NYUMBA YA MAAJABU 6




                   

Sophia akamuangalia kwa makini na kumuuliza,
“Tayari nini?”
“Tayari chakula kipo mezani”
“Mmh usinitanie Jane, haiwezekani zile ndizi ziwe zimeiva! Hebu acha utani”
Akaelekea na Jane mezani ila bado Sophia hakuamini na kumuangalia vizuri Jane kisha akamuuliza,
“Je wewe ni binadamu wa kawaida?”
Jane akamshangaa Sophia kwa swali lile.
*TUENDELEE...*

Kwa kweli Jane hakuweza kumjibu Sophia kwani lile swali pia halikuwa la kawaida na hata hivyo Sophia hakuonekana kawaida kabisa kwani alionekana ni mtu mwenye mashaka na Yule Jane.
Wakiwa bado wanatazamana, wakashtushwa na hodi na kufanya Sophia aende kufungua ambapo aliyeingia alikuwa ni mumewe Ibra ila muda huo huo Jane nae hakuweza kukaa kwani aliaga juu juu na kuondoka zake hata Ibra aliweza kuelewa kuwa lazima kuna tatizo kwavile hakuuelewa ule uagaji wa Jane na kuondoka.
Ibra akamuangalia mkewe na kumuuliza kuwa ni nini tatizo, Sophia akaamua kumueleza mumewe jinsi ilivyokuwa hadi kupelekea hali ile, Ibra akasikitika na kumuangalia mkewe kisha akamwambia,
“Unajua mke wangu kila siku napenda kukwambia kuwa uwe unafikiria kwanza kabla ya kuongea jambo lolote maana maneno yako huwa katika hali ya ukali sana. Nilivyokuzoea mimi ni tofauti na mwingine alivyokuzoea.”
“Hivi unafikiri ningemuulizaje jamani? Tatizo Ibra hukuwepo, yani mtu nimemwambia muda huo huo kuwa akapike halafu muda huo huo anaenda jikoni na kuniambia chakula tayari! Inakuingia akilini kweli? Nakwenda mezani nakuta kweli ameshaandaa chakula mmh! Kwakweli kwa upande wangu imekuwa ngumu sana kujizuia kwa hiyo hali jamani maana haiwezekani tena haiwezekani kabisa.”
Ibra akaongozana na mkewe mpaka mezani na kuangalia zile ndizi pale mezani kisha akachukua kijiko na kuzionja, halafu akakaa kimya kwa muda na kusema
“Mmmh ndizi tamu sana hizi sijapata kuona yani na njaa yangu hii hebu kaa hapo tuanze kula”
“Ila upikaji wake ni wa kustaajabisha mume wangu”
“Achana na mambo ya upikaji, mi nakujua Sophy mke wangu usikute ulimuagiza binti wa watu akapike halafu ukapitiwa na usingizi, mtu anakwambia chakula kimeiva unashtuka na kuona ni muda huo huo kwavile ulipitiwa na usingizi, hebu kaa tule”
Ibra akaweka chakula kwenye sahani na kuanza kula vizuri kabisa huku akimsisitiza Sophia nae aweze kula ambapo Sophia aliamua kula kutokana na vile ambavyo mumewe alimsisitiza.
Kwakweli chakula kilikuwa kitamu sana na kufanya waifurahie ladha ya kile chakula lakini bado Sophia alikuwa na mashaka sana juu ya upikaji wa kile chakula hata imani yake juu ya Jane ikapungua kabisa.
Walipomaliza kula, Ibra akamshauri mkewe kuwa waende wakamuombe msamaha Jane,
“Mmmh sijui atanifikiriaje sasa!”
“Usijali twende kisha mi nitazungumza nae maana mi ndio nakufahamu vizuri wewe”
Basi wakakubaliana na kuinuka wakielekea kwakina Jane.

Walipofika walimkuta mama Jane akiwa nje akichambua mboga, ikabidi Sophia ajichekeleshe kidogo na kuulizia kama Jane yupo,
“Jane karudi ila kapitiliza moja kwa moja chumbani, ngoja nimuite”
Mama Jane akamuita Jane kisha Sophia akakaa karibu na huyu mama akimsaidia kuchambua ile mboga, Jane alipotoka moja kwa moja Ibra akamuomba pembeni ili azungumze nae ambapo alisogea na Ibra kwaajili ya mazungumzo,
“Jane samahani kilichotokea kati yako na mke wangu naomba umzoee tu”
“Mimi sina tatizo nae ila sikumuelewa tu alivyokuwa akifoka na kuonyesha kunishangaa”
“Pole sana mdogo wangu, unajua nini huyu Sophy huwa ana matatizo ya kusahau anaweza fanya jambo kisha akasahau halafu muda mwingine anasahau muda sababu ya kusinzia naomba umsamehe sana”
“Mmh mi sikujua hilo, ila kama ana tatizo la kusahau basi sasa naweza kuelewa kwanini alikuwa akifoka vile. Nimemsamehe na wala sina mashaka nae”
“Kama umemsamehe ni vizuri, na usisite kuja kuendelea kututembelea tafadhali maana pale nyumbani huwa anabaki mwenyewe na upweke.”
“Ilimradi nimeshagundua tatizo lake basi haitanisumbua tena”
Kisha Ibra akamuita mkewe na kuwapatanisha ambapo Sophia na Ibra wakaaga baada ya lile tukio na kuondoka, huku Sophia akimsisitiza Jane aende kumtembelea tena kesho yake.
Walipoondoka tu, mama Jane akamuita binti yake ili kujua kilichoendelea kwani haikuwa kawaida kwa Jane kufatwa vile nyumbani kwao.
Jane hakumficha mama yake, akamueleza kila kitu ambacho kimetokea siku hiyo.
“Mmh kwahiyo chakula alishapika akasahau na kukwambia wewe ukapike?”
“Ndio hivyo mama, maana alinipa maelekezo sijui nyama ipo kwenye friji niitoe kisha niipike na ndizi, kuingia jikoni hakuna nyama kwenye friji ila nilipofunua sufuria nakuta ndizi zilishapikwa tayari tena zimenona balaa dah kafanya nimeondoka bila hata ya kula hata kidogo.”
“Kama ndio hivyo basi kusahau kwake ni babkubwa maana mmh! Mtu unasahau kabisa kama ulishapika, ila ni bora mumewe anajua tatizo la mke wake.”
“Ndio, kaniambia nimchukulie kama alivyo sababu ni tatizo lake la kusahau”
“Mmh haya mwanangu ila siku nyingine uwe makini na maneno yake”
Jane akakubaliana pale na mama yake kisha akarudi zake ndani huku akiamini kuwa Sophia alipika zile ndizi ila amesahau kutokana na tatizo lake la kusahau.

Ibra na Sophia walipofika nyumbani moja kwa moja Ibra akakumbuka kitu,
“Aaah! Hata nimesahau kumshukuru Yule binti kwa chakula kitamu, kwakweli anajua sana kupika”
Sophia akamuangalia mumewe na kumuuliza,
“Inamaana anajua kupika kushinda mimi?”
“Mmh mke wangu jamani huo sasa ni wivu, mimi nimemsifia tu wala sijasema kama amekupita wewe. Hata hivyo hakuna anayekufikia wewe mke wangu kwa chochote wala lolote”
Sophia akatabasamu kwani hizi sifa alizopewa na mumewe zilimfanya ajisikie vizuri sana, kisha Sophia akainuka na kuelekea meza ya chakula halafu akamuuliza mumewe,
“Wakati tunaondoka hivi tulitoa vyombo mezani kweli?”
“Mmh mi sikumbuki ila mezani nilikuacha wewe halafu niakenda kukaa kwenye kochi kwani vipi?”
“Kwa kumbukumbu zangu sikumbuki kama nilitoa vyombo kwakweli ila naona vimeshatolewa je nani kavitoa?”
“Aah Sophia jamani unakoelekea mke wangu siko kabisa yani mmh wewe kila kitu kwako kipo nyuma mbele. Kuna mtu aliniambia kuwa wanawake wajawazito huwa na tabia ya kusahau kwakweli leo naamini maneno yake. Hebu njoo kwanza mke wangu tujadili mambo ya msingi. Leo nimerudi mapema hata huniulizi kwanini mapema ila kila muda unazuka na jipya sijui ndio maisha gani haya mke wangu.”
Sophia akaamua kusogea pale sebleni na kukaa na mumewe ingawa katika kichwa chake kilikuwa na maswali mengi sana ila aliamua kuyapuuzia kwa muda, kisha akamuuliza mumewe kuhusu kuwahi kurudi kwake,
“Eeh mbona leo umewahi kurudi sana?”
“Kwanza kabisa leo nilipokuwa kazini mawazo yangu yote yalikuwa juu yako kwani nilikuwa nikiwaza juu ya upweke ambao utakuwa nao. Ndiomana nimewahi kurudi ili nikuliwaze mke wangu.”
Sophia akatabasamu kwavile aliyapenda sana maneno ya mumewe ya kumbembeleza, kisha Ibra akaendelea kuongea,
“Halafu nimepata wazo mke wangu, kwanini tusiwe na msichana wa kazi humu akusaidie saidie”
“Msichana wa kazi! Wa nini mimi? Kwakweli huwa sina imani na hao wasichana wa kazi mume wangu jamani nisije nikaibiwa bure bora ufikirie jambo lingine”
“Uibiwe nini mke wangu?”
“Nitaibiwa wewe”
“Mmh yani huo wivu wako majanga loh! Basi itabidi ukamshawishi mdogo wako Tausi aje hapa au unaonaje?”
“Hapo sawa, basi tutapanga ili nikaongee na mama nije nae hapa huyo Tausi anisaidie saidie ukizingatia hasomi wala nini”
Wakakubaliana pale kisha Ibra akaamua kwenda kukoga kwanza kuondoa uchovu wa siku hiyo ambapo alipomaliza kukoga akamwambia na mke wake nae akakoge, Sophia akainuka na kwenda kukoga ila alikuwa na mawazo mengi sana mle bafuni haswa kwa mambo ambayo yanamtokea halafu hayaelewi elewi, alikuwa akijiuliza vitu vingi sana bila ya kupata majibu.
Alipotoka bafuni alimkuta Ibra akiwa kitandani amejilaza ambapo Ibra alimuita mke wake huyu ili ende pale kitandani na wajumuike nae.
Sophia alisogea karibu na alipo mumewe ila alimuangalia tu na kufanya Ibra amuulize,
“Sophy mke wangu mbona wanitazama tu kama hujui nilichokuitia? Unajua nimekumiss sana mke wangu”
Kisha Ibra akamsogelea kwa karibu Sophia na kumkumbatia huku akimpapasa, ila Sophy alionekana kutofurahishwa kabisa na kumfanya Ibra amuulize kwa kumshangaa,
“Vipi Sophy mke wangu nini tatizo?”
“Sijisikii”
“Hujisikii kivipi?”
“Kwani mtu akisema hajisikii huelewi au?”
Halafu Sophia akainuka pale kitandani na kuelekea sebleni, kitendo hicho kilimfanya Ibra amshangae sana mke wake na moja kwa moja akafikiria kuwa ni mimba iliyomfanya awe katika hali ya namna ile kwani katika maisha yao ya kawaida haijawahi kutokea hata mara moja Sophia kuongea maneno ya vile wala kumbishia mume wake katika tendo lile.
Ibra alitulia tu pale chumbani akitafakari na kujiuliza kuwa imekuwaje maana ilikuwa ngumu kwake kuelewa.

Sophia alikwenda sebleni na kukaa kwenye kochi ila alijikuta akijifikiria sana kwa alichomjibu mumewe na moja kwa moja kujiona kuwa ana makosa, kwanza alijishangaa pia kuweza kumjibu mumewe vile wakati hajawahi hata siku moja kumkatalia hata kama akiwa hajisikii kweli.
“Mmh hivi Ibra atakuwa ananifikiriaje jamani loh! Kwanini nimefikia hatua ya kumjibu vile wakati ni mume wangu? Nina kila sababu za kwenda kumuomba msamaha maana jambo nililofanya si la kawaida kwakweli.”
Hivyobasi akainuka na kurudi tena chumbani ila alipoingia chumbani na kumuangalia Ibra pale kitandani hakumuona na kufanya ajiulize kuwa Ibra ameelekea wapi maana kama angetoka basi lazima angepita pale sebleni na yeye angemuona ila hakumuona kutoka, akajaribu kuita ila hakuitikiwa na Ibra. Moja kwa moja akahisi kuwa huenda Ibra yupo chooni hivyo akaamua kwenda chooni kumuangalia, ila alipofungua mlango wa choo hapakuwa na mtu yoyote na kumfanya Sophia apatwe na hofu moyoni.
Akaamua kwenda kukaa tena kitandani, alifika na kukaa huku akiwa na mawazo mengi sana alijiinamia kwa muda kisha akaamua kujitupa kitandani huku akiwaza alipokwenda Ibra. Ila alipojitupa tu alishtuka sana kwani alihisi kuwa kuna mtu amemlalia, kitendo hicho kilimfanya Sophia ageuke kuangalia ni nini akamuona Ibra akiwa amelala tena hana habari kabisa.
Kwakweli Sophia alishtuka zaidi kwani mwanzoni hakumuona huyu Ibra hapo kitandani, akashangaa imekuwaje.

 _Mwisho wa sehemu ya 6._

Itaendelea…………....!!!
✍ By: Atuganile Mwakalile.



No comments: