MREMBO WA WA KIJIJI SEHEMU YA KUMI NA NANE-18




MREMBO WA WA KIJIJI


      SEHEMU YA KUMI NA NANE-18

"Kwa sababu tayari wanakijiji wamekishtukia kijiji, kwa maana hiyo kaletwa mtaalamu wa kuwaumbua wachawi." Alisema mkuu wa kundi hilo la kina bibi Pili. Ukweli habari hiyo iliwachanganya sana wachawi hao,  kila mmoja alijikuta tumbo joto akihofia kuumbuliwa mchana kweupe. Jambo ambalo lilizua ukimya kila mmoja akawa anatafakari kivyake ndani ya akili yake. Lakini baadaye ukimya huo ulitoweka mara baada mkuu wao kusema "Hivyo basi ningependa kuona kila mmoja anajilinda kivyake kwa ukamilifu, lakini pia nawasihi mtu yoyote ikitokea kakamatika basi asitaje siri zetu hatakama ni mimi nitakaye kamatwa katu sitiweza kuvujisha siri za kundi langu, kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama kwa wale wajanja ambao wamefanikiwa kumkimbia yule mtaalamu "

" Sawa mkuuu, ila nina jambo nataka kulifahamu kwa undani zaidi kuhusu huyo mtaalamu"

"Jambo gani?.." Mkuu  alihoji baada kusikia kibaraka wake akihitaji kufahamu ukweli zaidi kuhusu mtaalamu aliyeletwa na wanakijiji ili kuwaumbua wachawi wa kijijini cha Ndaulaike.

"Kwani huyo mtaalamu ananini hasa mpaka athubutu kutuweka tumbo joto? Je, ananguvu nyingi kuliko sisi hadi tufikie hatua ya kumkimbia? Au wewe kama wewe umemuonaje labda" Alisema kibaraka huyo. Mkuu wake alipoyasikia maneno hayo alikaa kimya kwanza kisha baadaye kidogo akasema "Ukweli ndugu zangu kuhusu yule mtaalamu  simfahamu vilivyo uwezo na nguvu alizo nazo, na yote ni shauri ya papara ya kuwakimbia wanakijiji baada kutishia kunidhuru" Alisema hivyo mkuu huyo alimaarufu Mwenyekiti wa kijiji.

 Naam! Siku zote kundi la kinabibi Pili lilikuwa likiongozwa na mwenyekiti, na hata lile suala la kumgeuza ng'ombe mke wa mzee J mwenyekiti ndiye aliyehusika achilia mbali kuitembeza treni mahala pasipokuwa na reli.

"Ama tuachane kwanza na hili suala la mzee J tumalizane na huyu kiherehere anayetaka kuvuruga mipango yetu?.." Alihoji mwenyekiti.

 "Hilo nalo jambo jema mkuu, kwa sababu tusipo ziba ufa tutajenga ukuta. Kwahiyo maoni yako, yako sawa bila kipingamizi ama mnasemaje wenanzengo?"  Aliongea bibi Pili na kisha akawageukia wenzake ambapo ndelemo na vificho vilisikika wachawi hao wakimuunga mkono bibi Pili.

"Basi hilo limekwisha ingawa kwa sasa mimi maisha yangu nitakuwa naishi kama kunguru, hili lisiwape shida sana ila naomba vijana wangu Masile na Tobi muifanye kazi hii kwa haraka sana iwezekanavyo"

"Kazi gani mkuu?.." Tobi kijana aliyerithishwa uchawi na marehemu bibi yake alihoji. "Nataka mumfuatilie mahali anapoishi huyu mtaalamu kisha mje mnipe majibu" Alijibu mkuu. Mh. mwenyekiti.

 Vijana hao wawili walitii agizo la kiongozi wao, bila kupoteza muda walipotea wakaenda kutembea nyumba baada ya nyumba kumsaka mtaalamu. Uzuri walijua nyumba ipi inaingilika na nyumba ipi isiyoingilika kwa maana hiyo nyumba isiyoingilika ni ile ambayo ina mchawi kama walivyo wao, na ile nyumba inayo ingilika ni ile ambayo haina mchawi. Kwa muda wa nusu saa Masile na Tobi wakirudi.

 "Mkuu. Mtaalamu tumejua yupo nyumba gani.." Alisema Masile. Mh. mwenyekiti akamuuliza "Nyumba gani?.."

"Yupo kwa balozi, amempokea na kumpa hufadhi" Alijibu Masile.

"Ahahaha hahahaha" Vicheko vilisikika, wachawi wote waliokuwepo mahala hapo waliangua vicheko. Na mara baada ya kukatisha vicheko vyao mkuu wao akasema "Safi sana, ama hakika nyie ni wazee wa kazi sikudhania kama mngeweza kuniletea taarifa hizi. Halafu anaoneakana mtu wa kawaida sana, hauwezi moto wetu huyu mtu. Maana kama angelikuwa ni mtu hatari basi angejua ni nani anamfuatilia, ama aliwaona?.."

"Hapana mkuu, na kizuri zaidi amelala usingizi mzito sana" Alijibu Tobi. Kwa mara nyingine wachawi hao wakacheka sana "Aha hahahah hahahah hahahah" Punde si punde mkuu wao akanyanyua mkono juu kisha akashusha chini  kwa nguvu ghafla ikitokea ngoma, papo hapo akaanza kuitumbuiza kitendo kilicho weza kuzua fujo za ina yake wote kwa pamoja wakaanza kucheza na kuimba nyimbo za asiri.

   *********
Huku nyumbani kwa mzee J, kijana Chitemo alikosa lepe la usingizi. Muda wote alikuwa akimfikiria Saidon, hofu na woga vilitamalaki moyoni mwake akihisi kuwa huwenda akamkosa Chaudele kisa kijana huyo. Jambo hilo lilimchangaya sana hali iliyompelekea kuukosa usingizi kabisa ambapo mwisho alimuwa kunyanyuka kutoka kitandani akakaa kisha akawasha kubatali, punde si punde mzee Bidobido alionekana chumbani mwake, mzee huyo alikuwa yupo katika mavazi yake ya kichawi "Chitemo mbona huna raha? Vipi kuna tatizo?.." Alihoji mzee Bidobido, Chitemo aliposikia sauti ya baba yake mdogo alishtuka akainua uso wake kutazama kwenye kona ya chumba akamuona baba yake mdogo akiwa yupo kwenye mavazi ya kazi "Daah! Bamdogo mimi nahisi wewe na baba njama yenu ni moja tu. Mnanizuga kwamba mnafanya mkakati juu ya mimi kumuoa Chaudele lakini sivyo, mkakati gani huo usiotimia? Kama mmeshindwa simseme tu?.."

"Aah Chitemo useme hivyo bwana, unajua ngoja leo nikwambie ule ukweli sasa" Alisema mzee Bidobido. Chitemo akahoji "Ukweli gani?.."

"Ukweli ni kwamba mzee Nhomo baba wa binti yule unayemtaka hataki wewe umuoe binti yake.." Alisema mzee Bidobido, Chitemo akashtuka kisha akarudia kuhoji "Inamaana mimi simfai Chaudele? Na kama ni hivyo posa mmechukua?.."

"Hapana na hivi tupo katika vita nzito sana kwa sababu mzee Nhomo posa kaila na binti yake hataki kumtoa. Na hatakama akitulipa posa yetu, sisi hatukwenda kwa niaba ya kulipisha bali kwania ya kuchukuwa mke. Hivyo basi kuhusu hilo wewe ondoa shaka mke utapata tu kwa hali na mali " Alisema mzee Bidobido kwa msisitizo.

"Keli kabisa baba?.. "Aliuliza Chitemo huku akiachia tabasamu.

"Hahahaha " Akacheka mzee Bidobido kisha akajibu "Habari ndiyo hiyo" Kwisha kujibu hivyo upesi akapotea. Chitemo akashusha pumzi kisha akalala huku moyoni akiwa na matumaini kibao.

   Kwingeneko chini ya mti mkubwa kuliko yote kijijini, alionekana mzee J akiilia mizimu ili impe uwezo mara dufu wa kukabiliana na vita nzito inayo mkabili kwa sababu kama ni damu katu hana uwezo wa kumshinda mzee Mligo na kisha achukue damu ya mjukuu wake ambaye ni Saidon.

"Unataka nini Jaruooo?.." Mizimu ilimuuliza mzee J.

Mzee huyo huku akitetemeka akajibu "Naombeni mnipe njia nyingine, nipo chini ya miguu yenu"

"Hapana hiyo hiyo kama utashindwa hilo ni jukumu lako"  Ilisema mizimu hiyo na kisha ikapotea. Mzee J akalalama kuiita kwa kilio lakini haikuweza kurudi, na hivyo J kinyonge alinyanyuka akapiga mguu chini mara tatu  akapotea chini ya mti huo mkubwa. Siku hiyo kwake ilikuwa siku ya mapumziko, kwani hakuitisha mkutano wala kikao cha dharura. Akili yake  ilitulia, aliwaza ni vipi ataweza KUFUA DAFU kwa mzee Mligo? Kwani alihitaji damu ya mjukuu wake ili imuwezeshe kufanikisha mambo yake. Kwanini ilihusishwa damu ya Saidon? Kwa sababu kijiji kizima kijana huyo ndiye aliyesalia ambaye hajalishwa vyakula ama kitu chochote cha kichawi, damu yake Saidon ni kama dhahabu katika mlima wa sayuni.

   Kesho yake asubuhi palipo pambazuka, kijiji kizima cha Ndaulaike gumzo ilikuwa ni kijana Saidon tu. Mabinti walimzungumzia yeye, wazee walimsifia yeye wamama walimpenda pia kutokana na kile alichokionyesha siku ya jana. Hapo Saidon akabatizwa jina Pele wa Ndaulaike.

Kabla hata Saidon hajaamka vijana mbali mbali walifika nyumbani kwa mzee Mligo kwa dhumuni la Kuja kumuona  pia kumpongeza kwa kuwatoa kimaso maso "Jamaa wewe unajua sana kiukweli sema huna bahati ndugu yetu" Alisikika akisema moja ya vijana waliokuja nyumbani kwa mzee Mligo. Saidon aliposikia maneno hayo akatabasamu kisha akauliza "Kwanini?.."

"Kijiji hiki sio kabisa uchawi umekithiri sana, mfano jana umecheza kandanda Safi utashangaa wanaanza kukuroga" Alisema kijana huyo, maneno ambayo yalimshtua Saidon ambapo pole pole akahofia usalama wake. Lakini wakati akiwa katika hali hiyo kijana wa pili naye akasema "Ila usiwe na shaka kuna mtaalamu yupo kaja kwa niaba ya kuwaumbua hawa wachawi, na leo ndio leo kila kitu kutakuwa hadharani" Mzee Mligo akiwa ndani aliyasikia vilivyo hayo maneno ya  kijana huyo, na hapo awali alisikia tetesi za kumuhusu mtaalamu aliyeletwa.

"Doh naanza kuamini sasa, mmh hapa kazi ipo,Mligo naenda kuumbuka mchana kweupe mbele ya mjuu wangu" Alijisema maneno hayo mzee Mligo huku moyoni akiwa na hofu dhufo lihari, kamwe hakutaka mjukuu wake ajue kuwa yeye ni mshirikina, lakini pia hakuwa tayari kuumbuliwa na kupoteza uwezo wa kumlinda dhidi ya maadui wanao mzunguka ndani ya Ndaulaike.

Lakini kipindi Mwenyekiti, mzee J pamoja na mzee Mligo walipokuwa wakimuhofia mtaalamu kiboko ya wachawi aliyetia magumu ndani ya Ndaulaike, upande wa pili kijijini humo aliingia mgeni. Mgeni huyo alikuwa amevaa suti nyeusi na viatu vyeusi huku mgongoni akiwa amebeba begi ndogo na mkononi akiwa ameshika Biblia. Mgeni huyo alitembea kwa utashi na madaha, kichwa chake kikiwa kimelowa jasho shauri ya jua kali ndani ya kijiji hicho cha Ndaulaike..

MAMBO HAYO MIMI SIMO.. usikose sehemu ijayo. Mambo yanazidi kuwa makubwa..
    Na sheria ya Ndaulaike lazima mtu ajaribiwe..
SHEA MARA NYINGI ILI USIPITWE MUENDELEZO.. pia unaweza ukashea mara nyingi ukapata bahati ya kuipata Inbox.. Kazi kwako.



No comments: