Wanaume wakwepa kuongozana na Wapenzi wao clinic
Na Amiri kilagalila, Njombe.
Hamasa kwa wanaume kuongozana na wenza wao wajawazito kliniki kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu afya ya uzazi na lishe imeendelea kusuasua halmashauri ya mji wa makambako mkoani Njombe kutokana na mwamko mdogo wa wananume.
Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Makambako Alexander Mchome amewataka wanaume kuhudhuria kliniki ili waweze kupata elimu ya uzazi pamoja na lishe bora kwa mama mjamzito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ili kuondoa tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto.
Afisa lishe wa halmashauri ya mji wa Makambako Rahel Magafu amesema mkoa wa Njombe unaongoza kitaifa kwa udumavu kwa asilimia 53.6 kutokana wazazi hususani wanaume kutowajibika ipasavyo katika malezi hivyo amewataka wazazi wote kushiriki kikamilifu katika malezi ili kuondokana na tatizo hilo.
Kwa upande wake mratibu wa afya shuleni Exaveria Mtega amesema serikali imejipanga kuhakikisha shule zote za halmashauri zinatoa chakula cha mchana chenye virutubisho huku wakiendelea kuwahimiza wazazi kuona umuhimu wa maziwa kutolewa shuleni ili kuondokana na utapiamlo pamoja na udumavu.
Aidha mkuu wa wilaya ya Njombe Ruti Msafiri amewataka wanaume kushiriki katika kulea ujauzito kwa kuzingatia lishe bora katika familia zao.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa halmashauri ya mji wa makambako akiwemo Augustino Yohana,Hongera Mgecha pamoja na Irene Msangi Wamesema kinachosababisha wanaume kushindwa kuwasindikiza wenza wao kliniki ni kukwepa majukumu yao ya kulea huku wengine wakisema baadhi yao wanahofu ya kupimwa VVU.
Pamoja na hayo Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Makambako Rashid Njozi amesema mikakati ya halmashauri katika kukabiliana na tatizo la udumavu wamedhamiria kuunda sheria ndogo ndogo ambazo zitawabana wanaume ambao watashindwa kuwapeleka wenza wao clinik ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini.
Mkoa wa Njombe Umeendelea kuwa kinara kitaifa kwa udumavu na utapiamlo kwa asilimia 53.6 ukifuatiwa na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini ambayo ni mkoa wa Rukwa yenye asilimia 47.9 pamoja na Songwe yenye asilimia 43.3.
No comments: