Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 11)


ILIPOISHIA WIKIENDA…
“Wanasheria wake wanaweza kupinga asitolewe damu.”
“Tunawweza kutumia nguvu ya mahakama kumlazimisha atolewe damu kwa ajili ya uchunguzi wetu.”
“Sawa. Unadhani itakuwa vyema akamatwe leo?”
“Kesho asubuhi.”
“Anaweza kupatikana wapi?”
“Nyumbani kwake.”
“Sawa. Asubuhi tunaweza kwenda kumkamata kumhoji na kuangalia uwezekano wa kupima damu yake.”
SASA ENDELEA…
INSPEKTA Mwakuchasa alipokubali kwamba Azzal Mabruki akakamatwe asubuhi nilifurahi. Tulipomaliza mazungumzo yetu nilimuaga na kuondoka.
Mimi na mke wangu tuliondoka kazini muda mmoja. Tuliporudi nyumbani aliniuliza tumefikia wapi katika upelelezi wetu.
“Mpaka sasa tuna watuhumiwa watatu.”
“Si uliniambia mnawashuku watu wawili?”
“Ameongezeka mtu mwingine wa tatu.”
“Ni nani?”
“Azzal Mabruki, si unamkumbuka?”
“Yule aliyewahi kushitakiwa kwa kujihusisha na biashara ya meno ya tembo?”
“Ndiye huyohuyo.”
Mke wangu akacheka mpaka nikachukia.
“Sasa unacheka nini?” Nikamuuliza.
“Nimefurahi tu uliponitajia huyo mtu.”
“Ana nini?”
“Sasa Azzal Mabruki anahusikaje jamani?”
“Wewe huwezi kujua, lakini anaweza kuhusika. Unajua siku ile alipoachiwa na mahakama aliniambia maneno ya kutisha.”
“Alikwambia nini?”
“Aliniambia tutaonana. Maana yake nini?”
“Si alikwambia wewe. Ilimuhusu nini huyo msichana aliyeuawa?”
Hapo nikakumbuka sikupaswa kumueleza mke wangu habari ile. Nilitaka nimueleze kwamba Azzal Mabruki aliniona wakati ninashuka na Matilida kwenye teksi nyumbani kwake. Tulipoingia ndani alikuja kubisha mlango. Matilida akamfungulia wakati mimi nikiwa niko chumbani nimelala. Mabruki akachukua chupa na kumpiga nayo kichwani na kumuua ili nionekane nimemuua mimi.
Nilikuwa nimejisahau kidogo. Kama nisingeshtuka na kumueleza mke wangu maneno hayo, ningekiona cha moto. Ningekuwa nimemdhihirishia kuwa mimi ni malaya na ndiye niliyemuua Matilida. Kusingehitajika tena uchunguzi wa kumtafuta muuaji. Mke wangu angekwenda kuniripoti kuwa mimi ndiye muuaji wa Matilida.
Hapohapo nikageuza maneno.
“Nilisikia Mabruki alikuwa na uhusiano na Matilida na siku alipouawa gari lake lilionekana jirani na pale. Tuna wasiwasi kwamba yeye ndiye aliyemuua.”
“Sasa nani atakuwa muuaji wa kweli. Naona kila siku watuhumiwa wanaongezeka!”
“Si unajua taratibu za kipolisi. Tunakamata watu halafu tunawachuja. Katika hao watu watatu mmojawapo atakuwa muuaji.”
“Na hakuna hata mmoja aliyepatikana hadi sasa!”
“Mabruki tutakwenda kumkamata kesho asubuhi nyumbani kwake.”
“Mimi kwa mawazo yangu sidhani kama mtu kama yule anaweza kujihusisha na jambo la kipuuzi kama lile.”
“Watu kama wale ndiyo wanaofanya mambo ya kipuuzi zaidi.”
“Lakini si kama kumuua msichana bila sababu.”
“Wewe huwezi kujua, uchunguzi ndiyo utabaini kila kitu.”
Wakati ule tunazungumza, simu yangu ikaita. Nilipotazama skrini ya simu nikaona namba ya yule mhudumu wa Baa ya Nane Nane ninayewasiliana naye. Nikaipokea.
“Hujambo?” Nikamsalimia mara tu nilipopokea simu yake.
“Sijambo. Shikamoo.”
“Marahaba. Habari ya kazi?”
“Nzuri. Nilitaka kukufahamisha Mdachi amefika. Sasa ukichelewa ataondoka.”
“Yuko hapo anakunywa?”
“Ndiyo anakunywa!”
“Tunakuja sasa hivi.”
Sikuwahi hata kubadili zile sare zangu za kipolisi. Nikamwambia mke wangu.
“Nimearifiwa yule mtuhumiwa mmoja yuko Baa ya Nane Nane anakunywa pombe, acha twende tukamkamate.”
“Una maana kwamba unatoka tena?”
“Ndiyo ninakwenda hivi.”
Nilikuwa nimeshafika kwenye mlango. Nilisita kidogo nikamtazama mke wangu. Nilidhani angeniambia kitu, lakini alikuwa amenyamaza akinitazama. Nikafungua mlango na kutoka.
Nilirudi kituoni. Inspekta Mwakuchasa alikuwa ameshaondoka. Nikatoa taarifa kwa ofisa aliyekuwa akisimamia kituo, akanipa polisi watatu na gari.
Tukaondoka. Tulipofika tuliegesha gari mbele ya Baa tukashuka. Polisi wawili tuliingia baa, polisi wawili walibaki nje ya baa.
Nilizungusha macho kwenye viti. Kulikuwa na watu kadhaa wakinywa pombe. Macho yangu hayakuweza kumtambua yeyote. Kaunta palikuwa na mhudumu peke yake. Wenzangu wawili walibaki kwenye mlango, mimi nikaenda kaunta.
“Yupo?” Nikamuuliza mhudumu wa kaunta.
“Amekwenda kujisaidia, atatoka sasa hivi. Alikuwa amekaa meza ile pale.”
Alinionesha meza aliyokuwa amekaa Mdachi ambayo haikuwa mbali sana na kaunta. Kulikuwa na chupa mbili za bia zikiwa tupu na bilauri.
“Amevaa shati la rangi gani?”
“Amevaa tisheti ya bluu.”
“Sawa.”
Nilikwenda kukaa kwenye meza ileile.
Wateja walikuwa wametaharuki walipotuona. Pengine kutokana na hofu isiyo na sababu, wateja wawili waliacha kunywa, wakatoka. Wengine waliobaki walikuwa matumatu. Hawakujua kilichokuwa kikiendelea.
Ghafla nikamuona mtu aliyekuwa amevaa tisheti ya bluu akitokea uani. Nilipomtazama tu nikamtambua. Alikuwa Mdachi. Alipoona polisi wawili wamesimama kwenye mlango na mimi nimekaa kwenye meza aliyokuwa amekaa yeye, hakurudi tena kukaa. Akaelekea kwenye mlango wa kutokea. Nikainuka na kumshika bega.
“Uko chini ya ulinzi!” Nikamwambia.
Mdachi alishtuka, akanikazia macho.
“Nimefanya nini?” Akaniuliza.
“Nimekukamata kwa tuhuma za mauaji ya Matilida,” nilimwambia wazi.
Mdachi akashtuka tena na kuanza kupayuka.
“Kwani Matilida nimemuua mimi? Nani amesema kama nimemuua mimi? Sijamuua Matilida!”
Polisi waliokuwa wamesimama kwenye mlango walipoona Mdachi anapayuka, walisogea karibu wakamdhibiti.
“Twende. Wewe umeshaambiwa uko chini ya ulinzi unatakiwa kutii amri ya polisi!” Polisi mmoja alimwambia akiwa amemshika kwenye kiuno.
“Sasa nisiulize ninakamatwa kwa kosa gani?” Mdachi akauliza kwa taharuki.
“Unauliza nini? Kwani mnapofanya uhalifu mnafikiri nini?”
“Uhalifu gani nimefanya?”
“Usitujibishie. Twende!”
Tulimkokota hadi nje ya baa, tukampakia kwenye gari. Tulisahau kuchukua pingu. Tungekuwa nazo tungemtia nazo mikononi. Mtuhumiwa wa mauaji ni mtu hatari.
Tulikwenda naye kituo cha polisi. Tukamuingiza kwenye chumba cha mahojiano.
Kwa vile mimi nilikuwa mmoja wa wapelelezi wa kesi ile ndiye niliyemhoji.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Mdachi Mwinyihatibu.”
“Inaelekea baba yako ni mwinyi na alwatani wa hapa Tanga. Hili Mdachi ni jina lako halisi?”
“Hili nilipewa tu tangu nikiwa mtoto. Jina langu halisi ni Zuberi Mwinyihatibu.”
“Kwenu ni wapi?”
“Kijiji cha Mwarongo.”
“Una umri gani?”
“Miaka arobaini na mitano.”
“Mkazi wa wapi?”
“Chumbageni.”
“Unafanya kazi gani?”
“Biashara.”
“Biashara gani?”
“Ya kununua na kuuza vitu vilivyotumika.”
“Biashara yako unaifanyia wapi?”
“Hapohapo Chumbageni.”
“Hebu kunjua viganja vyako, nataka kuviona.”
Mdachi akakunjua viganja vyake.



No comments: