ya darasa la Nne. “Matokeo yako niliyaona lakini ya kwangu hukuyaona” alisema.

Anna aliendelea kuliza umati wa watu makaburini, kwa kusema, “ona makaburi haya yote ni yangu...mimi ni mdogo sana. Mliona wapi mtoto wa miaka 16 akibeba majeneza matano?...naomba mniombee (wazazi na wadogo zake) nami nife na mimi ni mwenzenu.”

Katika maombolezo, Anna alieleza wasiwasi wake wa kuendelea na masomo na kukidhi ndoto zake.

Aliwashukuru wazazi wake akisema walijitahidi kuwasomesha na wao hawakuwaangusha, kwani yeye na wadogo zake walikuwa wakifaulu vizuri.

Akilia mbele ya baba yake mdogo, Ibrahim Zambi, mara baada ya mtoto huyo kuwasili nyumbani alfajiri,

Anna alisema, “nina kuwa mzigo wenu…sijui kama nitasoma na kutimiza malengo yangu…Baba na Mama Anna (Ibrahim na mkewe) nipokeeni mnione kama mtoto wenu kama mnavyowaona Anna na John.”

Baba mdogo, Ibrahim alimhakikishia mtoto huyo kuwa atafanya kila liwezekanalo, kuhakikisha anatimiza malengo yake ya kielimu. Kwa mujibu wa baba mdogo, ndoto ya Anna ni kuwa Mwanasheria.

Daktari ashauri

Daktari Fredric Doya alisema anapaswa apumzike kwanza na aachwe apitie hatua zote za kupokea habari mbaya, kabla ya kuanza kupata ushauri wa kisaikolojia. Dk Doya ambaye yuko karibu na familia na wakati huo huo binti yake alikuwa akisoma shule moja na Anna, alitaja hatua hizo ni kukataa, hasira, kujiuliza maswali (kama taarifa husika ni za kweli) na kisha kukubaliana na hali halisi.

Alisema wakati akipitia hatua hizo, ni vizuri akaendelea kupata nasaha za kiroho na kuongeza kuwa hayo yakifanyika ipasavyo atarejea katika hali ya kawaida.

Shule ilivyozuia taarifa

Akizungumza kama mwakilishi wa wazazi wa watoto katika shule hiyo ya Mother Theresa of Calcutta , Doya alisema baada ya msiba, uongozi wa shule uliwathibitishia kwamba utahakikisha unazuia mianya yote, inayoweza kuruhusu taarifa hizo kuenea shuleni na kumfikia mtoto huyo, jambo lililotekelezwa.

Miongoni mwa mianya ya taarifa iliyozibwa kuhakikisha Anna hafahamu kuhusu msiba wa nduguze, ni pamoja na televisheni kutowashwa na pia kuhakikisha hakuna mawasiliano ya simu yanayowafikia wanafunzi.

Taarifa kutoka shuleni hapo, zinasema jana ndipo wanafunzi walipata taarifa hizo, baada ya wazazi kufika kuwachukua na baadhi yao kusikika wakitoa pole kwa uongozi wa shule, hali iliyosababisha vilio miongoni mwao.

Nasaha za Mchungaji

Akihubiri katika ibada ya shukurani iliyofanyika nyumbani hapo Goba, Mchungaji Hance Mwakisoja wa Kanisa la Moravian alisisitiza juu ya ukuu wa Mungu na kutaka Anna apewe zawadi ya kufarijiwa, badala ya machozi.

Amesema laiti jamii ingefahamu Anna ajaye atakuwa nani, kusingekuwa na majonzi.

Kwa upande wake, Mchungaji Gentleman Mwansile alihimiza kanisa lifuatilie maisha ya mtoto huyo ikiwa ni pamoja na kufahamu kama anasoma au hasomi.

Anna na baadhi ya wanafamilia wanatarajiwa kusafiri kwenda Mbozi mkoani Mbeya kwa ajili ya kupeleka msiba.





No comments: