NYUMBA YA MAAJABU 01




Ilikuwa ni siku ya furaha sana walipohamia kwenye hii nyumba nzuri na ya kupendeza, tena iliyovutia katika macho ya watu wengi sana.
Mke alisikika akimuuliza mume wake,
“Ibra, uliwezaje kuwekeza pesa nyingi za kununua nyumba nzuri kama hii?”
“Mke wangu Sophia, kwakweli mambo ya Mungu ni mengi sana, hata mimi sikutegemea kupata nyumba kama hii kwa ile pesa ambayo nilikuwa nayo. Kwakweli tushukuru tu kwa kupata mwanga wa maisha”
“Nadhani sasa mipango yetu itatimia mpenzi”
“Ndio mke wangu kwa hapa lazima mipango itimie”
“Hivi tulipanga kuzaa watoto wangapi vile?”
“Watatu tu wanatosha mke wangu”
“Baby kwa jinsi nyumba ilivyokubwa kwanini tusifanye wanne!”
“Wewe ndio mzaaji mke wangu kwahiyo vyovyote tu inawezekana”
Sophia akakumbatiana na mume wake kwa furaha kwani hii ilikuwa ni moja ya ndoto zake kwenye maisha.

Baada ya wiki moja, Sophia aliamua kwenda kuwatembelea majirani zake wa sehemu aliyokuwa akiishi mwanzoni. Alifika na kuwakuta wakiendelea na shughuli za hapa na pale kama kawaida, moja kwa moja aliamua kwenda kwa rafiki yake wa pekee Siwema ambapo alikaribishwa vizuri sana na rafiki yake huyo.
“Yani Sophia kama usingekuja kunisalimia kwakweli ningekuona ni mtu wa ajabu sana.”
“Hivi Siwema naachaje kuja kukusalimia wewe! Nitakuwa nimerogwa basi, tena nitakuwa ni binadamu asiye na wema wala shukrani”
“Eeh hebu kwanza niambie shoga yangu mmehamia wapi maana si kwa mbwembwe zile za kuondoka hadi vigoda vyako umeacha”
“Shoga mwenzangu, yani wewe ni shoga yangu wa damu kwakweli na kukuficha siwezi. Kwakweli mwenzio nadhani kuna vitu Ibra alikuwa ananificha”
“Kivipi? Na vitu gani hivyo alivyokuwa anakuficha?”
“Hivi unaweza kuamini kwamba Ibra amenunua nyumba na gari!”
“Mmh kwa hela gani? Katoa wapi hiyo pesa ya kununua nyumba na gari?”
“Tena ninavyokwambia nyumba ni nyumba haswa shoga yangu wala sio nyumba uchwara, nitakupeleka na wewe ukajishangalie maajabu ya mume wangu Ibra”
“Mmmh kwahiyo shoga biashara ya mamantilie hufanyi tena?”
“Naanzaje kufanya biashara ya mama ntilie kwenye nyumba ile! Shoga hujaiona na wala sijisifii tu, kwakweli Ibra ana pesa, mpango wangu kwasasa ni kuzaa tu nicheze na wanangu pale maana nikichelewa nitakuta mwana si wangu”
“Shoga tusiandikie mate wakati wino upo, ujue umenitamanisha sana, naomba twende sasa hivi na mimi nikajishuhudie huo mjengo. Ngoja nijiandae fasta twende.”
Sophia akakubaliana na Siwema pale kwahiyo akamsubiri ajiandae ili aweze kwenda nae.

Siwema na Sophia walifika kwenye nyumba husika ambapo nje tu ya nyumba hiyo Siwema alibaki kushangaa na kuduwaa kwani hakutegemea kama ile nyumba ipo vile kama alivyoikuta.
“Khee jamani Sophia mbona umeokota dodo kwenye muharobaini shoga yangu, hebu jibebeshe mimba mapemaa maana hapa utashangaa ushaibiwa shoga yangu”
“Yani hapa ninachotaka ni kuzaa tu, yani toka nimeuona huu mjengo na dawa za uzazi wa mpango nikaziacha pale pale saivi nawaza watoto wa kucheza nae kwenye nyumba hii”
“Hongera sana shoga yangu ila kuwa makini na Ibra maana asije akakuletea mke mwenza bure”
“Thubutuu huyo mke mwenza atapitia mlango gani!! Labda sio Sophia niliyepo humu ndani”
“Nakuaminia Sophia, kama uliweza kumchunga Ibra kule uswahilini ndio ushindwe kumchunga kwenye huu mjengo”
“Hapo sasa, yani hapa Ibra hazungushi amefika hapa Kigoma mwisho wa reli”
Sophia alikuwa akifurahi tu na shoga yake huyu, na leo walipika pamoja na kula pamoja hadi joini ambapo mume wa Sophia aliwasili kutoka kwenye mihangaiko yake ambapo alimkuta Siwema pale kasha Siwema akawapa hongera zao na kuwaaga.
“Hongera sana shemeji yangu Ibra, ila mimi ndio naomdoka shemeji”
“Mmh shemeji jamani ndio haraka haraka hivyo!”
“Shemeji nilikuwepo hapa tangu muda ila nitakuja tena maana ndio nishapapenda tayari ila saizi wacha niende”
Basi Ibra hakuwa na jinsi yoyote zaidi ya kumuaga tu huyu Siwema.
Kisha Sophia akatoka na kwenda kumsindikiza rafiki yake huyu,
“Kwakweli Sophia usizembee, pale ndio umshikirie vizuri Ibra yani umgande kama ruba maana ule mjengo si mchezo shoga yangu. Yani wambea wa mtaa watanikoma nitakavyokuwa najidai kuhusu wewe Sophy.”
Sophia akacheka tu kwani alikuwa akifurahia kile alichokuwa akiambiwa na Siwema.
“Usicheke tu Sophy ila yafanyie kazi maneno yangu”
“Ondoa shaka dada, mambo yataiva tu maana hata mimi nimetamani kuwa na watoto kwasasa”
Wakabadilishana mawazo pale kasha Siwema akapanda daladala na kuagana vyema huku Sophia akisisitiza kuwa awasalimie majirani zao wengine.

Sophy alirudi nyumbani kwake, kwavile giza nalo lilianza kuingia ikabidi aandae chakula cha usiku, na kilipokuwa tayari alikaa na mumewe na kuanza kula huku wakitabasamu.
“Mmmh Sophy muda wote unatabasamu tu mke wangu”
“Hivi naachaje kutabasamu Ibra!! Bahati tuliyoipata ni kubwa sana mume wangu kwakweli sikutegemea kama ipo siku tutaishi kwenye nyumba nzuri na kubwa kama hii, si unajua tulizoea chumba kimoja tu yani jiko hapo hapo, viti, vyombo, kitanda hapo hapo yani shaghalabhagala lakini sasa hivi eti tunaishi maisha ya kitajiri namna hii lazima nitabasamu mume wangu.”
Wakamaliza kula kisha Sophy akatoa vile vyombo na kuvipeleka jikoni huku akitaka kuviosha kwanza ndimbo aende kulala na mumewe, ila Ibra alimfata kule jikoni na kumwambia,
“Sophy mke wangu, vyombo utaviosha kesho bhana hebu twende tukalale”
Sophy akatabasamu kisha akaacha vile vyombo na kuongozana na mumewe hadi chumbani ambako muda mwingi walionekana wakitabasamu.
Kisha wakaenda kuoga pamoja na kurudi kitandani, Ibra alimkumbatia Sophy na kumuuliza tena,
“Hivi ulisema tuzae watoto wangapi vile?”
“Wanne mume wangu au wewe hupendi”
“Mmmh hakuna kitu ambacho unakipenda wewe halafu mimi nisikipende, si unajua jinsi nikupendavyo Sophy! Yani mimi na wewe letu ni moja mke wangu”
“Tena napenda wawili wawe wa kike halafu wawili wa kiume”
“Wow ni mpango mzuri sana hakuna tatizo, tutazaa kadri Mungu atakavyo tujaalia Sophy wangu.”
Wakatabasamu kisha wakalala kama kawaida.
Kulipokucha, kama ilivyoada Ibra aliamka mapema sana kisha akajiandaa kwaajili ya kwenda kwenye kazi zake, Sophy alitaka kujaribu kuinuka ili kumuandalia mambo mbalimbali mumewe ila ibra alimzuia na kumtaka mkewe aendelee kupumzika tu ambapo naye alifanya hivyo kwani alielewa ni jinsi gani Ibra alimpenda.
Kwenye mida ya saa mbili asubuhi, Sophy nae aliamka na kwenda kuoga ili kujiandaa kwa mambo ya hapa na pale.
Akaenda jikoni kwa lengo la kutaka kuosha vyombo vya jana na kujiandalia chakula cha asubuhi, ila alishangaa kuona vyombo vilishaoshwa na vilipangwa vizuri kabatini.
Hali hii ikamfanya Sophia ajiulize kuwa huenda Ibra alimzuia kuamka muda ule ili afanye kile kitu cha kumsahangaza. Kwakweli Sophia alitabasamu kwa jambo hili kwani aliweza kuona ni jinsi gani Ibra anampenda sana.
“Najua Ibra ananipenda sana ila safari hii kazidisha mapenzi jamani mmh yani amefikia hatua hata ya kunitaka mimi nilale halafu yeye akaosha vyombo, haya ni mahaba tena motomoto kwakweli nina kila sababu ya kumzalia watoto Ibra wangu. Kipindi kile nilikuwa najibana kuzaa sababu ya maisha duni ila kwasasa nina kila sababu ya kuzaa kwakweli.”
Kisha akajiandalia chakula pale na kuanza kukila halafu naye akatoka kwa lengo la kwenda kwenye mihangaiko yake mbalimbali.

Wakati yupo nje ya nyumba hiyo kuna mmama alipita na kumsalimia Sophia kisha Yule mama akamuuliza Sophia kama ndiye anayeishi mule ndani,
“Unaishi humo ndani dada?”
“Ndio mama”
Sophia akahisi kuwa huyu mama labda anamuona kuwa haendani na hiyo nyumba, ikabidi amuulize
“Kwani vipi mama yangu! Kuna tatizo?”
“Hapana ila sisi ni majirani kwahiyo ni vyema tukafahamiana, mimi naitwa mama Jane na wewe je?”
“Mimi naitwa Sophia, na hapa naishi na mume wangu yeye anaitwa Ibra”
“Basi ni vizuri, karibu kwangu nyumba ya jirani tu hapo”
“Asante nitakaribia”
“Karibu sana, usiogope kitu sisi ni majirani tu na ni vyema kufahamiana ingawa kufahamu watu waishio humo huwa ni ngumu sana”
“Usijali utatufahamu tu”
Kisha Sophia akaagana na huyu mama halafu yeye kuendelea na safari zake.

Jioni ya siku hiyo Sophia akiwa ndani na mumewe akamsimulia kuhusu huyo mama aliyekutana nae wakati anatoka na vile alivyozungumza nae,
“Kwa kweli ni vizuri kufahamiana na majirani ukizingatia takea tumefika hapa hakuna jirani tuliyemsogelea kumsalimia”
“Basi tutafanya hivyo mume wangu. Ila kitu kingine sasa mmmhh”
Sophy akatabasamu kwanza kabla ya kuongea na kumfanya Ibra amuulize,
“Kitu gani hiki mpaka umeguna Sophy?”
“Mmh naona mapenzi yamenoga mume wangu hadi leo umeosha vyombo!”
Ibra akacheka kisha akasema,
“Mmh acha kunichekesha Sophy yani na uvivu huu mimi nikaoshe vyombo kweli!!”
“Sasa nani kaviosha vile vyombo asubuhi?”
“Nikuulize wewe uliyebaki nyumbani”
Sophia akakaa kimya kwa muda kwanza kwani hakuelewa hapo.

Itaendelea……………………!!!




No comments: