NYUMBA YA MAAJABU 18




                 

Neema alimuangalia Ibra bila ya kumjibu kitu chochote na kufanya Ibra amuulize tena,
“Neema si naongea na wewe, kafanyaje huyo?”
Safari hii Neema naye alimuuliza swali Ibra ila suali lake lilikaa kibabe sana na alionekana kujiamini kupita maelezo,
“Na wewe unataka?”
Ibra alijikuta akitetemeka kwa uoga huku akihofia kitu ambacho anaweza kufanyiwa na huyo Neema kwani alikosa ujanja ghafla.
*TUENDELEE...*

Ghafla alimuona Neema akicheka kisha akasema kama kwa masikhara hivi,
“Kumbe kaka ni muoga kiasi hiki!!”
Akajichekesha zaidi ila Ibra alikuwa kimya kabisa,
“Kaka usiwe hivyo bhana mi nilikuwa nakutania tu wala sikuwa na maana yoyote mbaya. Dada leo amechoka sana na ndiomana unamuona yupo hivyo”
Ila bado Ibra aliendelea kuwa kimya kwani ilikuwa ni vigumu sana kwake kuamini zile kauli za Neema ukizingatia na yale aliyoambiwa na Jane ndio kabisa yalikuwa yakimchanganya kichwani, ila bado Neema aliendelea kujibabaisha ili aonekane kuwa ni mtu mzuri kwani alishauona wasiwasi wa Ibra.
“Kaka jamani usiwe hivyo, ngoja nimuamshe na dada”
Neema alimsogelea Sophia pale alipolala na kumtingisha kidogo ambapo Sophia alishtuka sana tena huku akihema juu juu na kumfanya Ibra ashtuke na kumsogelea mke wake huku akimuuliza kuwa tatizo ni nini, Sophia aliwatazama Ibra na Neema kwa muda kidogo ndipo alipowajibu sasa,
“Nimepatwa na ndoto mbaya sana”
“Pole Sophy, ni ndoto gani hiyo?”
“Nimeota nakimbizwa na watu wa ajabu sana, yani walikuwa wanataka kunikamata kabisa. Walipokuwa wananikaribia ndio mmenishtua.”
“Duh pole mke wangu”
Kisha Neema nae akaingilia kati na kuanza kuwaambia tafsiri za ndoto,
“Ndoto ya kukimbizwa sio ndoto mbaya kabisa, nilipokuwa mdogo bibi aliniambia kuwa mtu anapoota anakimbizwa ajue kuwa watu wanamuhimiza kwaajili ya maendeleo yake, na vile anavyokimbia ndio anavyokimbilia maendeleo yake. Kwahiyo ikiwa hadi umeamka wale watu hawajakushika basi ujue kuna maendeleo makubwa sana yanakuja mbele yako”
“Mmmh ndoto ya kukimbizwa ndio inamaana hiyo?”
“Ndio maana yake hiyo kwahiyo hata usiwe na mashaka kwa hiyo ndoto. Halafu kikubwa ni kuwa muende mezani mkajipatie chakula kwani najua nyote mmeshachoka tayari”
Ibra sasa ndio akaongea na Neema kwa kumjibu muda huu,
“Asante Neema ila ngoja kwanza tukajimwagie maji ndio tuweze kula vizuri”
Kisha Ibra akamshika mkono mkewe Sophia na kumuomba waende chumbani ambapo Sophia alifanya hivyo.

Walipofika chumbani, kitu cha kwanza kabisa ambacho Ibra alimuuliza Sophia ni kuwa alilala muda gani,
“Unafikiri nakumbuka basi muda niliolala! Hata sikumbuki mume wangu na hata sijui imekuwaje nadhani ni sababu ya hii mimba”
“Itakuwa ni kweli maana mimba nazo zina mambo sana, pole mke wangu ila kuna jambo napenda tuzungumze kidogo”
“Jambo gani hilo tena?”
Ibra aliamua kumueleza Sophia kuhusu kumpeleka Neema kwa mjumbe na umuhimu wa wao kufanya hivyo,
“Mmh umezungumza jambo jema sana mume wangu, kwakweli kuna umuhimu mkubwa wa kufanya hivyo maana akipata matatizo huyu tutakimbilia wapi? Hata sijui kwanini hatukuwa na wazo hilo tokea mwanzo”
“Nadhani kwasababu ya kutingwa na mambo, ila nashukuru kwa kunielewa mke wangu maana sikujua kama ingekuwa rahisi hivi kwa wewe kunielewa.”
“Ni vichache ambavyo sielewi ila sio kwa jambo la msingi kama hilo, duniani majanga ni mengi na mtu hujui la mbele bora kutoa taarifa mapema.”
“kwahiyo sasa twende nae lini kwa mjumbe?”
“Linalowezekana leo lisingoje kesho mume wangu bora kwenda nae leo leo”
“Kama leo basi inabidi tuwahi maana nilisikia kuwa mjumbe wa mtaa huu ni mtu wa dini dini sana bora tumuwahi mapema kabla hajaenda kwenye ibada zake”
“Hakuna tatizo, twende basi tukaongee na Neema ili twende naye kwa huyo mjumbe”
Wakakubaliana kwa pamoja kisha kutoka sebleni ambapo leo Neema hakuwa pale sebleni na wakajua wazi kuwa kaenda chumbani kwake na wakaamua kumuita, walipomuita tu Neema aliitika na kwenda pale walipo kisha akakaa kwenye kochi na kuanza kuwasikiliza walichomuitia ambapo Sophia aliamua kuanza kumueleza.
“Neema tumeishi na wewe hapa kwa siku mbili tatu na kwakweli tumependa sana uwepo wako hapa ila kuna jambo moja tulilisahau kabla ya kukukaribisha hapa nyumbani”
“Jambo gani hilo?”
“Neema, unajua sisi ni binadamu na hatujui ya leo wala ya kesho sasa tunapaswa twende na wewe kwa mjumbe ili atambue uwepo wako mahali hapa maana sisi hatuwafahamu hata ndugu zako, mwisho wa siku usije ukapata matatizo bure halafu tukashindwa kujieleza kwa jamii”
Neema akacheka kidogo kisha akawauliza,
“Kwahiyo mnataka mnipeleke mimi kwa mjumbe?”
“Ndio Neema”
“Kwani mkinipeleka kwa huyo mjumbe ndio anaweza kufanya nisipatwe na matatizo?”
“Hapana sio hivyo ila inakuwa vizuri hata ukipatwa na tatizo tunajua wapi pa kuanzia”
“Ila mimi si nilishawaambia kuwa ndugu zangu hawanitaki kwahiyo ni sawa na kusema kuwa sina ndugu kabisa, sasa mnataka nikifika kwa mjumbe nikajieleze tena kuwa nimekataliwa?”
“Neema naomba utuelewe kidogo, Yule mjumbe hautamueleza yote hayo. Tunachotaka sisi atambue ni kuwa tunaishi na wewe humu ndani, ni kweli ndugu zako walikukataa ila kwetu umekuwa kama ndugu tayari kwa hizi siku chache tulizoishi pamoja. Tunahitaji kuishi na wewe kihalali”
“Ila bado sioni sababu ya nyie kunipeleka mie kwa mjumbe, ingekuwa vyema kama mngenipeleka pale mwanzoni ila kwasasa hapana”
Ibra na Sophia wakatazamana kwa muda kisha Ibra akamuuliza Neema kwa ukali kidogo,
“Kwani Neema una nini hadi hutaki kwenda kwa mjumbe?”
“Kwani wewe unaniona mimi nina nini?”
“Hivi unajua kama hapa ni nyumbani kwangu na mimi ndiye mtu pekee mwenye mamlaka na nyumba hii! Unatambua hilo kweli?”
Neema akacheka kwa dharau, kitendo hicho kilimchukiza sana Ibra na kujiuliza kuwa kwanini huyu neema anajiamini kiasi kile kwenye nyumba yake mwenyewe, kisha akamwambia tena kwa hasira
“Unataka kwa mjumbe utaenda, hutaki kwa mjumbe utaenda. Hii ni nyumba yangu siwezi kupangiwa cha kufanya na mgeni kwahiyo kwa pamoja sasa tunakwenda kwa mjumbe”
“Unaniamuru hivyo kwa mamlaka ya nani?”
Sophia pia akamshangaa huyu Neema na kumuuliza,
“Kheee hivi ndio wewe Neema tuliyekukuta njiani ukilia kuwa una matatizo? Ni wewe kweli? Mmmh hapana, umekuwaje leo?”
“Ni mimi mwenyewe na hivi ndivyo nilivyo, sipendi kuendeshwa kwa lolote wala chochote”
Ibra alizidi kupatwa na hasira sana na kuzidi kumuuliza Neema kwa hasira,
“Wewe Neema unajiamini hivyo kama nani humu ndani? Unapata wapi kiburi cha kujiamini kiasi hicho?”
Kisha akamuangalia Sophia na kumwambia,
“Mke wangu, umeona sasa madhara ya kuokota okota haya, yani tumekwenda kuokota na visivyookoteka”
Neema akawaangalia kisha akawaambia,
“Msijali, ngojeni nikajiandae twende huko kwa mjumbe”
Kisha akaondoka pale na kuelekea kwenye chumba chake.

Sophia na ibra walimsubiri pale seblani ili atoke na waanze kuelekea huko kwa mjumbe, muda kidogo Neema alitoka akiwa vile vile hata wakamshangaa kuwa alichokwenda kujiandaa kilikuwa ni kitu gani, kisha akawaambia kuwa waende huko kwa mjumbe. Walitoka kwa pamoja hadi nje ambapo Ibra alielekea kwenye gari yake ili wapande waende ila Neema aliwauliza
“Kwani huko kwa mjumbe ni mbali?”
“Hapana sio mbali sana”
“Basi hakuna sababu ya kupanda gari, twendeni tu kwa mguu”
Nao wakaafikiana nae kisha wakatoka nje kwa pamoja na kuanza kutembea wakielekea huko kwa mjumbe ila walikuwa kimya kabisa njia nzima kwani hakuna aliyemuongelesha mwenzie.
Walitembea kwa muda mrefu sana bila ya kufika kwa huyo mjumbe hadi Sophia akaamua kumuuliza mumewe sasa maana yeye ndio alikuwa akipajua nyumbani kwa mjumbe
“Khee mbona hatufiki kumbe ni mbali hivi?”
“Hata mimi mwenyewe nashangaa kuwa kwanini hatufiki na wala hata sio mbali, sijui tumekosea njia maana sielewi kabisa”
Neema alikuwa kimya kabisa, walizidi kutembea hata giza liliwakutia njiani wakiwa hawajafika kwa mjumbe wala nini na kufanya Ibra afikirie kuhusu gari yake kuwa ni bora hata wangekuja na gari maana walishachoka tayari.
Baada ya mwendo mrefu na giza kuingia sana wakaona vyema warudi nyumbani kwao kwani walichoka vya kutosha na miguu ilianza kuwauma kwa uchovu, Ibra alimuangalia mkewe na kumuomba msamaha kwa kumtembeza kiasi kile
“Nisamehe mke wangu kwa kukutembeza hivi, hata sijui imekuwaje tumepotea njia”
“Na huko nyumbani tunarudije sasa?”
Wakatazamana tu kwani kiukweli walikuwa wamepotea njia na hata ya kurudia hawakuikumbuka tena. Sophia akamuangalia Neema na kumwambia,
“Tusaidiane mawazo Neema jinsi ya kurudi nyumbani maana tumeshapotea”
“Ndiomana mimi nilikataa hayo maswala ya kwa mjumbe ona sasa kilichotupata yani tumechoka balaa hata mimi mwenyewe sikumbuki njia”
Ibra hakuwa na la kusema zaidi ya kukazana kuwaomba msamaha kwani alijiona yeye kuwa ndio chanzo cha kuwatembeza wenzie kiasi kile, kisha akamuangalia Neema na kumwambia
“Neema samahani maana ningekusikiliza tangu mwanzo basi sasa hivi tungekuwa nyumbani. Tusaidiane tuweze kurudi nyumbani maana ni usiku sana sasa hivi na hatufiki kwa mjumbe wala nyumbani hatufiki, tusaidiane jamani”
Neema akainama kama mtu aliyechoka sana kisha akaanza kucheka huku wao wakimshangaa kinachomchekesha ila wakati wanamshangaa wakajikuta ghafla wakiwa nyumbani tena ndani sebleni.

Kila mmoja alimuangalia mwenzie kwani ilikuwa kama ni maajabu hivi kuwa wamewezaje kurudi hapo, ila miguu yao ilikuwa imejaa vumbi balaa na walikuwa wamechoka sana. Ibra akatazama miguu ya Neema haikuonekana kuwa na vumbi kabisa kanakwamba ni mtu ambaye hajatoka hata nje kwa siku hiyo, kwakweli kati ya Ibra na Sophy hakuna aliyeweza kusema chochote kisha wakaamua kwenda chumbani kwao kukoga ambapo walichukua muda mfupi tu kukoga na kutoka bafuni huku kila mmoja akitafakari kivyake. Ila Ibra aliamua kumuuliza mkewe
“Hivi hiki kilichotokea umeelewa kweli mke wangu?”
“Mmh mpaka saa hizi sielewi, hivi tumewezaje kurudi humu ndani”
“Je unakumbuka mara ya mwisho ilikuwaje?”
“Nakumbuka ndio, mara ya mwisho Neema alikuwa ameinama akicheka na sisi tulikuwa tukimshangaa”
“Je unahisi huyu Neema ni binadamu wa kawaida kweli?”
Sophia akasita kidogo kujibu kisha na yeye akamuuliza mume wake,
“Unamaana gani Ibra?”
“Aah wewe niambie tu kwa mawazo yako kuwa je umuonavyo Neema ni mtu wa kawaida kweli?”
“Kama sio mtu wa kawaida je atakuwa ni mtu wa aina gani?”
“Mimi sielewi ila huyu Neema ananipa mashaka sana”
“Sasa tutafanyaje mume wangu?”
“Wazo langu ni kuwa tumtimue”
“Mmh mume wangu, tukimtimua ataenda wapi?”
“Kwani wewe anakuhusu nini huyu? Je ni ndugu yako? Tumtimue bhana kuliko kuongeza balaa ndani tena tumtimue leo leo”
“Usiku huu mume wangu!”
“Kwani usiku kitu gani, waswahili husema heri nusu shari kuliko shari kamili. Huyu tumtimue tu kwani nahisi ni mchawi mkubwa sana”
“Kheee mi sijui kama nitaweza hilo mume wangu maana kuna muda huruma inanijaa juu yake”
“Utajijua na huruma zako maana kila siku zinatuletea mabalaa tu katika maisha haya, ngoja mi nikafanye ninavyojisikia”
“Ila Ibra kwanini tusingesubiri hadi kesho?”
“Kesho mbali bhana, linalowezekana leo lisingoje kesho”
“Haya baba maamuzi ni yako ila mimi namuonea huruma sana”
Ibra hakutaka kupoteza muda katika kujadiliana na mke wake kwani anamtambua ni jinsi gani huwa anaponzwa na huruma yake ambayo badae hugeuka majuto kwani hadi huyo Neema kukaribishwa hapo kwao ni kutokana na huruma ya mkewe.
Ibra akaamua kwenda kufanya kile ambacho roho yake inamwambia.
Akatoka hadi sebleni ambapo aliangaza macho yake huku na kule ili kumuona Neema ila hakumuona na kumfanya ashangae kwani kawaida ya Neema ni kukaa pale sebleni akiangalia Tv, Ibra alipotazama Tv aliikuta ikiwaka na kuona kuwa ile ni sababu tosha ya kumtimua Neema kuwa anaachaje Tv inawaka wakati yeye hayupo pale sebleni.
Ibra akasogea sasa karibu, alipotazama kwenye kochi alishtuka sana baada ya kuona kuna nyoka amekaa juu ya kochi akiwa amejiviringisha na kichwa amekiinua juu.

Itaendelea........…….



No comments: