Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 6)
ILIPOISHIA WIKIENDA…
“Alikuja, lakini Matilida hakuwepo. Akatuuliza sisi tukamwambia Matilida anaumwa. Sasa hatuji kama alimfuata nyumbani kwake.”
Kwa vile picha ya mtu tuliyekuwa tunamtuhumu ukiacha ile ya Charles niliingiza kwenye simu yangu, nilifungua simu na kumuonesha ile picha.
“Ni huyu hapa?” Nikamuuliza.
“Ndiye yeye Mdachi!”
Nikaona sasa kazi imekuwa nyepesi.
“Tuseme alipoondoka hapa alikwenda nyumbani kwake akagombana naye na kumuua?”
SASA ENDELEA…
NILIKUWA nikisema peke yangu, lakini yule mhudumu alinisikia. Akabetua mabega na kunijibu.
“Hatujui, hatukuwepo.”
“Inawezekana kuwa ni hivyo. Uchunguzi wetu umeonesha mauaji yake yametokana na wivu wa kimapenzi. Sasa kama alimfuma na mwanaume mwingine, tutajua hapo baadaye, lakini muhimu kwa sasa ni kumtafuta huyo Mdachi, atakuwa mtuhumiwa wetu namba moja. Wewe ndiye utakayetusaidia kumpata.”
“Mimi sifahamu anapoishi.”
“Tafadhali jaribu kutupa ushirikiano. Itakuwaje usifahamu anaishi wapi wakati ni mwanaume wa rafiki yako?”
“Mimi nimemfahamu kwa kumuona hapahapa baa, hata Matilida alijuana naye hapahapa baa.”
“Hebu nieleze tabia yake ikoje?”
“Ni mtu mwenye wivu mwingi na pia ana hasira za harakaharaka.”
“Unaamini kwamba anaweza kuwa muuaji?”
“Hapo ndiyo sina uhakika napo.”
“Lakini ulishawahi kuwaona wakigombana?”
“Walishawahi kugombana.”
“Hapahapa baa?”
“Ndiyo, hapahapa baa.”
“Sasa unadhani tutampata wapi huyu Mdachi?”
“Anakuja kunywa hapa kila siku. Muda wake ni saa mbili au tatu usiku. Anakaa hapa hadi saa sita tunapofunga baa anaondoka na Matilida.”
“Sasa sikiliza, nitakupa namba yangu. Ukimuona tu amefika hapa nipigie simu unifahamishe, lakini usimueleze chochote. Jifanye kama hujui kama Matilida ameuawa.”
“Sawa.”
Nikampa msichana huyo namba yangu ya simu, akaiandika kwenye simu yake.
“Sasa ufanye hivyo. Ukimuona tu nipigie bila kumshtua. Tutafika mara moja kumkamata. Sawa?”
“Sawa.”
Nikamuaga msichana huyo na kuondoka. Maelezo ya msichana huyo yalinipa matumaini makubwa. Niliendesha gari nikiwa nimejaa faraja ya kufanikiwa kwa uchunguzi wangu katika dakika za mapema.
Uwezekano wa Mdachi kumuua yule msichana ndiyo uliokuwa katika akili yangu.
Wakati nipo kwenye Barabara ya Chumbageni huku mawazo yangu yakiwa kwa Mdachi, niliipita pikipiki moja. Aliyepanda pikipiki hiyo alikuwa mtu aliyefanana sana na huyo mtu niliyeambiwa anaitwa Mdachi. Niligundua hivyo kutokana na kuitazama mara kwa mara picha yake iliyokuwa kwenye simu yangu.
Ilibidi nisimamishe gari pembeni mwa barabara ili niweze kumuona vizuri. Pikipiki ikanipita tena, lakini sura ya mtu huyo aliyekuwa akiiendsha ilikuwa ni ileile ya Mdachi. Mawazo yangu yakaona yule alikuwa Mdachi. Nikimuacha huenda hatutampata tena na nitajuta kwa nini nilipomuona sikumkamata.
Nikaanza kumfukuza. Sikuweza kufahamu ni kitu gani kilichomshtua, mtu huyo, naye akaongeza mwendo kama aliyekuwa akinikimbia mimi.
Tukaanza kufukuzana kwenye Barabara ya Chumbageni, tukaingia Barabara ya Kisosora. Pikipiki mbele, gari la polisi nyuma.
Tulivuka daraja la Mtofu, sasa tukawa tunaelekea eneo la Amboni. Nikaona mtu huyo atanifikisha mbali, nikambana njia huku nikimuonesha ishara ya kumsimamisha. Kwa vile ilikuwa pikipiki iliweza kuchomoka kwa pembeni mwa barabara ikaendelea na safari. Kama ningembana zaidi, kutokana na kasi yake kingekuwa ni kifo.
Huko mbele kulikuwa na gari linakuja na ndilo lililomchanganya. Alikwenda kujiingiza mwenyewe mbele ya gari hilo, akarushwa juu kisha akatua kwenye boneti ya gari hilo.
Nusura ilikuja kwa sababu gari hilo lilikuwa tayari limesimama. Mtu huyo akasalimika.
Nilisimamisha gari pembeni mwa barabara kisha nikashuka haraka kwenye gari. Nilimfuata mtu huyo na kumuuliza.
“Ulikuwa unakimbia nini?”
Mtu huyo alikuwa akihema tu, hakunijibu chochote.
“Shuka kwenye boneti ya gari,” nikamwambia.
Alishuka kutoka kwenye boneti, akasimama mbele yangu. Nilimtazama vizuri.
Kusema kweli sasa niligundua tofauti kati ya Mdachi niliyemuona kwenye picha na huyu.
Nikataka kumuuliza jina lake, lakini niliona angeweza kunidanganya. Nikamwambia.
“Nipe leseni yako.”
Akatia mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa pochi yake ambayo aliifungua na kunitolea leseni yake.
Nilisoma jina lake kwenye leseni. Leseni iliandikwa jina la Ibrahim Shukuru.
“Wewe unaitwa Ibrahim Shukuru?” Nikamuuliza.
“Ndiyo.”
“Unamfahamu mtu anayeitwa Mdachi?” Nikamuuliza.
Akatikisa kichwa.
“Simfahamu.”
“Huna undugu naye?”
“Sina undugu naye,” akanijibu.
“Sasa niambie ulikuwa unakimbia nini hadi ukasababisha ajali?”
“Sikuwa nikikukimbia wewe. Nilikuwa na haraka zangu mwenyewe.”
“Haiwezekani. Nilihisi wazi kuwa ulikuwa unanikimbia mimi. Umebeba nini kwenye pikipiki yako?”
“Ni mbogamboga tu.”
Pikipiki ilikuwa imelala miguuni kwangu. Nikainama na kukifungua kifurushi kilichofungwa nyuma ya siti.
Baada ya kikufungua nikakuta mirungi iliyokuwa imefungwa kwenye majani ya mgomba.
Kwa vile niligundua hakuwa Mdachi nikaona kilichomkimbiza baada ya kuona gari la polisi, ilikuwa ni ile mirungi aliyokuwa amebeba.
Niliinusa kisha nikamuuliza.
“Nini hii?”
“Mirungi,” akaniambia.
“Ndiyo iliyokufanya unikimbie?”
Akanyamaza kimya.
Nikaona gari la polisi lililokuwa likitokea upande wa Amboni likisimama hapohapo.
Sajenti mmoja alishuka na kuniuliza.
“Vipi afande?”
“Huyu jamaa alikuwa ananikimbia akaja kugongana na gari. Kumbe alikuwa ananikimbia kwa sababu ya hii mirungi.”
“Alikuwa na hii pikipiki?”
“Ndiyo alikuwa akikimbia kwa kutumia pikipiki hii.”
“Hao ndiyo zao. Tunaweka doria, lakini siku hizi wanatumia pikipiki ili waweze kupita njia za panya kutukwepa.”
“Sasa mtashughulika naye. Mirungi yake hii hapa.”
Nilimpa ile mirungi nikarudi kwenye gari na kuondoka. Wakati mwingine matukio ya aina hii hutokea katika kazi zetu. Kumkamata mtu au kumfukuza mtu na hatimaye kugundua siye aliyekuwa anatafutwa.
Watu wengine huwakimbia polisi wakiwa na sababu nyingine na wengine wakiwa hawana sababu yeyote. Wanakuwa na uoga tu wa kipumbavu.
Nikarudi kituoni kwangu.
Niliingia ofisini kwa bosi wangu Inspekta Mwakuchasa na kumuelea kuhusu upelelezi nilioufanya ulioniwezesha kugundua kuwa yule mtu tunayemtafuta anaitwa Mdachi.
Mbali na kumueleza kuhusu mtu yule niliyemfukuza na kugundua kuwa hakuwa Mdachi, nilimueleza maelezo niliyoyapata ambayo yalionesha kuwa Mdachi ndiye aliyemuua Matilida.
“Umefanya kazi nzuri sana. Hata kama huyo mtu hatujampata, lakini ile kugundua kuwa anafahamika na watu, ni matokeo mazuri. Ninaamini kuwa tutamkamata,” Mwakuchasa akaniambia na kuongeza;
“Unajua nini kimetokea. Mimi nahisi kwamba huyo Mdachi alipokwenda hapo baa jana usiku na kumkosa mpenzi wake huyo alimfuata nyumbani kwake na akamkuta anakunywa pombe na mtu mwingine. Kwa kuwa ni mtu mwenye hasira za harakaharaka kama ulivyosema waligombana na matokeo yake aliamua kumpiga chupa ya kichwa na kumuua kisha akakimbia.”
“Hivyo ndivyo ninavyofikiri mimi, lakini yule msichana nimemuachia namba yangu ya simu, akitokea tu pale baa atanipigia na kunifahamisha.”
“Umefanya kitu kizuri kumpa namba yako.”
Wakati ninazungumza na Inspekta Mwakuchasa, akaingia Sajin Meja mwenzangu, Sajin Meja Mwinchumu ambaye alikuwa mtaalam wa alama za vidole.
Itaendelea…
No comments: