*NYUMBA YA MAAJABU 9



                       

Ibra aliingia ndani huku nae akishangaa kwani halikuwa jambo la kawaida, Sophia alishikwa na hasira sana na kumsogelea Jane pale kwenye kochi na kumkurupua kwa kumpiga ambapo jane nae alishtuka kama chizi na kuanza kupiga kelele za mwizi tena kwa nguvu kabisa.
*TUENDELEE...*

Zile kelele zilifanya watu waanze kukusanyika nje ya nyumba ya Ibra, kitu ambacho Ibra hakuona kuwa ni sahihi na kuanza kumtuliza Jane aliyekuwa na mawenge ya usingizi, kisha kutoka nae nje na kuwaomba watu msamaha kuwa hakuna jambo lolote baya ila Sophia alitamani wale watu wampige Jane kwani alikuwa sawasawa na mwizi kuingia kwenye nyumba ya watu wakati wao wamefunga milango, watu walipoanza kutawanyika kwakweli bado ilikuwa ngumu sana kwa Sophia kukubaliana na uwepo wa Jane mahali pale,
“Tafadhali Ibra, huyo binti sitaki kumuona yani sitaki kumuona kabisa huyo binti ni mchawi, nimesema sitaki kumuona yani naweza kumfanya kitu kibaya”
Ilibidi Ibra amuombe Jane aende kwao, kwakweli Jane aliondoka huku analia kwani hakuipenda ile kauli ya Sophia ya kumuita kuwa yeye ni mchawi.
Ingawa Jane alikuwa akiondoka huku analia ila bado Sophia aliokota kitu chini na kumpiga nacho Jane kwa nyuma na kufanya Jane aanguke, kwakweli Ibra alishangaa sana kwani ilikuwa ni kitendo cha ghafla ambacho hakukitarajia kabisa kufanywa na mke wake Sophia.
“Khee Sophia umefanya nini sasa? Mbona unataka kuleta mabalaa tena jamani?”
Ibra akamkimbilia Jane pale chini na kujaribu kumuinua ila Jane alikuwa akitokwa na damu puani, kitu ambacho kilimuogopesha Ibra na kuona wazi mkewe amemdhuru Jane. Ibra aliamua kumbeba Jane na kukimbilia kumpakiza kwenye gari yake ili kumkimbiza hospitali ambapo Sophia nae alipanda kwenye hilo gari kisha Ibra akatoa gari lile na hata wakasahau kufunga milango kwani ilikuwa kama kuchanganyikiwa.

Walipofika hospitali walipokelewa na wahudumu kama kawaida kisha Jane kukimbizwa wodini na daktari kuitwa ambapo ilibidi Ibra amuombe daktari amtibie Yule mgonjwa huku akimpa pesa ili asiambiwe maswala ya PF3,
“Ila hii kitu tunafanya kinyume na utaratibu maana hairuhusiwi kisheria”
“Tafadhali nakuomba daktari nisaidie naomba”
Daktari akaanza kumchunguza Jane ni kitu gani kimempata mpaka kupelekea atoe damu puani kwani ilikuwa ikitoka nyingi huku Jane akiwa amepoteza fahamu.
Kwakweli Ibra alikuwa kama kachanganyikiwa huku akingoja hatma ya Jane kwa wakati huo, ila Sophia yeye alikuwa kwenye gari tu wala hakushika kufatilia kama Jane atatibiwa au la kwani moyoni mwake alijikuta akiwa amemchukia Jane kupita maelezo ya kawaida na ukizingatia yale maelezo aliyopewa kuhusu uchawi wa jane na vile walivyomkuta ndani ndio kabisa vikamfanya Sophia aamini kuwa Jane ni mchawi tena ni mchawi aliyekubuhu ndiomana kila siku anamletea stori za ajabu ajabu ili kumtisha na mambo yake ya kishirikina.
Ibra alirudi kwenye gari na kumuangalia mke wake kisha akamuuliza,
“Hivi Sophia una mapepo au kitu gani? Akili yako ni nzima kweli?”
“Usiniulize hayo maswali kwasababu ya Yule firauni Jane, laity ungejua kwamba Yule binti hafai kiasi gani wala hata usingenilaumu yani tena ungenisifia mna kunisapoti kuwa tummalize kabisa”
“Jamani Sophia ni roho ya wapi hiyo uliyonayo? Kwakweli sio mke ambaye nilikuzoea mimi jamani sio kabisa kabisa, kwakweli Sophia unanishangaza tena unanishangaza sana”
Kisha Ibra akashuka tena kwenye lile gari ili kwenda kusikilizia hali ya Jane inaendeleaje.
Alimkuta daktari ndio ametoka kwenye kile chumba walichompeleka Jane kisha akamfata daktari huyo na kumuuliza kuwa imekuwaje kuhusu Jane.
“Anaendelea vizuri ingawa aliumia sehemu za nyuma ila kuna dawa tutawapa ili awe anakunywa kwaajili ya kumrudisha katika hali ya kawaida.”
“Kwahiyo tutaweza kurudi nae nyumbani?”
“Yeah itawezekana ingawa muda utakuwa umeenda sana kwani sasa tumemuweka mapumziko kwa muda”
Ibra alikakubaliana na maneno ya daktari kisha akatoka nje na kwenda kukaa kwenye gari huku akisubiria muda uende ila alimkuta Sophia akiwa amejilaza mle kwenye gari, hakutaka kumsumbua na kumuacha alale tu.
Ibra nae alikuwa kimya mle kwenye gari huku akitafakari mambo mbali mbali kwani akili ya mke wake hakuielewa kwakweli ingawa hakuelewa zaidi kuhusu Jane kuwa amewezaje kuingia ndani ilihali walifunga milango yote asubuhi wakati wa kuondoka? Akabaki na maswali mengi sana kichwani bila ya kupata majibu ya aina yoyote ile.

Kwenye mida ya saa nne usiku ndipo waliporuhusiwa kuondoka na Jane ambaye alikuwa amezinduka muda huo hata fahamu nazo zilikuwa zimemrejea, wakapatiwa na dawa ambazo zitazidi kumsaidia Jane.
Ibra alifungua mlango wa nyuma ambapo Jane alipanda kwani pale mbele alikaa Sophia na hata hivyo hakuweza kuwaweka Sophia na Jane mahala pamoja kwa muda huo kwani alijua wazi kuwa bado Sophia ana kinyongo na Jane.
Ibra aliondoa gari, na alipofika mahali alisimamisha na kuagiza chips ili waweze kula wakifika nyumbani kwani alijua wazi kuwa ni ngumu kupika kwa muda huo. Muuzaji aliwafungia vizuri zile chips na kuwapatia kisha safari yao ya kurudi ikaendelea, ila Jane aliwaomba wampeleke kwao moja kwa moja ambapo Ibra alimuuliza,
“Kwanini tusiende nyumbani kwanza ule halafu ndio tukupeleke kwenu!”
“Hapana nitaenda kula nyumbani na hata hivyo sijisikii kula chips”
“Ila unajua muda umeenda sana Jane, sidhani kama utakuta chakula kwenu”
“Kwetu hawanaga tabia ya kumaliza chakula chote, nitakikuta tu”
“Basi sema chakula unachotaka tukanunue hata hotelini uende nacho kwenu ukale”
Sophia akaingilia kati yale mazungumzo,
“Jamani si ameshasema anataka kwenda kwao, hebu tumpeleke maana mada zinakuwa nyingi sasa”
Ibra hakuongeza neno lolote kwani hakutaka Sophia aongee zaidi maneno mabaya na kumkwaza Jane. Moja kwa moja walimpeleka Jane nyumbani kwao ambapo Ibra alishuka na kuongozana nae huku akimuomba Jane kuwa asiseme chochote juu ya kilichotokea kwa mama yake,
“Tafadhali Jane, usimwambie chochote mama yako”
“Akiuliza nilipokuwa je!”
“Mdanganye hata tulikupeleka kutembea ila usiseme chochote kuhusu kilichotokea, nakuomba Jane”
“Sawa”
Kisha wakafika mlangoni na kugonga ambapo mama Jane ndiye aliyetoka kuwafungulia na alipowaona tu kuwa ni wao alianza kuongea,
“Yani leo mmenikwaza jamani yani toka asubuhi mpaka muda huu kweli! Jane umeondoka hapa asubuhi hadi saa hizi jamani, mtatuuwa kwa presha maana wengine hatupo sawa jamani”
Ikabidi Ibra ajaribu kumuomba msamaha pale,
“Tafadhali mama tusamehe sisi maana hatukutoa taarifa yoyote juu ya kuondoka na Jane, kuna mahali tulienda nae kutembea ila kwa bahati mbaya ndio tumechelewa kurudi tafadhali mama tusamehe sana”
“Sawa ila mmenikwaza kwakweli”
Kisha Ibra akaagana nao pale halafu akarudi kwenye gari na kuelekea nyumbani kwao akiwa na Sophia.

Walifika na kukuta geti limefungwa vizuri ambapo Ibra alishuka na kufungua kisha akarudi kwenye gari na kuingiza gari ndani halafu akalipaki ambapo akashuka pamoja na Sophia na ule mfuko wa chips kisha akarudi kurudishia geti, alimuacha Sophia akiwa amesimama tu na alipotoka kufunga geti alimkuta kasimama vile vile na kufanya amuulize kwa mshangao,
“Khee mbona hufungui mlango wa ndani?”
“Fungua mwenyewe, mi sitaki miujiza”
Ibra alikuwa akimshangaa tu mkewe kisha akachukua funguo ambazo Sophia ndiye aliyemkabidhi funguo hizo na kufungua halafu wakaingia ndani ambapo kila mmoja alikuwa na mawazo yake ya kutosha tu na kuwafanya wakae pale sebleni kwanza, Kisha Sophia akamuuliza Ibra
“Hivi kwa kumbukumbu zako wakati tunampeleka Jane hospitali tulifunga milango?”
“Mmmh kwakweli sikumbuki”
“Mi basi nakumbuka vizuri maana funguo nilikuwa nazo mimi, milango hatukufunga wala nini. Sasa jiulize ni nani kafunga?”
“Kwahiyo unataka kusema Jane kafunga?”
“Jane sio mtu mzuri mume wangu ingawaje unamtetea, yani Yule binti sio mtu mzuri kabisa. Asubuhi tumeondoka hapa na milango yote tumefunga cha kushangaza tumerudi na kumkuta ndani je alipitia wapi? Yule binti ni mchawi mume wangu wala usijitahidi kumtetea”
Ibra alikaa kimya kwanza maana hilo suala kidogo lilimchanganya na kuhisi huenda kuna ukweli ndani yake. Kisha akainuka na kwenda kuleta sahani ili waweke zile chips na kuweza kula, alipofika na sahani akachukua ile mifuko ya chips ili aweke ila wakapatwa na mshangao kwani kwenye ile mifuko hawakukuta chips wala nini.
Walijikuta wakishangaa na kutazamana kwa zamu zamu, Ibra alimuuliza mkewe
“Ni nini hiki Sophy?”
“Sasa unaniuliza mimi naelewa?”
“Makubwa haya, sijawahi kutapeliwa hivi. Inamaana wale wauzaji hawakutupimia chips au?”
“Hata usiwalaumu wauzaji, kwa macho yangu niliwashuhudia wakipima na kuweka kwenye mifuko, tatizo ni kuwa tumenunua hizi chips tukiwa na Jane. Yule mtoto si mtu mzuri itakuwa amezichukua kiuchawi”
“Mmh naanaza kuamini sasa, au ndiomana alikataa kuja huku na kujifanya hataki kula chips!”
“Ndio hivyo Ibra, binti gani asiyependa chips? Jiulize tu utapata jibu, kwanza walivyo na dhiki pale kwao eti huwa hawana tabia ya kumaliza chakula chote loh wakati huwa wanakula hadi wanagombaniana mmh! Leo tumeingia choo kibaya mume wangu”
“Sasa tutakula nini?”
“Yani kale katoto kabaya kanataka tulalae na njaa loh!”
Ibra akafikiria na kuona kuwa ni vyema hata wakakoroga uji ili angalau wale kitu na kwenda kulala,
“Ngoja nikakoroge uji mke wangu, kwakweli leo tumepatikana dah!”
Ibra alienda jikoni na kuanza kukoroga uji ambao baada ya muda ulikuwa tayari kisha akaanza kunywa na mkewe,
“Kheee kwani huu uji umeweka nini?”
“Sijaweka chochote zaidi ya sukari tu”
“Mmh mbona mtamu hivi?”
“Hata mimi mwenyewe nashangaa, halafu hata haujachelewa kuiva yani”
Wakanywa na kumaliza, kisha Sophia akapeleka vyombo jikoni halafu yeye na mumewe wakaelekea chumbani kwa lengo la kulala, ila Sophia alidai amechoka sana kiasi kwamba hata kukoga anaona uvivu.
“Kwakweli nimechoka, mi sikogi bhana leo”
“Shauri yako ila uchafu unafanya watu waote ndoto mbaya”
“Mmh ushaanza maneno yako”
“Sio hivyo, ukumbuke wewe una mimba utamfanya mtoto nae awe mchafu kwa sababu yako”
“Aah yani mi sijisikii kabisa kukoga yani”
“Kama hujisikii sikulazimishi maana kukoga ni hiyari ya mtu”
Kisha Ibra akaenda kukoga ila aliporudi alimkuta mkewe akiwa ameshalala muda mfupi uliopita ambapo naye akaungana nae na kulala nae.
Ibra alimsogelea mkewe na kumkumbatia ambapo alipofanya hivyo, Sophia alishtuka kamavile kapatwa na jambo baya kwani alisema kwa nguvu
“Niache”
Kwakweli Ibra alimshangaa ila Sophia alikuwa akihema sana huku jasho likimtoka,
“Khee Sophia umepatwa na nini si umelala sasa hivi tu jamani”
“Hata sielewi”
Huku akihema sana, Ibra alijaribu kuwa nae karibu ili kumfanya arudi kwenye hali ya kawaida kwani alihisi kuwa huenda ameota ndoto mbaya ya ghafla.
Baada ya muda kidogo wakaamua tena kulala na kulala pamoja.

Kulipokucha leo Sophia ndio alikuwa wa kwanza kuamka na kumuamsha mumewe ambapo Ibra nae akaamka kisha kwa pamoja wakenda kukoga, wakati wanajiandaa Ibra akamuuliza mkewe
“Kwahiyo na leo tena kwa Siwema?”
“Sio lazima unipeleke maana naona unataka kuniwekea vikwazo”
“Ila Sophy mke wangu kwani umekuwaje siku hizi jamani? Unajua hukuwa hivi zamani yani tunaongea kamavile ni watu wenye maugomvi mke wangu dah!”
“Sio maugomvi, mimi nataka kuokoa nyumba yetu wewe unaona ni ujinga ndiomana naongea hivi”
“Haya unataka kuiokoaje hii nyumba?”
“Hii nyumba imeingiliwa na adui Jane kwahiyo lazima niiokoe”
“Sawa ila je kuiokoaje?”
“Wee subiri tu nitakupa majibu baadae”
“Haya twende nikupeleke huko kwa Siwema”
Wakamaliza kujiandaa na kutoka kisha safari ikawa ni kuelekea nyumbani kwa Siwema kwanza kisha ndio Ibra aende kwenye safari zake nyengine.

Walifika nyumbani kwa Siwema ambapo Sophia alishuka kisha Ibra akaondoka zake, moja kwa moja Sophia alikwenda kugonga mlango wa Siwema ambaye hakukawia kutoka na kusalimiana na Sophia kisha akamwambia amsubiri ajiandae haraka haraka waende.
“Karibu ndani basi unisubirie”
“Aaah acha tu nikusubirie hapa hapa nje bhana”
“Kama unaona ni sawa basi sawa, ngoja nijiandae haraka haraka”
Siwema akaingia ndani kujiandaa kwani alikuwa tayari ameshakoga, Sophia nae akainuka na kuusogelea mti wa mpera pale karibu na kwa Siwema ili kuangalia kama una mapera ili achume japo moja atafune ingawaje anajua wazi kuwa ule mti hauna historia ya kuwa na mapera.
Alipokuwa chini ya ule mti, alishtuliwa na bibi mmoja ambaye alikuwa anapita mahali hapo na kumfanya Sophia ashtuke sana huku akimuangalia bibi huyo, Yule bibi akamwambia Sophia
“Pole kwa kukushtua”
Sophia alimuangalia kwa muda kidogo kisha akamjibu,
“Asante”
“Huu mti wa mpera si mzuri”
“Kwanini?”
“Huwezi kupata pera hata moja hapo kwavile huu mti umechezewa sana”
“Khee unaujua huu mti wewe?”
Huyu bibi akacheka kidogo na kusema,
“Naujua sana huu mti, hata nyumba yako naijua”
Sophia alimshangaa na kumuuliza,
“Nyumba yangu unaijua kivipi?”
“Nyumba yako ni ya maajabu”
Sophia akashtuka na kuzidi kumshangaa huyu bibi.

Itaendelea………………..!!!
✍ By, Atuganile Mwakalile.



No comments: