RIWAYA:: MAISHA YANGU YA UVUVI SEHEMU YA NANE 08
ENDELEA........
................Tuliendelea kutulia pale mpaka mida ambao dereva aliona kuwa unafaa ndipo akatugeukia sisi watatu sote. Kwanza mimi nilihisi kama ndoto kuwa kwenye yale mazingira kwani nikikumbuka umbali wa maisha nilioanzia nilitaka kukata tamaa kabisa lakini juhudi zangu niliamini kama zinanifanya kufika hadi maeneo niliyopo kwa sasa na maombi kwa Mwenyezimungu.
"Haya vijana mko watatu, Nani anataka kuwa dereva wa hili boti nimfundishe ili kazi yake iwe hiyo tu!"
Kila mmoja alikaa kimya kwa uwoga japo nafsi zinatusuta kwa kutaka kujua kile kisemwacho.
"Nauliza nani afunfishwe ili muanze kazi au kama hamtaki nimpigie simu Mr Paul". Hapo ndipo Jamaa mmoja aliyejulikana kwa jina la Manyota alinyoosha mkono huku akisema
"Mimi hapa nitakuwa dereva".
Akamuangalia kwa makini kisha akauliza "kwa hiyo nyinyi vipi hamtaki?".
"Hapana ila naamini akiwa huyo dereva sisi tutafanya kazi zingine" maneno hayo aliongea Jamaa aliyejulikana kwa jina la Musa. Mimi nilikaa kimya tu.
"Haya nyinyi wawili kaeni nyuma kisha wewe Manyota njoo karibu hapa uniangalie kisha nisikilize kipi nazungumza sawa?" Kila mmoja alielekea kule ambako aliambiwa mimi na Musa tulikaa nyuma na Yule Dereva pamoja na Manyota wakakaa mbele.
Waliyokuwa wanafundishana huko waliyafahamu wenyewe ila tuligundua tu jinsi chombo kilivyokuwa kinapelekwa Mrama tunaamini kuwa Mwanafunzi kashikilia mtambo na kikienda sawa basi mwalimu kashikilia usukani. Tulitumia masaa kama Manne kuzunguka fukwe yote na jmbali kidogo kutoka pale nchi kavu.
Muda ulipotimia ndipo tukarudishwa pale hotelini tuliwakuta wazungu wakipata chakula, jamani mimi sifichi elimu sikuwa nayo hivyo nilipita mbali na watu wale kwanza hata kukaa nao karibu sikupendi kikubwa zaidi lugha yao tu ilikuwa shida kwangu maana nilishazoea lugha ya mtaani pamoja na kiswahili.
Tulipelekwa juu lakini kila tulipokuwa tunakatiza walituangalia sana alafu walikuwa wanacheka hiko ndicho kilizidi niwachukie wazungu niliona kama dharau sijui walikuwa wanatuchukulia kama wachoma Mkaa sikuelewa kabisa.
Tulifika kwenye meza moja hivi ndipo ilikaa muda kidogo akaja muhudumu hapo ndipo kimbembe kilianza.
Wahenga wanasema kama hujui hujui tu na ni bora watu wajue kama hujui ila usijifanye unajua hali hujui na ukawafanya watu wewe kukuona unajua nasema utapata tabu sana. Hii ilitokea hapo. Muhudumu kafika akiwa na ile Menu ya chakula kabla ya kutupatia akauliza
"Samahani, nyinyi ndio vijana wa Mr Paul?" Tukaangaliana ndipo tukaitikia kwa kichwa kuashiria kuwa Ndio.
"Ok! Karibuni Menu ya chakula ni hii mtachagua chakula mkipendacho kisha nitawaletea". Kha! Nilijiuliza kitu ina maana hiko chakula tutakachoagiza analipa nani? Niliichungulia ile Menu Looh! Nikaona hainifai chakula kuanzia 5000/= Mh! Hiyo ndio bei ya chini nikawaachia wale Musa na Manyota wahangaike nayo niligundua kwa kuangalia bei ya vyakula japo sikufahamu ile lugha. Wakati wale wameshika ile Menu mimi nikamuita yule dada
"Dada samahani! Kwani kuna vyakula gani hapa vinapatikana?" Nilimuuliza
"Kaka unanishangaza Menu iliyotolewa pale ina idadi zote za vyakula ila kiufupi kila chakula unachokitaka kinapatikana". Nilijihisi aibu sana mbele ya yule dada maana kama nilizalilika "samahani mimi sijasoma kile kiingereza mlichoandika pale sijui mimi kama mfanyakazi mpya ambae nimeletwa hapa kuja kuanza kazi kama nyinyi".
"Ahaa! Basi subiri nichukue huduma kwa hawa wenzako alafu nitakuletea Menu yenye lugha ya kiswahili". Nilirudi nikitulia huku nikiwashangaa Musa na Manyota pindi wakiniambia mimi mshamba.
"Mnali unatuangusha sana unashindwa hata kujua kama hiki chakula gani, aaah! Ona mimi lile boti nimefundishwa sekunde kadhaa nimelielewa". Ndipo yule dada alipokuja na wenzake wawili wakileta chakula na yeye akanipatia ile Menyu ndipo nikachagua Wali nyama. Nilitamani Kucheka sana pindi majamaa hasa Manyota alipoletewa Mchuzi wenye nyama kama supu.
Baada ya kumaliza alikuja dada kisha Manyota akauliza "dada kwani supu ya nini ile maana ni tamu sana". Yule dada akatabasamu. "Hapa tuna supu aina nyingi kuanzia ya Mbuzi, Ng'ombe, Samaki, Nyoka na Chura". Tuliangaliana "Ehee na ile uliyoniletea?" Manyota akauliza "usiseme niliyokuletea sema niliyoagiza".
"Sawa ile niliyoagiza?"
"Ile pale ni vyakula vya watu wa kichina kama unavyoona hapa Chinese Food. Na yule ni Chura".
Jamaa ilibidi azuge tu. "Daaah! Kumbe hata chula mtamu mamaa nimekula Chula". Dada aliondoka huku tukibaki na kicheko cha ajabu. Ghafla alikuja Meneja wa ile Hotel ndipo akatuchukua na gari kutupeleka mahali fulani. Tulienda kukamilisha baadhi ya vitu ndipo tukakabidhiwa Rasmi usiku huo kuanza kuvua Samaki wakati huo Bosi akiandaa Boti mbili zije tugawane majukumu zaidi.
Tulilala palepale Mpaka majira ya saa sita usiku tukachomoka kuelekea Kwenye fukwe ili kuanza kazi.
Tulihakikisha Nyavu ziko sawa ndipo tukawasha taa ili kuwavutia samaki, tukatundika vyema ile Nyavu kisha tukaanza kusubiria huku tukitembea, ilifika Majira ya saa kumi Samaki hatukupata wengi walikuwa wanahesabika. "Jamani, mnaona sasa hakuna samaki na bosi anatarajia kuwa leo tumfurahishe inakuaje hapa?" Mimi niliwauliza swali.
"Aaaah! Na yeye pia binadamu anajua kuwa kuna kupata na kukosa leo sio bahati yetu kwa hiyo turudi maana najisikia uvivu hata kuendesha nimechoka".
Manyota kachoka alafu yeye ndie dereva sasa inakuaje Musa pia alikubaliana na Manyota. Ndipo tuliyoyoma taratibu tukiwa na samaki wetu kadhaa ambao ni kama aibu kabisa kuonyesha.
Kikubwa kilichonifanya niogope ni gharama alizotumia bwana Paul kwa kutuhudumia sisi na kutuahidi fedha nyingi sana. Tulipofika ufukweni Saa Kumi na Moja watu wanaokuja kununua samaki wanaanza kuingia pia nilijua kuwa Muda mfupi tu wale mabosi watakuja kuchukua mzigo. Niliwageukia wale wenzangu na kuwambia jambo.
"Oyaa! Sikieni tunatumia boti lenye Sauti kubwa kule linasababisha kelele mnaonaje tuchukue Mtumbwi hata dakika kadhaa tuongezee hawa?"
Kila mmoja alinicheka na alikuwa tayari kachoka kalala ndani ya hilo boti. Nilitoka kisha nikachukua Mtumbwi sikujua wa nani nikachukua wavu nikapiga kasia kuingia tena Majini.
Kilichotokea huko nyuma sifahamu. Nilitega kisha nikazubaa mpaka usingizi ulinikamata ghafla yalinichukua masaa mawili mpaka nashtuka mtumbwi unaelemewa, nashtuka naona nyavu imekamata Samaki nikajitahidi kuwavuta lakini nilishindwa. Mtoto wa Masikini furaha yangu kuona nafanikiwa mbona sasa napata shida?.
Nilijisemea mwenyewe mara upepo ulianza kuvuma ukawa unanisogeza taratibu nchi kavu huku nimeikusanya Neti na nikiwa makini kutoiachia mpaka nchi kavu nakuta gari likiwa lipo pale.
Walikuja kunisaidia hadi kuvusha nao daah! Nilimshukuru sana mungu kiasi cha samaki niliowapata niliona wanaridhisha kuliko wale wengine. Niliona ajabu naingizwa ndani ya gari na kuambiwa nibadilishe nguo nawakuta Musa na Manyota wakiwa wameninunia huku Manyota akisema tunaharibiana siku.......
TUKUTANE TOLEO LIJALO

No comments: