RIWAYA:: MAISHA YANGU YA UVUVI SEHEMU YA KWANZA 01
ENDELEA..............
.................Niliweza kuishi Maisha ya tabu baada ya kufukuzwa kazi ambayo niliamini kuwa ndio kitegemea uchumi wangu. Maisha yangu kiukweli nilishindwa kuendelea kwa kuwa Nilishindwa kumudu familia niliyonayo. Nilibahatika kuwa na watoto wawili nikiwa na mke wangu.
Baada ya kukaa kwa muda mrefu sana ndipo siku moja mke wangu aliniita. Nilienda kumsikiliza pale alikoniita.
"Mume wangu nina jambo nataka kukushauri".
Moyo wangu uliahtuka baada ya kuona jambo la ajabu sana kwa mke wangu. Kwani sikubahatika kupata neno kama hilo kutoka kwa mke wangu.
"Ehee! Nakusikiliza mke wangu nambie".
Nilimuelea huku nikikaa vyema ili nipate nipate kunsikiliza vizuri.
"Unajua kuwa mpaka sasa tuna maisha magumu sana pia, mtoto wetu hapa anahitaji ada ya shule...unaonaje ukatafuta kazi".
Mke wangu aliniambia.
"Kiukweli, Mke wangu jambo ambalo unaliongea limeniingia akilini kabisa, ila sasa nilikuwa nawaza kazi gani ambayo itaniwezesha kupata Fedha kwa muda mfupi ili nifanikiwe na kujikwamua na maisha haya?"
Nilibaki nikiduwaa baada ya kumueleza jambo lile.
"Sawa ila kumbuka kuwa Mtafutaji hachoki na akichoka basi kapata, sitaki nikuvunje moyo tafuta kazi yeyote halali pia mafanikio hayaji kwa wepesi kama unavyofikilia jitihada zako ndizo zitafanikisha kupata yale uyatakayo, kikubwa sisi tutakuombea mungu na utafanikiwa kabisa".
Maneno ya Mke wangu, yalinifanya nijione kuwa ni mtu wa kipekee kabisa.
Nilijiona sasa mwenye nguvu na kuamini kama kweli nina mke ambae anapenda sana mafanikio yetu.
Nilimpa moyo kuwa nipo tayari kufanya kazi yeyote halali ambayo inaweza kunipatia kipato cha halali.
"Mke wangu hakika nakushukuru, wewe ni mke ambae unajua majukumu yako ndani ya familia hii nakuahidi kuwa naelekea sasa hivi kwa bwana Kibona nadhani nikirudia nitakuwa na akili mpya".
Nilimuacha Mke wangu akiwa anaendelea kunisindikiza kwa macho yake yaliyojaa mapenzi na huruma. Safari yangu ilifika hadi kwa bwana Kibona.
Nilimfika hadi kwa bwana Kibona, nilimkuta akitengeneza Mtumbwi wake vizuri. Kwa maisha ya Pangani ambayo niliyazoea kama huna elimu basi utaishia kuvua samaki mtoni au baharini.
"Bwana kibona, habari yako ndugu naona hapo mambo yamepamba moto".
Nilimsalimu.
"Eeeh! Ni kweli ndugu bwana karibu sana nilikuwa namalizia hapa kutengeneza huu mtumbwi kisha nifungefunge nyavu yangu hapa kisha baadae nielekee kazini".
Nilitamani sana ile kazi japo nilikuwa na uwoga nayo mwanzo. Kitu ambacho nilikuwa nina hofu kubwa kutokana na maji ya bahari aikupenda kua karibu nayo kwa kuwa sikujua hata kuogelea.
Bwana Kibona alinikaribisha kwa bashasha sana ndipo nilipomsogelea na kuketi karibu na yeye.
"Ndugu yangu kama unavyofahamu kuwa tangu niache kazi yangu kule nina muda sasa, na halo yangu kama unavyoifahamu sina hili wala lile nilikuwa naomba sasa unishauri au hata kunipa kibarua katika kazi zako hizi ili niweze kupata chochote kitu."
"Mh! Teh teh teh! Teh......bwana unanishangaza sana.."
Alikuwa anacheka baada ya kauli yangu kumueleza kuwa nipate hata kibarua kupitia kazi yake ya Uvuvi.
"Sasa unacheka jambo gani?" Nilimuuliza
"Unajua, bwana Mnali ukisema kuwa nikupe kibarua unanishangaza sana kwa kazi gani hapa...sema tuungane tuifanye kazi hii kwa pamoja na si eti nikupe kibarua..."
Nilimshukuru sana maana niliona sasa matumaini yangu ya kuendelea kuishi vyema mimi na familia yangu ilionekana. Niliondoka pale na kunyoosha njia ya nyumbani huku nikiwa na Imani kubwa sana ya kupata kazi kupitia kwa bwana Kibona.
Nilipofika nyumbani nilimuita Mke wangu kisha nikamueleza kwa kila kitu ambacho kiliendelea mimi na Kibona.
"Mke wangu ndio kama hivyo nimeongea nae na kazi yenyewe ni Uvuvi........"
Nilishangaa kumuona mke wangu akikasirika baada ya kumueleza kuwa kazi ya uvuvi. Ilinibidi nitumie nguvu ya ziada kuendelea kumuuliza na kumtuliza.
"Sasa...wewe umenishauri nitafute kazi lakini mbona sasa umebadili na uso?"
"Ndio ile kazi mbaya bwana Mtu mwenyewe hujui hata kuogelea kabisaaa ukidondoka humo ndani ya maji nani atakuokoa...tafuta nyingine".
Maneno yake yalionyesha hali ya ukakasi kwangu lakini sikuwa na jinsi ilibidi nilazimishe lakini bila hata yeye kujua, niliamua kufanya kazi ile mpaka pale nitakapohisi nina uhitaji wa kutafuta nyngine.
"Sawa mke wangu ila itakubidi uvumilie mpaka niikpata........"
Majira ya jioni bwana Kibona aliniambia kuwa nifike kule kwake. Nilielekea na nilimkuta akiwa anamalizia kupanga shughuli zake. Baada ya kumaliza alinijia na kunikamatisha vifaa kadhaa ikiwemo Magunia yaliyowekwa kwenye ndoo.
Nilibeba zile ndoo huku akili yangu ikiwaza nyumbani kwa mke wangu pindi atakapojua kuwa nipo baharini.
Yote niliyaacha na nikafanya kile ambacho kipo mbele yangu. Tulifuatana hadi baharini muda ulikuwa jioni sana na kiza kilianza kuingia zaidi. Tulipofika sehemu hiyo bahari ilikuwa shwari kabisa mawimbi hayakuwa makubwa sana yalikuwa madogomadogo. Tulikaa kusubiri muda ufike usiku hapo ndipo aliponielekeza mambo kadhaa.
"Ndugu yangu umekubali kufanya kazi hii lakini fahamu kuwa inahitaji uvumilivu sana,juhudi pamoja na ushujaa......kuna kukosa na kupata".
Baada ya hayo maneno ndipo tukaelekea kwenye mtumbwi.
Safari ilianza kufika kwenye kina kirefu cha bahari. Niliwasha chemli ndipo tukatundika nyavu kisha tukatulia. Kibona alikuwa mzoefu mimi nilikuwa muoga sana hata kusimama pale kwenye mtumbwi.
"Ukijifanya muoga haki ya nani utaishia humuhumu ndani ya Maji kuwa makini". Kibona hakuwa mzito alinieleza ukweli kabisa uliotokana na uoga wangu.
Baada ya muda tukaanza kuvuta nyavu na hatimae samaki wakubwa wakubwa tuliwakamata.
Tulifika ufukweni na kutupa nyavu iliyokawa nzito sana.
"Eeeeeeh!, hakika leo ni maajabu sana sijawahi kupata samaki wengi kama hawa tangu nianze kazi hii tena wakubwa sana...."
Alinishangaza kiasi kwamba nikajihisi kuwa mimi ni mtu mwenye bahati sana. Muda ulikuwa umekwenda ndipo Kibona aliniruhusu nifike nyumbani kisha adubuhi na mapema niweze kurudi kwa ajili ya kuangalia Mapato.
Kwa kawaida baada ya kuwapata samaki basi wanunuzi wengi sana wanajitokeza pamoja na zile biashara za kuagiza ambazo ndio nyingi sana.
Niliondoka majira yale japo yalikuwa magumu sana yani muda mbaya. Nilimuodikia Mke wangu. Kumbe alikuwa hajalala alikuwa ananisubiria mimi.
Alifungua mlango, niliingia nilimsalimu lakini hata hakuitikia. Nilichofanya nikaelekea chooni haraka nilioga kisha nikarudi kitandani. Mke wangu alinijua kuwa natoka baharini kutokana na harufu ya samaki.
Asubuhi na mapema bado alikuwa kanuna japo nilijua kipi kimemfanya anune.
"Mke wangu nitarejea muda si mrefu"
Japo nilimuambia lakini hata hakujibu. Nililazimisha kuondoka asubuhi hiyo kuelekea kwa bwana kibona.
Nilimkuta tayari kashafanya biashara na akanipatia kiasi cha pesa na ndipo nikarejea nyumbani.
TUKUTANE TOLEO LIJALO

No comments: