Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 7)



ILIPOISHIA IJUMAA…
“Umefanya kazi nzuri sana. Hata kama huyo mtu hatujampata, lakini ile kugundua kuwa anafahamika na watu, ni matokeo mazuri. Ninaamini kuwa tutamkamata,” Mwakuchasa akaniambia na kuongeza;
“Unajua nini kimetokea? Mimi nahisi huyo Mdachi alipokwenda hapo baa jana usiku na kumkosa mpenzi wake huyo alimfuata nyumbani kwake na akamkuta anakunywa pombe na mtu mwingine. Kwa kuwa ni mtu mwenye hasira za harakaharaka kama ulivyosema waligombana na matokeo yake aliamua kumpiga chupa ya kichwa na kumuua kisha akakimbia.”
“Hivyo ndivyo ninavyofikiri mimi, lakini yule msichana nimemuachia namba yangu ya simu, akitokea tu pale baa atanipigia na kunifahamisha.”
“Umefanya kitu kizuri kumpa namba yako.”
Wakati nazungumza na Inspekta Mwakuchasa akaingia Sajin Meja mwenzangu, Sajin Meja Mwinchumu ambaye alikuwa mtaalam wa alama za vidole.
SASA ENDELEA…
AFANDE kuna jambo limetushtua na kutushangaza,” akamwambia Inspekta Mwakuchasa.
“Jambo gani?”
“Katika chupa ya bia ambayo haikuvunjwa tulikuta alama za vidole vya Afande Denis Wiliam Makita!”
Kama unalikumbuka jina langu, Denis Wiliam Makita nilikuwa ni mimi. Chupa ile niliishika usiku halafu nikasahau kufuta alama zangu za vidole.
Nikajiambia mbio za sakafuni huishia ukingoni. Na ukingoni kwangu ndiyo hapa!
Pengine utashangaa na kujiuliza jinsi mtaalam huyo wa alama za vidole alivyozijua alama zangu wakati hakuniita kuchukua alama zangu na kuzilinganisha na hizo aliozikuta kwenye chupa.
Unapoajiriwa katika jeshi la polisi alama zako za vidole zinachukuliwa na kuwekwa katika maktaba yetu ya alama za vidole. Siku hizi kuna mitandao ya komputa ambapo alama zote huwekwa humo kuanzia alama za wahalifu wanaokamatwa, watumishi muhimu katika Serikali na wengineo. Ukiweka tu alama za vidole, jibu linakuja ni alama ya nani.
Hivyo ndivyo alama zangu zilivyotambulika. Kama alama zangu za vidole zisingekuwepo katika maktaba yetu, pengine ingemuia vigumu mtaalam huyo kujua kuwa alama hizo zilikuwa ni zangu.
Sasa nikajiuliza nitatumia uongo gani nijiokoe. Kama unavyojua binadamu hakubali kufa kirahisi. Lakini kabla sijawaza chochote nilimuona Inspekta Mwakuchasa akinitazama kwa taharuki.
“Imekuwaje? Mbona ni alama zako wewe zilizokutwa kwenye ile chupa?” Akaniuliza akiwa amenikazia macho.
“Wakati ule wa uchunguzi nafikiri niliishika ile chupa,” nikamjibu ingawa nilitambua jibu hilo lisingetosheleza.
Mwakuchasa akatikisa kichwa kusikitika.
“Unasemaje? Uliishika ile chupa kabla ya kupigwa picha?”
“Wakati ule hata hayo mawazo ya kuchukua alama za vidole hatukuwa nayo.”
Mwakuchasa aliendelea kutikisa kichwa.
“Lakini si unatambua kanuni zetu kwamba vielelezo kama vile ni lazima vipigwe picha za kutambua alama za vidole?”
“Unajua afande ile chupa ilikuwa mbali na mahali alipouawa marehemu. Sikufikiria kama ingehusika.”
“Sasa unatuchanganya. Maelezo yako hayaridhishi. Ni lazima ujieleze kwa maandishi ni kwa nini alama zako za vidole zimekutwa katika chupa ile. Vinginevyo unaweza kuwa mtuhumiwa namba moja.”
“Nitajieleza kwa maandishi afande. Ilikuwa kama bahati mbaya tu.”
“Bahati mbaya si sababu ya kueleza. Tueleze kitu cha msingi kitakachotufanya tusikutuhumu wewe.”
“Sawa. Nitaandika maelezo yangu.”
“Sawa. Sasa uwende hospitalini Sajin Meja mwenzako mkachukue alama za vidole za marehemu.”
“Sawa afande.”
Nikainuka kwenye kiti na kumpigia saluti mkuu wangu. Sajin Meja Mwinchumu naye akapiga saluti yake kisha tukatoka.
Wakati tuko kwenye gari tukielekea Hospitali ya Bombo nilijikuta nikimwambia Mwinchumu.
“Unajua nilifanya kitendo cha kizembe sana kuishika ile chupa kabla ya kupigwa picha.”
“Ni kweli, unajua tulishangaa sana tulipogundua ilikuwa na alama zako. Sikufikiria kabisa kwamba uliishika kwa uzembe wala kwa bahati mbaya.”
“Kwanza mimi sikuona kama chupa ile ilikuwa na umuhimu wa kupigwa picha. Umuhimu ulikuja baadaye tulipogundua kuwa marehemu alikuwa anakunywa bia na mpenzi wake.”
“Sasa ajabu ni kwamba tulikuta alama zako peke yake. Hakukuwa na alama zingine. Kama ingeshikwa na watu wawili alama zenu nyote zingeonekana.”
“Labda wakati wa kuishika nilizifuta.”
“Labda, lakini si kawaida.”
Nikanyamaza kimya na kuhisi kuwa mawazo ya wenzangu yalikuwa yameshaanza kubadilika.
Tulipofika hospitalini tuliingia mochwari ulikowekwa mwili wa yule msichana. Sajin Meja Mwinchumu akachukua alama zake za vidole kisha tukaondoka.
“Unajua Denis kutokana na kukua kwa teknolojia, unatakiwa uwe mwangalifu sana. Mara moja unaweza kujisababishia matatizo usiyoyatarajia.”
“Ni kweli,” nikamwambia.
“Mimi bado niko kwenye tukio la alama zako za vidole kukutwa kwenye ile chupa.”
“Nilishakuelewa. Ninajua nilifanya kosa.”
“Unaona afande hakuelewi. Anakwambia lazima uandike maelezo kwa nini alama zako za vidole zikutwe kwenye ile chupa.”
“Anajaribu tu kunifanyia nongwa, lakini bahati mbaya pia ipo ingawa yeye anaikataa.”
“Unajua ni kwa nini anakataa? Ni kwa sababu ya cheo chako. Kufanya kitu halafu unasema umekifanya kwa bahati mbaya, hawezi kukuelewa. Angalau angekuwa polisi mdogo asiye na uzoevu….”
“Kwa vyovyote vile ninafahamu kuwa nitashutumiwa. Na mimi kwa vile nimefanya kosa lazima nikubali shutuma.”
“Si kwangu mimi. Mimi sina tatizo.”
Mwinchumu aliponiambia hivyo tukanyamaza kimya, lakini nilifahamu kitendo changu hakikuwafurahisha wenzangu.
Jioni nilipotoka kazini nilimueleza mke wangu mkasa uliotokea na jinsi alama zangu zilivyokutwa kwenye chupa ambayo tuliichukua katika tukio kwa ajili ya uchunguzi.
“Kwani wewe ulikuwa hujui kwamba huruhusiwi kugusa kitu ambacho kinatakiwa kuchukuliwa alama za vidole?” Mke wangu akaniuliza.
“Ilitokea kama bahati mbaya tu.”
“Ukisema bahati mbaya wenzako watakufikiria vingine.”
“Vingine vipi?”
“Hicho ni kitendo cha kizembe.”
“Mama yangu! Mke wangu pia unaniambia hivyo?”
“Usinielewe vibaya, lakini hivyo ndivyo walivyochukulia ingawa hawakukwambia wazi, lakini mimi ninakuambia.”
Nikanyamaza kimya. Na mke wangu naye akanyamaza. Pengine alikuwa anajiuliza kama alikuwa sahihi kuniita mzembe.
Kwa vile marehemu nilikuwa naye mimi sikuona sababu ya kukasirika. Nikatuliza moyo wangu.
“Hivi sasa tunamtafuta huyo Mdachi. Tukimpata tutakuwa tumefanikiwa kumpata muuaji.”
“Mpaka iwe ni yeye kweli. Alama za vidole ziwe za mtu mwingine halafu muuaji awe mtu mwingine?”
Swali la mke wangu lilikuwa la msingi sana.
“Mazingira yanaonesha ni yeye.”
“Kwa ushahidi gani mlioupata?”
“Yule mhudumu wa baa anakofanya kazi marehemu aliniambia marehemu hakufika kazini usiku wa jana. Huyo Mdachi alipofika alimuulizia, akaambiwa Matilida hakufika kazini. Alipomalia kunywa alimfuata nyumbani. Iliwezekana alimkuta na mwanaume ndipo alipompiga chupa na kumuua.”
“Hayo sasa unayapanga wewe. Nani alikwambia huyo Mdachi alimfuata huyo msichana nyumbani kwake? Nani alikwambia kama alimkuta na mwanaume? Na nani kakwambia kwamba yeye ndiye aliyempiga chupa na kumuua?”
Mke wangu alizidi kunikoroga.
“Uchunguzi wetu ndiyo umeonesha hivyo,” nikamwambia.
“Una maana kwamba unahusisha mambo yasiyo na ushahidi.”
“Ushahidi utapatikana. Tunamtafuta muuaji huku tukiwa kwenye uchunguzi.”
“Sasa kwa nini afande Mwakuchasa anataka ujieleze kwa maandishi? Ina maana hakuamini au….?”
“Yeye ni mkubwa. Kwa hiyo anataka kuonesha ukubwa wake. Kama hili suala angeliacha isingekuwa chochote.”
“Kwani kuna tatizo gani. Si unaandika tu maelezo yawekwe kwenye faili basi.”
“Nitaandika maelezo. Hilo halina tatizo.”
Ilipofika saa tatu usiku msichana mhudumu wa Baa ya Nane Nane alinipigia simu. Nilikuwa nimekaa sebuleni na mke wangu tukinywa bia mojamoja. Nikapokea simu yake.
“Hello, naongea na Afande Denis?”
“Ndiyo. Bila shaka wewe ni mhudumu wa Baa ya Nane Nane?”
“Ndiyo. Yule mtu wako ameshafika.”
Nikagutuka.
“Amefika, yuko hapo?”
“Amefika na ameagiza bia.”
“Hajakuuliza wala kukwambia chochote?”
“Amefikia kwenye meza, hajafika hapa kaunta.”
“Sawa. Usimwambie chochote. Sisi tunakuja.”
Nikakata simu na kusimama.
“Yule mtu tunayemtafuta ameshafika pale baa. Acha twende tukamkamate.” Nikamwambia mke wangu.



No comments: