Upendo Ulivyookoa Maisha Yangu



Alex alishikilia simu yake akijaribu kumpigia mkewe lakini simu iliita bila kupokelewa, alionekana kuwa na wasiwasi sana mpaka mfanyakazi mwenzake akamuuliza.. “Vipi, mbona una wasiwasi sana, kuna nini?” Bila kuongea alitingisha kichwa kuashiria kua hakuna kitu. Lakini kadri kadri gari ilivyokuwa inachanja mwendo ndivyo alivyozidi kuwa na wasiwasi mpaka akashindwa kuvumilia.
“Mkuu samahani mnaweza kuniacha hapa nikarudi nyumbani kidogo, nitakuja na basi?” Alex alimuuliza Bosi wake ambaye alikua amekaa siti ya mbele, walikua na wafanyakazi wenzake wakielekea Morogoro kwenye sherehe ya mfanyakazi mwenzao. “Kwani kuna shida gani, kuna nini? Bosi aliuliza kwa wasiwasi… “Hakuna kitu mkuu, ni nyumbani tu kule, sijaagana na Mama vizuri..sasa….”
Hakumalizia kuongea wafanyakazi wenzake walianza kucheka na kumtania, nikweli walikuwa wakifahamu namna alivyokuwa akimpenda mkewe na yeye mara nyingi hakuficha mapenzi yake. Walijaribu kumshawishi lakini Alex alikataa katakata na kushuka, walikuwa wameshakaribia Ubungo hivyo alichukua bodaboda aili kuwahi nyumbani Temeke alipokuwa akiishi na mkewe.
Wakati wa kuondoka walikuwa wamekorofishana kwani mkewe alitaka kwenda kwenye ile sherehe na yeye alisisitiza kuwa ni kwaajili ya watumishi tu. Kilichomfanya mkewe kukasirika nikuwa mke wa mfanyakazi mwenzake alimuambia mkewe kuwa anaenda Morogoro hivyo mkewe kuona kama alikuwa anadanganywa.
Alex alirejea nyumbani na kumkuta mkewe akiendelea na shughuli za pale. Mkewe alishangaa kumuona lakini alimuambia “Nimeshindwa kuondoka tukiwa tumenuniana, safari ina mengi lolote linaweza kutokea, sitaki kumbukumbu yangu ya mwisho kwako iwe ni kukorofishana, naomba unisamehe na kama hutaridhika basi sioni hata haja ya kwenda hiyo safari…”
Mkewe alistuka kusikia vile, alimuangalia mumewe na machozi kuanza kumtoka. Nikweli walikuwa wakipendana  lakini hakujua ni kwakiasi kile. “Nenda kwa amani mume wangu, Yale yameshaisha ni mimi mwenyewe nilichanganya kumbe aliyeniambia mwenyewe anaenda kwa upande wa mke alialikwa huko na haendi na mumewe, nilishasahau hayo na nilipanga ukifika nikupigie simu..”
“Whoooo!…” Alex alipumua kuashiria kupata nafuu na ahueni flani. “Nilifikiri bado umekasirika hasa nilipokuwa nakupigia simu hupokei..?”
“Simu! Hata sijaisikia mume wangu… nimeiacha ndani kwenye chaji hata sijui kama ilikuwa inaita…” Aliongea huku akitabasamu. Alex alimkumbatia mkewe kisha akapanda bodaboda ile ile ili imuwahishe Ubungo apande magari ya Morogoro. Nikweli aliwahi na kupata gari akaanza safari.
Walipokua wanakaribia Mikese, kilometa chache kutoka Morogoro Mjini walikutana na ajali, gari dogo iliyokuwa ikitokea Dar iligongana uso kwa uso na lori la mizigo na kupinduka. Magari yalikua yamesimama kwani bado lori lilikua halijaondolewa. Watu walishuka na alipofika chini alikuta gari dogo ambalo liligongana na lori lilikua ni gari la ofisini ambalo lilikuwa wafanyakazi wenzake wane na wote wlaifia palepale.
Alex alikua ni mtu wa tano ambaye alipaswa kuwepo katika lile gari. Hakuamini kuwa upendo wake kwa mkewe ndiyo uliokoa maisha yake, alipiga magoti palepale kumshukuru Mungu, hakuna kitu ambacho angeweza kufanya kwa wafanyakazi wenzake, machozi yalimtiririka kama maji, akiwamabia watu aliapswa kuwepo kwenye ajali ile lakini Mungu alimuokoa. Alimpigia simu mkewe na kumshukuru kwa upendo waliokuwa nao ambao uliyaokoa maisha yake.




No comments: