NYUMBA YA MAAJABU 11




                   

Muda kidogo Jane nae aliwasili ambapo cha kwanza kabisa alipofika mlangoni alishangaa kuona kama unga unga na kumuuliza Sophia,
“Dada ni nini hiki mlangoni?”
“Wewe pita tu kuna vitu vilianguka”
KwakweliSophia hakupendezwa kabisa na hili swali la Jane kwani alizidi kujidhihirisha kuwa ni mchawi, Jane aliingia ndani na kukaa pale sebleni kisha Sophia akaenda jikoni kumletea ile juisi.
Wakati Sophia akitoka jikoni na ile juisi akamshangaa Jane akiwa ametulia kabisa akiangalia Tv ambayo yeye hakuiwasha kwavile alikuwa akimsubiri fundi atakayeletwa na mumewe, kwahiyo Sophia alimuuliza Jane kwa mshangao,
“Kwanini umeiwasha hiyo Tv Jane ni mbovu”
“Sijaiwasha dada, nimeshangaa imewaka tu”
*TUENDELEE...*

Sophia alimuangalia Jane kwa jazba sana tena kwa mshangao mkubwa sana kwani aliona akimtungia maneno tu muda ule, akamuuliza tena
“Inamaana imejiwasha?”
“Mi sijui, nilihisi labda umeme ulikatika na ukasahau kuizima sasa ndio umerudi na kuwaka moja kwa moja”
“Haiwezekani yani ni haiwezekani kabisa, hata hivyo karibu juisi”
Sophia akampatia Jane ile glasi ya juisi, ambapo Jane nae aliipokea na kushukuru.
Sophia alikaa kwenye kochi huku akimsubiria Jane anywe ile juisi ila Jane alikuwa kimya kidogo huku kaishikilia ile juisi na kumfanya Sophia amuulize,
“Mbona hunywi sasa!”
“Nakunywa dada, nilikuwa naiombea kidogo”
“Kheee inamaana huniamini?”
“Hapana dada, nakuamini sana tu ila mama jana alinifundisha vitu vingi sana na ndiomana saivi nataka kuanza tena kumrudia Mungu”
“Kwahiyo amekufundisha kutokuamini watu na kuombea kila wanachokupa?”
“Usinifikirie vibaya dada ila jana kuna makala nilisoma ilinifundisha vitu vingi sana ndipo nilipomuuliza mama nae akanielezea mambo mengi, tunatakiwa kukabidhi kwa Mungu kila kitu tunachofanya. Kama ile juzi ningemuomba Mungu aniongoze basi yasingenitokea yote yale yaliyonitokea ila kwavile nilitumia akili zangu za kibinadamu ndiomana ikawa vile. Natakiwa kukabidhi kwa Mungu kitu chochote kile hata nilichokitengeneza mwenyewe”
Kisha Jane akanywa kidogo ile juisi ila alishusha glasi na kutoka nje na kuitema, kwakweli Sophia alimshangaa sana hata ghadhabu yake ikazidi maradufu na kumfuata nje na kumuuliza kwa ukali,
“Yani unatema juisi niliyokupa! Kama ulikuwa hutaki si ungesema tu kwani ningekulazimisha jamani?”
“Dada jamani hebu shika na wewe uionje, hii juisi ni chungu wala sijaitema kwa kutaka”
Sophia alichukua ile juisi ila alishindwa kuionja kwavile alijua wazi kitu ambacho ameweka kwenye ile juisi, kisha akarudi sebleni na ile glasi ya juisi ambapo Jane nae alirudi pale sebleni ambapo ile Tv iliendelea kuonyesha kama kawaida.

Walipokuwa wamekaa Sophia akamuangalia tena Jane na kumuuliza,
“Inamaana hii juisi kweli ni chungu?”
“Hata wewe ionje dada ni chungu kweli labda ni kikombe”
“Toka lini juisi ya embe ikawa chungu?”
“Mi sijui dada ndiomana nimesema labda ni kikombe”
“Mmmh una mambo yako tu wewe na hata sio kwamba juisi ni chungu”
“Kama unabisha dada ionje na wewe uhakikishe nisemayo”
“Nionje ili nife!”
Jane akamshangaa sana Sophia maana juisi kaileta mwenyewe halafu yeye huyohuyo anakataa kuionja, moja kwa moja Jane akahisi kuna uwalakini kwenye ile juisi na kisha akamuuliza Sophia,
“Kwani dada umeweka nini kwenye hiyo juisi?”
“Unahisi nimeweka nini?”
“Mi sijui maana uliyetengeneza ni wewe”
“Sijaweka chochote”
“Basi labda maembe uliyotengenezea yalikuwa mabovu”
“Unayajua maembe mabovu wewe au unaongea tu”
“Dada usipaniki tafadhali”
Mara Tv ikajizima tena na kufanya watazamane ambapo moja kwa moja Jane alihisi kuwa umeme umekatika,
“Mmmh umeme umekatika nini?”
“Umeme ungekatika friji lingeendelea kuunguruma?”
“Khee dada mbona unaongea kwa hasira hivyo jamani! Mi nimeuliza tu”
“Si nilishakwambia kuwa hii Tv ni mbovu sasa maswali gani unauliza hayo”
“Basi yaishe dada”
Mara mlango ukagongwa na aliyeingia alikuwa ni Ibra, ila alishangaa uwepo wa Jane mahali pale kuwa imekuwaje hata ikawa rahisi sana kwake kusahau kilichotokea juzi. Ila alimkaribisha vizuri tu,
“Oooh Jane nafurahi sana kukuona upo hapa na mke wangu, kwakweli karibu sana”
“Asante ila mimi ndio napaswa kukukaribisha wewe sababu ndio umenikuta”
“Ni kweli nimekukuta ila hapa ni kwangu na nina haki ya kukukaribisha”
Ibra akakaa kwenye kiti ila macho yake yalienda mezani moja kwa moja ambapo aliona glasi ya juisi, ila alishangaa kitu na kuuliza kwa mshangao,
“Kheee hii juisi nyekundi ni juisi gani?”
Sophia na Jane kwa pamoja walijikuta wakiiangalia ile juisi ambapo Jane nae aliuliza kwa mshangao,
“Mmh hii juisi si ilikuwa na rangi ya njano hapa, imekuwaje imebadilika?”
Sophia alizidi kushangaa tu bila kusema neno lolote kwani alihisi huenda ile dawa aliyoweka kwenye ile juisi ndio imeibadilisha baada ya kukaa kwa muda.
Ibra akachukua ile glasi ya juisi na kuiangalia kwa karibu ila alishtuka sana kuona kama vitu vikicheza cheza ndani ya glasi ile, ambapo aliiacha chini na kumwambia Sophia,
“Hebu angalia ndani ya hiyo glasi, hivi ni juisi kweli hiyo?”
Jane akadakia kujibu,
“Ndio ilikuwa ni juisi sema ilikuwa chungu”
Kisha na yeye Jane akachukua ile glasi kuangalia ila alichokiona kilimshtua zaidi na kumfanya aiachie ile glasi ambapo ilianguka chini na kupasuka, ila kilichotapakaa baada ya ile glasi kupasuka kiliwashtua wote kwani ilikuwa kama damu ya mtu imemwagika.
Ibra alikuwa wa kwanza kuuliza,
“Ni mambo gani haya jamani?”
Huku akiamini kuwa huenda maneno ya mke wake kuwa Jane ni mchawi ni ya kweli, alimuangalia Jane na kumuuliza,
“Ni wewe uliyetengeneza hii juisi?”
“Hapana, mi mwenyewe nililetewa na dada ili ninywe”
Ibra akamuangalia kwa makini mkewe ila Sophia hakuweza kusema chochote kwani alikuwa akitetemeka tu na ukizingatia alikuwa anajua kinachoendelea, Ibra aliamua kumuuliza mkewe sasa
“Unaweza kuniambia hii juisi imekuwaje?”
“Sijui imekuwaje ila nitakueleza ninavyojua mimi ila naomba Jane aondoke na tuongee kifamilia”
Jane hata hakutaka kuangaliwa na kuambiwa ondoka kwani pale pale aliaga na kuondoka zake.

Ndani ya nyumba alibaki Sophia na mumewe Ibra sasa ambapo Ibra alihisi kuna kitu mkewe anakijua na kumfanya amkazanie ili amueleze kuwa ilikuwaje,
“Naomba unisamehe mme wangu, nimefanya yote haya ili kuiokoa familia yetu”
“Kuiokoa familia yetu kivipi?”
“Kwanza niahidi kuwa utanisamehe”
“Sasa Sophy nisipokusamehe wewe nitamsamehe nani? Wewe ndio mke wangu, mama wa watoto wangu na hapo ulipo umebeba mwanetu tumboni mwako hivi naanzaje kutokukusamehe kwa mfano”
“Ngoja nikueleze basi ilivyokuwa”
“Wewe nieleze tu hata usiwe na wasiwasi”
Ikabidi Sophia amueleze Ibra mlolongo mzima wa yeye na Siwema kwenda kwa mganga wa kienyeji hadi yeye kupatiwa dawa ya kumdhuru Jane ambapo ndio aliiweka kwenye hiyo juisi.
“Mmmh kama ndio hivyo basi hiyo dawa ni kiboko mke wangu, ila siku nyingine usirudie tafadhali. Kwanza nikuulize una ushahidi gani kuwa Jane ni mchawi?”
“Mume wangu ni kutokana na mambo yanayotokea humu ndani, na mganga kasema kuwa yote yanasababishwa na huyo Jane”
“Najua wewe habari za waganga huzijui vizuri mke wangu ila kwavile umeamua kujihusisha nao basi utazijua mwanzo mwisho, ila siku nyingine usijaribu hiki kitu. Hivi mfano Jane angekufa humu ndani tungempelekaje kwao mke wangu? Tena ushukuru Mungu huyo Jane ana imani zake na Mungu wake maana angekunywa tu hiyo juisi iliyogeuka kuwa damu basi kungekuwa na habari nyingine muda huu. Tafadhali mke wangu kuwa makini sana, Siwema atakupoteza wewe”
Kisha Ibra akaenda kuchukua tambara ili kuweza kufuta pale chini ila alikuta ile damu imeganda kamavile iliwekwa kwenye barafu kwahiyo alifanya kazi ya kuigandua na kwenda kuitupa nje kisha akapasafisha kabisa pale na kutulia huku akimuangalia mkewe ambaye alikuwa kimya tu kwa muda huo. Ibra aliamua kumuuliza tena,
“Je hiyo dawa bado unayo?”
“Hapana, niliitoa yote kama nilivyoelekezwa na Yule mganga”
“Ninachokuomba mke wangu usije ukarudia tena tafadhali, saivi kuwa makini na hiyo mimba. Kwanza vipi kuhusu kuanza kliniki?”
“Nitaanza tu mume wangu hata usijali”
“Basi ukiona imefika kipindi muafaka cha kuanza useme ili niwe nakupeleka”
“Sawa hakuna tatizo”
Wakati wakiendelea kuongea, mara kidogo Tv ikajiwasha kama kawaida na kumfanya Ibra ashtuke na kumuuliza mkewe kwa mshangao,
“Si nilisema hii Tv isiwashwe jamani Sophy na jana nikaizima hadi kwenye soketi imekuwaje tena?”
“Huyo Jane wako unayemtetea ndio aliyeleta tena mauza uza ya hiyo Tv maana hata mimi nilimshangaa akajitetea kuwa imejiwasha”
Ibra akapata hasira na kuinuka kisha akaenda kuchomoa nyaya zote za Tv ili kusiwe na muunganiko wowote kati ya umeme na Tv kisha akamuomba mkewe kuwa waende chumbani.
Sophia akainuka huku akiambatana na mumewe na kuelekea pamoja chumbani, ila walipofika tu cha kwanza kabisa Ibra alimuuliza mkewe
“Eeeh leo tunakula nini”
“Hata sijui maana sijapika”
“Kwahiyo mawazo yako leo ilikuwa ni juu ya kumuangamiza Jane tu hata ukasahau lishe dah! Basi jiandae twende hotelini tukale”
Sophia alijiandaa kisha wakatoka pamoja na mumewe kuelekea hotelini kula.

Walifika hotelini na kuagiza chakula, kisha kilipoletwa walianza kula na kumaliza ambapo Ibra alifurahi kwakweli maana mkewe siku hizi alikuwa na matatizo kiasi kwahiyo alihisi labda atatapika au atakataa kula hapo hotelini, kisha akamuuliza Sophia,
“Vipi leo hujajisikia vibaya mke wangu maana umeweza kula hapa hotelini hadi nimeshangaa”
“Kwasababu tumebadilisha hoteli ndiomana nimeweza kula, lile li hoteli lako silitaki kabisa”
“Ila si nilishasema kuwa ile hoteli hatutaenda tena kutokana na yale wanayotutegeshea njiani, kwakweli hata mimi ile hoteli siitaki tena na kama nilivyoahidi haitokuja kutokea tena niende kwenye ile hoteli”
“Hapo sawa mume wangu maana hoteli nyengine  zimekaa kiushirikina tu”
“Vipi tubebe chakula kingine twende nacho nyumbani?”
“Mmh hapana jamani maana kama mimi hapa nimeshiba balaa, kesho nitapika tu”
“Basi turudi nyumbani sasa”
“Labda tununue juisi maana si unajua hata usiku haujaanza kuingia vizuri”
“Lakini si ulitengeneza juisi wewe mpaka ukampa Jane!”
“Aaah achana na ile juisi bhana, kwanza tukirudi naimwaga yote”
Ibra akacheka tu kisha wakamuita muhudumu na kumuagiza juisi ya boksi na alipoleta walibeba na kuelekea kwenye gari yao kwa lengo la kurudi nyumbani.
Wakiwa njiani ndani ya gari, wakakatisha kwenye moja ya kituo cha daladala ila ghafla wakasikia sauti ikiita kwa nguvu jina la Sophia na moja kwa moja wakahisi kuwa huenda kuna mtu kwenye kituo cha daladala anayemfahamu Sophia kwahiyo Ibra akasimamisha gari yao ili kumuangalia mtu huyo. Ila ghafla mlango wa nyuma wa gari yao ukafunguliwa na akaingia mtu, ambapo kwa pamoja waligeuka na kumuangalia mtu huyo, wakamuona ni Yule mtoto ambaye huwa wanamkuta njiani akiwafanyia vituko cha kwanza walishangaa sana.
Kwakweli Ibra alipatwa na hasira ya ghafla kisha akashuka kwenye gari na kwenda ule mlango wa nyuma na kuufungua ambapo alimtoa mtoto huyo kwa ghadhabu kubwa sana kisha akamrusha nje ila Yule mtoto hakuanguka wala nini kama kwamba Ibra alimuondoa na kwenda kumsimamisha ila bado Ibra hakushangazwa na lile swala bali alirudi kwenye gari na kuondoa gari yao kwenye lile eneo huku akiwa amechukia sana kwani chanzo cha wao kubadilisha hoteli na njia ni huyo huyo mtoto.

Walipofika nyumbani, kabla hata ya kushuka kwenye gari ili afungue geti, wakaona kitu kama nyoka kikimalizikia kuingia ndani kwao kwa kupitia chini ya geti ila waliona mkia tu ambapo Sophia ndio alikuwa wa kwanza kushtuka na kumwambia mumewe,
“Mmh sio nyoka Yule?”
“Hata mimi nimeona kama nyoka vile”
“Duh mbona makubwa!”
Ikabidi washuke wote na kuingia kwa tahadhari ili kama ni nyoka basi wajue cha kufanya kabla ya kuingiza gari ndani, ila walipoingia tu getini waliona nyoka mkubwa akiwa amejiviringisha pembezoni mwa mlango wao wa kuingia ndani kama kwamba anawasubiria kuwa waingie nae.

Mwisho wa sehemu ya 11

Itaendelea ……………………!!!




No comments: