*NYUMBA YA MAAJABU 17

   

Neema aliinua sura yake na kumuangalia Ibra, kwakweli Ibra hakuweza kumtazama Neema mara mbili kwani macho ya Neema yalikuwa yakiwaka moto na kumfanya Ibra apige kelele za woga kwa mara ya kwanza katika maisha yake.
*TUENDELEE...*

Ila kelele zile za Ibra hazikufika popote zaidi ya kuishia mle mle ndani kwani Ibra alianguka chini muda huo huo na kuwa kama mtu aliyepatwa na usingizi mzito sana.
Mtu ambaye alishtuliwa na kelele zile alikuwa ni Sophia ambaye alishtuka usingizini ila alijikuta ghafla hajali kuhusu zile kelele na kumfanya ajigeuze na kulala vizuri zaidi ambapo na yeye alipatwa na usingizi mzito kushinda wa mara ya kwanza.
Alipopitiwa na ule usingizi safari hii Sophia alipatwa na ndoto ambapo alijiona mahali na mbele yake alimuona mtoto mdogo ambaye sura yake ilionekana kufanana nae sana kitu kilichomfanya Sophia amwite Yule mtoto ‘mwanangu’ ila alipojaribu kumsogelea Yule mtoto alisogezwa mbele zaidi, kisha kuna sauti ikamwambia Sophia,
“Ni kweli mtoto huyu ni mwanao ila hutaweza kumshika wala kumgusa zaidi zaidi utakuwa unamuona tu wakati umelala”
Sophia akajikuta akihoji kwenye ile ndoto peke yake,
“Kwanini nisiweze kumshika wala kumgusa wakati ni mwanangu mwenyewe?”
“Pole sana Sophia, ila hii ni zawadi yetu sisi. Tunapenda sana watoto”
Sophia alijikuta akiumizwa sana kwani kila alipoitazama sura ya Yule mtoto ilionyesha simanzi kubwa, iliyomfanya Sophia asiweze kukubaliana na ile hali kwahivyo akaanza kumfata Yule mtoto ambapo alishtuka usingizini kabla ya kumkaribia Yule mtoto na tayari palikuwa pameshakucha.

Sophia alikaa kitandani akitafakari kuhusu ile ndoto na je kwake ilikuwa na umuhimu gani, alijikuta akilishika tumbo lake na kusema,
“Uwe salama mwanangu, nakupenda sana”
Kisha akamuangalia Ibra aliyekuwa hoi na usingizi na kumfanya amuamshe kwani muda wa kujiandaa kwenda kazini ulikuwa umewadia, Ibra alishtuka sana ila alionekana kuwa na uchovu uliopitiliza, Sophia akamuuliza mumewe
“Kheee mbona umechoka sana mume wangu?”
“Dah yani hata sijielewi kwanini nimechoka hivi”
Kisha akainuka na kwenda kukoga halafu akarudi kuvaa ila kuna vitu vilionekana kumweka kwenye mawazo sana, alijikuta akijiuliza kuwa alichokiona usiku wa jana kilikuwa ni kweli au ni ndoto tu iliyompitia, akajikuta akisema kwa sauti
“Kama ilikuwa ni kweli basi nilichukua maamuzi gani? Na kama ni ndoto kwanini nilipiga kelele? Au zile kelele nazo zilikuwa ni ndoto?”
Ibra alikosa jibu ila kwavile Sophia alimsikia Ibra anachojihoji aliamua kumuuliza kuwa ni kitu gani ambapo Ibra kabla ya kujibu akamuuliza Sophia,
“Hakuna kelele zozote ulizozisikia usiku Sophy?”
“Kuna kelele nilizisikia usiku tena ilikuwa kama sauti yako hivi”
“Sasa ulipozisikia ulichukua hatua gani na mimi nilikuwa wapi kwa wakati huo?”
“Nilishtuka kutoka usingizini ila wewe nilikuona pembeni yangu ukiwa hoi na usingizi hivyo nami nikajigeuza na kuendelea kulala. Kwani ni vipi mume wangu?”
“Hakuna kitu mke wangu ila akili yangu ikiwa sawa nitaweza kueleza kile ninachofikiria kichwani”
Sophia ilibidi amkubalie tu mumewe kwani kumpinga pinga alishachoka tayari, kwavile Ibra alikuwa kashamaliza kujiandaa akamuomba tu mkewe amsindikize nje kama kawaida yao.
Ibra na Sophia walitoka hadi sebleni ambapo walimkuta Neema kisha kusalimiana nae na Ibra kuwaaga ila Neema akamuomba kitu,
“Kaka kabla hujaondoka itakuwa ni vyema ukanywa chai kwanza, leo nimeamka mapema sana ili nikuandalie chai naona unashinda na njaa kwa muda mrefu”
“Dah asante Neema ila nimechelewa muda huu”
Sophia nae ikabidi aanze kumsisitiza mumewe,
“Kwani kunywa chai inachukua muda gani Ibra jamani, si ungekunywa tu ili uwe na nguvu huko uendako jamani mume wangu!”
“Ni kweli msemayo ila naomba chai nianze kunywa kesho maana leo nimeshachelewa”
“Jamani kaka sio vizuri hivyo jamani, yani nimeandaa kwa ajili yako”
“Nisamehe bure Neema”
Kisha Ibra akenda kufungua mlango na kuondoka kwani hakutaka kuendelea kukaa hapo ili wasije kumpa vishawishi zaidi wakati tayari alikuwa na mawazo yake kichwani.

Ndani alibaki Sophia na Neema ambapo Sophia akasema ni vyema hiyo chai akanywe yeye ila Neema akamkataza na kumwambia ya kwake bado hajamuandalia.
“Hakuna shaka Neema ila chai si chai tu!”
“Yeah chai ni chai tu ila kuna chai bora kwa mama mjamzito, tulia nikuandalie. Sitaki unywe hii sababu utashiba na kushindwa kunywa chai bora kwaajili yako, subiri nikuandalie dada na mwenyewe utafurahia”
Sophia hakuhoji sana kisha akaelekea chumbani kwa lengo la kukoga na kuweka chumba chao vizuri.
Ila alipokuwa chumbani alifikiria sana kwani hakuona kama kunakuwa na tofauti ikiwa kuna wajawazito wanaokunywa chai za pamoja na familia zao, akajiuliza sana kuwa kwanini Neema amemkataza kunywa ile chai ila hakupata jibu, kwa upande mwingine alihisi kuwa pengine kuna kitu ambacho Neema ameweka kumdhuru mume wake ila akajiuliza kwanini amdhuru maana hakuona kama kuna sababu yoyote kwa Neema kufanya hivyo, ikabidi apuuzie yale mawazo yake.
Alipomaliza shughuli zake alitoka na kumkuta Neema kama kawaida akiwa amekaa kuangalia Tv, ila kabla na yeye hajakaa kujumuika na Neema akamwambia kuwa asikae kwanza aende mezani kwa lengo la kunywa chai ambapo Sophia alifanya hivyo na kukuta akiwa ameandaliwa chai ya maziwa na chapati pamoja na nyama ya kurosti. Sophia alikunywa kisha akarudi kukaa sebleni na kumuuliza maswali Neema,
“Samahani Neema kuna kitu naomba nikuulize”
“Niulize tu dada hakuna tatizo”
“Hivi maziwa yamenunuliwa muda gani humu ndani? Inamaana Ibra analeta vitu bila ya kuniambia?”
“Mbona maziwa yapo mengi dada ndiomana mimi nimeyapika tena kwa afya yako ni vizuri sana ukinywa mara kwa mara”
“Suala ni kwamba yaliletwa lini? Unajua hujawahi kunidai hela ya mboga hata siku moja ila kila siku tunakula vizuri tu je hizi mboga zinatoka wapi na huyo Ibra kazileta muda gani?”
Safari hii Sophia hakujibiwa chochote ila ghafla akapatwa na usingizi na kulala pale kwenye kochi kwani usingizi ule ulikuwa ni usingizi mzito sana.

Ibra alifanya shughuli zake leo huku akiwa na mawazo sana, alijikuta akiwaza mambo mbali mbali haswa lile swala la kuona macho ya Neema yakitoa moto lilimkosesha raha kwani alizidi kujiuliza kuwa ile ilikuwa ni ndoto au ni kitu gani, suala la Jane kukimbia pia lilimpa mawazo na kumfanya awahi kufunga shughuli zake siku hiyo ili aweze kwenda kwakina Jane kuzungumza nae kuhusu kilichomkimbiza kiasi kile.
Alipomaliza tu kufunga, aliingia kwenye gari yake na safari yake ilikuwa moja kwa moja kwakina Jane ambapo alimkuta Jane akiwa ametulia tu nje kwao, kisha akamuita pembeni na kusalimiana nae halafu kuanza kuzungumza kuhusu jambo lililompeleka mahali pale.
“Jane kwanza kabisa samahani kwa kilichotokea jana kwani sikutarajia kama ungekimbia kiasi kile”
“Nisamehe mimi kaka ila kwakweli sikuweza kuendelea kuwepo pale kwenu na sidhani kama nitaweza kuja tena”
“Hebu niambie kwanza kilichokukimbiza wewe ni nini, na kwanini ulishikwa na woga kiasi kile? Na kwanini useme huwezi kuja tena pale kwetu?”
“Siwezi kuja kwasababu ya Yule mgeni wenu siwezi kabisa yani siwezi”
“Ndio uniambie kwanini?”
“Siwezi tu, nadhani damu yake na yangu haviendani”
“Hebu Jane niambie ukweli maana kwa mujibu wa Yule binti ndani ni kuwa wewe ni mchawi”
Jane akacheka kicheko cha mshangao na kusema,
“Kheee mimi mchawi! Huo uchawi niutolee wapi mimi ikiwa hata mama yangu hajui kuhusu uchawi? Mimi mwenyewe narogwa je mchawi huwa na yeye anarogwa? Hapa nilipo huwa naonekana sijielewi sababu nimesharogwa sana. Na kama amewaambia hayo maneno Yule mgeni wenu basi jueni kwamba yeye ndio mchawi na sio mtu mzuri kabisa.”
“Kwanini unasema hivyo na nipe sababu ya kukimbia kwako”
“Sikia kaka nikwambie kitu, mimi sina akili ya darasani ila nina akili ya maisha, na akili hii nimeipata kwa kuangalia maisha ya watu mbalimbali na kusoma makala mbalimbali. Mimi ni mpenzi wa kusoma hadithi za kutisha na kusisimua ila humo nimejifunza vitu vingi sana. Kuna makala mengi huwa yanaeleza kuwa unapokutana na mtu mbaya kwa mara ya kwanza basi mwili wote husisimka na nywele kusimama. Sasa mimi nilipomuona Yule mgeni wenu hiyo hali ndiyo imenikuta kwa mara ya kwanza katika maisha yangu na aliponiangalia nilihisi kutetemeka mwili mzima ndiomana sikuweza kukaa pale na kuamua kukimbia”
“Kwamaana hiyo Yule ni mtu mbaya?”
“Sijui kwa nyie mnamuonaje ila kwa mie hapana kwakweli Yule si mtu wa kawaida, sijawahi kupatwa na ile hali katika maisha yangu yani ilikuwa ndio mara ya kwanza. Nakumbuka mama alinifundisha kuwa nikikutana na kitu kibaya niondoke eneo lile huku nikiomba Mungu anisaidie maana siwezi jua kuwa kitanipata nini na ndivyo nilivyofanya”
“Bado sikuelewi Jane kwahiyo Yule ni mtu mbaya mle ndani?”
“Mmh kwani nyie mmemtoa wapi kaka?”
Ikabidi Ibra amueleze Jane jinsi yeye na mkewe walivyokutana na Neema na mpaka kumkaribisha nyumbani kwao na kuamua kuwa awe mdada wa kuwasaidia kazi za ndani.
“Mmmh kaka kweli kabisa mnamchukua mdada wa kazi ambaye hamfahamu hata nyumbani kwao je akipata matatizo mtafanyaje?”
“Kwakweli hatuna la kufanya kwani ilikuwa ni katika kumsaidia ukizingatia kasema kuwa ndugu zake hawamtaki, na sijui katokea kijiji gani huko”
“Basi kabla ya yote mlitakiwa mumpeleke kwa mjumbe ili ajue kuwa kuna mtu asiye na kwao mnaishi nae na lolote likiwapata mtakuwa salama maana mlishatoa taarifa. Maisha yanataka umakini sana, unamchukua mtu awapikie, awafulie, aangalie nyumba yenu halafu hamjui kwao mnategemea nini? Kuna mtu duniani asiye na kwao? Mngeenda kwanza kwa mjumbe”
“Ila Jane umeniambia jambo la msingi sana ambalo hata sikulifikiria kabisa, licha ya kusema ni mtu mbaya na nini na nini ila hilo suala la kwa mjumbe ni la muhimu sana ambalo nilikuwa nimelisahau kabisa yani. Asante mdogo wangu.”
“Hata usijali kaka ila mimi kuja kwenu tena hapana, ila ngoja kuna kitabu nikuletee ukakisome unaweza kuwa na mawazo mapya ya maisha”
Jane akaelekea ndani kwao na kutoka na kitabu kidogo kisha akamkabidhi Ibra, kitabu kile kiliandikwa juu yake “Fahamu kuhusu majini” Ibra akashtuka sana na kumuuliza Jane,
“Unamaana gani kunipa hiki kitabu?  Hivi unajua kuwa majini ni viumbe wa ajabu sana ambao huwezi kustahimili kukutana nao! Au unamaana kuwa Neema ni jinni? Uliona wapi jini anapika, anaosha vyombo, anafua, analala uliona wapi?”
Kisha Jane akakichukua tena kile kitabu na kumwambia Ibra,
“Hiki kitabu ni tofauti kabisa na unavyokifikiria lakini najua ipo siku utakihitaji na utakisoma na kukielewa, kwa leo acha nikae nacho mwenyewe ila zingatia suala la kwenda kwa mjumbe kwanza”
Jane akamuaga Ibra na kurudi ndani kwao kwani hakutaka kuongea nae zaidi halafu alihisi kama kichwa kikimgonga hivi.

Ibra alirudi kwenye gari yake na kupanda huku akitafakari kwa muda kabla ya kuondoka pale kwakina Jane kwani lile wazo la Jane la kumshauri kuwa wampeleke Neema kwa mjumbe kwanza lilikuwa likifanya kazi katika akili yake, kisha akataka kuondoa gari yake ili aondoke ila kabla ya kuondoka kuna mdada alitoka ndani kwakina Jane na kumfata Ibra na kuanza kumgongea kwenye kioo ambapo ikampasa Ibra afungue kioo cha gari yake ili amsikilize ila Yule dada aliongea kwa kufoka,
“Umemfanya nini Jane?”
“Kumfanya nini kivipi?”
“Katoka kuongea na wewe hapa karudi ndani analalamika kuwa kichwa kinamuuma sana na analia tu”
Ibra akashangaa sana na kumfanya ashuke kwenye gari kisha kuongozana na Yule dada mpaka ndani ambapo Jane alionekana akigalagala chini huku akilalamika kuhusu maumivu ya kichwa, Ibra akatoa wazo kuwa ni vyema wakampeleka hospitali hivyo akasaidiana na Yule dada ili wamkongoje waende nae huko hospitali ili kujua kinachomsumbua Jane ni kitu gani.
Wakati wanatoka akatokea mama Jane na mama mwingine ambao kwa pamoja walishangaa na wakaelezwa hali halisi ya Jane na kuwa wanamuwahisha hospitali ila Yule mama mwingine alisema Jane arudishwe ndani ili aweze kumfanyia maombi ambapo Ibra hakuweza kupingana nao kisha wakamrudisha Jane ndani kisha Ibra alitoka nje na kuwaacha.
Ibra akiwa nje alijiuliza maswali mengi sana kuwa wale watu wako vipi yani wanathamini sana maombi kuliko afya ya ndugu yao, akatingisha kichwa kwa kusikitika.
“Badala mtu wamuwahishe hospitali eti wenyewe wanataka wamuombee kwanza, ngoja niondoke zangu mie”
Ibra akarudi kwenye gari yake kisha akaondoka eneo lile na kuelekea nyumbani kwake.

Alipofika nyumbani kwake aliona nyumba ikiwa kimya sana kama kwamba ndani hapakuwa na mtu yeyote, kisha akaingiza gari na kufungua mlango wa sebleni ambao ulifunguka kama kawaida na kuingia ndani. Akamuona mkewe akiwa amelala hoi kwenye kiti tena alionekana hajitambui kabisa, kisha Ibra akamuuliza Neema bila hata ya salamu
“Vipi huyo kafanyaje?”
Neema alimuangalia Ibra bila ya kumjibu kitu chochote na kufanya Ibra amuulize tena,
“Neema si naongea na wewe, kafanyaje huyo?”
Safari hii Neema naye alimuuliza suali Ibra ila suali lake lilikaa kibabe sana na alionekana kujiamini kupita maelezo,
“Na wewe unataka?”
Ibra alijikuta akitetemeka kwa uoga huku akihofia kitu ambacho anaweza kufanyiwa na huyo Neema kwani alikosa ujanja ghafla.

Itaendelea….......……..!!!
.



No comments: