Valentine day wakenya wanatumia pesa nyingi zaidi Duniani kufurahisha wapenzi

FAUSTINE NGILA NA CECIL ODONGO
WAKENYA wanaongoza kote duniani kwa kutumia kiasi kikubwa zaidi cha fedha kujionyesha jinsi walivyokolea kimapenzi wakati wa siku ya wapendanao, maarufu kama Valentino, utafiti umeonyesha.

Utafiti huo wa shirika la Mastercard unaeleza kuwa Wakenya hutumia kiasi kikubwa cha fedha kuliko mataifa mengine duniani msimu wa Valentino ambayo inasherehekewa kila Februari 14.
Kulingana na ripoti hiyo, utoaji fedha kwenye akaunti hapa Kenya huongezeka kati ya Februari 11-14 sherehe hizo zinapofika kilele.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watu waliokodisha hoteli iliongezeka 2019 kwa asilimia 65 kutoka 2017.
Hii ni zaidi ya asilimia 22 ya wastani iliyosajiliwa katika mataifa mengine kote duniani wakati wa Valentino.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Wakenya wana mtindo wa kuadhimisha siku hii kwa kukodisha hoteli za kifahari na kuzuru maeneo ya burudani kama njia ya kuonyesha kukolea kwa mapenzi kwa wapendwa wao.
Ripoti hiyo pia inaeleza kwamba mnamo 2019 Wakenya walitumia asilimia 37 zaidi ya fedha zilizotumika 2017 kununua tiketi za ndege huku wapendanao wakitalii maeneo mbalimbali nchini na duniani.

Mada ya mwaka huu ya siku hii ni ‘mioyo miwili inayodunda pamoja’.

Wakati huo huo, wito umetolewa wananchi watoe damu ili kukidhi upungufu unaoshuhudiwa katika hospitali nyingi nchini. Mama Taifa Margaret Kenyatta, leo katika ukumbi wa KICC anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa kampeni ya kuhakikisha Wakenya wanatoa damu katika vituo 31 kote nchini.
Kampeni hiyo yenye mada ‘Inuka toa damu’inalenga kuwafikia vijana ambao ni asilimia 70 ya watu wanaotoa damu.
Shirika la Huduma ya Kitaifa ya Kutoa Damu (KNBTS) ndilo linashirikiana na Wizara ya Afya kuandaa hafla ya leo huku ikibainika taifa linahitaji painti milioni moja za damu ili kutosheleza mahitaji ya wagonjwa. “Tunalenga kuhakikisha Wakenya wanazoea kutoa damu,” ikasema taarifa ya KNBTS.




No comments: