KAMA PENZI LAKO HALINA MSISIMKO HII INAKUHUSU-2











Tulianza kuangalia mbinu zinazoweza kukusaidia kurudisha msisimko kwenye penzi lililopoteza mwelekeo na tuliona kwamba jambo la msingi la kuanza nalo ni kujiuliza kuhusu chanzo cha tatizo kisha baada ya hapo, ukubali kuwajibika.
Kuwajibika ninakokuzungumzia hapa ni ile hali ya kuacha kumtupia lawama mwenzako kwamba ndiye amesababisha mpaka mkafika hapo. Lazima ukubali kwamba na wewe ni sehemu ya tatizo lililowafanya mkafikia kwenye hatua hiyo.
Katika hatua za kuwajibika, yapo mambo unayotakiwa kuyafanya kuonesha kwamba hufurahishwi na aina ya maisha unayoishi na mwenzi wako. Unajua kama kuna jambo linakuumiza, ni vizuri kumuonesha mwenzi wako badala ya kuendelea kujifanya kichwa ngumu.
Akishajua kwamba unaumizwa na maisha mnayoishi, itakuwa rahisi kwako na kwake pia kuanza kushirikiana katika kuamsha upya hisia za mapenzi kati yenu. Anza kumfanyia yale mambo unayojua yanamfurahisha.
Ni vizuri unapoishi na mwenzi wako, ukamsoma na kuelewa mambo ambayo huwa yanamfurahisha hata anapokuwa na mudi mbaya. Kwa kuwa mmeshaishi pamoja kwa muda mrefu ni matumaini yangu utakuwa umepata muda wa kutosha wa kumsoma nini anachokipenda zaidi.
Mfanyie yale mambo yanayomfurahisha, kwa mfano unaweza kumtoa ‘out’ na kumpeleka sehemu anazozipenda, ambazo awali mlipokuwa mkienda pamoja alikuwa akiinjoi vya kutosha.
Jenga utaratibu mpya wa kuwa unamnunulia zawadi mwenzi wako kwani wataalam wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa kitendo hicho kinasaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha upya hisia za mapenzi.
Wapo baadhi ya watu ambao wanapokuwa kwenye hatua za mwanzo za uhusiano wao, huwa wepesi sana kuwanunulia wenzi wao zawadi mbalimbali lakini wakishazoeana, utaratibu huo hukoma.
Anza tena utaratibu wa kuwa unamnunulia zawadi, hata kama ni ndogo au hata kama ataonesha kutozifurahia, wewe endelea na taratibu utaanza kuona mabadiliko. Tafsiri ya kumnunulia umpendaye zawadi, ni kwamba huwa unamfikiria hata unapokuwa mbali naye.
Jitahidi kuwa mwema kwake, najua ni vigumu kwa binadamu kutofanya makosa kwa sababu hatujakamilika lakini kama kweli umedhamiria kurudisha msisimko kwenye penzi lako, jitahidi kupunguza makosa kadiri uwezavyo.
Mwenzi wako anapokuwa ameanza kurudisha hisia halafu ukafanya tena kosa jingine litakalomuumiza moyo wake, utakuwa umemrudisha nyuma na kufanya kazi izidi kuwa ngumu.
Muhimu kuliko yote, jiapize kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako kwa moyo wako wote, endelea kumfanyia mambo mazuri, msamehe kwa yote aliyowahi kukosea na wewe muombe radhi kwa uliyowahi kumkosea, mfanye aamini kwamba unampenda yeye peke yake na unamjali.
Taratibu utaanza kuona mabadiliko, hisia tamu zitaanza kurudi upya na ukiongeza juhudi, utayafurahia mapenzi pengine kuliko hata ilivyokuwa siku za mwanzo za uhusiano wenu.


No comments: