NYUMBA YA MAAJABU 20



               

Neema alikuwa kimya tu hakujibu chochote kile na kumfanya Sophia azidi kumshangaa kwani haikuwa kawaida kabisa kwa Neema kufanya hivyo. Sophia akainuka pale alipokaa na kusogea alipo Neema ili kumshtua kwa kumshika kabisa, ila aliposegea ili amguse ghafla akashangaa kuwa pale hapakuwa na mtu yoyote yani Neema hakuonekana ghafla.
Kwakweli Sophia alipigwa na butwaa kwani muda wote alikuwa akimuona Neema mahali hapo halafu tena ghafla Neema ametoweka, alijikuta akitetemeka tu na kuwa kama mtu asiyejielewa.
*TUENDELEE...*

Akiwa anajitetemekea pale mara akamuona Neema akitoka chumbani na kuja pale sebleni na ndio hapo woga ulipomzidia na kujukuta akishindwa kustahimili na kuanguka chini na kuzimia.
Sophia akiwa amezimia alijiona sehemu ya mbali sana, alijiona mahali akiwa amekaa mwenyewe halafu mbele yake aliwaona watoto watatu wakimuangalia kwa huruma sana na kumfanya na yeye apatwe na huruma kisha akainuka pale alipokuwepo na kuanza kuwafata ila kila alipowasogelea nao walizidi kwenda, kisha akajikuta akisogea na kusogea bila ya kuwafikia na kumfanya sura yake ikiingiwa na simanzi zaidi.
Muda kidogo akajikuta ameshtuka na kujiona yupo sebleni kwenye kiti huku pembeni yake akiwepo Neema ambaye alimpa pole baada ya kushtuka, kisha Sophia akamuuliza Neema kuwa ni kitu gani kilitokea
“Sijui ni kitu gani dada ila ulianguka ghafla tu”
Sophia alijaribu kuvuta kumbukumbu nyuma ili kuweza kukumbuka kilichomtokea ila hakuweza kukumbuka kitu chochote kile, alijikuta akiangaza tu macho yake huku na kule ila Neema alimuomba anyanyuke na aende kula chakula cha mchana ili kupata nguvu kwavile alikuwa hajala chochote toka alivyokula asubuhi.
Sophia akainuka na kwenda moja kwa moja mezani kula chakula alichoandaliwa na Neema na kuanza kula chakula kile.

Ibra alimrudisha Lazaro hadi nyumbani kwake ambapo walipokelewa na mke wa Lazaro kisha Lazaro akamuomba mkewe amfanyie maombi (dua) maana hali yake haikuwa sawa, mke wa Lazaro hakujifikiria mara mbili na moja kwa moja alianza maombi (dua).
Ibra alikuwa kimya kabisa akiwatizama huku yale maombi (dua) yakiendelea mpaka kuna muda ambao Lazaro alidai kuwa anajihisi nafuu sasa na anaweza kuzungumza, kisha akamuangalia rafiki yake na kumwambia,
“Ibra pendelea kufanya maombi (dua) kwenye nyumba yako”
“Maombi gani ambayo napaswa kuyafanya? Maana mimi sijazoea hayo mambo kwakweli”
“Hivi unajua ukubwa wa Mungu Ibra? Nyumba yako imetawaliwa na mambo mabaya, sio kwamba nakuonea wivu hapana ila kuna vitu nimevihisi kwenye nyumba yako”
Ibra akafikiria kidogo na kumuuliza rafiki yake huyu,
“Hivi wakati naongea na Yule Neema mbona ulikuwa hunisikilizi?”
“Mimi sijamuona huyo Neema ndani kwenu na wala sijakusikia kama kuna muda umeongea nae zaidi ya kuning’ang’aniza nimsalimie mtu nisiyemuona”
Mke wa Lazaro alisikia yale maongezi na kutamani kujua zaidi kuhusu huyo mtu ambapo Ibra aliamua kuwaeleza kwa kifupi jinsi walivyokutana na Yule Neema hadi kwenda nae nyumbani kwake, ila mke wa Lazaro nae alimuuliza kama kuna taratibu zozote alizofanya ili kumtambulisha huyo Neema kwa mjumbe na kuwafanya wawe huru nae nyumbani kwao,
“Yani hapo ndio kwenye tatizo, Yule Neema hataki kabisa twende nae kwa mjumbe yani kashatugomea kabisa kasema tungetaka kumpeleka kwa mjumbe basi tungekwenda nae toka mwanzoni”
“Mmh shemeji poleni sana, lakini katika maisha hakuna kitu kibaya kama kuishi na mtu usiyemfahamu maana huwezi jua hi mtu wa aina gani na ndiomana kuna utaratibu ili kitakachokupata chochote au kumpata huyo binti watu watajua ni jinsi gani wanakusaidia. Kusaidia mtu njiani sio tatizo ila tatizo ni kutofata taratibu”
“Basi labda kama mtaweza shemeji mje siku moja nyumbani kwangu na kunisaidia kumshawishi Yule binti niweze kwenda nae kwa mjumbe maana mie amenikatalia kabisa na nimeshindwa hata kufanya hivyo”
Mke wa Lazaro alimkubalia Ibra ila Lazaro aligoma kwenda tena nyumbani kwa Ibra,
“Ndugu yangu tafadhali nisamehe bure tu ila sitaweza kuja tena nyumbani kwako, kama nilivyokwambia tafuta watu wa maombi (dua) kwanza”
“Usijali, mimi nitakwenda, siku ukipata muda shemeji njoo unifate niende huko kwako”
“Sawa mke wangu ila ile nyumba inahitaji uwe na umakini wa hali ya juu”
Wakakubaliana pale kisha Ibra akaaga na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake huku akiwa na mawazo sana kwani hakuelewa kuwa nyumba yake imekumbwa na kitu gani hadi kushauriwa na watu juu ya maombi(dua). Kwanza kabisa alikumbuka maneno ya Jane kisha akakumbuka alichoambiwa na Lazaro pamoja na mke wa Lazaro kwakweli akili yake ilikuwa ikitembea bila ya majibu yoyote yale hadi alipofika nyumbani kwake bado alikuwa na mawazo.

Ibra aliingia ndani na kumkuta Neema akiwa pale sebleni ambapo alimsalimia kisha akamuuliza alipo mke wake,
“Yupo chumbani kalala”
“Mbona kalala mapema sana”
“Labda ni uchovu tu”
“Sawa, ila Neema mbona muda ule wakati yupo mgeni nilipokuwa nikikuuliza kitu ulikaa kimya tu?”
Neema akamuangalia Ibra na kutabasamu hivyo akafanya Ibra azidi kupatwa na maswali mbalimbali kisha akamuuliza tena,
“Mbona unatabasamu?”
“Yule rafiki yako hawezi kurudi tena hapa”
“Kwanini?”
“Sio mtu mzuri Yule na amekuonea wivu sana wewe kumiliki nyumba kama hii kwani hata yeye ametamani ingekuwa yake”
“Kwahiyo ndio ulishindwa kunijibu sababu ananionea wivu?”
“Huwa sipendi kuongea na watu wabaya, nimeshawaambia hili mara nyingi sana mwenzenu siwezi kuzungumza na watu wabaya”
“Sawa, ila kwanini pia hupendi twende kwa mjumbe?”
“Mimi sio kwamba sipendi, nyie mkipata muda tu twendeni sina tatizo juu ya hilo kabisa”
Ibra alishangaa sana leo kujibiwa kirahisi hivi na huyu Neema kwani haikuwa kawaida yake ukizingatia ukizungumzia tu suala la mjumbe alikuwa mkali sana ila leo alionekana kukubali kwa haraka zaidi. Kisha Ibra kaelekea chumbani alipo mkewe na kumkuta kweli amelala na hivyo kumuamsha kwanza, Sophia aliamka kama mtu aliyekuwa amezidiwa sana na usingizi na kumfanya Ibra ampe pole kwa kumuamsha kwa haraka vile.
“Kwani kuna kitu gani mume wangu?”
“Hakuna kitu ila nilikuamsha ili angalau nikusalimie, halafu ndio uendelee kulala”
Sophia hakujibu cha zaidi kwani alijilaza tena pale kitandani na ilionekana usingizi kumchukua kwa muda huo huo. Ibra alitulia akitafakari kisha kuamua kwenda kukoga ambapo alikwenda kukoga kwa haraka sana na kurudi tena chumbani ila akashangaa pale kitandani hakumuona tena mkewe na kumfanya ashtuke kuwa mkewe atakuwa amekwenda wapi kwani alimuacha hapo akiwa amelala fofofo.
Ibra akavaa haraka haraka na kwenda sebleni kumuangalia mabapo alimkuta Neema tu pale sebleni na kumuuliza,
“Dada yako kaenda wapi?”
“Kwani hayupo chumbani?”
“Nilimkuta amelala lakini nimetoka kukoga ghafla simuoni tena”
“Aah acha masikhara bhana kaka, sasa atakuwa ameenda wapi?”
“Sijui kwakweli na ndiomana nimekuja kukuuliza wewe labda umemuona kuwa ametoka”
“Hapana mimi sijamuona, na ninachojua yupo chumbani kwenu amelala”
“Chumbani hayupo nielewe hivyo Neema”
“Je unaniruhusu twende pamoja tuakamuangalie huko chumbani”
“Twende ukaone”
Neema alitabasamu kisha akainuka pale kwenye kiti na kuongozana na Ibra hadi chumbani kwao, walipofika tu pale chumbani Sophia alionekana kitandani na kumfanya Neema amwambie Ibra,
“Si huyo hapo amelala jamani, nikusaidie kumuamsha?”
Ibra akatingisha kichwa kwani tayari woga ulishamjaa moyoni, Neema alisogea kwenye kitanda na kukaa kisha akamgusa Sophia ambaye alishtuka kutoka usingizini na kuamka kabisa huku akimshangaa Neema kuwa ameingiaje kwenye chumba chao.
“Usijali dada, ni kaka kaniruhusu kwa lengo la kukuamsha wewe”
“Sawa hakuna tatizo Neema nimeshaelewa”
Sophia alikaaa pale kitandani kisha Neema akainuka na kutoka ambapo Ibra alisogea alipo mkewe na kumuangalia kwa makini sana ambapo Sophia pia alimuangalia mumewe kwa macho makali huku akimuuliza,
“Kwanini umemruhusu Neema aingie chumbani kwetu? Inamaana wewe hukuweza kuniamsha mwenyewe hadi aje Neema?”
“Unanilaumu bure mke wangu, kwa hali ilivyokuwa sikuweza kuacha kumlaumu aingie humu chumbani”
“Halafu badae unaanza kulalamika ooh hatumfahamu vizuri na umemruhusu mwenyewe kuingia mpaka chumbani”
“Nisamehe kwa hilo mke wangu”
Kisha Sophia akainuka na kuelekea bafuni kwa lengo la kujimwagia maji kwanza ili aweze kupata nguvu.

Sophia akiwa bafuni ghafla alipiga kelele na kurudi chumbani huku akilia na kumfanya Ibra ashangae sana kuwa ni nini kinamsumbua,
“Vipi mke wangu nini tatizo tena?”
“Sielewi, sielewi, sielewi Ibra”
“Huelewi kitu gani tena Sophy jamani, kwani kuna nini au umeona kitu gani?”
“Sijui hata ni kitu gani kwakweli sijui Ibra”
“Khee sasa makubwa haya, yani ukimbie ulie na usielewe unacholilia wala kilichokikimbiza kweli? Ni kitu gani umeona?”
“Nitakwambia tu mume wangu ila naomba unisindikize tu nikanawe vizuri”
Hilo halikuwa tatizo kwa Ibra ila tatizo ni kuwa mke wake amekumbwa na kitu gani huko bafuni ndio kulimkosesha jibu kabisa. Kisha akainuka nae na kuelekea nae bafuni ambako kulionekana kuwa kawaida tu halafu Sophia akajimwagia maji haraka haraka na kutoka nje.
Ibra alikaa huku mkewe akivaa nguo, kisha akaamua kuzungumza nae tena kuwa ni kitu gani kilimtokea bafuni wakati akikoga na kumfanya akimbie na hata kuanza kulia,
“Nimekwambia sielewi Ibra yani sielewi kabisa”
“Sasa huelewi kivipi Sophy yani inawezekana vipi mtu kupatwa na jambo usilolielewa?”
“Sijui ila sielewi”
“Basi ngoja nikuulize hivi, umeona nini huko bafuni?”
Kabla hajajibu wakagongewa mlango na Neema ambaye alikuwa akiwaita ili waweze kula chakula ila leo Sophia alikuwa wa kwanza kusema kuwa anajihisi kushiba sana na kumfanya Ibra nae kusema kuwa ameshiba, hivyo Neema hakuwagongea tena na ukimya nao ukatawala ambapo Ibra alimwambia mkewe kuwa ni bora walale tu kwa muda huo.
“Ila leo nimelala sana Ibra hata sidhani kama nitapata usingizi sasa hivi”
“Pole mke wangu ila inatakiwa ulale maana ni usiku huu si unajua tena mambo ya usiku”
“Naelewa ila sina usingizi mume wangu”
Wakiwa wanabishana kuhusu suala la kulala ghafla umeme ukakatika na kufanya kuwe na giza la haswaa chumbani kwao na kumfanya Sophia amkumbatie kwa nguvu Ibra kwa woga aliokuwa nao kwa muda huo,
“Itabidi tuwashe tochi ya simu sasa”
Ibra akaanza kupapasa ilipo simu yake ila hakufanikiwa kuipata na kushangaa kuwa siku hiyo aliweka wapi simu yake, akajaribu kuinuka huku akiwa ameshikiliwa na Sophia na kuendelea kapapasa sehemu mbalimbali na mwisho wa siku hawakuwa na la kufanya zaidi ya kumuita Neema ambaye alienda na kuwapelekea mshumaa pamoja na kiberiti ili ikitokea umeme umekatika tena wawashe tu.
Walimshukuru sana Neema na muda kidogo umeme nao ukarudi, Ibra alikuwa kashika ule mshumaa na kiberiti kisha Sophia akamuuliza mumewe
“Hivi wakati umeme umekatika hadi tukamuita Neema humu ndani, je alifungua mlango wa chumbani kwetu saa ngapi na ametoka saa ngapi?”
“Kwanini umeuliza hivyo Sophy?”
“Maana sikumbuki kama mlango ulifunguliwa ila ninachokumbuka ni kuwa Neema alileta mshumaa na kiberiti, pia sikumbuki muda aliotoka ila tu nimeona umeme umerejea”
“Hata mimi sikumbuki mke wagu ila nakuona sasa ufahamu umeanza kukurudia”
Kisha Ibra akamuomba mkewe kwa muda huo waweze kulala tu kwani hakuona umuhimu wa wao kuanza kumzungumzia Neema kwa muda huo.

Kulipokucha Sophia alikuwa wa kwanza kuamka kwa safari hii, kisha akamuamsha mumewe na kumwambia kuwa angependa siku hiyo amuandalie chai yeye mwenyewe ili aweze kunywa kabla ya kuondoka,
“Leo umeota nini mke wangu?”
“Nimeamua tu Ibra sababu nakupenda na pia naijali afya yako”
Ibra aliinuka na kwenda kuoga kisha Sophia alitoka chumbani kwao, alipofika sebleni alimuona Neema akiwa amekodolea macho kwenye Tv kisha yeye akenda jikoni ambako alimkuta Neema akikosha vyombo na kufanya Sophia aanze kupiga kelele.

Itaendelea.....…………..!!!





No comments: