Barua Ya Wazi Kwa Kijana Wa Kitanzania(kama una miaka kati 20 mpaka 30 soma hapa)


Hakuna kipindi kigumu kwenye maisha ya mwanadamu kama muongo wa tatu wa maisha yaani kati ya miaka 20 mpaka 30. Huu ni wakati ambao una changamoto nyingi sana za maisha na ni wakati ambao unaweza kujenga au kubomoa maisha yako moja kwa moja. Kama wewe upo katika kipindi hiki endelea kusoma hapa ili uweze kupata mwanga pale mambo yanapokwenda usivyotarajia. Kama umri wako umezidi hapo unaweza kusoma pia na ukawashauri wadogo zako au watoto wako. Na hata kama umri wako uko chini ya hapa sio vibaya ukajifunza na kujua ni nini unakwenda kukutana nacho mbele.
Huu ni wakati mgumu sana kwako.
Kwa maisha yetu ya kitanzania, kijana wa miaka kati ya 20-30 anakuwa anaingia elimu ya chuo, yuko chuoni, amemaliza chuo, anatafuta kazi au ndio ameanza kazi. Pia ni wakati ambao kijana huyu anakuwa kwenye mahusiano ya mapenzi, uchumba na hata kuingia kwenye ndoa. Pia ni wakati ambao wengi wanaondoka kwenye mikono ya wazazi au walezi na kwenda kujitegemea wenyewe. Mambo yote haya yameleta changamoto kubwa sana kwa kijana na kwa changamoto hizi kijana anaweza kujijenga au kujibomoa.
Changamoto kubwa anazokutana nazo kijana katika wakati huu ni;
1. Kumaliza elimu ya sekondari na kwenda kuanza maisha ya tofauti kabisa vyuoni. Kuna tofauti kubwa sana ya elimu ya sekondari na elimu ya chuo, wakati sekondari unasimamiwa sana, chuoni unakuwa na uhuru zaidi. Kwa uhuru huu vijana wengi wamejikuta wanafanya mambo ambayo yanasababisha washindwe kufatilia masomo yao vizuri.
2. Kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na kuvunjika kwa baadhi ya mahusiano. Mahusiano sio rahisi katika umri huu, kijana anakutana na mwenzake ambaye anafikiri wanapendana sana na siku moja watakuwa mume na mke baada ya muda anagundua mtu aliyeingia nae kwenye mapenzi hakumjua vizuri. Hii inapelekea mapenzi kuvunjika na kuumizwa sana.
3. Kukabiliana na maisha ya masomo vyuoni na maisha mengine ya kijamii. Licha ya masomo kuna shughuli nyingi za kijamii na binafsi pia. Kuna vijana wanajikuta wakiendekeza starehe sana na kusahau masomo, wengine wanajikuta wakikazana na masomo sana na kusahau nini kinaendelea kwenye jamii.
4. Kupata ajira baada ya kumaliza chuo. Hii ndio changamoto kubwa sana hasa nyakati hizi. Vijana wanatoka vyuoni wakiwa na habari nzuri walizodanganywa kwamba ukisoma na kufaulu vizuri utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Ni pale wanapojikuta mtaani mwaka mzima wakizunguka na bahasha bila ya kupata kazi ndio wanagundua maisha sio rahisi kama walivyodanganywa.
5. Kuanza kazi na kukabiliana na changamoto za kazi. Kupata kazi ni kitu kimoja, kufanya kazi na kuridhishwa nayo au kuifurahia ni kitu kingine. Kuna changamoto nyingi sana kwenye kazi hasa kwa wafanyakazi wageni, pia jinsi ya kuchangamana na watu wenye haiba tofauti ni kazi kubwa sana kwa kijana.
5. Kuanza maisha ya kujitegemea mwenyewe na kuweza kufanya maamuzi sahihi. Katika wakati huu kijana anaweza kuona ana uhuru mkubwa sana wa kufanya yale aliyokuwa anashindwa kufanya wakati yuko kwenye mikono ya wazazi au walezi. Ni katika wakati huu wengi wanafanya starehe kupitiliza na kujikuta wanapotelea katika ulevi.
6. Kuingia kwenye ndoa na kuanza maisha ya kifamilia. Katika wakati huu kijana anaingia kwenye ndoa na kuanza maisha ya familia. Maisha ya ndoa ni tofauti sana na maisha ya mapenzi na uchumba, hapa ndipo kijana anamfahamu vizuri mwenzake na kwa kushindwa kupambana na changamoto za ndoa, ndoa nyingi zinaishia kuvunjika mapema sana.
Kutokana na ukosefu wa elimu ya kupambana na changamoto hizi za maisha vijana wengi sana maisha yao yamepotelea kwenye kipindi hiki na kuja kushtuka baadae wakati umri umekwenda na kujiuliza ni wapi mambo yalikwenda hovyo.

Kijana ufanye nini kukabiliana na changamoto hizi?
Hapa nitazungumzia mambo kumi na moja muhimu ambayo kijana anatakiwa kufanya au kujua ili kuweza kuvuka salama kipindi hiki kigumu.
1. Jali sana afya yako.
Katika maisha yako afya ndio kila kitu, utaweza kufikia malengo makubwa kwenye maisha yako kama utakuwa na afya njema. Utaweza kuwasaidia wale unaowapenda kama utakuwa na afya njema. Hivyo kabla ya kufanya jambo lolote jiulize linakusaidiaje kulinda afya yako. Bila ya kuwa na afya bora huwezi kuwa na maisha bora, jikinge na maradhi, kula vizuri na fanya mazoezi.

2. Kuna wakati hutajua unafanya nini.
Katika kipindi hiki cha maisha kuna wakati hutajua ni nini unafanya kwenye maisha yako au ni wapi maisha yako yanaelekea. Usikatishwe tamaa na hali hii bali weka mipango na malengo ya maisha yako na ujitahidi kutekeleza.
3. Maisha hayatakuwa vile unavyopanga au kufikiri yatakuwa.
Mambo yanabadilika tena kwa kasi sana, pamoja na kuwa na mipango mizuri bado hutoweza kuitimiza yote hasa ndani ya kipindi hiki. Utajitahidi sana lakini kuna ambavyo vitakushinda. Usife moyo, endelea na maisha yako mwisho wa siku maisha lazima yataenda. Kingine cha muhimu zaidi jua unahitaji muda ili kufikia mafanikio yoyote unayofikiria, hakuna kitu kinachokuja haraka na kwa urahisi.
4. Sio kila mtu anayekuja kwenye maisha yako atakaa.
Hili nalisema hasa kwenye mahusiano ya kimapenzi. Usifikiri mpenzi uliyempata ni lazima uje uishi naye, kuna uwezekano mkashindwa kuendana na kila mtu akachukua hamsini zake. Badala ya kulaumu na kuharibu maisha yako furahia kwamba huyo ni mmoja wa watu ambao walikuwa wakupita tu kwenye maisha yako. Umekuwa na marafiki wengi kwanzia utoto mpaka sasa, wengi kwa sasa hujui hata wako wapi, ndivyo maisha yalivyo. Kuna watakaokuja na kukaa, kuna wengine watapita tu.
5. Uhuru una mipaka yake.
Kwa kuwa umefika wakati wa wewe kujitegemea na kuwa huru na maisha yako, haimaanishi unaweza kufanya chochote unachotaka na maisha yako. Ni lazima uwe na busara ya kujua ni kipi kizuri kwenye maisha yako na kipi kibaya. Kama unaenda disko na kulewa kila mwisho wa wiki kwa sababu ulikosa haya ulipokuwa nyumbani, fikiria maisha yako ya mbele unataka yaweje kisha punguza mambo ambayo yatakuzuia kufika kule.
6. Jaribu mambo mengi sana katika wakati huu.
Jaribu kufanya vitu vingi sana kwenye kipindi hiki, usiridhike na kazi moja unayotafuta au uliyopata. Huenda mpaka sasa hujajua ni nini unafurahia kufanya au hujajua vipaji vyako. Katika wakati huu ambao bado hujawa na majukumu makubwa unaweza kujaribu kufanya vitu vya tofauti kwenye maisha yako ili kujua ni nini unafurahia kufanya. Muhimu zaidi tengeneza vyanzo mbadala vya kipato katika wakati huu.
7. Jifunze, jifunze, jifunze
Vijana wengi wanaomaliza elimu zao huona kujifunza ndio kumefika mwisho. Au watajifunza tena wakienda kuongeza masomo. Hili ni kosa kubwa sana, jifunze kila siku kutoka kwa watu na kwa kujisomea vitabu vya kukuendeleza. Kama unakosa kabisa cha kujifunza tembelea AMKA MTANZANIA na utajifunze mengi sana. Kama hujifunzi unarudi nyuma na kama unarudi nyuma hutoweza kupambana na changamoto za maisha hivyo maisha yako yatakuwa magumu sana.
8. Dunia haiko sawa.
Kuna wakati kijana unafikiri dunia ingetakiwa kuwa sawa na kuona kama unaonewa. Ukweli ni kwamba dunia haijawahi kuwa sawa na haitokuja kuwa sawa. Unaweza kufanya kazi kwa bidii na maarifa halafu mwenzako akaja kuchukua pongezi zako, unaweza kufanya haki na bado ukaingizwa kwenye uhalifu, unaweza kuwa na elimu kubwa na ufaulu mzuri ila ambaye hana elimu ndio akawa bosi wako kazini, unaweza kuwa na roho nzuri na ukazulumiwa, haya yote ni maisha.
9. Chocote kitakachotokea jua huo sio mwisho wa dunia.
Hata litokee jambo baya kiasi gani kwenye maisha yako kama bado upo hai basi jua unaweza kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Usikubali changamoto yoyote iharibu maisha yako, jua itapita na maisha yataendelea. Kila kitu kinapita, hata hayo magumu unayopitia yatapita, hakikisha maisha yako yanakuwa imara baada ya mapito hayo.
10. Safiri.
Jitahidi sana katika kipindi hiki jitahidi sana usafiri sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Kusafiri na kwenda sehemu ngeni kunakufanya ufikiri tofauti na uwe na mtizamo mpana sana kwenye maisha yako. Kama umezaliwa moshi ukasoma na kukulia moshi, ukafanya kazi na kuishi moshi utakuwa na mawazo mgando sana kwa sababu unaona mambo na changamoto zile zile kila siku. Ila unaposafiri na kuishi na watu wenye maisha na mitizamo tofauti na ya kwako hapo ndipo unapoweza kujifunza zaidi.
11. Furahia kila hatua ya maisha yako.
Kama unatamani nyakati ngumu zifutike kwenye maisha yako hujajua umuhimu wake. Kila changamoto unayokutana nayo inakujenga uwe mtu bora zaidi. Furahia kila hatua unayopitia kwenye maisha yako, iwe ni ya kufurahisha au ya kuumiza. Kuna somo muhimu la kujifunza kwenye kila jambo na kila mtu unayekutana naye.
Kijana haya maisha ni ya kwako, yapangilie maisha yako na uyaishi. Usiogope changamoto unazokutana nazo hizi ndizo zinazokusaidia ukue zaidi. Usilalamike wala usilaumu yeyote, chukua hatua juu ya maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika wakati huu mgumu sana kwenye maisha yako, nina imani utavuka wakati huu ukiwa salama na ukiwa na malengo makubwa.
Kumbuka , TUKO PAMOJA.
Mshirikishe kijana mwenzako mafunzo haya ili naye ajifunze, bonyeza kitufe cha facebook hapo chini kuwashirikisha wengine.



No comments: