NYUMBA YA MAAJABU 10



               
“Huu mti wa mpera si mzuri”
“Kwanini?”
“Huwezi kupata pera hata moja hapo kwavile huu mti umechezewa sana”
“Khee unaujua huu mti wewe?”
Huyu bibi akacheka kidogo na kusema,
“Naujua sana huu mti, hata nyumba yako naijua”
Sophia alimshangaa na kumuuliza,
“Nyumba yangu unaijua kivipi?”
“Nyumba yako ni ya maajabu”
Sophia akashtuka na kuzidi kumshangaa huyu bibi.
*TUENDELEE....*

Kisha akamuuliza kwa mshangao
“Nyumba yangu ya maajabu kivipi”
Mara Siwema akamuita Sophia ambapo Sophia alimtazama Yule bibi na kwenda alipoitwa na Siwema, kisha Siwema akamwambia Sophia
“Yani unapoteza muda wako kabisa unaongea na Yule bibi!”
“Kwani ana tatizo gani dada?”
“Yule bibi ni mwanga yani kashindikana nakwambia, ni mchawi hakuna mfano. Unavyomuona hakuna hata mtu mmoja anayezungumza nae mtaani kwake yani Yule bibi hafai tena hafai kabisa kabisa”
“Alikuwa ananiambia eti nyumba yangu ni ya maajabu”
“Mmh usimsikilize kabisa, alikuwa anajaribu kukuteka tu kwakweli Yule bibi hafai mdogo wangu”
“Halafu kasema eti ule mpera wako umechezewa sana na kamwe hauwezi kuzaa mapera”
“Sophy, achana na Yule bibi yani kuhusu huo mpera ndio kauandama balaa achana nae kabisa. Tena bahati yako hajagundua kuwa una mimba maana hakawii kuvuruga mimba za watu Yule.”
“Mmh dada tuondoke asije akaniletea makubwa bure, nampenda mwanangu”
Kisha wakatoka pale na kuanza safari yao ya kuelekea kwa mtaalamu.

Walifika kwa mtaalamu na kukuta watu wengi sana wakisubiri kuingia humo, ikabidi wapange foleni na wao ili zamu yao ikifika waweze kuingia. Kwa upande wa Sophia hii ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kwenda kwa mganga wa kienyeji kwahiyo ile hali aliishangaa sana,
“Kheee kumbe ndio kunakuwa na watu wengi hivi!”
“Na hapa bado, ndiomana jana nikakataa na kukwambia kuwa muda umekwenda sana maana nilijua lazima tungekuta foleni kubwa zaidi”
“Mmh! Kwahiyo waganga wote ninaowasikia ndio huwa wanajaza watu hivi?”
“Hapana si wote, mara nyingi watu hujaa kwa wataalamu wa ukweli maana mtu unakuwa umeona mafanikio na kuwaambia wengine, ila kwa upande wa wale matapeli hata hawanaga watu wengi kivile wanadanganya sana na watu wamewashtukia hawaendi”
“Mmh yani sijawahi kwenda kwa waganga mie kwakweli Yule Jane kaninyoosha”
“Mama yenu nae hajawahi kweli? Maana mi mama yangu ndio kanifundisha haya mambo, yeye sasa ni kitu kidogo tu anaenda kwa mganga. Kwani Jane umeonana nae tena?”
“Tena ngoja nikusimulie kisanga cha jana”
Sophia akaanza kumueleza Siwema yale yaliyotokea jana waliporudi nyumbani kwao na kumkuta Jane ndani ilihali walifunga milango wakati wa kutoka hadi kuhusu kuyeyuka kwa zile chips.
“Kheee huyo mtoto mbona mchawi kiasi hicho! Hadi namchukia kabla sijamuona jamani loh, yani milango ulifunga sasa ndani kaingiaje? Na hizo chips uwiiii huyo mtoto ni wa kumuogopa kama ukoma. Tena ikiwezekana tumuombe mtaalamu atupe dawa ya kummaliza kabisa huyo binti maana si kwa uchawi huo jamani.”
“Ndio hivyo yani toka nimfahamu mambo ya ajabu nayo yanaongezeka jamani, nilikuwa siamini mambo ya uchawi ila Yule mtoto kaninyoosha. Alikuja na gia ya kunisimulia stori zake za kutisha hadi nikaanza kuiogopa nyumba yangu kumbe ana malengo yake.”
“Huyo mtoto ni wa kumuepuka kabisa yani tukipata dawa ya kummaliza nitashukuru sana”
Muda wao ukafika na kuwafanya waingie kwa mtaalamu ambaye aliwapokea kwa kicheko na kuwafanya wawe kimya kimshangao, ambapo muda kidogo mtaalamu akaanza kuwaambia,
“Tatizo lenu nalijua, mmekuja kwasababu ya binti mmoja anayewasumbua akili zenu anaitwa Jane”
Kwakweli Sophia alishangaa sana jinsi huyu mganga alivyoweza kugundua tatizo lao kwa urahisi kiasi kile, kisha Siwema akamwambia mganga
“Yani huyo binti anatutesa sana babu tafadhali utusaidie”
“Mnataka tumfanye nini?”
“Naomba tummalize kabisa maana hata hatutaki kumuona machoni petu babu, tafadhali tusaidie”
“Basi mimi nitawapatia dawa ya kuweza kummaliza na hatoonekana tena mbele yenu”
“Asante babu”
Basi Yule mganga akachukua unga unga na kuufunga kwenye karatasi vizuri kabisa kisha akawapa huku akiwaambia masharti ya ile dawa,
“Dawa hii mnatakiwa kumkaribisha Jane nyumbani kwenu, ukiona anakaribia kuja unainyunyuzia mlangoni. Kisha akija ataingia ndani, halafu nenda kamchukulie kinywaji chochote juisi, soda au maji muwekee hiyo dawa mpelekee anywe yani akinywa tu kwisha habari yake hamtasikia cha Jane wala ujinga gani”
Sophia akaguna kidogo,
“Mmh nitawezaje kumshawishi Jane aje nyumbani wakati jana nilimtimua?”
Yule mganga akatoa jani dogo kisha akampa Sophia na kumwambia,
“Chukua jani hili, ukiwa unaenda huko alipo Jane litafune halafu ukifika zungumza nae aje nyumbani hawezi kukataa hata kidogo maana jani hili huwa linawavuta wachawi, halafu akija unafanya hiyo dawa kisha mchezo unaisha”
Sophia akachukua lile jani na kuona sasa kazi itakuwa rahisi sana katika kumshawishi Jane ili akampatie dawa ya kummaliza kabisa.
Kisha wakaweka pesa na kuondoka kwenye kile kijumba cha mganga, kwakweli Sophia alifurahi sana na kujikuta akipanga mipango ya kummaliza Jane wakati mumewe hayupo.
“Yani dada nitahakikisha kesho naikamilisha hii kazi ila sitaki Ibra agundue maana anavyojifanya anahuruma na Yule binti balaa tupu”
“Ibra nae ndiomana mwisho wa siku yanamtokea puani jamani maana anatetea hadi maradhi mmh!”
“Ila dada inamaana atafia nyumbani kwangu?”
“Mi nadhani akishakunywa tu mtimue arudi kwao maana nahisi atakaa kaa hata dakika tano ndio afe kwahiyo wewe mtimue arudi kwao.”
“Basi nitafanya hivyo dada yani simpendi Yule binti balaa, amenifika hapaa kwakweli simpendi jamani dah”
“Unahaki ya kutokumpenda kwakweli maana hakuna mtu nayewapenda wachawi kwa maisha yao ukizingatia wanatutesa sana”
Safari yao sasa ilikuwa ni kurudi nyumbani kwa Siwema ambapo Sophia aliona ni vyema akamsubirie mumewe huko.

Leo Ibra aliwahi kutoka kwenye shughuli zake ila alipoenda kwa Siwema ili akamchukue mkewe hakuwakuta wote wawili na kufanya aondoke tena ili akazunguke zunguke kidogo huku akipanga kurudi tena badae.
Ila akapata wazo la kwenda kumuangalia Jane nae anaendeleaje maana hakujua hali yake tangu ile jana walipomuacha pale kwao, moja kwa moja Ibra akaelekea nyumbani kwakina Jane na ikawa vyema kwani alimkuta Jane akiwa nje amepumzika tu.
Ibra alienda pale alipo Jane na kumsalimia kisha kumpa pole kwa kilichotokea na kuanza kumuuliza kuwa anaendeleaje.
“Vipi hali yako lakini Jane”
“Niko safi tu, naendelea vizuri”
“Vipi lakini dawa unatumia?”
“Ndio natumia dawa vizuri tu”
“Pole sana yani kwakweli jana dah hata mimi sielewi elewi vizuri kwakweli, kwani ulipofika nyumbani jana ilikuwaje hadi ukaingia ndani?”
“Mimi nilivyofika jana nilikuta geti likowazi nikaingia na kulirudishia kidogo kwani nilijua dada amesahau kufunga kama kawaida yake ya kusahau. Nilipofika mlangoni nikagonga ila sikufunguliwa, nikajaribu kufungua mlango nikakuta uko wazi na kufanya niingie ndani ila nilimuita dada bila ya kuitikiwa ila kwa haraka haraka nikahisi labda dada amekwenda sokoni na kusahau kufunga milango kwahiyo nikakaa kumsubiri. Ila sielewi ilikuwaje maana nilipatwa na usingizi mzito sana hadi nyie ndio mmenishtua halafu nilikuwa na maruwe ruwe ya usingizi na kuhisi labda pamevamiwa ndiomana nikaanza kupiga kelele za mwizi”
Maelezo haya ya Jane yalimfanya Ibra awe na mawazo kiasi kwani hakuelewa kuwa ilikuwaje Jane akute mlango wao uko wazi wakati walifunga.
“Kwanza kabisa Jane usitufikirie vibaya maana asubuhi tulivyoondoka milango ilifungwa kabisa na mke wangu ndiomana tuliporudi jioni alipatwa na mshangao sana kuwa wewe umeingiaje ndani”
“Sasa kama milango, mlifunga unafikiri mimi ningeingiaje ndani? Inawezekana mkeo alisahau kama kawaida yake na kufikiri kuwa alifunga”
Ikabidi Ibra ajivunge hapo hapo kwani alijua wazi aking’ang’ania kauli yake ya kusema milango walifunga wakati huyu Jane kasema alikuta wazi atakuwa fika anamkandamiza huyu Jane kwa kumuhisi vibaya.
“Kweli bhana Jane, inawezekana kabisa ni mke wangu aliyesahau kufunga na kudai kuwa alifunga maana mke wangu ni msahaulifu sana ila tafadhali naomba unisamehe mimi Jane”
“Nimekusamehe ila kwa stahili hii nahisi siku moja nitatolewa roho na mke wako kwa matatizo yake ya kusahau. Mi nadhani ni vyema kama nisije kwenu tena”
“Hapana Jane, wewe ndio faraja ya mke wangu ila hujui tu. Tafadhali usitufanyie hivyo.”
Ibra akajaribu kumbembeleza Jane ili asijione vibaya kuwa anachukiwa na mkewe kwani bila kufanya hivyo alijua ni rahisi sana kwa Jane kugundua kuwa Sophia ana chuki za wazi sana juu yake. Kisha Ibra akaaga na kuondoka zake kuelekea kwa Siwema sasa.

Alipofika kwa Siwema aliwakuta nao ndio wamerudi muda huo huo ila hakutaka kupoteza sana muda na kumuomba mkewe kuwa warejee nyumbani ambapo walienda kupanda gari yao kisha safari ya kurudi kwao ikaanza, njiani Sophia alimuuliza mumewe
“Vipi leo hatununui chips?”
“Kwahiyo una hamu na chips?”
“Ndio au unahisi zitayeyuka kama jana?”
“Aaah achana na habari za jana Sophy, ngoja tununue”
Ibra akasimamisha gari na kununua hizo chips kisha safari yao kuendelea.
Walipofika nyumbani tu, kitu cha kwanza Sophia alichukua sahani na kuweka zile chips na kumuomba mumewe kuwa wale huku akimwambia,
“Si unaona leo hazijayeyuka”
“Unamaanisha nini Sophy?”
“Jana tulinunua tukiwa tumeambatana na mtu mbaya mume wangu”
“Aah Sophy jamani wale ni majirani zetu tena yatupasa tuwaombe msamaha”
“Labda nitamuomba msamaha huyo Jane siku akiwa kaburini”
“Sophy usiongee maneno hayo mke wangu”
Waliendelea kula na walipomaliza tu, Ibra alimuuliza mkewe kuhusu alipoenda na Siwema,
“Tulienda kutembea tu, kupunga upepo na kubadilisha mazingira”
“Mmh ila Sophy usipende sana kumuamini Siwema maana Yule ni mswahili sana”
Sophia akatabasamu tu kwani aliona mumewe kamavile anampigia mbuzi gitaa tu, wakaenda kukaa sebleni huku wakitazama luninga ila mara kidogo tu ile Tv ikazimika na kufanya washtuke kwani ilikuwa kama mtu kaizima hivi, Sophia akamuuliza mumewe kwa mshangao
“Ni nini hiki?”
Ibra nae akashangaa tu, ila ile Tv ikawaka tena na kuwafanya washtuke zaidi. Kwakweli kitendo hiki kilimfanya Ibra anyanyuke na kuizima ile Tv huku akimuomba mkewe waende chumbani tu.
Sophia akamuuliza mumewe,
“Kwani unaelewa hapo ni nini tatizo?”
“Sijui ila nahisi inataka kuharibika, nitamleta fundi aiangalie kuwa tatizo ni nini ila twende chumbani tu tukajiandae kulala”
Walienda chumbani na kukoga kisha kulala.

Kulipokucha kama kawaida Ibra alijiandaa na kwenda kwenye shughuli zake, kisha Sophia nae akaamka na kujiandaa kisha akaelekea kwakina Jane kwani alishajipanga kutimiza anachokitaka kwa siku hiyo.
Kama alivyoambiwa na Yule mganga yani alipokaribia tu kwakina Jane akatafuna kile kijani kisha akafika na kumuulizia Jane ambapo walienda kumuitia, Jane alitoka na kushangaa aliyemfata pale kwao kisha akamsikiliza lengo lake ambapo Sophia alimwambia kuwa anamuomba nyumbani kwake. Jane alitaka kukataa ila akakumbuka maneno ya Ibra kuwa yeye ndio faraja ya huyu Sophy mke wa Ibra kwahiyo Jane akakubali na kumwambia kuwa akikoga tu atakwenda.
Akaagana nae pale, kisha Sophia akawa anarudi nyumbani kwake huku akifurahia kuhusu Yule mganga kuwa ni kiboko kwani hakutegemea kama Jane angekubali kirahisi namna ile.
Sophia alipofika tu kwake, akachukua ile dawa na kuinyunyuzia mlangoni kisha akenda jikoni na kuweka juisi kwenye glasi kisha kuweka na ile dawa ili Jane akija tu ampe juisi hiyo.
Muda kidogo Jane nae aliwasili ambapo cha kwanza kabisa alipofika mlangoni alishangaa kuona kama unga unga na kumuuliza Sophia,
“Dada ni nini hiki mlangoni?”
“Wewe pita tu kuna vitu vilianguka”
Kwakweli Sophia hakupendezwa kabisa na hili swali la Jane kwani alizidi kujidhihirisha kuwa ni mchawi, Jane aliingia ndani na kukaa pale sebleni kisha Sophia akaenda jikoni kumletea ile juisi.
Wakati Sophia akitoka jikoni na ile juisi akamshangaa Jane akiwa ametulia kabisa akiangalia Tv ambayo yeye hakuiwasha kwavile alikuwa akimsubiri fundi atakayeletwa na mumewe, kwahiyo Sophia alimuuliza Jane kwa mshangao,
“Kwanini umeiwasha hiyo Tv Jane ni mbovu”
“Sijaiwasha dada, nimeshangaa imewaka tu”
Sophia alimuangalia Jane kwa jazba sana tena kwa mshangao mkubwa.

Mwisho wa sehemu ya 10

Itaendelea…………………..!!!
✍ By, Atuganile Mwakalile.



No comments: