NJIA SAHIHI YA KUONDOKANA NA WIVU KATIKA MAHUSIANO YA KIMAPENZI
Wivu ni chachandu, vilevile ni kionjo cha mapenzi. Wakati mwingine ni sumu ya uhusiano, hali kadhalika hutokea kuwa kikwazo cha penzi endelevu. Ni vizuri kulitambua hilo ili ujue jinsi ya kuishi kwa kuendana na mazingira yanayofaa.
Mtu mwenye mafanikio kwenye mapenzi ni yule anayeamini katika saikolojia ya kujitambua. Hapa nikupe msisitizo kuwa ni lazima ujitambue ili uweze kuwa bora kwenye mapenzi. Kama hujitambui, maana yake hutajua ulitendalo.
Ikiwa utashindwa kujua ulitendalo, wewe utageuka kuwa kero kwa mwenzi wako. Ukifikia hatua hiyo, unadhani ni nani anaweza kukuelewa? Ni vema ujijue, ujifahamu kasoro na uimara wako katika uhusiano wako. Kama unamfurahisha au kumchukiza, yote yanafaa kugota ndani ya kichwa chako.
Je, una wivu? Hilo unapaswa kulitambua kwa sababu lipo ndani yako. Bahati mbaya ni kwamba watu wanakuwa na wivu wa kupitiliza lakini wakiambiwa wanakuwa wakali. Wanadai wanasingiziwa.
Ni vizuri ukatambua upungufu ulionao kabla ya kuelezwa na mtu wa pili.
Wivu wako umekugharimu mara ngapi? Makala haya yanatosha kuwa tiba yako ya kudumu. Pengine hujawahi kukaa, ukatafakari na kugundua kuwa wivu wako unakupeleka njia isiyo sahihi kimapenzi, hapa chini kuna mambo ambayo ni muongozo madhubuti.
Jifunze kwa watu wengine.
Mara nyingine ni rahisi kugundua kuwa unafanya makosa baada ya kuwaona wengine na kujifunza kutoka kwao. Hivyo basi, jaribu kuwaangalia watu wengine walio kwenye uhusiano. Fuatilia mtindo wao wa maisha, mafanikio yao kisha ujitazame wewe.
Bila shaka hapo ulipo, utakuwa umeshawahi kujionea wanaume na wanawake wenye wivu, jinsi wanavyotenda mambo yao, wanavyoudhi na kuchukiza kwenye uhusiano. Kama ndivyo, basi hilo ni somo kwako kwa kuepuka yale yaliyowafanya wachukize.
Inawezekana ukawa umeona kupitia kwa macho yako au umesimuliwa. Muhimu kutambua ni kwamba hulka za wivu, hususani unapozionesha mbele za watu wa pembeni ni mbaya. Kwa mantiki hiyo, kama utaweza kutambua na kuelewa alama za wivu, sina shaka kuwa utakuwa unaweza kujua jinsi ya kuishi katika mazingira salama.
No comments: