Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 3)
ILIPOISHIA IJUMAA…
Pembeni mwa kichwa chake kulikuwa na vipande vya chupa ya bia iliyovunjika ambavyo navyo vilikuwa na damu. Nilishuku kwamba chupa hiyo ndiyo iliyokuwa na bia aliyokuwa akiinywa msichana huyo.
“Sasa hili ni balaa!” Nikawaza.
Kutokana na mbinu zetu za kazi ya upolisi, mimi niliyekuwa na msichana huyu ndiye ninakuwa mtuhumiwa namba moja. Lazima nikamatwe na kuwekwa ndani kwa tuhuma za mauaji. Balaa limeshaniangukia mimi wakati msichana mwenyewe hata simjui ni nani!
SASA ENDELEA…
KUSEMA kweli nilijuta kukutana na msichana huyo na kukubali kuingia nyumbani kwake wakati nikiwa simfahamu. Kumbe janga lilikuwa linanisubiri.
Nikajiuliza huyu msichana ameuawa na nani na kwa sababu gani? Nikajiuliza tena polisi wakifika hapa watamkamata nani?
Kama watanikamata mimi na ni lazima wanikamate mimi niliyekutwa kwenye tukio, nitafikiriwa nini? Si nitafikiriwa kwamba mimi ni polisi mlevi na malaya na kwamba nilifika nyumbani kwa msichana huyo kuendeleza umalaya wangu kukatokea kutokuelewana, nikachukua maamuzi ya kumuua!
Dhana hii ya kuwa mimi ni polisi mlevi na malaya haikunipendeza hata kidogo. Ilikuwa dhana iliyokuwa kinyume na ukweli na ingenidhalilisha na kufanya nionekane kuwa nilikuwa kijana nisiye na maana si tu katika jeshi la polisi bali kwa jamii nzima.
Kibaya zaidi ni kuwa upo uwezekano mkubwa wa kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa sababu mimi ndiye niliyekutwa na marehemu. Hivyo basi ili kuepukana na balaa kubwa zaidi, niliona niondoke haraka mahali hapo kabla hakujakucha na kabla ya kufahamika kwamba msichana huyo ameuawa.
Nilirudi tena mle chumbani nilimokuwa. Unaweza kunicheka nikikwambia kwamba nilirudi humo chumbani kwa kunyata kama vile nilitaka hatua zangu zisisikike. Kitasa cha mlango wa chumba hicho nilikifutafuta kwa kitambaa na safari hii nilikishika kwa kitambaa na kufungua mlango. Hakukuwa na kitu chochote cha maana kilichofanya nirudi humo chumbani zaidi ya kukitupia macho hicho chumba.
Niliporidhika kwamba hakukuwa na kitu changu chochote nilichokiacha, nilitoka, nikafunga mlango kwa kutumia kitambaa. Sikukishika kitasa hicho kwa mikono mitupu. Niliogopa alama zangu za vidole zisije zikabaki hapo. Kama zitabaki, hata kama ningeondoka humo ndani, alama hizo zingeweza kuja kunikamatisha.
Nilipofika sebuleni napo niliangaza macho kabla ya kuuruka mwili wa msichana huyo uliokuwa chini usawa wa mlango wa kutokea nje. Nilipotoka nje, bado niliona chembechembe za damu mbele ya mlango.
Nilipotoka nje, nilifunga mlango kisha nikakipangusa kitasa cha mlango kwa kutumia kitambaa. Sikupenda nifute alama zilizokuwa kwenye kitasa hicho kwa sababu alama za muuaji zingeweza kupatikana hapo, lakini niliona kwa vile nilikuwa nimeingia ndani kwa kutumia mlango huo kulikuwa na uwezekano wa kuwepo alama zangu. Ndipo nikaona nikifute hicho kitasa ili nijiondoe kwenye matatizo.
Baada ya hapo, nikasepa. Nilitembea kwa miguu harakaharaka kuelekea mtaa wa pili ambako kulikuwa na kituo cha teksi. Nikakodi teksi iliyonipeleka nyumbani kwangu. Wakati ninafika nyumbani ilikuwa saa kumi na moja na nusu. Ilibaki nusu saa tu kuwa saa kumi na mbili kamili asubuhi ambapo mke wangu angerudi kutoka kazini.
Nyumba yangu ilikuwa katika kambi ya makazi ya polisi iliyokuwa karibu na kituo chetu cha polisi.
Teksi iliponishusha niligundua kuwa sikuwa na pochi ya pesa mfukoni. Iliwezekana pochi niliiangusha nyumbani kwa yule msichana au msichana huyo alinichomolea pochi yangu alipoona nimelala.
Nikafikiria, kurudi tena Kwaminchi kuitafuta pochi yangu, lilikuwa jambo la hatari sana. Ilikuwa ni sawa na kujipeleka mwenyewe kwenye tatizo nililokwisha kulikimbia. Muda ule kulikuwa kumeanza kupambazuka, ningeweza kuonekana na watu nikiingia au nikitoka humo ndani au ninaweza kuja kufumwa na mtu yeyote atakayefika nyumbani kwa msichana yule kwa dharura yoyote ile.
Nikajiuliza nilikuwa nimeweka vitu gani ndani ya pochi ile? Wakati nikijiuliza hivyo nilikuwa nikijipekua kwenye mifuko yangu mingine kutafuta kitambulisho changu ambacho ndicho kilichonitia shaka.
Kitambulisho changu nilikuwa nacho kwenye mfuko wa ndani wa koti langu. Ndani ya pochi yangu mlikuwa na pesa tu ambazo hazikuzidi shilingi laki moja. Kupoteza pesa hizo kwa ajili ya kuokoa maisha yangu sikuona tatizo.
Kwa vile pochi iliyokuwa na pesa zangu sikuwa nayo, nilikosa pesa ya kumlipa dereva teksi.
“Subiri nikuchukulie pesa,” nikamwambia dereva wa teksi huku nikielekea kwenye mlango wa nyumba yangu.
Nilitoa funguo nikafungua mlango na kuingia ndani. Niliingia chumbani nikafungua kabati na kuchukua shilingi elfu hamsini na kuzitia mfukoni mwangu.
Nilitoka tena nikamlipa dereva teksi pesa aliyoitaka kisha nikarudi ndani. Kitu cha kwanza nilikwenda kupiga mswaki kuondoa harufu ya kilevi kinywani mwangu kisha nikaoga maji baridi.
Baada ya kuoga nikaingia chumbani kwangu na kujitupa kitandani. Lengo langu halikuwa kulala, lilikuwa ni kujituliza na kuwaza kuhusu lile tukio lililotokea.
Nikajiuliza ni nani aliyemuua yule msichana na alitokea wakati gani? Wazo la kwanza kunijia ni la wezi. Nilishuku kwamba wakati nikiwa nimelala kuna wezi walivunja mlango na kuingia ndani ambapo walimuua yule msichana ili waibe.
Wazo hilo la wezi lilikataliwa akilini mwangu. Nilijiambia kama ni wezi mbona hakukuwa na kitu chochote kilichoibwa na wala mlango haukuwa umevunjwa? Nikaona hawakuwa wezi.
Nikawaza tena huenda aliyemuua msichana yule ni mwanaume wake aliyemfungulia mlango na kugombana naye kutokana na kuingiza mwanaume mwingine mle ndani. Wazo hilo ndilo nililoliona lilikuwa sahihi.
Nikafahamu kuwa kama ni kuripotiwa, tukio hilo lingeripotiwa katika kituo chetu na iliwezekana kwamba hata mimi ningehusika katika uchunguzi huo.
Ingawa usingizi ulikuwa umeniruka, sikutaka nilale kwa sababu saa moja asubuhi nilitakiwa niwe kituoni.
Saa kumi na mbili na robo mke wangu akawasili nyumbani. Sare yake ilikuwa imechafuka.
“Habari ya asubuhi?” Nikamsalimia.
“Nzuri. Umeamkaje?”
“Nimeamka salama.”
“Ulikwenda kwenye part?”
“Nilikwenda, lakini sikukaa sana nikarudi nyumbani.” Nikamdanganya.
“Part yenyewe ilikuwaje?”
“Ilikuwa nzuri ila niliona niondoke mapema niweze kulala kidogo kwa sababu asubuhi ninatakiwa kazini.”
“Bia zilikuwepo za kutosha?”
“Zilikuwa za kumwaga.”
“Mmh…ulikunywa mpaka..!”
“Sikunywa sana. Nilikunywa chupa mbili tu.”
“Mmh…usinidanganye…”
“Nakwambia ukweli, nilikunywa chupa mbili tu nikaondoka…”
Ili kubadili yale mazungumzo nikamuuliza.
“Mbona umechafuka?”
“Nilipangwa kwenye doria ya usiku. Si unajua kufukuzana na wezi na wavuta bangi, sehemu nyingine ni za mashimo. Inabidi uchafuke.”
“Kumbe ulipangwa kwenye doria?”
“Tumezunguka na gari usiku kucha. Saa kumi na mbili ndiyo tumerudi kituoni. Nimechoka. Hapa nataka kulala tu.”
“Njoo ulale. Mimi natoka, nakwenda kazini.”
“Mpaka nioge kwanza. Si umeona nilivyochafuka. Kuna vibaka tuliwafufukuza usiku nikamshika mmoja. Sasa akawa ananiminya ili nimuachie akaniangusha chini na yeye akaanguka kwa sababu nilikuwa nimemshika…”
“Hao vibaka walikuwa wanafanya nini?”
“Tuliwakuta wamekaa kikundi tukahisi walikuwa wanavuta bangi au wanapanga njama za kwenda kuvunja nyumba za watu. Wale walikuwa wezi. Mahali walipokuwa tulikuta bisibisi mbili na koleo.”
“Hizo bisibisi na koleo zilikuwa za kuvunja kufuli.”
“Tumewakamata watatu, wengine waliingia kwenye vichochoro na kutupotea.”
Wakati tunazungumza tulikuwa chumbani. Nilikuwa nimekaa kitandani, nikainuka.
“Saa ngapi?” Nikamuuliza.
Mke wangu akaitazama saa yake mkononi.
“Saa moja kasoro robo,” akaniambia.
“Ngoja nivae nitoke.”
Nikavaa sare zangu za polisi nikimuacha Miriam akivua sare zake na kuvaa khanga. Alichukua sare hizo na kutoka nazo chumbani.
Baada ya kuvaa sare zangu, nilivaa kofia, nikachukua kifimbo changu cha umeja na kukishika mkononi kisha nikatoka chumbani. Nilikwenda uani mwa nyumba yetu nikamuaga mke wangu na kuondoka.
Mahali ilipokuwa kambi yetu na kilipokuwa kituo cha polisi, ulikuwa ni mwendo mfupi sana. Dakika chache tu baadaye nikawa kituoni hapo. Filimbi ya paredi ilipopigwa polisi wote tulijipanga msitari na kufanya paredi kabla ya kufanyika ukaguzi wa usafi na ndevu. Ndevu katika jeshi la polisi haziruhusiwi. Kinachoruhusiwa ni sharubu.
No comments: