Kifo Mikononi Mwangu (Sehemu ya 9)
“NIMEKUWA na shaka naye sana. Katika pitapita zangu nilipata habari kwamba huyu Mabruki alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Matilida. Nilisikia siku aliyouawa Matilida, Mabruki alikuwa ameegesha gari lake nyumbani kwa akina Salma, huyu msichana niliyekuja kumuonesha picha.”
Nikaendelea kumwambia.
“Sasa wasiwasi wangu isijekuwa kulikuwa na mambo ya kufumaniana kati ya Mdachi na Mabruki na kusababisha Mabruki amuue yule msichana….”
ILIPOISHIA IJUMAA…
Sikukumbuka kwamba usiku ule niliporudi na Matilida niliona gari hilo kwenye ile nyumba.
Lakini kama lilikuwepo, basi ni Azzali Mabruki aliyemuua Matilida. Alituona wakati tunashuka kwenye teksi na akatambua kuwa nilikuwa ni mimi. Baadaye akaja kubisha mlango. Matilida alipomfungulia, akampiga chupa ya kichwa na kuondoka.
Hili suala nisingeweza kulichunguza peke yangu. Ilinipasa nitengeze hoja ya kulifikisha kituoni ili Mabruki akamatwe.
SASA ENDELEA…
BADALA ya kurudi kituoni nilikwenda Gofu kwenye Baa ya Nane Nane, nikamuona yule msichana ninayemkuta kaunta.
Alikuwa kwenye sehemu yake ya kazi akihudumia wateja. Nikamsubiri pembeni mwa kaunta.
Alipomaliza kuhudumia aliokuwa akiwahudumia alinifuata.
“Shikamoo.” Akaniamkia.
“Marahaba. Hujambo?”
“Sijambo. Mambo vipi?”
“Mambo ni poa tu.”
“Umetutembelea leo?”
“Nimekuja kukuuliza, vipi yule mtu hajafika tena hapa?”
“Hajafika. Angefika ningekupigia.”
Nilinyamaza kidogo kwa fadhaa kabla ya kumuuliza;
“Unahisi ni kwa nini ameacha kawaida yake ya kuja hapa?”
“Sijui mwenyewe.”
“Siyo kwa sababu ameona ameua?”
“Sijui.”
“Sisi tunadhani ni kwa sababu ameona ameua na anatafutwa na polisi.”
“Labda.”
“Mtu anayekimbia polisi aghalabu anahisi ana hatia.”
Msichana alinyamaza kimya.
“Sijui huyu mtu tutampata wapi?”
“Tatizo ni kwamba sisi sote hapa hatufahamu anakoishi.”
“Mlishaulizana?”
“Tuliulizana, lakini hakuna aliyefahamu anaishi wapi.”
“Mimi naamini iko siku atafika. Hawezi kupotea moja kwa moja. Atakapoona watu wamesahau atafika tu. Sisi tutaendelea kumtafuta hata kwa mwaka mzima.”
“Nitakapomuona siku yeyote nitakupigia.”
“Ole wake nitakapomtia mikononi kwa maana amenisumbua sana.”
Nilitamani ninywe bia moja, lakini nikakumbuka nilikuwa kazini. Inspekta Mwakuchasa akinisikia ninanuka pombe nitakuwa nimejipalia makaa ya moto.
Nikamuaga yule msichana na kurudi kwenye gari, nikaondoka.
Nilirudi kituoni nikamfahamisha Mwakuchasa kuwa nimesharudi kisha nikaenda ofisini kwangu. Wakati nimekaa nikitafakari, nikawaza kwamba muuaji lazima awe ni mtu mmoja. Na kama ni watu wawili, mmoja atakuwa ametumiwa. Lakini kwenye meza yangu kulikuwa na watuhumiwa zaidi ya mmoja. Kulikuwa na Mdachi na mwenzake na sasa nimemtumbukiza Azzal Mabruki.
Unaweza kuhisi ni suala la kujichanganya, lakini siyo hivyo. Siku zote polisi hukamata watuhumiwa wengi ingawa anayetakiwa ni mmoja tu.
Watuhumiwa hao wakishakamatwa inakuwa ni rahisi kuwachuja na kujua ni yupi mhusika halisi. Hata hivyo, katika suala la kuuawa Matilida, nilikuwa ninamtuhumu Azzal Mabruki kwa asilimia nyingi kuliko nilivyomtuhumu Mdachi.
Kwa upande wa Mdachi nilimtuhumu kumuua Matilida kutokana na wivu wa mapenzi. Imani yetu ni kwamba Mdachi alipoingia nyumbani kwa Matilida na kumkuta akinywa pombe na mtu mwingine au alipokuta mtu amelala chumbani kwake, alikasirika na kuamua kumpiga chupa Matilida na kukimbia.
Tuhuma hizi zina ushahidi wa kukisia kuliko uhalisia. Lakini Azzal Mabruki huenda alikuwepo wakati ninawasili na Matilida nyumbani kwake. Kwa vile alikuwa na kisasi na mimi, akaona atumie nafasi hiyo kumuua Matilida ili kunikomoa mimi. Hapa utaona tuhuma dhidi ya Azzal Mabruki zina mashiko zaidi ya Mdachi.
Baada ya saa moja hivi alikuja polisi akaniambia ninaitwa na Inspekta Mwakuchasa. Nilipofika ofisini kwake aliniambia.
“Kaa kitini.”
Nikakaa kwenye kiti. Mezani kwake kulikuwa na bahasha ya kaki na karatasi nyeupe yenye maandishi ya yaliyopigwa chapa.
“Matokeo ya sampuli ya damu iliyokuwa kwenye vipande vya chupa na ile michirizi iliyopatikana barazani nyumbani kwa Matilida imewasilishwa sasa hivi kutoka kwa mkemia mkuu,” Mwakuchasa aliniambia huku akiishika ile karatasi iliyokuwa juu ya meza.
Akaendelea kuniambia.
“Damu iliyokutwa katika vipande vya chupa ni tofauti na damu iliyokutwa kwenye ile michirizi iliyokutwa barazani upande wa nje.”
Mwakuchasa alisita akanitazama kuonesha mshangao.
“Sisi tulihisi hii damu yote ni ya marehemu,” akasema.
“Kwani ni damu ya nani?”
“Damu iliyokutwa kwenye vipande vya chupa ilikuwa ya marehemu, lakini ile iliyokuwa kwenye michirizi ni damu ya mtu asiyejulikana!”
“Ni aina ya damu tofauti au ni ya watu wawili tofauti?”
“Makundi ya damu yenyewe ni tafauti. Damu ya marehemu ni kundi A na damu iliyokuwa kwenye michirizi ni kundi O.”
“Unadhani ilikuwaje?”
“Hapa tayari umeshaingia utata…”
Nikawaza kidogo kisha nikamwambia.
“Unaweza usiwe utata afande. Hii damu iliyokutwa nje itakuwa ni ya yule mtu aliyempiga chupa marehemu. Huenda alikatwa kiganjani na vipande vya chupa baada ya kumpiga Matilida. Sasa wakati ule anakimbia damu ikawa inamtiririka.”
“Ni pointi nzuri uliyotoa. Inawezekana ilikuwa hivyo. Kwa hiyo mtuhumiwa ni lazima awe na mambo mawili. Kwanza damu yake iwe kundi O kama hili na pili awe na jeraha la kukatwa na chupa kwenye moja ya viganja vyake.”
“Sawasawa.”
“Hawa watu tunaowatafuta ni lazima tupime damu zao, tukague na viganja vyao. Tukimuona mtu na jeraha hata kama ni dogo tunamchuguza damu yake, ikionekana kundi lake ni kama hili tutakuwa tumeshampata muuaji.”
“Sawasawa.”
Matokeo hayo kidogo yalinipa ahueni. Kama tuna ushahidi wa sampuli ya damu ya muuaji isingekuwa rahisi kutuhumiwa mimi hata kama ndiye niliyekuwa na Matilida.
Pia mimi sikuwa na jeraha mkononi mwangu. Hivyo hata kama utapatikana ushahidi kuwa aliyeshuka na msichana huyo kwenye teksi nilikuwa mimi, lakini itaonekana siye niliyemuua.
Wazo hilo lilinipa amani kidogo moyoni mwangu.
Kingine kilichonifurahisha ni kwamba hatutakuwa na sababu ya kuwalazimisha watuhumiwa wakiri kosa. Kazi yetu itakuwa ni kutazama jeraha kwenye viganja pamoja na kuwapima damu. Tukimpata Mdachi tunampima damu na tukimkamata Mabruki pia tunampima damu.
Nikawaza kimoyomoyo, sasa kazi ni kumkamata Mabruki. Ilikuwa ni lazima niandae hoja ya kumkamatisha hata kama ni za uongo.
“Sasa naona tumepiga hatua nyingine nzuri zaidi katika uchunguzi wetu.” Inspekta Mwakuchasa aliniambia.
Hapohapo nikaoana nimueleze inspekta huyo kuhusu Azzal Mabruki.
“Afande kuna kitu nataka pia tukiingize katika uchunguzi huu.”
“Kitu gani?”
“Unamkumbuka Azzal Mabruki, yule mshitakiwa wa meno ya tembo aliyeachiwa na mahakama.”
“Namkumbuka, ana nini?”
“Nimekuwa na shaka naye sana. Katika pitapita zangu nilipata habari kwamba huyu Mabruki alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Matilida. Nilisikia siku aliyouawa Matilida, Mabruki alikuwa ameegesha gari lake nyumbani kwa akina Salma, huyu msichana niliyekuja kumuonesha picha.”
Nikaendelea kumwambia.
“Sasa wasiwasi wangu isijekuwa kulikuwa na mambo ya kufumaniana kati ya Mdachi na Mabruki na kusababisha Mabruki amuue yule msichana.”
“Huyo Salma ndiye aliyekuambia hivyo?”
“Hizo habari nilizipata mitaani tu, lakini Salma aliniambia Mabruki ana mpenzi wake nyumba anapoishi yeye. Inawezekana amenificha. Habari za kuaminika ni kuwa Matilida ndiye aliyekuwa mpenzi wake.”
“Wewe ulikuwa unashauri nini?”
“Nashauri kwamba na yeye tumuingize katika orodha yetu ya watuhumiwa ili aweze kukamatwa.”
Mwakuchasa aliwaza kidogo kisha akaniambia.
“Kuna watu ambao kidogo ni wazito, wana wanasheria wao. Unapompa mtu wa aina hiyo tuhuma kama hiyo ni lazima uwe na ushahidi wa kutosha.”
“Afande umesahau, tuna sampuli ya damu yake na tuna alama ya jeraha kwenye kiganja. Huo ni ushahidi wa kutosha.”
“Wanasheria wake wanaweza kupinga asitolewe damu.”
“Tunaweza kutumia nguvu ya mahakama kumlazimisha atolewe damu kwa ajili ya uchunguzi wetu.”
“Sawa. Unadhani itakuwa vyema akamatwe leo?”
“Kesho asubuhi.”
“Anaweza kupatikana wapi?”
“Nyumbani kwake.”
“Sawa. Asubuhi tunaweza kwenda kumkamata kumhoji na kuangalia uwezekano wa kupima damu yake.”
No comments: