HADITHI: REBEKA ( Zaidi ya Mwanamke) SEHEMU: 03
HADITHI: REBEKA ( Zaidi ya Mwanamke)
SEHEMU: 03
ILIPOISHIA:
"Ni jambo zuri mwanamke yoyote duniani uliomba usiku na mchana, ni kweli usemayo au ndio kutaka kuuchezea mwili wangu kwa kisingizio cha kunioa lakini ukitapa ulichokitaka uniache kama wasemavyo mjini kwenye mataa."
"Nimekuelewa nia yangu ni mke si ngono suala la ngono liondoe akilini mwako tutakutana kimwili baada ya kuwa mke wangu wa halali."
"Siamini maneno yako, kweli wewe ni mwanaume wa kwanza kutotanguliza ngono mpaka siku ya ndoa yetu."
SASA ENDELEA…
"Kuku wangu mwenyewe kwa nini nimshikie manati au nidokoe finyago ya nyama kwenye chungu wakati nyama ipo kwa ajili yangu."
Walijikuta wamefika kijiji cha pili bila kujijua Mabogo alimkalibisha Rebeka kwa shangazi yake.
"Ooh, baba! Karibu sana mbona usiku?"
"Shangazi si unajua siku zangu zimeisha kesho narudi mjini."
"Na kweli...Oooh samahani nimesahau kumkaribisha mgeni, karibu mama."
"Asante shangazi."
"Mabogo na huyu ni nani?"
"Mkweo mtalajiwa."
"Ooh! Karibu mkamwana wangu tena wewe mwenyewe kamkamatie kuku umchinjie nimpikie mkamwana wangu."
"Shangazi muda umekwenda tutachelewa."
"Hapana ulijua unakuja na mkamwana wangu ilikuwaje ukaja naye usiku hawezi kuondoka mpaka nimempatia heshima yake asijesema mkwe mchoyo au unataka nije kwako aninyime chakula?"
Mabogo hakuwa na jibu ilibidi akamate kuku na kumchinja kisha shangazi yake amtengeneze kwa ajuli ya chakula cha mgeni. Japo alijua Rebeka anaweza kuchelewa lakini hakuwa na jinsi, waliondoka kurudi kijijini kwao kiza kikiwa kimeingia.
Shangazi yake aliompa Rebeka zawadi ya kuku ili awapelekee wazazi wake kama ishara ya kukubalika. Rebeka aliipokea kitu kilichompa faraja moyoni kwa kujua hata kama akiingia nyumbani saa ngapi anacho cha kujitetea na muongeaji wake mkubwa atakuwa Mabogo.
Waliwasiri kijijini majira ya usiku, kijiji kilikuwa kimya wengi walikuwa wameisha lala. Kama kawaida vijijini majira ya saa tatu nyumba nyingi huwa wameisha lala. Rebeka na Mabogo waliwasiri nyumbani kwao na kukuta wameisha jifungia ndani lakini aliwasikia wazazi wake wakizozana juu ya Rebeka kutokuonekana.
Baba yake alimshtumu mkewe kwa kitendo cha kumkataza asipike labda walikuwa na lao jambo.
"Mume wangu kuna ubaya gani kumpumzisha mtoto kwani yeye ni punda?"
"Siku zote mtoto wa kike hatakiwi kudekezwa atakuja kututia aibu akiolewa ataonekana goigoi."
"Kama kumpumzisha mwanangu nimefanya kosa basi sikatai lakini bila yeye leo tusingekula."
Rebeka hakutaka waendelee kubishana alijua kama atachelewa wanaweza kushikana bila sababu za msingi siku zote mama Rebeka huwa hakubali kuonewa. Aliamua kugonga mlango sauti kutoka ndani iliuliza ni nani anayegonga Rebeka alijibu.
"Ni mimi."
"Wewe nani?" baba yake aliuliza.
"Mimi Rebeka."
"Unatoka wapi?"
"Baba Rebeka sasa hivi tulikuwa tunataka kukatana masikio kwa ajili ya Rebeka badala ya kumfungulia unamuuliza maswali kama anafukuzwa?"
Mama Rebeka alisema yale huku akitoka sebuleni na kwenda kufungua mlango
"Ooh! Mwanangu ulikuwa wapi mama? He! na kuku umemtoa wapi usiku huu na huyu ni nani?" mama Rebeka aliuliza.
Rebeka kabla hajamjibu mama yake wakati huo na baba yake alikuwa ameisha toka nje alimkaribisha Mabogo.
"Mabogo karibu japo ni usiku hapa ndipo kwetu na walio mbele yako ni wazazi wangu baba na mama."
"Asante sana... samahani sana wazazi wangu kwa kumrudisha mwenenu usiku mkubwa kama huu, najua sio tabia yake naomba kwanza mnisamehe kwa hilo."
"Sawa baba, lakini wewe ni nani?"
"Naomba nimwache Rebeka azungumze kwanza, mimi nitakuwa mjibuji wa maswali mtakayo niuliza."
Rebeka alieleza habari zote kuanzia kufahamiana na Mabogo kuanzia shule ya msingi na asubuhi alivyo msaidia kuni na jioni walipokutana na maongezi waliyo yaongea na kuku yule alipomtoa.
"Baada ya maelezo hayo wazazi wangu napenda kuwaomba radhi kwa kitendo nilichokifanya cha utovu wa nidhamu kwa kuondoka kwenda kijiji cha jirani bila ruksa yenu," Rebeka aliwaomba radhi wazazi wake.
"Mwanangu Rebeka nakujua vizuri siwezi kukuhukumu ila nakusameheni wote...sasa wewe na mwenzio mmefikia hatua gani?"
"Hakuna hatua yoyote zaidi ya nyinyi wazazi wangu mtambue kuna kitu gani mbele yangu ni nyinyi kusikiliza na kutoa maamuzi."
"Hakuna anayepinga jambo la heri la muhimu kijana walete wazazi wako kwanza wewe ni mtoto wa nani hapa kijijini?"
"Mtoto wa marehemu Mkama Mabogo."
"Acha utani na wewe ndiye nani?"
"Naitwa Mabogo."
"Ooh! Kijana kumbe ni mtoto wa rafiki yangu marehemu Mkama wa Mabogo, wewe ni mwanangu hakuna kitakacho badilika kamilisha vitu vyote kulingana na mila zetu.”
Mabogo aliagana na wazazi wa Rebeka na kurudi kwao kulala ili asubuhi aondoke tayari kurudi na kukamilisha mipango yote ya harusi jukumu kubwa alimuachia shangazi yake na mdogo wake Lyasi.
Rebeka kwa upande wake usiku ulikuwa mfupi kwake muda mwingi aliwaza juu ya ndoa yake, aliona kama miujiza kuolewa mjini kitu alichokiomba usiku na mchana aliogopa kuolewa kijijini kwa kuogopa kuchakazwa na kuzalishwa bila mpangilio miaka kumi kwenye ndoa na watoto kumi kila mtoto na mimba juu hupumziki.
*****
Mipango ilikwenda kama ilivyo pangwa hatimaye Rebeka aliolewa na Mabogo kwa sherehe kubwa iliyokuwa simulizi pale kijijini na kuhamia mjini na mumewe. Baada ya harusi aliyaanza maisha mapya mjini kama mke wa mtu na kufanya mabadiliko makubwa na maisha yake.
Hali ya maisha ya mumewe ilikuwa ya kawaida kipato cha kawaida lakini kilikidhi mahitaji yote muhimu. Ndani mwake hakuna kilichopungua yalikuwa ni maisha ya kati ambayo mtu huwa halali na njaa na kula anachokitaka sio anachokipata.
Mumewe alionyesha mapenzi ya dhati kwa mkewe naye Rebeka alionyesha mapenzi ya dhati kwa mumewe. Ilikuwa ndoa iliyojaa neema na Baraka, katika miezi miwili Rebeka alishika ujauzito hapo mapenzi kwa mumewe yaliongezeka na alipo karibia kijifungua kama zilivyo mila nyingi za kiafrika alirudi nyumbani kwao kujifungua.
Mungu alimjalia kujifungua salama mtoto wa kike waliomwita Nyangeta jina la mama yake Mabogo.
Baada ya arobaini kuisha alirudi mjini kuendelea na maisha yake. Maisha waliyoishi Rebeka na mumewe yaliwaumiza wengi waliojiuliza wanasiri gani ya kuishi muda wote huo bila kukosana.
Siku zote palipo na neema hapakosi fitina watu walitafuta kila njia ya kutafuta urafiki na Rebeka mpaka wakafanikiwa jambo ambalo mumewe alimuonya kuwa asipende mashoga wa mjini wengi wao ni wahalibifu wa ndoa za watu zilizotulia.
Mwanzo aliweza kumsikiliza mumewe lakini hawakuchoka alifikia hatua ya kukubali kuongea nao. Mwanzo walianza kama marafiki wema ambao walimfundisha mambo mengi ya maisha ambayo aliyaona kama kufunguka macho angejuaje bila kumkaidi mumewe.
Mawazo waliyompa ni mwanake kujishughulisha asiwe golikipa kuna leo na kesho mumewe anaweza kufariki ghafla atashindwa aanzie wapi pia walitaka kujua maisha yake ya kijijini. Rebeka bila kuficha alianika mambo yake hadharani hapo ndipo walipo mwambia:
"Ona shoga kama ulivyosema familia yako ni hohehahe kwa nini uendelee kumtegemea mumeo?" wa kwanza alisema na wa pili aliongezea:
"Hivi kama ukifanya kazi ukipata pesa zako ambazo hazitahusiana na mumeo unaweza kusaidia wazazi wako hata kumpunguzia mzigo mumeo hata kukunyanyasa hawezi."
"Mimi ningejuaje?" Rebeka alisema kwa unyonge.
Inaendelea
🔞WAKUBWA TU:TAZAMA VIDEO ZA WAKUBWA LIVE UJIONEE STAILI KALI ZA KUMFIKISHA KILELENI MPENZI WAKO
No comments: