THAMANI YA FUKARA. Sehemu ya tatu-03.





Jambo la Layla kumfikiria sana Gabi lilisababisha aanze kushuka kimasomo,kwenye nafasi kumi za juu hakuwemo tena,mda mwingi alikuwa mtu wa mawazo, wazazi wake walipojaribu kumuuliza tatizo hakuweza kuliweka wazi.
Ilikaribia mitihani ya mwezi ya sita,Doris rafiki yake Layla alijaribu kumshauri kuwa aachane na yale mawazo lakini Layla hakutaka kusikia la mtu,furaha yake ingerejea pindi ambapo angeliweza kumuweka Gabi mikononi mwake,lakini angemweka vipi mikononi mwake ilihari moyo wake ni mzito hautaki kusema hisia zake?yalikuwa maumivu ya kila siku.
"Shoga yangu utanisaidia vipi ili nimuweke kwenye himaya yangu?",Layla alimuuliza Doris,
"Kwakweli shoga yangu bado ni mtihani mgumu sana, nadhani tufikirie masomo kwanza halafu haya mambo tutayafanya baada ya kumaliza mtihani"aliongea Doris,
"Nini?"aliwaka Layla,yaani tuachane nayo?hivi unajua moyo wangu unaumia kiasi gani?au hujui kila siku natoa chozi kwa ajili ya Gabi?sasa unaponiambia hizi habari tuziweke kando nashindwa kukuelewa kabisa".
"Naelewa shoga yangu lakini huna budi kuyaacha hayo mambo,unatakiwa ufikirie mitihani itakayoanza wiki ijayo"aliongea Doris akijaribu kumtuliza Layla lakini juhudi zake ziligonga mwamba Layla hakutaka kusikia chochote.Wakiwa kwenye maongezi yale mara mbele yao alipita Gabi,Layla alinyanyuka na kumuita Gabi lakini hakusimama zaidi alikaza mwende,Layla alibaki amesimama huku machozi nayo hayakuwa mbali.
"Umemuona?umeona alivyo sijui nimfanyie nini mimi"aliongea Layla huku kitambaa kikiwa mikononi mwake kwa ajili ya kufutia machozi.Doris alikuwa na kazi ya kumfariji Layla,
"Kesho nitaandika  barua kisha nitakupa umpelekee"aliongea Layla kwa sauti ya chini na yenye huzuni ndani yake.
"Basi jitahidi twende darasani shoga yangu"aliongea Doris huku akimuinua Layla.Hata mda wa masomo macho ya Layla yalikuwa kwa Gabi mda wote.Mda wa masomo ulipoisha wanafunzi waliruhusiwa kwenda makwao,Gabi alifika nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa nje anachambua njugu mara baada ya salamu maongezi ya hapa na pale yalishika nafasi,
"Leo nimekimaliza kila kibarua hivyo saa moja jioni naenda kuchukua hera halafu soksi nitakununulia kesho"aliongea mama yake Gabi,
"Soksi ninazo tayari kuna rafiki yangu kanipa tena ni mpya kabisa"aliongea Gabi,mama yake alishtuka na taharuki akauliza,
"Usije kuwa umeiba halafu unadanganya"
"Hapana mama we niamini tu mimi sina sifa za wizi"alijibu Gabi,mama yake alifurahi hiyo hera aliyokuwa amepanga kununua soksi ilifanya matumizi mengine.
Usiku huo kwa upande wa Layla ulikuwa mgumu kabisa,hakupata hata lepe la usingizi,hakuukumbuka tena kuwa kuna mitihani itakayoanza siku chache zijazo,kalamu ilikuwa mkononi mwake huku karatasi ikiwa juu ya meza,alikuwa ameliangalia paa la nyumba huku mkono wake mmoja ukiwa shavuni,alifikiria maneno ya kumwandikia Gabi,lakini alipokuwa kwenye hali ile mara machozi yalimtoka na kudondokea kwenye ile karatasi,alitafuta nyingine lakini nayo aliilowesha kwa machozi,hadi inafika saa saba za usiku alikuwa bado hajaandika neno lolote pale kwenye karatasi,alifikiria maneno yatakayomfurahisha Gabi lakini kila neno aliliona halifai,mpaka usingizi ulimpitia pale pale akiwa bado hajaandika neno hata moja.Asubuhi ya siku ile alichelewa kuamka mpaka pale mama yake alipomuamsha,alinishangaa kujikuta akiwa amelala pale pale mezani,mikono yake ilikuwa na upele uliosababishwa na kung'atwa na mbu,alipoitazama karatasi ile alikumbuka kuwa jana yake usiku alikuwa ameiandaa kwa ajili ya kumwandikia barua Gabi,
"Au shuleni utaenda kesho? maana mda umeenda sana sahivi saa mbili"aliongea mama yake Layla,
"Hapana mama wacha niende, mwambie Juma ajiandae basi"aliongea Layla huku machoni kwake kukiwa bado na usingizi,
"Sasa nisipoenda shuleni Gabi wangu nitamuona wapi?lazima niende hata kama ni saa nne"alijisemea Layla.Majira ya saa mbili nanusu asubuhi ndo alikuwa anafika shuleni,alikuta vipindi vikiwa tayari vimeanza,lakini hakuhofia kitu chochote,alishuka kwenye gari na kuingia darasani ambapo alimkuta mwalimu akiwa anaendelea na kipindi,yule mwalimu hakumuuliza kitu chochote zaidi ya kumrusu kuingia darasani,walimu waliokuwa wanamjua baba yake Layla hakuna aliyeweza kumpiga Layla tofauti na Bernard ambaye alikuwa mwalimu mgeni kwenye shule ile.Baada ya kuketi kwenye nafasi yake Layla alihakikisha anamuangalia Gabi kwanza,alipohakikisha amemuona alitoa madaftari yake na kuanza kujisomea,lakini hakukawia usingizi ulimpitia,hadi kipindi kinaisha yeye alikuwa bado amesinzia.
Jumatatu mitihani inaanza hivyo kwenye somo langu ukipata chini ya hamsini ujue ntakula nawe sahani moja"aliongea yule mwalimu aliyekuwa anafundisha somo ya kiswahili,sauti ile ilimshtua Layla aliyekuwa usingizi alikurupuka usingizini na kumkuta mwalimu akimalizia kipindi.Mda wa kipindi cha mwalimu Bernard uliwadia,kila mwanafunzi alijiandaa kwa kipindi na mda mfupi aliingia mwalimu Bernard,Kama kawaida yake fimbo zilikuwa mikononi mwake,
"Shikamooni mwalimu"wanafunzi wote waliinuka na kumsalimia,
"Sihitaji salamu zenu,nawaomba mketi chini huku kila mwanafunzi daftari lake alifunue na kuliweka juu ya meza,au kama unajua hujaifanya kazi yangu pita mbele mapema tusije kusumbuana"aliongea mwalimu Bernard.Layla ile kazi hakuifanya hivyo alipita mbele mapema,mwalimu Bernard alianza kukagua mmoja baada ya mwingine, hatimaye alimfikia Gabi, alibaki kumtazama kazi alikuwa ameifanya lakini kati ya maswali matano hakupata hata moja,
"Nyie ndo vilaza darasani sasa mitihani inaanza jumatatu mnategemea nini?hebu shika huko fimbo tano zinakuhusu"aliongea mwalimu Bernard,Layla aliweza kuliona tukio lile hakuwa tayari kumuona Gabi akiadhibiwa kwa kuwa alikuwa amesimama mbele hivyo alianza kuzipiga hatua kumfuata mwalimu Bernard alikuwa tayari kumuadhibu Gabi.
Layla atafanya nini?nakusihi baki nami.





No comments: