KAMA PENZI LAKO HALINA MSISIMKO HII INAKUHUSU











Mada ya leo kama inavyojieleza ni maalum kwa watu ambao tayari mpo kwenye uhusiano wa kimapenzi, iwe ni wapenzi wa muda mrefu, wachumba au wanandoa. Umewahi kuhisi kwamba japo unaishi na mpenzi, mchumba au mke/mume huna tena ule msisimko uliokuwa nao wakati mnaanzisha uhusiano wenu?
Yaani upoupo tu, zile hisia tamu za mapenzi ulizokuwa nazo wakati mnayaanza mapenzi yenu hazipo tena, hufurahii kuwa naye, hamzungumzi mkaelewana badala yake kila siku ni ugomvi na migogoro isiyoisha!
Kila unachokisema au atakachokisema hata kama ni kizuri vipi kwako unakiona kibaya na hakina maana. Kila mnapoanza kuzungumza, hata kama ni jambo zuri lazima muishie kutukanana, kufokeana au kupigana!
Unaishi naye lakini hujisikii chochote juu yake, hata akiugusa mwili wako unaona kero na hutaki hata kumtazama usoni. Hujisikii hamu tena ya kuwa naye faragha, kila unachokifikiria kuhusu yeye kinakupandisha hasira na kukuudhi!
Unatamani uhusiano wenu ufikie mwisho hata sasa hivi ingawa hujui uanzie wapi… Ukiona hayo yote niliyoyataja na mengine mengi yanakutokea, huo ni uthibitisho kwamba unaishi kwenye mapenzi yaliyokosa msisimko.
Wengi wanapofikia hatua hii ya kuishi kwenye mapenzi yaliyokosa msisimko, huwa wanadhani njia pekee ni kuachana. Lakini je, hakuna mbinu zinazoweza kurudisha hisia kwenye mapenzi? Hebu twende pamoja.
MBINU ZA KURUDISHA MSISIMKO
Hatua ya kwanza, jiwekee nadhiri kutoka ndani ya moyo wako kwamba upo tayari kulifufua penzi lako na kurudisha hisia zilizopotea. Yawezekana wewe umeamua hivyo lakini mwenzako hayupo tayari, hilo lisikukatishe tamaa. Jiambie moyoni kwamba utafanya kila kinachowezekana kurudisha furaha, amani, hisia za mapenzi, msisimko na upendo kama ilivyokuwa wakati mnaanzisha uhusiano wenu.
Jipe muda wa kutafakari nini kilisababisha mwanzo mkawa na furaha na kupendana sana. Jaribu kukumbuka mambo uliyokuwa ukimfanyia mwanzo mpaka akakupenda na kuwafanya muishi kwa amani na upendo.
Anzia hapohapo, anza kufanya yale yaliyomfanya akupende mwanzo, kuwa mpole kwake, acha kumuonesha kisirani, dharau, jeuri au kujibizana naye. Badili hisia zako za ndani, badala ya kufikiria mabaya yake, fikiria mazuri aliyowahi kukufanyia.
Kubali kuwajibika. Japokuwa wengi huwa wanashindwa kwenye kipengele hiki, jibebeshe mzigo wa lawama wewe mwenyewe hata kama si kweli kwamba wewe ndiyo mwenye makosa. Jiambie mwenyewe kwamba wewe ndiyo umesababisha mfikie hapo mlipofika kwa sababu kama alikukosea, ungeweza kumsamehe kuanzia siku ya kwanza na wala msingefikia hatua hiyo.
Ukishakubali kuwajibika, utakuwa kwenye hatua nzuri ya kuzidi kumkaribia, hata ile chuki uliyokuwa nayo, utashangaa inayeyuka kama barafu iyeyukavyo juani na mapenzi yanaanza kuchanua upya moyoni mwako.


No comments: