RIWAYA:: MAISHA YANGU YA UVUVI SEHEMU YA PILI 02
ENDELEA.................
................Nikiwa na furaha ya kupata kipato kizuri kama kile ambacho sikutarajia kabisa. Nilitembea njiani nikiwa na faraja moyoni mwangu pia nikiwa na shauku kuwa mke wangu atafurahi mimi kupata ile pesa yenye kutosheleza mahitaji yangu.
Lakini ilikuwa ni tofauti kabisa na vile nilivyotarajia kwa mke wangu kwani pindi aliponiona tu ndipo alizidi kukasirika. Nilifika pale nyumbani kisha nikachukua kiti na kuketi karibu pale alipo mke wangu, lakini yeye aliondoka pale alipokaa na kuingia ndani. Kiukweli aliniumiza akili sana kuwaza mke wangu anahitaji jambo gani zaidi na kibaya kipi nilichofanya.
Nilinyanyuka na kuelekea kule chumbani ndipo nilimkuta akiwa kajilaza kitandani hana hata hamu ya kuonana na mimi. Nilijiuliza mwanamke wa aina gani ambae hataki hata kunielewa, wanaume wengi huwa tunapata tabu sana kwa wake zetu pindi hali inapokuwa ngumu ya kimaisha inafikia hatua mwanamke anafanya vituko vya ajabu ili umzingue kama kumpiga apate sababu ya kuondokea kwako.
"We!..weweee!" Nilimshtua kwa kumshika mgongo wake ili apate kunisikiliza japo alikuwa kimya kama kobe aliyeonewa.
"Mke wangu....ebu! Kaa tuongee...!"
Niliendelea kumuamsha.
"....Aaah! Sitakiiiii wewe si kiburi sana siku hizi endelea...". Aliwaka kama kifuu na ikawa ngumu kumzima. Niliona ushenzi kabisa kama huu siupendelei kabisa.
Niliujua udhaifu wa mke wangu, pindi akinuna najua nini nimfanyie.
Nilinyanyuka ndipo nikaamua kumuita mtoto wangu mmoja aliyejulikana kwa jina la Asante. Mtoto huyu ni wa kwanza kabisa kuzaliwa na niliamua kumpatia jina hili kutokana na matatizo kadhaa ambayo yaliyotokea ndipo nikabahatika kwa kumpata mtoto huyo na ndipo niliona nimpatie jina la Asante. Nikimaanisha nikimshukuru mungu.
Nilimpa kiasi cha fedha kisha nikamuagiza akanunue mboga pamoja na mchele wa kutosha, kutokana na maisha ambayo tulikuwa tunaishi kununua kiasi kama kile cha mchele kiliweza kumshangaza sana Mama Asante.
Baada ya Muda alirejea kisha nikampatia mke wangu.
"Mama Asante, haya pika kwanza kisha tuongee vizuri hali tumeshashiba."
Alipokea japo kwa shingo upande akayafanya maandalizi tosha kwa ajili ya mapishi. Alipomaliza tulikula wote hapo ndipo niliona furaha ya mke wangu ikijitokeza mbele yangu. Nilimshika mkono na kumpeleka kitandani kisha nikamuangalia kama mara tatu.
Baada ya kumtazama ndipo nilipombusu na kumpa maneno mazuuri ya mapenzi. Hakika hakuna ambae nilikuwa nampenda kama mke wangu kwani tulikuwa tunapendana na kuhurumiana.
"Mke wangu, nakuomba uvumilie kazi ya Uvuvi nahisi ndio chaguo langu kutokana na uhaba wa elimu na uwezo tulio nao nakuomba ubariki kazi yangi hii ambayo inatupatia kila kitu.
Baada ya hapo ndipo tulikubaliana kuwa mimi niendelee kufanya kazi na yeye akawa ananibariki.
Siku hiyo mapema nilitoka nikiwa na furaha sana baada ya Mke wangu kukubali mimi kufanya kazi. Niliondoka hadi kwa bwana Kibona, bwana kibona nilimkuta anaandaa nyavu kwa ajili ya kazi. Nilimsaidia kufanya maandalizi hayo ili iwe rahisi kumaliza jioni tuondoke kwa ajili ya kazi.
Nilikuwa na furaha, nilifanya kazi huku nikitabasamu, nilifanya kwa morali mpaka bwana Kibona akanishangaa.
"Mnali kipi kinakufurahisha hivyo"
Aliniuliza swali.
"Mimi nafurahi kwa kuwa naenda kufanya kazi"
Niliweza kumjibu kwa kujiamini kabisa.
"Haya ila furaha yako iwe ya kheri japo kule hakutabiriki...ulishawahi kusikia stori au hadithi za bahari pamoja na huu mto pangani?"
Swali lake lilikuwa gumu kwa kiasi chake kwani eneo la pangani kwangu lilikuwa ni geni sana hivyo kauli yake ilinishitua kwa kiasi chake.
"Mh! Bwana kibona unajua kuwa wewe ndie mwenyeji mimi tangu niamie hapa nina muda wa mwaka mmoja tu! Sasa kuhusiana na mto huu pamoja na bahari hii hapana sifahamu kabisa."
Nilimueleza ukweli kwamba sifahamu chochote kuhusiana na yale maeneo.
"Haya! Ina sifa nyingi sana kwa miaka ya babu yangu akiwa anafanya kazi hizi aliweza kunihadithia kipindi ananifundisha njia za uvuvi, kuna ule wa kupata samaki wengi na kuna ule wa kupata samaki wachache".
Aliongea bwana Kibona.
"Mh! Natamani kujua hizo aina mbili za uvuvi na je? Sisi tunafanya uvuvi wa aina gani?"
Niliweza kumuuliza.
"Aaaaah! Ahsante kwa swali zuri sana, uvuvi wa kupata samaki wengi tunatumia nyavu zenye matundu madogo na kutumia mabaruti kwenda kupiga chini ya bahari kwenye mazalia ya samaki kisha tunawakusanya huku juu, hapa tunapata kila aina ya samaki wadogo kwa wakubwa. Pia wa kupata samaki wachache basi tunatumia nyavu kama hii tunapata samaki wakubwa tu kama unavyowaona wale wa jana".
Maelezo yake yalinishangaza sana. Jioni ilifika ndipo tukaingia ndani ya maji tukatega nyavu zetu kisha tukasubiria kuna wale ambao tuliwapata kwa Ndoano japo wachache sana, muda ulipowadia tulivuta nyavu mpaka ukingoni mwa bahari tulichambua lakini tulibahatika kupata samaki sita tu tofauti na siku zote. Tulifanya kazi ngumu yenye ujira mchache.
Kibona alinieleza mengi sana kuhusiana na ile hali kuwa niivumilie tu.
Ilipita kama Miezi mitatu sasa. Siku moja ya mwezi Nilikuwa Naumwa sana Kibona alikuja kuniangalia nahukuru. Ndipo alipotaka kuondoka kwenda mtoni.
"Sasa...nimesikia leo bahari imechafuka sana lakini nyumbani hakuna mboga wala fedha ya kula".
Aliniambia hayo huku akiwa ananishika mkono.
"Daaah! Bwana Kibona ni bora ukae nyumbani kama bahari imechafuka sio vyema kwenda huko kabisa".
Rafiki yangu aliniambia huku akinisisitiza kuwa lazima aende huko ili akapate chochote cha kula. Mimi sikuweza kumkataza kwa sababu yeye mzoefu pia ni maarufu.
Tuliachana pale mimi nikiwa kitandani. Nakumbuka siku hiyo ilikuwa ya Majonzi bwana Kibona kutomuona tena. Habari iliyosikika ni kuwa Kibona Kapotea Baharini hakika iliniuma sana......
TUKUTANE TOLEO LIJALO

No comments: