NYUMBA YA MAAJABU




                     

Sophia akakaa kimya kwa muda kwanza kwani hakuelewa hapo.
*TUENDELEE...*

Akamuangalia mumewe kama kwamba amwambie kuwa alichokuwa anakisema kilikuwa ni utani tu kisha akamwambia tena,
“Acha masikhara Ibra”
“Wewe ndio uache masikhara, unajua fika kuwa mimi ni mvivu wa kimataifa haya sasa huko kukosha vyombo ningeanzia wapi? Hebu kaandae chakula tule kwanza”
“Lakini Ibra….”
“Lakini nini Sophy? Wewe kaandae chakula tule bhana, mada nyengine achana nazo usifikirie ni rahisi hivyo mimi kuosha vyombo”
Sophia akaenda jikoni huku akiwa na mawazo sana ila kuna wakati alihisi kuwa Ibra anatania tu kwani kule ndani walikuwa wao wawili tu kwa hivyo akahisi kuwa ni lazima Ibra ndio aliosha hivyo vyombo ila anajigelesha tu, alijiaminisha hivyo huku upande mwingine akiwa na mashaka kiasi.
“Kesho nitampigia simu Da’ Siwema nimsimulie, Yule ni mtu mzima anaelewa vizuri sana”
Kisha akaendelea na uandaaji wake wa chakula cha usiku.
Akapeleka mezani na kuanza kula na mumewe Ibra,
“Yani leo nimechoka Sophy maana nimejikuta nikiwa na kazi nyingi sana”
“Pole mume wangu ila ndio ukubwa huo”
“Kweli kabisa ukubwa jaa maana sio kwa kuchoka huku”
Walipomaliza kula, leo Sophia hakutaka kuacha vyombo vichafu kwa hivyo alikwenda kuvikosha na kuvipanga kisha kwenda chumbani kulala na mume wake ambapo alimkuta ameshalala tayari.
“Mmmh kweli leo Ibra kachoka jamani maana yupo hoi kabisa”
Kisha na yeye akatafuta usingizi pale na kulala, alipopitiwa na usingizi tu akajiwa na ndoto.
Kwenye ndoto hii alijiona yeye akiwa mjamzito ila mumewe alionekana kutokuifurahia kabisa ile mimba na alionekana kuongea maneno machafu sana ya kumkaripia,
“Aliyekwambia ubebe mimba nani? Na utaenda kuzalia kwake huyo mtu, sitaki ujinga mimi”
Sophia akashtuka sana kutoka kwenye ule usingizi huku akiilaani ile ndoto na kuona kuwa ni kitu cha ajabu sana kwake kwani haikuwa rahisi kwa Ibra kuikana mimba yake kiasi hicho ila ndoto hiyo ilimfanya asipatwe na usingizi tena hadi panakucha.
Ibra alipoamka tu, Sophy nae alikuwa macho na swali la kwanza ambalo Sophy alimuuliza Ibra ilikuwa ni kuhusu mimba.
“Hivi kwa mfano mimi nikiwa na mimba yako je utafurahi mume wangu?”
“Sophy, ninavyokupenda hivi naachaje kufurahi? Pia nahitaji mtoto Sophy wangu, na mimi napenda niitwe baba. Nakupenda sana mke wangu, najua watoto ndio watakamilisha furaha yetu mpenzi.”
“Asante Ibra”
Kisha Ibra akaanza kujiandaa pale halafu akamuaga Sophy kwa kumbusu kwenye paji la uso.
Ibra alipoondoka tu, Sophy nae akaamka na kwenda kukaa sebleni ili kujipotezea mawazo mbalimbali huku akiona wazi kuwa ile ndoto ni uchizi tu na ni kitu cha kusadikika.
“Ndoto nyengine kama zimetumwa loh! Ndoto gani sasa ile? Yani Ibra kabisa akane mimba thubutuu, yani ile ndoto ishindwe na ilegee ujinga ujinga sitaki.”
Muda ulipoenda kidogo akampigia simu Siwema na kuanza kuzungumza naye kuhusu kilichotokea jana na vile ambavyo Ibra alimjibu kuwa hakuosha hivyo vyombo.
“Hayo ndio mahaba mdogo wangu, mwenzako Ibra anakupima tu lakini vyombo kaosha mwenyewe, we unadhani ataosha nani wakati ndani mpo wawili tu?”
“Ndio hapo dada nimeshindwa kuelewa kwakweli maana mimi nimekuta vimeoshwa halafu ni yeye aliyesema nisivioshe halafu anakataa kuwa hajaviosha loh!”
“Anakuchanganya akili tu huyo mdogo wangu, kwani wanaume hujawajua tu, wanapenda kutupima Sophy mdogo wangu. Hata usiwe na shaka mwaya mwenzio saivi anakuonyesha mahaba kimya kimya”
“Kweli dada haya ni mahaba maana ila hapendi kuosha vyombo, hata niumwe ataviacha hadi nipone ila kuona ameosha safari hii tena nikiwa mzima kabisa kweli ni mahaba”
“Ndio mapenzi hayo mdogo wangu hata usistaajabu sana, hapo ndio kupendwa yani wewe jiongeze tu.”
Sophia akafurahia sana ushauri aliopewa na Siwema kwani aliona ushauri huo ukimfaa sana, kisha akaagana nae kwenye simu na kuendelea na mambo mengine.
Wakati akifanya shughuli zake za hapa na pale mule ndani, akasikia hodi na kwenda kufungua mlango ambapo alimkuta Yule mama ambaye walikutana siku ya nyuma huku akiwa ameambatana na binti aliyeonekana kufanana nae sana, Sophia akawakaribisha vizuri sana watu hao ndani kwako huku akitabasamu,
“Karibuni sana jamani”
“Asante tumekaribia Sophy”
Wakaingia ndani huku Yule mama akianza utambulisho kwa binti aliyeongozana nae,
“Huyu ni binti yangu anaitwa Jane”
“Wow ndio mana umefanana nae sana mama, hongera kwa kuwa na binti mzuri”
Huyu mama akatabasamu kidogo kisha akaendelea,
“Nimeona ni vyema akufahamu jirani yetu ili hata siku akiwa mbweke nyumbani basi aje akutembelee, unajua huyu mtoto ametoka kumaliza kidato cha nne kwa hivyo tunangoja matokeo tu kwa sasa. Mara nyingi anashinda nyumbani kwa hivyo akija kuongea ongea hapa si vibaya.”
“Umefanya jambo jema mama maana hata mimi huwa na upweke sana maana huwa nashinda mwenyewe mahali hapa, pia hongera sana Jane kwa kuhitimu kidato cha nne.”
“Unampa hongera ya bure tu huyu, akili yake yenyewe sijui kama atafaulu huo mtihani, na akifeli ndio atakaa nyumbani atafute mume aolewe tu”
“Jamani mama usiseme hivyo inakuwa kama unamuombea mabaya mtoto”
“Mabaya kajiombea mwenyewe hata sio mimi, mtu gani alikuwa anajijua kabisa kuwa ana mitihani ila ndio tamthilia sijui michezo kila kitu anakijua yeye na hatma yake inakuja kwabkweli naona kabisa zero ikimuangalia.”
Jane alionekana kuwa kimya kabisa kwani ilionyesha wazi hakupendezewa na maneno ya mama yake, ili kuondoa ule mzozo ilibidi Sophia abadilishe mada kisha akaenda jikoni na kuwaletea wageni juisi huku wakizungumza mawili matatu.
Muda kidogo Ibra alirudi hata kumshangaza Sophia kwani alionekana kuwahi sana siku hiyo na alionekana kuwa na uchovu.
Sophia akamkaribisha mumewe na kumtambulisha kwa wale wageni ambao walifahamiana na kusalimiana, ingawa Ibra alikuwa amechoka ila alivunga kidogo kwenda chumbani ili wale wageni wasijihisi vibaya, ila huyu mama nae aliaga muda ule ule kwahiyo Sophia akatoa zile glass na kupeleka jikoni kisha akamuaga mumewe na kwenda kuwasindikiza wale wageni, ambapo Sophia alienda nao hadi nyumbani kwao ili kuweza kupafahamu wanapoishi watu hao.
Sophia aliweza kuona mazingira ya uswahili anayoishi huyu mama ila hakushangaa sana kwa vile ndio mazingira ambayo hata yeye amekulia na ameyaishi kwa kipindi kirefu sana.
“Sophia, ukiwa na tatizo usisiste kuja, hapa ni kama nyumbani kwenu tu kwahiyo usiogope chochote”
“Usijali mama tupo pamoja”
Sophia hakukawia sana kwani aliaga na kuondoka.
Aliporudi nyumbani kwake hakumkuta Ibra pale sebleni na moja kwa moja akahisi kuwa Ibra atakuwa amekwenda chumbani kupumzika tu, kisha nae akenda chumbani alipo Ibra kwani alipenda kujua kwanini mumewe amechoka kiasi kile.
Alimkuta Ibra amejilaza kitandani, akamfata na kumsogelea karibu mumewe kisha akakaa pembeni yake na kumuuliza kuwa tatizo ni nini,
“Vipi tena Ibra mume wangu, nini kimekukumba?”
“Kwa kweli hata sielewi ila nimechoka mwili na viungo vyote”
“Pole sana mume wangu, ngoja nikuandalie chakula ule kwanza ndipo ulale”
“Usijali kuhusu hilo, nimekwenda jikoni nimepakua chakula na nimekula tayari”
“Dah nisamehe mume wangu jamani”
“Usijali kitu mke wangu, wale ni wageni wetu sote kwa hivyo hata usijali na ndiomana hata mimi sikuona tatizo kwenda jikoni na kujipakulia chakula”
“Pole sana mume wangu, basi ngoja nikakuandalie maji uoge”
“Kwakweli sijisikii kuoga kwasasa subiri nipumzike kwanza ndio nitaoga”
Sophia alitulia kwa muda akiitafakari hali ya mume wake kwani haikuwa kawaida kabisa kwa Ibra kuwa vile alivyokuwa.
Alikwenda sebleni huku akihisi kuwa huenda Ibra akawa na malaria ila ndio hivyo anajikaza kwavile ni mwanamme, kisha akaelekea jikoni na kufunua sufuria alilopikia chakula na kukuta kweli kilipakuliwa kwa maana hiyo ni kweli Ibra amekula kile chakula kisha akaangalia Ibra alipoweka sahani aliyotoka kula nayo ila hakuona sahani wala nini hapo ndipo aliposhangaa na kwenda tena sebleni kuwa huenda ameiacha huko ila hakuona sahani yoyote chafu, wazo likamjia kuwa aangalie na zile glasi ambazo wageni wamenywea juisi ila hakuziona pale zaidi aliziona zimeshawekwa kabatini tena zikiwa safi kabisa,
“Mmh huyu Ibra si anaumwa huyu sasa iweje ameosha vyombo vyake alivyolia na zile sahani jamani wakati mtu ni mgonjwa? Haya ni maajabu mapya kwangu, sasa nitamuulizaje na anaumwa? Ila lazima nimuulize?”
Sophia akatoka jikoni na kuelekea chumbani tena alipo Ibra kwa lengo la kumuuliza kulikoni maana hakuelewa kabisa.
Alimkuta Ibra akiwa bado anagalagala tu kitandani kwani hata usingizi haukumjia, kisha akamuuliza,
“Mume wangu leo umechoka sana ila kwanini umeosha vyombo ulivyolia chakula?”
“Sophy, toka lini hunijui mimi jamani! Mimi naoshaje vyombo mke wangu, kwanza naumwa halafu wewe unaniletea habari nyengine l kwanini unakuwa hivyo Sophy?”
“Samahani mume wangu ila ningependa twende hospitali”
“Sijisikii kwenda hospitali kwakweli, tafadhali niache nipumzike”
Sophia hakumuelewa Ibra kabisa na akahisi huenda Ibra ana malaria ambayo imempanda kichwani na ndiomana amekuwa vile alivyokuwa.
Sophia aliamua kuinuka tena ili atoke mule chumbani ila kabla hajafika mlangoni alijihisi kichefuchefu na kumfanya aanze kukimbilia chooni ili atapike ila kabla hajafika chooni alijikuta kashatapika tayari kwahiyo chooni alienda kama kumalizia tu na alitoka akiwa amechoka sana ila hakuweza kuvumilia kuangalia yale matapishi yake yaliyotapakaa chumbani kwao karibia na mlangoni wa chooni, hivyobasi Sophia akaenda jikoni kuchukua tambara na maji kwa lengo la kufuta matapishi yale.
Ila aliporudi chumbani ili afute alikuta yale matapishi yalishafutwa na pale palishakaushwa kabisa, kwakweli Sophia alichoka gafla, akamuangalia Ibra pale kitandani ila Ibra alionyesha kutokuwa na habari yoyote kwani alikuwa amejilaza vile vile.

Mwisho wa sehemu ya 2.

ITAENDELEA..................!!!




No comments: