NYUMBA YA MAAJABU 7



                     

Akaamua kwenda kukaa tena kitandani, alifika na kukaa huku akiwa na mawazo mengi sana alijiinamia kwa muda kisha akaamua kujitupa kitandani huku akiwaza alipokwenda Ibra. Ila alipojitupa tu alishtuka sana kwani alihisi kuwa kuna mtu amemlalia, kitendo hicho kilimfanya Sophia ageuke kuangalia ni nini akamuona ibra akiwa amelala tena hana habari kabisa.
Kwakweli Sophia alishtuka zaidi kwani mwanzoni hakumuona huyu Ibra hapo kitandani, akashangaa imekuwaje.
*TUENDELEE...*

Aliamua kumtingisha Ibra na kumuamsha ambapo Ibra aliamka huku akimshangaa Sophia kwa kumuamsha kwa nguvu vile,
“Yani kwa muda mfupi tu Ibra ndio umelala usingizi wa kiasi hicho? Kwanza niambie ulienda wapi?”
“Kwenda wapi kivipi?”
Ibra alikuwa akimshangaa mkewe, kisha Sophia akamueleza vile ambavyo yeye alikwenda sebleni na alivyorudi chumbani bila ya kumkuta pale kitandani na alipojaribu kumuita na kumuangalia sehemu mbalimbali bila ya kumuona na vile alivyofika pale kitandani na kushtukia kuwa amelala.
Kwakweli Ibra alijikuta akicheka tu huku akimuangalia mkewe mpaka Sophia akapata hasira na kumuuliza Ibra kwa ukali,
“Sasa kinachokuchekesha?”
“Jamani Sophia mke wangu kwakweli naona sasa hiyo mimba imeanza kukuendea kombo maana si kwa mambo unayoyafanya mmh!! Hivi inakuingia akilini kweli eti mimi usinikute hapa kitandani halafu urudi tena unikute, jamani aah! Mi nilikuwa nimelala hapa maana siwezi kubishana na wewe ukizingatia ushakataa ninachokitaka, ila uzuri ni kuwa natambua hali yako na ndiomana nikaamua kulala tu ila hilo swala lako la kutokuniona na kuniona ndio linanichekesha kwakweli”
- Ingawa Ibra aliongea hayo ila ilikuwa ngumu sana kumuingia akilini Sophia ukizingatia ni jambo ambalo anajua wazi limetokea hata kama ikiwa ni kupoteza kumbukumbu basi si kwa staili ile.
“Sogea tulale mke wangu”
Ibra akamkumbatia Sophia na kumsogeza karibu yake ili wapate kulala kwani aliweza kuona kuwa mawazo ya Sophia hayakuwa sawa kwa muda huo.

Kulipokucha kama kawaida Ibra aliamka na kujiandaa kwaajili ya kwenda kwenye shughuli zake, kama kawaida yake akamuaga Sophia kuwa anatoka ila kabla hajatoka Sophia akamzuia kutoka na kufanya Ibra amshangae na kumuuliza,
“Mbona unanizuia Sophy?”
“Usiende kazini leo sitaki kubaki peke yangu”
“Jamani Sophy mke wangu kwa staili hii tutaendelea kweli? Tutapata wapi pesa kwa ajili yetu na mwanetu mke wangu? Kwanini uwe hivyo jamani!”
“Nisamehe Ibra ila sijisikii kubaki mwenyewe”
“Basi inuka twende kwakina Jane tumuombe urudi nae hapa na ushinde nae, tafadhali tufanye hivyo mke wangu maana kazi nayo ni muhimu pia kwenye maisha yetu haya”
Sophia akakubali juu ya hilo, kisha akainuka pale kitandani na kutoka pamoja na mumewe wakielekea kwakina Jane.
Walifika na kuwagongea hata mama Jane alishangaa kuwaona asubuhi yote ile pale nyumbani kwake, ikabidi watumie Kiswahili cha kumvutia ili aweze kumruhusu Jane kwenda muda huo na Sophia nyumbani kwake. Mama Jane alielewa na kwenda kumuamsha Jane kisha kumwambia kuhusu ujio wa wakina Sophia.
“Mmh mama asubuhi yote hii jamani?”
“Naelewa kama ni asubuhi mwanangu ila hawa ni majirani zetu inapaswa kuwa nao karibu.”
Jane akaamka na kutoka nje kisha kuwasalimia Sophia na Ibra halafu akawaambia akaoge kwanza ajiandae ndio aende, ila Sophia akamuomba Jane,
“Beba tu nguo, twende ukaoge nyumbani Jane”
Jane akafikiria kidogo na kukubali, kisha akaenda kuchukua nguo na kutoka halafu wakaingia kwenye gari ya Ibra ambapo aliwaacha pale nyumbani kwake kisha yeye kuelekea kwenye shughuli zake.

Sophia na Jane waliingia ndani ambapo kabla ya yote Jane aliomba kuonyeshwa uwani ili aweze kuoga na kujisafisha, Sophia alifanya hivyo kisha nayeye akenda kukoga maana hata yeye alikuwa bado hajakoga kisha walipomaliza wakaandaa chai na kunywa halafu wakaanza stori za hapa na pale ambapo kwanza kabisa Sophia alimuomba msamaha Jane kwa kile ambacho kilitokea.
“Usijali dada nimeshakusamehe”
Sophia akatabasamu ingawa kiukweli bado alikuwa na maswali mengi sana moyoni mwake kuhusu hali halisi ya maisha yaliyopo pale.
Muda kidogo Jane alianza na stori zake,
“Basi bhana jana usiku nimesoma stori hiyo inatisha hadi nikaogopa kulala, yani usingizi ukachelewa kuja balaa ndiomana mpaka saizi nina usingizi”
“Yani wewe kwa stori zinazotisha hujambo, hivi unazipendea nini jamani? Mwenzenu stori ambazo hazina uhalisia wala huwa sizifagilii”
“Uhalisia upo dada, unajua mara nyingine mtu unaweza ukalala halafu ukaota ndoto mbaya sana na usipokuwa makini ile ndoto inakutokea kwenye maisha halisi”
“Sasa kuhusu ndoto mbaya unakuwaje makini hapo?”
“Unajua inatakiwa ukiota ndoto mbaya ukishtuka tu Swali ili Mungu akuepushe na yale mabaya uliyoyaota”
“Mmmh ila Jane wewe unanifurahisha sana, hayo mastori yako ya kutisha ndio yamekufundisha hivyo? Kitu kama kipo kipo tu hata mtu ufanye nini”
“Ila na wewe dada kwa kupinga sikuwezi mmh. Ila kwakweli nina usingizi sana, nataka nilale tu hapa hapa kwenye kochi.”
“Hakuna shida wewe lala tu”
Sophia alitulia akiangalia runinga huku Jane akiwa amejilaza kwenye kochi.
Wakati jane akiwa amelala hoi kabisa, Sophia akasikia kama vyombo vikilia jikoni na kumfanya ashtuke sana huku akisikilizia kwa makini, kadri alivyozidi kusikiliza ndivyo mlio wa vyombo ulivyozidi kwakweli woga ukamshika na kumfanya amshtue Jane kutoka usingizini ambapo Jane alishtuka sana huku akimuangalia Sophia kwa mshangao.
Sophia akamuuliza Jane kwa uoga flani hivi,
“Umesikia huko?”
Ila muda huo ile sauti ya vyombo haikusikika tena na kumfanya Jane azidi kumshangaa Sophia kwavile yeye hakusikia kitu chochote kile.
“Sisikii chochote”
Sophia akakaa kimya kwa muda na kupumua kwa nguvu kama kwamba kitu ambacho kilikuwa kimetokea kilikuwa kikubwa sana, kisha Jane akamuuliza
“Kwani kulikuwa na kitu gani kikilia?”
Sophia alijikuta akishindwa kumjibu Jane kwani mdomo wake ulijawa na uzito ghafla.
Walikaa pale wakitazamana ambapo Jane aliamua tena kujilaza kwenye kochi ila Sophia aliogopa hata kwenda chooni kwa muda huo.

Muda wa mchana Jane alishtuka na kudai kuwa kwasasa usingizi umeisha na anaweza akafanya vitu vyengine, kwavile Sophia aliogopa kwenda jikoni kutokana na mlio wa vyombo akaamua kumuomba Jane akapike chakula ili waweze kula.
“Mmh dada usije ukanifanyia kama mambo ya jana!”
“Hapana siwezi kufanya hivyo”
“Haya ngoja niende huko jikoni, ila unataka nipike nini?”
“Kuna maini kwenye friji, uyachukue halafu upike na wali”
“Hakuna tatizo”
Jane akainuka na kuelekea jikoni ili aweze kuandaa hicho chakula, ila alipofika jikoni kama alivyoona jana ndivyo alivyoona leo kuwa sufurua zimefunikiwa jikoni, akasogea na kufunua akaona maini yakiwa yameungwa vizuri sana tena yakiwa bado yamoto, kisha akafunua sufuria jengine ambapo napo akaona wali ukiwa umepikwa vizuri sana.
Jane akatabasamu na kujiuliza zaidi kuhusu tatizo la Sophia,
“Yani anapika mwenyewe halafu anasahau, basi hapo nikienda kumwambia mbona umeshapika atashtuka sana bora leo nisimwambie. Ngoja nirudi nimwambie vinachemkia nione kama anaweza kukumbuka kuwa ni yeye mwenyewe ndio alipika”
Kisha Jane akatoka jikoni na kwenda sebleni ambapo alimwambia Sophia kuwa ameacha vinachemkia, akamuona Sophia akipumua kidogo kwavile aliona kuwa siku hiyo hakuna maajabu yaliyotokea halafu wakaendelea kupiga stori mbili tatu ambapo Jane alimuuliza Sophia kuhusu swala lake la kupoteza kumbukumbu,
“Hivi tatizo lako la kupoteza kumbukumbu lilianza lini dada?”
“Tatizo la kupoteza kumbukumbu! Mi sina tatizo la kupoteza kumbukumbu”
Jane akacheka kisha akasema,
“Ama kweli mgonjwa huwa hajijui, yani dada hujui kabisa kama una tatizo la kupoteza kumbukumbu?”
“Sina hilo tatizo Jane, niamini jamani hilo tatizo sina kabisa”
“Haya basi ngoja nikusimulie kitu, kuna stori moja nilisoma kuhusu misukule yani unaweza ukaishi na misukule ndani bile kugundua”
Sophia akashtuka kidogo na kumuuliza Jane,
“Kuishi nayo kivipi”
“Unaweza ukashangaa unakaa kwenye nyumba labda umepanga kumbe mwenye nyumba ana misukule yake basi ukikaa unashangaa kama mtu kapita halafu humuoni huyo mtu kumbe ndio hiyo misukule”
“Uwiii mbona yanatisha hayo mambo!”
“Pole dada nilisahau kama hizi stori huzipendi”
“Kweli sizipendi ila ngoja kwanza, mtu unawezaje kugundua kama misukule ipo ndani na unawezaje kuiepuka?”
“Ila dada wewe si ulisema kuwa haya mambo ni ya kufikirika halafu hupendi stori za kufikirika, naomba niishie hapo, au umesahau kama ulisema kuwa hakuna misukule duniani ni stori tu wanazitunga”
Kisha Jane akainuka na kuelekea tena jikoni huku akiwa amemuacha Sophia akiwa na maswali mengi sana. Cha kwanza aliwaza uwepo wa misukule na matukio ambayo huwa anayaona kwenye ile nyumba kwani kwa kifupi yalikuwa yakimstaajabisha.
Jane akarudi tena na kumwambia kuwa ameshaandaa chakula mezani ila Sophia alijikuta akitaka kufahamu mengi sana kuhusu hiyo misukule na kujikuta akimuuliza maswali Jane ambapo jane akamuomba wakaulizane maswali hayo wakati wanakula.
Sophia alielekea mezani na kujiwekea chakula huku Jane nae akiwa amejiwekea cha kwake kisha Sophia akamuuliza tena Jane ila Jane bado alimpa masharti.
“Si vyema kuongea wakati wa kula dada, inatakiwa tumalize kwanza kula halafu ndio tutaendelea na maongezi”
Walikuwa wakila pale ila kichwa cha Sophia kilijawa na maswali mengi sana.

Walipomaliza kula jane alipeleka vile vyombo vyote jikoni kisha wakarudi kukaa sebleni ambapo Sophia akaanzisha tena maswali yake,
“Tafadhali Jane naomba unijibu maswali yangu”
“Haya niulize sasa nikujibu”
“Je misukule inaweza kufua nguo?”
“Kufua nguo! Mmmh! Sijui labda mwenye ile misukule akiiongoza”
“Sasa misukule inaweza kufanya vitu gani?”
“Mi ninachojua misukule inaweza ikala chakula chako ndani, huwa inapelekwa kulima nadhani hata mwenye misukule akiamua kuwa iwe inafua inaweza kufanya kazi hizo maana wale ni binadamu wa kawaida ila tu huwa wanaondolewa ufahamu”
“Basi niambie mtu unawezaje kujua kuwa unaishi na misukule na vipi unaweza kuiepuka?”
“Kuhusu kuishi nayo unaweza kugundua kama kukuta vitu vimefanyika ndani ndivyo sivyo ila kuiepuka sijui maana mi mwenyewe ile stori sijaimalizia”
“Mmh je misukule inaweza ikamdhuru mtu?”
“Misukule haina ufahamu dada, sidhani kama inaweza ikamdhuru mtu”
Sophia akawa kimya kwa muda ambapo Jane akaendelea kuongea,
“Kweli leo nimeamini kuwa kumbukumbu zako huwa zinapotea maana nakumbuka ulivyonikanusha kuhusu hizi stori halafu leo wewe  ndio umekuwa wa kwanza kutaka kujua undani wake mmh kweli dada unasahau sana”
“Unajua nini Jane, kiukweli hizo stori mimi huwa siziamini ila kuna mambo flani hivi yananichanganya ndio mana nikakuuliza ila siku moja utayajua tu”
Wakiwa wanazungumza pale, Ibra nae akawa amerudi kutoka kwenye mihangaiko yake ambapo Sophia alimkaribisha mumewe na moja kwa moja akaenda kumpakulia chakula kwanza huku Ibra akimshukuru sana jane kwa kuweza kushinda na mkewe kwa muda wote toka ameondoka,
“Usijali kaka, mi nipo pamoja nanyi”
Sophia akamkaribisha mumewe mezani ambapo Ibra alikula chakula kile huku akikisifia sana kuwa ni kitamu, kisha akauliza
“Nani kapika?”
“Jane huyo”
“Khee huyu mtoto anajua kupika sana”
Sophia akatabasamua tu, baada ya Ibra kumaliza kula Sophia akatoa vile vyombo na kwenda kuviweka na vingine vichafu pale jikoni kisha akarudi sebleni ambapo Jane nae hakutaka kukaa zaidi kwani aliaga na kufanya Sophia na mume wake kuinuka na kumsindikiza ila hawakumfikisha hadi kwao, kisha Ibra akamuomba Jane uwepo wake kesho yake tena.
“Tafadhali Jane naomba kesho tuje tukufate tena ushinde na mke wangu”
“Hakuna tatizo kaka”
Kisha wakarudi na kumuacha Jane nae akielekea kwao.

Walirudi ndani huku Sophia akifurahia uwepo wa mume wake,
“Kwakweli nafurahi siku hizi unawahi sana kurudi”
“Lazima niwahi kurudi mke wangu maana siwezi kukuacha na hali yako hiyo”
Sophia akamuacha mumewe akakoge kisha yeye akaelekea jikoni ili akoshe vyombo na aweze kukaa na mumewe kuzungumza mawili matatu.
Alipoingoia jikoni alishangaa sana kuona vyombo vyote vimekoshwa na vimeshapangwa kabatini kwakweli alijikuta akipiga kelele na kumfanya Ibra amfate kwa haraka sana,
“Vipi Sophia nini tena mke wangu?”
“Misukule”
“Misukule! Misukule imefanyaje?”
Ibra alikuwa akimshangaa mkewe na kuangaza macho yake huku na kule kuangalia kama kuna chochote.

 _Mwisho wa sehemu ya 7_

Itaendelea ………………!!!
✍ By, Atuganile Mwakalil



No comments: