Kutoolewa Au Kuchelewa Kuolewa Ni Laana?

KATIKA nyakati tulizonazo, wanawake wengi wanahangaika mno! Wanazunguka na kufuatilia kila semina. Wanakwenda kufunguliwa kwa mitume na manabii. Wanatoa sadaka maalum kanakwamba wanaweza kumhonga Mungu ili wapate waume. Wengine wanalala na mitume na manabii uchwara ili kuondoa mikosi.

Wengine wanakwenda kwa waganga wa kienyeji. Wanakwenda kukanyaga mafuta na maji ya upako na mengine mengi ya aibu.
Wanafanya mambo haya yote kwa sababu wameaminishwa kwamba hawaolewi kwa sababu kuna laana inafuatilia maisha yao.
Wanaamini wana laana kwa sababu ya mafundisho ya watumishi wanaowaamini.
Masomo ya laana ni biashara nzuri kwa watumishi feki.

MSINGI WA UPOTOSHAJI
Kuna baadhi ya maandiko yanaonesha kwamba laana inaweza kupatilizwa hadi kizazi cha tatu na cha nne. Kwa hiyo mwanamke ambaye hajaolewa na miaka inayoyoma baada ya kupita umri wa miaka 30, jambo la kwanza anaingizwa kwenye mtego wa kuulizwa kama kwenye ukoo au familia yake kuna wanawake ambao hawajaolewa au walichelewa kuolewa?

Endapo jibu ni ndiyo, basi mtumishi uchwara atachukua kigezo hicho kukutangazia kwamba kuna laana kwenye ukoo wako.
Kuna watu watakwambia kwa sababu ulizaa na kijana fulani akakuacha, ndiyo maana roho ya kukimbiwa na wachumba inakuandama. Au alikuachia damu ambayo bado ina uhalali juu yako.

Cha ajabu ni pale unapoona kijana yule ameoa na anaendelea vizuri! Mwingine atakwambia kwa sababu ulitolewa usichana wako na mtu fulani, basi huyo ndiye mumeo halali. Kwa hiyo huwezi kuolewa na kama ukiolewa ndoa yako itapata shida. Ni wapi Biblia inaeleza kwamba damu ya ukeni inatumika kuweka agano?

Mwingine atakwambia ufunge siku 21 ili Mungu ajibu maombi yako kama Danieli kwa sababu kuna mkuu wa Uajemi amemshikilia mume wako kwenye ulimwengu wa roho. Usipoifahamu kweli, lazima utanyooshwa tu.

Mambo mengine yanatokana na kurithi tabia au mienendo ya wazazi ndiyo maana unaweza kupata changamoto au kujikuta kwenye aina ya maisha kama walioishi wazazi wako. Ishu nyingine ni malezi tu ya familia.

Ukifuatilia kwa umakini, wanawake wengi waliolelewa katika mazingira fulani, wanapenda sana harakati za ukombozi wa mwanamke.

Siyo jambo baya ikiwa wanaelewa wanajikomboa kutoka kwenye kitu gani.
Wanawake wengi waliolelewa katika mazingira fulani, hawaamini kuwa mwanaume ni kichwa cha familia kwa sababu wameona mama zao wakiongoza kila kitu. Kwa hiyo ukimwambia mwanaume ni msemaji wa mwisho, lazima ujiandae kumwelekeza kwa muda mrefu na kwa ufasaha.

Kwa bahati mbaya wengine wameona mama zao wakijihusisha na biashara ya ngono (hata kama mama alikuwa na anko wawili waliokuwa wanampa pesa na kufaidi penzi lake ni biashara tu) nao wakajiingiza kwenye uasherati tangu utotoni na kujikuta wamepoteza sifa njema, lakini umri ulipokwenda ndipo sasa wanahitaji kuolewa na kutulia.

Wanawake wengi waliolelewa kwenye mazingira fulanifulani hawana heshima, wabishi, wakali na hawapendi kushauriwa kwa sababu wana mitazamo mibaya kuhusu wanaume na wengine wamelelewa na mama ambao kwa bahati mbaya hawakufanyika kuwa kielelezo bora, wakarithi tabia mbaya bila kupenda.

Kuna maswali kadha wa kadha ambayo mtu unaweza kujiuliza, kama mtu amefikia hatua ya kwenda kwa
waganga, unafikiri kwa mara ya kwanza kabisa aliona wapi kitu cha namna hiyo?

Kama mtu ana tabia ambazo wanaume hawazipendi na wanamwambia, lakini hataki kubadilika, unafikiri ni mwanaume gani atamuoa?
Ninakuhakikishia hata kama utafunga na kuomba ni kazi bure, labda ubahatike kupata mwanaume ambaye hajakuf-ahamu.
Umewahi kujiuliza ni kwa asilimia ngapi tabia za kwenu au malezi uliyopata utotoni yanakufanya uonekane mtu wa ajabu?

Je, elimu yako au pesa zako zimekufanya uwe mwenye kiburi?
Hakuna laana au mkosi unaofuatilia maisha yako ikiwa umemwamini Mungu na anaishi ndani yako. Badili fikra zako sasa!

Tathmini tabia zako, mwenendo wako, mitazamo yako na mwonekano wako uone kama lipo ambalo limekuwa kikwazo kwa wanaume kukuchumbia kisha umwombe Mungu akusaidie ubadilike na akupe kibali. Usimsingizie shetani, mambo mengine ni yako mwenyewe.

Kimahesabu wanawake wako wengi kuliko wanaume kwa hiyo mambo mengine ni ya kimahesabu tu, usipoelewa utajikuta unagawa penzi ukidhani unaongeza nafasi ya kuolewa kumbe ndiyo unaharibu zaidi.



No comments: