LEYLA..! (Binti bikra) ~Sehemyu ya14~


LEYLA..!
(Binti bikra)


~Sehemyu ya14~

Ilipoishia..
Eti nilikuta kitandani kwangu limewekwa gauni zuri jeupe kama wanalovaa mabibi harusi, hapo ndio niliishiwa nguvu kabisa na kujikuta nikidondoka chini na kupoteza fahamu kwa mara nyengine tena..

Endelea..
Nilikuja kuzinduka ilikua tayari kulishakucha, nakumbuka ilikua ni saa4 asubuhi ambapo niliamka na kujikuta nimelala kitandani jambo ambalo hata sikulifanya, kumbukumbu yangu ya mwisho inasema nilidondoka na kupoteza fahamu palepale mlangoni kabla hata sijafika kitandani, sasa inakuaje niamke nikiwa nipo kitandani.
Wakati najiuliza maswali hayo hayo mara ghafla nikasikia mlango wangu ukigongwa, nilinyanyuka ili nikaufungue, hee ile nafungua tu nikamkuta mvulana mzuri ajabu huku akitanasamu, yule mvulana wala hakusema kitu aliingia mpaka ndani bila ya kukaribishwa.
Alipoingia tu ndani harufu ya chumbani kwangu ilibadilika na kunukia harufu ya mafuta mazuri, yaani kama mchanganyiko wa marashi na karafuu.
Yule kijana alizidi kuniangalia usoni kisha akaanza kwa kusema.
" Hivi Leyla unaijua thamani yako..?" Aliniuliza swali ambalo hata sikulitarajia.
"Sikuelewi unajua.. kwanza haujajitambulisha halafu unaniuliza vitu ambavyo binafsi vinaniumiza kichwa..!" Nilijibu kwa hamaki.
" Leyla.. mimi naitwa.. aaah.. jina nitakutajia mwishoni kabisa, kwanza nilikuandalia nguo pamoja na pete jana usiku hapo kitandani kwako, lakini nikagundua bado hujawa tayari kunipokea kwani kila nilipokua nikijitokeza katika umbo langu halisi ulikua ukizimia..
Sasa leo nimekuja katika umbile kama lenu binaadamu wa kawaida.." alisema yule kijana ambapo hata sikuweza kusikia maneno yake amalizie kwani nilishapoteza fahamu zamani baada ya kujua kuwa kumbe hakua binadamu wa kawaida.

Nilikuja kuzinduka saa7 mchana, na kilichonishtua ni adhana iliyokua ikipigwa msikitini, hapo niliamka na kusimama kutaka kwenda kujimwagia maji, lakini nilipoangalia kwenye kochi nilishtuka baada ya kumuona tena yule kijana akiwa amekaa huku akiniangalia.
"Huna haja ya kuniogopa Leyla.. taratibu utaizoea hali ya kuonana na mimi, hakika wewe ni binti mwenye bahati sana..
Kwasasa hivi nawahi kwenye kikao ila nitakuja kukuchukua usiku nikupeleke sehemu ambayo hutakuja kuisahau katika maisha yako.." Alimaliza  kuelezea mtu yule na kupotea palepale.
Yaani mtu yule kama alikua anajua kitu kilichomo moyoni mwangu, kwani nilijishangaa safari hii nilimsikiliza mpaka mwisho bila ya kuzimia..

Basi nilikwenda kuoga na kurudi ndani kuvaa, kisha nikaenda kutafuta chakula.
Niliporudi nilikuta kitandani kwangu limewekwa lile gauni la jana usiku pamoja na ile pete, kwa pembeni kulikua na kikaratasi cheupe.
Nilikwenda kuichukua ile karatasi na kuanza kuisoma.
"Hilo gauni na pete utavaa siku utakayokua tayari kunipokea ili ulimalize tatizo lako, mimi sio binadamu wa kawaida ila kamwe siwezi kukudhuru kwani wewe ndie kiumbe ninaekupenda, naahidi kukulinda na kukutimizia kila utakachohitaji, mengi zaidi tutaongea usiku nikija kukuchukua..!" Looh.. mwenzenu nilichoka hoi baada ya kumaliza kukisoma kikaratasi kile, moyo wangu ulikua ukienda mbio sana, ghafla nikajikuta nakaa chini na kuanza kulia bila kujua hatma ya maisha yangu itakuaje.

Siku hiyo nilishinda ndani bila kutoka nje kabisa, nilikua nikijaribu kutafakari juu ya nini cha kufanya ili niiepuke mitihani inayokua ikiniandama kila siku.
"Sasa mimi nimekosea wapi..! Mbona toka nilivyozaliwa kwangu ni mitihani tu.. eeh.. mungu wangu..!" Nilijikuta najiuliza bila kupata majibu huku machozi yakizidi kunitoka.
Sijui hata ilikuaje nikajikuta napitiwa na usingizi.
Nakumbuka ilikua saa4 usiku baada ya kumaliza kula, nikaenda chooni kujimwagia maji ili nijiandae kulala.
 Nikiwa chooni najipaka sabuni, ghafla nikasikia harufu ya marashi na karafuu, nikahisi ni ile harufu ya kama mchana, hivyo ilinibidi ninawe maji usoni harakaharaka kutoa sabuni ili niweze kufumbua macho, loh.. tobaa.. yule mtu wa mchana alikua amenisimamia mbele  yangu huku akinikodolea mimacho yake.
"Wewe umeingiaje huku..!" Nilijikuta nauliza huku nikiwa natetemeka na kujiziba kwenye uke wangu ili asinichungulie.
"Huna haja ya kunihofia Leyla.. siwezi kukudhuru naomba uniamini, naamini hautajuta kukutana na mimi katika maisha yako.. nakusubiri tuondoke.." Alisema yule mtu na kupotea palepale.
Basi kwa wenge nililokuanalo hata sijasubiri nimalize kuoga, nilichukua taulo na kuanza kujifuta maji na mapovu, kisha nikatoka hadi ndani kwangu ambapo nilimkuta yule mtu akiwa amekaa kwenye kochi kunisubiria.
Aliniambia nivae nguo yoyote niipendayo lakini ni lazima iwe ni nguo yenye rangi nyeusi..

Basi baada ya kumaliza kuvaa alinisogelea na kunishika mikono yangu miwili kwa mbele huku akiniangalia usoni kwa jinsi nilivyokua nikimuogopa, kisha akaniambia nifumbe macho yangu.
"Haya fumbua.." Aliniambia maneno hayo yule mtu.
Heee.. jamani.. nilipofumbua macho yangu nilishindwa kujua pale nilikua nipo wapi, ila nilichokijua ni kuwa tulikua tumekaa juu ya jiwe kubwa sana mfano wa jabali ambalo kwa chini lilikua limezungukwa na maji ya bahari..
Hakika niliogopa sana..
"Hapa tupo wapi jamani..!" Niliuliza kwa uoga wa kuogopa kutupiwa baharini.
"Usiogope Leyla.. hapa upo katika ufalme wangu, hakuna kiumbe mwengine yeyote mwenye mamlaka ya kupita maeneo haya..!" Alijisifu yule mtu.
"Sasa huku tumekuja kufanya nini..?" Nilizidi kuuliza kwa hofu kubwa.
Badala ya kunijibu, yule mtu alinyoosha kidole chake mbele na kuniambia.
"Angalia pale mbele Leyla.. kuna kitu nataka ukijue leo..!" Aliniambia mtu yule ambapo nilishanga kuona imekuja kama scrin au tv kubwa mbele yangu na kuonyesha matukio ambayo mwanzo sikuyafahamu, ila baadae ndio nilianza kuyafananisha.
Katika Tv ile niliweza kumuona mama mmoja akiwa anagombana na mawifi zake kwakua alikua hapati mtoto, ndipo alipoamua kwenda kwa mganga wa kike kuomba amsaidie.
Yule mama aliingiziwa mimba na yule mganga wa kike kwa njia za miujiza kwa kutumia maji ya bahari, ambapo alipewa masharti na makubaliano kuwa lazima amtoe kafara mumewe ambae kifo chake kilipangwa kiwe siku ambayo atakayojifungua mtoto huyo.
Pia baada ya mtoto huyo kuzaliwa, lazima aolewe na mrithi wa utawala utakaokuwepo kwa kipindi hicho..
Heee.. jamani.. eti katika ile Tv niliweza kumuona yule mama mganga ambae ndio mlezi wangu wa Zanzibar.
Mh.. kiukweli nilichoka sana.
"Yule mama aliyekua anatafuta mtoto, ndio mama yako mzazi, nimeona nikuonyeshe japo sura yake angalau umuone mlivyofanana..! na mrithi wa utawala kwa sasa ndio mimi.. ila sitokulazimisha uolewe na mimi Leyla.. nenda nyumbani ukafikirie kuhusu hatma ya maisha yako kwanza..!" Alisema mtu yule na kutaka kuondoka, lakini kabla hajaondoka nilimuuliza swali.
"Na kwanini kila mwanaume ninaekutananae kimapenzi unamuua..? Kama haunilazimishi unioe kwanini usiniache huru sasa niishi na binadamu wenzangu.!" Nilimuuliza huku nikilia kwa uchungu.
"Leyla.. mama yako aliingia mkataba na viumbe wengi sana bila ya kujua.
Katika viumbe hao, wapo viumbe wazuri na wabaya pia, jukumu langu kwako lilikua ni kukulinda ili uwe salama, ila kuhusu tatizo la kuuwa hao binadamu ni la viumbe wabaya ambao nao watakuja kutaka kukuoa pia, ila kama utanikubalia nikuoe mimi hawatoweza kukufikia kamwe na tatizo hilo litaisha kwangu..
Kwa sasa nenda kafikirie, ukihitaji msaada wowote na wakati wowote ivae ile pete tu nitakuja hapohapo.. kwaheri Leyla..!" Hayo ndio yalikua maongezi ya mwisho ya yule mtu.

Mara ghafla nikajikuta nipo kitandani naamka, kumbe tayari kulishakucha..

Itaendelea..!



No comments: