MREMBO WA WA KIJIJI SEHEMU YA NANE-08




MREMBO WA WA KIJIJI


     SEHEMU YA NANE-08

Saidon alimtazama Chaudele kwa jicho pembe, na Chaudele naye alipomtazama Saidon. Saidon alimkonyeza, kitendo ambacho kilimfanya Chaudele kutabasamu. Hapo ndipo kijana Saidon alipohisi kumuhitaji mrembo huyo, iwe usiku iwe mchana kwani alimpenda kwa vyovyote vile.

 "Ndio mzee mwenzangu naona tumepata mgeni kijijini kwetu" Wakati Saidon na Chaudele walipokuwa wakichokozana, upande wa pili mzee Nhomo alisikika akimwambia  mzee Mligo. Mligo alicheka kidogo kisha akajibu "Eeh mjukuu wangu huyo, kafika siku ya jana"

"Anhaa doh kanaonekana kastarabu sana" Aliongeza kusema mzee Nhomo.
 Mligo akajibu "Kama babu yake" Hapo kicheko kilizuka, wote kwa pamoja wakaangua kicheko. Baada ya kicheko hicho, mzee Mligo akasema "Haya sasa fungu moja bei gani?.."

"Hapa bwana fungu shilingi elfu mbili na mia tano tu" Alitaja bei mzee Nhomo. Mzee Mligo aling'aka baada kusikia bei hiyo, na mwishowe akasema "Ndugu yangu mbona upo juu sana?.."

"Mbona unalia mzee mwenzangu? Haya niambie wewe unashilingi ngapi"

"Elfu mbili tu. Nifanyie uungwana ili mjukuu wangu akale nyama ya swala bwana " Alijibu mzee Mligo.

"Sawa leta hiyo hela" Upesi mzee Mligo alizama mfukoni akachomoa shilingi elfu mbili akamkabidhi mzee Nhomo. Kisha Nhomo naye akamkabidhi mzee Mligo nyama. Hapo akamtaka Saidon na mwenzake wakuitwa Maige waondoke kurudi nyumbani. Saidon aliponyanyuka kutoka sehemu aliyokuwa amekaa alimtazama Chaudele kwa mara nyingine kisha akampungia mkono wa kwaheri, ambapo mrembo Chaudele  bila hiyana akiwa amejawa na tabasamu pana alijibu kwa kumpungia mkono kijana Saidon. Mchezo wote huo Maige alikuwa akiuona na hivyo alipanga kumueleza rafiki yake ukweli kuhusu mrembo Chaudele. Lakini wakati Maige analipanga Hilo, mara ghafla nyuma yao alionekana mzee Nhimo akiwajia mbio huku akisema "Mligo Mligo simama kidogo tafadhali"

Mzee Mligo aliposikia sauti ya mzee Nhomo ikimtaka asimame, haraka sana alisimama kisha akawaambia Saidon na Maige watangulie "Bwana Mligo umesema kijana wako kaja jana?.. "Aliuliza mzee Nhomo baada kumfikia mzee Mligo.

" Ndio, kwani kuna tatizo? "

" Aah hapana  lakini mzee mwenzangu naomba umuase mapema mjukuu wako, ujue hapa kijijini kuna vita kubwa mno ya kichawi inaendelea chini chini. Kwahiyo muelekeze mjukuu wako atulie asije akakusababishia makubwa" Mzee Mligo alishtuka baada kuyasikia maneno ya mzee Nhomo.

 "Vita. Vita gani tena?.." Aliuliza kwa taharuki kubwa. Mzee Nhomo alishusha pumzi ndefu kisha akasema "Inamaana upo hapa kijijini hujui kuwa mzee J kanitangazia uhasama? Ujue J ni mtu ambaye nilikuwa namuheshimu sana hapa kijijini. Ila kupitia hili, nimemdharau tena namuona kama mbwa tu"

"Mungu wangu, chanzo cha yote hayo ni nini?.."  Kwa mara nyingine tena mzee Mligo alihoji kwa mashaka makubwa, ndipo mzee Nhomo alipoanza kumsimulia kisa hasa ambacho kimepelekea wawili hao kuwa na uhasama. Lakini wakati mzee Nhomo anamsimulia mzee Mligo chanzo cha ugomvi wake na mzee J. Upande mwinginine Maige alisema "Saidon..."

"Naam Maige"

"Bila shaka umemuona yule binti pale tulipotoka kununua mboga?.." Aliuliza Maige. Aliachia tabasamu kidogo Saidon kisha akaitikia "Ndio nimemuona na nimetokea kumkubali sana. Nafikiri yule ndio atakuwa mpenzi wangu kwa muda wote nitakao kuwa hapa kijijini. King  nimesema" Jibu hilo la Saidon lilimshtua sana Maige ambapo alishusha pumzi kwa nguvu kisha akasema "Saidon rafiki yangu. Kwa upande wangu napenda kukushauri yule binti achana naye kabisa"

"Kwanii Maige? Kwani kaolewa?.." Alirudia kuhoji Saidon.

 "Hapana hajaolewa ila pale alipo kuna jamaa mmoja anamfukuzia kwa udi na uvumba. Na istoshe jamaa alishatangaza ubaya kwa kijana yoyote atakaye muona naye" Alijibu Maige. Maneno hayo yalimshangaza sana Saidon ambapo alikaa kimya kidogo huku akiyatafakari. Baada ya kimya hicho mwishowe akasema "Kwanini jamaa anaamuwa kuwatangazia unyama huo. Kwa kipi hasa alicho nacho. Je, mzuri sana. Ama anapesa nyingi? Au anakipi hasa cha kutegemea"

"Ahahaha hahahah" Maige alicheka kidogo kisha akajibu "Vyote hivyo ulivyotaja wala hana, ila anachojivunia jamaa ni baba yake. Baba yake mchawi wa kuogopwa hapa Ndaulaike"  Maneno hayo yalimtisha sana Saidon alipigwa na butwa, lakini wakati yupo katika hali hiyo punde si punde babu yake alifika na hivyo wakaendelea na safari wakati huo Saidon akiwa kichwa chini akiyatafakari maneno aliyomwambia Maige. Ukweli alimpenda sana mrembo Chaudele ila tatizo lipo hapo. Uchawi.

      Kwingineko, nyumbani kwa bibi Pili alionekana bibi huyo akila chakula na mjukuu wake. Viazi vilivyochemshwa na karanga za kukaangwa ndicho chakula walichokuwa wakila  muda huo. Na wakati wanakula, maongezi kadhaa yaliendelea ambapo bibi Pili alisikika akisema "Pili mjukuu wangu. Unajua mimi bibi yako nakupenda sana, kwahiyo sitaki nikuone ukijutia kuishi. Nitakutetea pindi utakapo onewa. Na ili kuthitisha hilo ngoja uone kile nitakacho muonyesha Chitemo"

"Hahaha hahaha" Alicheka Pili na kisha akasema "Yani bibi we acha tu, kisa Chaudele amedai eti hanipendi hanitaki kwa maana hiyo alikuwa namimi kwa niaba ya kunichezea"

"Na ndio maana nataka nimuonyeshe kuwa wewe sio uwanja wa mazoezi, bahati yake hujanasa mimba   naapa mimba hiyo angeibeba yeye na mwisho wa siku angejifungua chura mjinga mkubwa yule" Alidakia kwa kusema hivyo bibi Pili huku akionyesha kugazibika. Sasa maneno hayo yalimpa faraja Pili kwani alijua fika bibi yake akiongea neno ni mwepesi kutekeleza.

   Usiku ulipoingia, upande wa mzee J alirudia tena pale msufini. Safari hiyo hakuitaka mizimu bali alipofika tu mara ghafla kundi la wachawi lilitua. Hapo nyimbo na ndelemo zilifuatia, shangwe hizo zilidumu kwa muda wa nusu saa kisha mzee J akapasa sauti kuzikomesha.

"Jamani ahsanteni kwa kutii wito wangu. Najua wengi mtakuwa mnajiuliza leo nina kipi kipya" Baada ya kimya, mzee J alisema.

"Ndio"

"Naam"

"Hasawaaaa" Waliitikia wachawi hao kwa sauti tofauti tofauti. Mzee J  kiongozi wao alikaa kimya kidogo, alikunywa mara tatu damu iliyo kuwa ndani ya kibuyu, kisha akaendelea kusema "Sawa Sawa. Basi usiku wa leo tunakazi ngumu sana. Kwanza mnatambua kuwa kijijini kwetu kuna kijana mgeni kaingia?." Swali hilo halikujibiwa kwa haraka lakini punde zikasikika sauti mbili tatu zikiitikia "Ndioooo"

"Taarifa hiyo ninayo mkuu"

"Wangapi wanafahamu hili jambo? Nyoosheni mikono Juu" Aliongeza kusema mzee J. Wachawi hao wakanyoosha mikono juu.

" Moja mbili ta... Naam shusheni nimewaona. Sasa basi Nafikiri kila mmoja anaelewa utaratibu wetu hasa timu hii ya mzee Jaruo.."

"Ndio mkuuu" Walitikia wachawi hao. Mzee J akaongeza kusema "Basi hakuna cha kupoteza, utaratibu wetu ni ule ule. Mgeni akija lazima ajaribiwe ili kupima uwezo wake. Haya kila mmoja apande ungo wake safari kuelekea kwa mzee Mligo" Amri hiyo ilitekelezwa haraka sana iwezekanavyo, punde si punde wachawi hao walipanda nyungo zao wakapaa angani mithili ya  mbayuwayu kwa kasi ya ajabu, walielekea nyumbani kwa mzee Mligo kwa dhumuni ya kumfuata kijana wa mjini Saidon ili kumjaribu. Lakini wakati wachawi hao walipokuwa wameligubika anga la kijiji cha Ndaulaike wakielekea kwa mzee Mligo mara ghafla...

NI NINI KIMETOKEA? Je, mzee Nhomo kakiwasha? Au bibi Pili kalianzisha? SAIDON yupo matatani. Hayo na mengine mengi tukutane sehemu ijayo.
  SHEA MARA NYINGI ILI USIPITWE NA KIGONGO HIKI.



No comments: