UTAJUAJE KAMA UPO MAPENZI HATARISHI?SOMA HAPA
MATUKIO ya wanandoa kuwaua wenzi wao au kuwafanyia ukatili wa kutisha, yanazidi kuongezeka. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya mume kumuua mke, mke kumuua mume au kusababishiana vilema vya kudumu
Lakini si kwa waliopo kwenye ndoa pekee, hata wale waliopo kwenye uhusiano wa kawaida wa kimapenzi au wachumba nao wapo kwenye mkumbo huu wa kufanyiana ukatili wa kutisha.
Kiasili mapenzi yanapaswa kuwa na amani, huwezi kufurahia mapenzi kama una hofu juu ya mwenzi wako, kila siku mnatukanana, mnapigana au hata kutishiana maisha. Kwa bahati mbaya, watu wengi wapo kwenye aina hii ya mapenzi, mapenzi hatarishi au kwa Kiingereza Violent Love na hawajui nini cha kufanya, huku wengine wakichukulia kuwa ni kitu cha kawaida.
Kutofautiana katika mapenzi ni jambo la kawaida, lakini kwa nini mfikie hatua ya kutishiana maisha, kupigana, kutukanana au hata kuuana? Wengi wanaopoteza maisha yao au kupata vilema, ni kwa sababu walishindwa kuchukua hatua mapema, waliliona tatizo lakini hawakuwa wanajua kama ni kubwa kiasi hicho au hawakuwa na mbinu za kujitoa.
Unapoona upo kwenye uhusiano uliojaa vurugu, hutakiwi kupuuzia. Unatakiwa kuchukua hatua haraka kwa sababu maisha lazima yaendelee, unaweza kuendelea kufurahia maisha hata bila ya uwepo wake. Sasa utajuaje kama upo kwenye penzi hatarishi?
Hebu jiulize maswali yafuatayo: Huwa unapatwa na hofu ndani ya moyo wako unapokuwa karibu na mwenzi wako? Huwa unaogopa kukosea hata yale makosa ya kibinadamu ukiwa karibu na mwenzi wako? Unajihisi kama muda wote wewe ndiye unayefanya makosa? Haupo huru hata katika mazungumzo ya kawaida ukihofia kumkasirisha umpendaye?
Bila shaka kila mmoja atakuwa na majibu yake. Kadiri majibu yako yanavyokuwa ‘ndiyo’, basi ndivyo dalili kwamba upo kwenye uhusiano hatarishi zinavyoongezeka. Hebu jiulize tena maswali mengine yafuatayo: Mwenzi wako ana kawaida ya kukufokea au kukutolea lugha chafu?
Ana kukosoa mara kwa mara hata pale unapoamini kwamba upo sahihi? Anathamini zaidi pesa zako au anakutumia kama chombo cha starehe? Anakulazimisha kufanya tendo la ndoa au anakulazimisha kumtimizia mahitaji ambayo huna uwezo nayo? Anapandwa na jazba hata kwa vitu vidogo.
Majibu utakuwa nayo mwenyewe na kama ilivyokuwa hapo juu, ukipata majibu ya ndiyo mengi, basi jua upo kwenye hatari. Watu wengi huwa wanaamini mapenzi hatarishi ni yale tu ambayo mwenzi wako anakupiga au anatishia kukuua. Ni kweli kupigana au kutoleana vitisho ni jambo la hatari, lakini huwa ni dalili za mwisho za hatari. Dalili za awali ndiyo mbaya zaidi na usipozichukulia hatua, zitawafikisha pabaya.
Wengi wanaamini kwamba wanaume ndiyo pekee wanaofanya ukatili, lakini utafiti unaonesha kwamba mara nyingi wanawake ndiyo huanza kwa kuonesha dalili hizo za awali niliozitaja hapo juu, mwisho mwanaume anashindwa uvumilivu na kuchukua maamuzi yanayomshangaza kila mtu.
Katika matukio yote ya kikatili wanayofanyiana wanandoa unayoyasikia, yalianza kwa dalili za awali na wahusika kushindwa kuchukua hatua, mwisho yakatokea ya kutokea. Hakuna mtu anayependa kufanyiwa ukatili na mwenzi wake, si mwanaume wala si mwanamke.
Hakuna anayependa kusikia ndugu yake, rafiki yake, mwanaye au mtu wake wa karibu amefanyiwa ukatili na mtu ambaye awali walikuwa wakipendana. Kama ni hivyo, basi ni jukumu la kila mmoja, kumsaidia mtu aliyepo kwenye uhusiano hatarishi. Unadhani unawezaje kumsaidia mtu aliyepo kwenye uhusiano hatarishi
No comments: