MREMBO WA WA KIJIJI SEHEMU YA KUMI NA SITA - 16





MREMBO WA WA KIJIJI

         SEHEMU YA KUMI NA SITA - 16

"Ajabu sana hii,binadam ageuke ng'ombe?.." 

"Mmmh tusubili tuone"

"Lakini kama mkuu aliweza kuitembeza treni mahala pasipokuwa na reli, atashindwaje kumgeuza binadamu kuwa ng'ombe?.." Walijaji wachawi baadhi baada kusikia mkuu wao akinena kuwa anataka kumgeuza ng'ombe mke wa mzee J. Mazungumzo hayo yaliyokuwa yakiongelewa kwa sauti ya chini, mkuu wao aliweza kuyasikia. Na hivyo aliyakatisha kwa sauti kali alisema " Sijitaji maswali, muda  huu ni muda wa kazi kwahiyo kila mmoja akae kwenye usafiri wake aondoke mahala hapa " Amri hiyo ilitekelezwa kwa haraka sana ambapo wachawi wote waliokuwepo hapo walipanda kwenye nyungo zao kisha wakapaa ilihali huku nyuma punde mke wa mzee J alionekana chini miguu ya mkuu wa timu ya kina bibi Pili. Mkuu huyo aliangua kicheko, alipo katisha kicheko chake akamnyooshea kidole mama Chitemo kufumba na kufumba  akawa katika umbile la  ng'ombe.

Kwa mara nyingine tena akaangaua kicheko, safari hiyo alipokatisha kicheko hicho alipampanda na safari ikawa imeanza.
   Upande wa pili nyumbani kwa mzee Mligo, vita ilikuwa imepamba moto. Kwani siku hiyo Mligo hakuona haja ya kumuogopa mzee J, hivyo alijitokeza na kisha kupigana nae kiume kwa kutumia nguvu za kichawi. J akiwa na kundi lake lilimshambulia Mligo, ila Mligo kutokana na uzoefu wa miaka mingi aliokuwa nao miaka kadhaa nyuma aliweza kuwamudu vizuri.

"Mkuu tufanye njia gani maana kushindwa kwetu ni mwiko" Alisema mmoja ya wachawi aliokuwa nao mzee J, hapo ni baada kuona mzee Mligo makombora yake yanakasi na pia yanauzito wa hali ya juu. Mzee J kabla hajamjibu kibaraka wake akapotea. Muda mchache baadae akaonekana nyuma ya Mligo, bila kupoteza sekunde akamtupia kombora.

Mzee Mligo akahisi hatari nyuma yake, upesi akapotea, kombora lile la mzee J likaenda kumpata kibaraka wake ambapo kibaraka huyo lilipomfikia alianguka chini huku akipiga mayowe iliahali nguo zake zikiwa zimeshika moto. J hakujali zaidi aliendelea kutupa makombora mfurulizo, Mligo bado alionyesha umahili wa kuyapangua.

Muda mchache baadaye naye alianza  kujibu mashambulizi, wakati bwana J alipokuwa akijitahidi kurusha makombora yake yenye moto, mzee Mligo yeye akajibu  ya visu. Visu vya kichawi, kisu kisichokatiwa kitunguu wala nyanya bali visu hivyo ni mahususi kwa suala nzima la kupigana na wachawi. Style hiyo ilioneakana kumchemsha mzee J, akaamua kutoa ishara ya kuwataka vibaraka wake wapotee ili asilie mwenyewe uwanjani.  Wananzengo hao walitii matakwa ya kiongozi wao, walitoweka mmoja baada ya mwingine mpaka wote wakaisha akabaki mzee J. Mpambano ukawa umeshika hatamu.

Lakini pindi mpambano huo unaendelea mara ghafla eneo hilo alikatiza yule kiongozi wa kundi la Bibi Pili akiwa na mtu aliyemgeuza ng'ombe. Kwa macho ya kawaida J asingemuona ila kwa kuwa alikuwa na macho matatu yaani macho yake mawili huku moja likiwa ni jicho la kuona mambo yaliyojificha kutokana na nguvu za giza. Ilipelekea kuweza kumuona mkewe akiwa amefanyiwa kitendo cha ajabu sana kuwahi kutokea katika maisha yake ya uchawi, hapo hakuona haja ya kuendelea kupigana na mzee Mligo, haraka sana akapotea  akaibukia mbali kidogo na mahali ilipo nyumba ya mzee Mligo. Punde si punde mbele yake ukatokea ungo akapanda na kuanza kumkimbia yule bwana aliyemgeuza mkewe ng'ombe na kisha kumpanda juu kama farasi, kimo cha mbuzi mzee J aliutembeza ungo wake akimkimbiza  mchawi yule kwa kasi ya kimbunga. Kabla hajamfikia alisikia sauti ikisema "Jaruooo mbona unatafuta matatizo?.." Sauti hiyo lisikika ikiambatana na ngurumo nzito na tetemo ya ajabu iliyomfanya mzee J kuangaka chini.

 "Jaruo tulikwambia nini?.." ilihoji sauti hiyo.

 J akihema kwa kasi akajibu "Lakini yule mtu ailicho nifanyia sio kitu kizuri, iweje amfanye vile mke wangu?.."

"Aha hahahah" Iliangua kicheko sauti hiyo, na mara baada kukatisha  kicheko ikasema "Hatakama, kumbuka Jaruo tulikwambia unahitaji damu ili uweze kukabiliana na jopo la maadaui lilopo mbele yako. Tambua huna  adui mmoja, na huyo unayemfuatilia ni moja ya maadaui zako wakubwa sana..."  Ilisema sauti hiyo.

"Sa.. Sa..sasa nifanyeje eeh?.." Mzee J akauliza.

"Damu" Ilijibu  kwa mkato sauti hiyo iliyobeba tetemo kubwa na mwangwi wa ajabu kisha ikatoweka akabaki mzee J kijasho kikimtoka huku akigugumia maumivu ya kuanguka chini. Punde baada sauti hiyo kutoweka watu wake walifika, wote kwa pamoja wakastaajabu kumkuta kiongozi wao yupo chini huku ungo wake ukiwa pembeni ukionekana kufumka baadhi ya sehemu.

"Mkuu kulikoni?.." Alihoji mchawi mmoja huku akimgusa mabega ya mzee J.

 "Ndugu zangu huu ni mtihani, hapa sio mahala pakuongelea naombeni kesho tukutane mbuyuni ili nizunguze nanyi kwa mapana zaidi" Alijibu mzee J huku akigugumia maumivu.

"Unataka kutuambia yule mzee kathubutu kutushinda?.." Aliuliza mchawi wa pili, swali ambalo lilionekana kumkera mzee J ambapo kwa sauti kali akajibu "Msitake kunipanda kichwani, nimeshasema kesho tutaongea kila kitu lakini bado unauliza uliza unataka nini? Haya nikisha kujibu utafaidika nini? Haraka sana poteeni hapa"

"Sawa mkuuu" Walijibu kwa pamoja hao wachawi waliofika eneo la tukio. Kwisha kutii amri hiyo  mmoja baada ya mwingine akapotea, mwishowe ikasilia vumbi kwani kila mchawi aliyekuwa akipotea alipotea na mshindo mzito ulioweza kutimua vumbi.

"Mnauliza uliza tu maswali ya kijinga wakati nimeshachanganywa na
 mimi" Alijisemea mzee J baada watu wake wote kuondoka.

 Mwishowe naye alipotea akaibukia ndani ya nyumba yake, akazipiga hatua kuelekea chumbani kwa Chitemo akamkuta yupo amelala usingizi mzito kisha akingia chumbani kwake ambapo alikuta kitanda cheupe. Hakika J akajihisi kuchoka kabisa, akaketi kitandani akashusha pumzi ndefu huku moyoni akijisemea "Hivi ni nani huyu anayecheza na familia yangu badala ya kucheza na baba mwenye nyumba? Je, atakuwa ni bibi Pili huyu huyu? Na kama ni bibi Pili mbona yule niliyemuona kamfanya kitendo kile mke wangu ni mwanaume? Ooh naona hapa ni sipo wajibika kama mwanaume kwenye nyumba yangu basi kuna watu watanisaidia majukumu"

"Ngoja niwajibike" Aliongeza kusema mzee J  safar hiyo akizivua hirizi zake.
   Upande mwingine mzee Nhomo bado alikuwa na mtihani mzito wa kuwakimbia wale wachawi waliokuwa wakimfuata nyuma, ila mwishowe wachawi wale waliachana na zoezi hilo baada kupokea taarifa kuwa wanahitajika nyumbani kwa bibi Pili. "Bahati yake la sivyo tungemuonyesha utofauti wa wigi na nywere" Alisema moja ya wachawi waliokuwa wakimkimbiza mzee Nhomo.

"A hahahah kabisa yani sikupingi" Alijibu mwenzake kisha wakagongeana mkono, na mara moja kwa kasi ya ajabu wakaziendesha nyungo zao kuelekea nyumbani kwa bibi Pili kutii amri.

    ************
Kesho yake asubuhi nyumbani kwa mwenyekiti walionekana wanakijiji wakiandamana baada kuchoshwa na mambo kadhaa yanayotokea kijijini kwao. Mzee mmoja wa makamo alisikika akisema "Hatukubali kijiji kimekuwa kama dangulo la uchawi? Uchawi umekisili hapa kijijini lazima leo mwenyekiti utuambie kwanini unawafuga watu hawa? Tofauti na hapo tunaanza na wewe kisha wengine watafuatia" Maneno ya  mzee huyo yaliungwa mkono na jopo hilo la wanakijiji lililofika nyumbani kwa mwenyekiti kuzungumza ukweli wa kile kinacho endelea kijiji cha Ndaulaike. Punde si punde mwenyekiti akafungua mlango, kwa sauti ya upole akasema "Haya semeni nini shida yenu nawasikiliza, ongeni mmoja mmoja ili niwaelewe"

"Shida yetu mwenyekiti, kijiji hiki kimejaza wachawi tangu wageni wakina fulani waingie. Kwahiyo kwa hali hii wanakijiji tumechoka" Alisema mwanakijiji mmoja ambaye hakutaja Jina lake. Mwenyekiti akakohoa kidogo kisha akajibu "Utamjuae mtu kama mchawi hali ya kuwa wewe sio mchawi?.."

"Mwenyekiti na ndio maana tumemtafuta mtaalamu aje atuondolee wachawi, kwahiyo tumekuja kwako kama muhusika alivyosema. Kibali chako kitamfanya atembee kifua mbele bila kubuguziwa na mtu yeyote yule hapa kijijini" Alijibu mwanakijiji wa pili.

"Sawa tu muacheni aanze" Aliisema mwenyekiti ikiwa akihisi mapigo ya moyo wake kwenda mbio mithili ya saa mbovu.  Mtaalamu huyo aliyeletwa Ndaulaike kwa dhumuni la kuwaumbua wachawi baada kupata kibali kutoka kwa mwenyekiti wa kijiji, alikohoa kidogo kisha kwa tabasamu bashasha akasema "Ahsante sana ndugu mwenyekiti kwa kibali chako, hakika wewe ni kiongozi  sahihi kabisa hapa Ndaulaike kwani unajali hitaji la wanakijiji wako. Aah lakini kwa kuwa tumepanga tupite nyumba moja baada ya nyingine, basi ni vyema kama nitaanzia hapa kisha nifuatie nyumba nyingine"

"Uanzie wapi? Mimi ni mwenyekiti, siwezi kujihusisha na ushirikina mimi ebo. Kuwa  na heshima ama la kama umeshindwa ondoka" Alisema mwenyekiti kwa hasira akimwambia mtaalamu wa kuwaumbua wachawi. Suala hilo la mwenyekiti kumgomea mtaalamu lilijenga sintofahamu kubwa kwa wanakijiji ambapo wote kwa pamoja waliligomea sanjari na kupiga fujo kumshinikiza mwenyekiti akubaliane na matakwa ya mtaalamu. Lakini bado mwenyekiti aliweka kipingamizi. Alipoona analizimishwa zaidi akapotea mbele yao ikabaki vumbi mlangoni.






No comments: