Riwaya:THE TRUE LOVE. SEHEMU YA TATU (03).
Riwaya:THE TRUE LOVE.
SEHEMU YA TATU (03).
Na ukweli wenyewe ulihusiana na kifo cha baba Imma kwani katika muda ule baba huyo alifariki dunia ghafla akiwa kitandani kwake na haikujulikana aliugua ugonjwa gani.Kiukweli taarifa hiyo kutoka kwa mama yake mzazi ilimuumiza sana kijana Imma hadi akawa anahisi dunia tayari imeshaanza kuwasaliti bila kosa.Imma alilia lakini katu ukweli ukabaki kuwa vile vile kwamba baba yake ndo hivyo tena ameshaenda.Kuna muda wakati akilia na kunyamaza alifikia hatua ya kuanza kumlaumu Mungu kwamba amewaacha lakini mama yake alimpa moyo huku akimsihi atulie kwani Mungu anawapenda na anawawazia mema siku zote."Mama hivi sisi Mungu tumemkosea nini? Tumemkosea nini Mungu maana kila gumu linatupata sisi tu,kwa nini lakini?" Hayo ndo yalikuwa maneno ya kijana Imma maana kama ni Uvumilivu ulikuwa umemshinda kwani uchungu uliugubika sana moyo wake ."Mwanangu Mungu bado naamini anatupenda na ninavyojua mimi hajatuacha wala hakuna tulichomkosea,m
wenyewe ndiye aliyemtoa baba yako na amemtwaa pia japo inaumiza lakini siku zote yeye atabaki kuwa Mungu na jina lake litazidi kutukuzwa".Ni maneno kutoka kinywani kwa mama Imma ,mama alijipa ujasiri wa hali ya juu akaamua kuyatamka mbele ya mwanae.Basi mara baada ya kumaliza kuyatamka aliingia ndani ya chumba kile kuangalia utaratibu wa kufanya......Ndani ya siku hiyo hiyo watu wakataarifiwa kuhusiana na msiba huo na siku ya mazishi ikapangwa.Siku yenyewe ilikuwa ni juma nne ya mwezi huo huo wa pili ,,,siku hiyo ilipofika na mnamo mishale ya jioni saa kumi ,baba Imma alizikwa ndani ya maeneo ya Makaburi ya kanisa moja la Kirutheri lililokuwepo hapo mjini,hadi kufikia mida ya usiku usiku saa moja hivi watu wengi tayari walikuwa wameshatawanyika kurudi makawao wakabaki watu wachache tu akiwemo mama mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina la mama Rachel ,cha kushangaza katika huo msiba Wanjera hakuja pamoja na kwamba zile taarifa alizipata .Hadi zinamalizika siku tatu bado binti huyo hakuwa amefika nyumbani kwao hata kwa bahati mbaya.Wiki moja tu ilipokatika bila ya yeye kuonekana nyumbani mama yake alianza kwanza kwa kumsamehe popote alipo kisha akamuachia Mungu tu,ina maana kwa muda huo ni Imma pekee ndiye aliyekuwa yu bega kwa bega na mama yake katika kipindi hicho kigumu.Basi msiba ulimalizika na ukawa umekatika mwezi mmoja maisha yakaendelea......hayo yote kijana Imma aliyasahau akaamua kuendelea kufanya kazi kwa kadri ya uwezo wake huku akiamini ridhiki yake ipo na katika ule mtihani wa kidato cha sita aliokuwa ameufanya atafaulu tu na atazidi kusonga mbele.Siku moja akiwa amejipumzikia zake shambani karibu na ploti zake za mboga mboga chini ya mti aina ya Mkuyu huku akiwa amejiinamia akisinzia sinzia.Kwa mbali kwenye upenyo wa kinjia chembamba cha kuingilia ndani ya bustani ile alionekana binti mdogo mweupe mwenye umri wa miaka kama kumi na mbili hivi akija.Msichana huyo mtashi na asiyeliacha tabamu usoni mwake alikuwa amevaa sketi nyeusi na blauzi nyekundu yenye maua meupe na kwa kumtazama tu usingesita kuja na jibu la kusema huyu ni mtoto kutoka katika familia yenye uwezo,na ndivyo ambavyo ilikuwa.Binti aliziacha hatua chache tu nyuma akajikwaa kwa bahati mbaya akawa amedondoka chini na hapo hapo akaanza kulia kwa uchungu.Imma akiwa pale mtini,pamoja na kuendelea kusinzia lakini alishtuka baada ya kusikia sauti ya mtu akilia,akainua kichwa chake akawa anayaangaza macho huku na huko asimuone huyo mtu anayelia.Alisema hapana hebu ngoja nisimame......alisimama akaanza kuyazungusha macho yake kila upande,alipoyaz
ungusha tu nyuma yake alishtuka kumuona binti mdogo akihangaika kusimama huku akilia akaamua kumfuata msichana huyo kwa mwendo wa haraka na akawa amemfikia .Baada ya kumfikia hakujisumbua kuanza kumuuliza maswali yasiyokuwa na maana zaidi ya kumsaidia kwanza,alimnyanyua na uzito wake akawa amembeba,maana hako kasichana pamoja na kuwa na huo umri lakini kalikuwa kameshiba.Imma alikabeba juu akawa anakapangusa yale machozi huku akijitahidi kukatuliza hatimaye kakatulia nako kakawa kanamtazama sana usoni."Pole mdogo wangu " Alisema Imma mara hii akikashusha chini."Asante Kaka yangu nimeshapoa sijaumia" kalisema na kisha kakawa kanatabasamu tu na urembo wa kenyewe ukawa unaonekana dhahiri.Kusema ukweli kama kangekuwa katoto kangu mpaka hapo ningetafuta mbwa tu wa getini maana Mh!! Acha kabisa sema ndo hivyo tena.Basi Imma akaandaa maswali ya kukauliza."Mtoto mzuri samahani unaitwa nani?" Aliuliza Imma,kakacheka kidogo kabla ya kulijibu hilo swali."Mi naitwa Jack mtoto wa mama Rachel naishi mtaa wa kati tu pale".Kaliongea utadhani ka mtu kazima."Aha!! Unasoma darasa la ngapi Jack?" Imma aliuliza kwa mara nyingine tena."Mimi nasoma darasa la tano".Kalimjibu kakaendelea kumtazama Imma usoni kana kwamba kuna kitu kalikuwa kakikichunguza kutoka kwake."Jitahidi kusoma mdogo wangu sawa ee? Jitahidi sana basi hapa umekuja kununua nini nikupe?" Alisema Imma ."Nimekuja kununua bilinganya mama amenituma nije ninunue huku,ila na wewe Kaka naomba uniambie jina lako". Kalizungumza kakampa nafasi Imma aongee."Mimi niite Kaka Imma sawa Jack?" Alisema Imma baadae akaja na kukauzia zile bilinganya,wakati wa kuondoka kalimsihi sana waondoke pamoja kakamtaarifu mama wa kenyewe ukarimu wa kijana Imma ,Imma mwenyewe alikataa kataa lakini mwisho akakubali wakaondoka.Walikuja kulifikia jumba moja kubwa la kifahali,geti likafunguliwa wakaingia,,,sasa Imma baada ya kuliona kwa uzuri jumba hilo aligoma kulisogelea zaidi na zaidi na mbeleni karibu na kibalaza kipana cha jumba hilo alionekana binti mmoja mweupe dada ake na hako ka Jack akiwa amekaa akichezea chezea simu.Msichana huyo alikuwa akiitwa Rachel na alikuwa na umri wa miaka kumi na nane.Kitendo kilichomfanya Imma agome kulisogelea lile jumba alikuwa amejitizama na kujiona yeye si kitu hususani ukilinganisha na zile nguo ambazo amezivaa.Sasa kale kasichana baada ya kumuona Imma anaona aibu kusogea nako mbele kalimfuata kakamshika mkono wa kulia kisha kakaanza kumvuta ili kwa pamoja wasogee.Wakati kakiendelea kufanya hivyo mara mama Rachel akaonekana akitokea ndani akasimama mbele ya yule binti aliyekuwa amejikalia zake akajishika kiunoni."Wewe Jack kwa nini unamfanyia hivyo huyo kijana? Imma karibu ndani ".Baada ya mama huyo kuyazungumza hayo maneno,Imma alishtuka akawa anashangaa huku akijiuliza mama huyu jina langu amelifahamia wapi maana katika kumbukumbu zake hakuwahi kumuona ila ninaweza kusema itakuwa labda alisahau kwani mama huyo alikuwa ni mmoja wa waombolezaji wakubwa kipindi cha msiba wa baba yake.Hivyo alibaki kimya tu akaongozana na Jack hadi pale kibalazani."Jack hebu mfuatie kiti Kaka Imma akae".Alisema mama Rachel,muda huo huo Jack akaingia haraka ndani akaziweka zile bilinganya akachukua kiti na kutoka nacho nje,alifika akakiweka mbele ya Imma,Imma akakaa ."Rachel mbona husalimiagi wageni wewe? Kulikoni?" Aliuliza mama yake lakini Rachel angali akiendelea kuchezea simu yake hakumjibu chochote mama yake zaidi alisimama akamtazama Imma kidogo tu na kuondoka eneo hilo akaingia ndani na kwenda kutulia humo.
Mama huyo kile kitendo cha bintiye kuondoka kilimpa tafsiri kichwani mwake akajua tu binti huyo amemdharau Imma kwa jinsi alivyo lakini wala hakujali sana."Imma karibu nyumbani jisikie vizuri wala usiwe na hofu".Alisema mama Rachel,"Nashukuru mama,shikamoo?" Aliitikia Imma kisha akasalimia."Marahaba mwanangu,,,ila nikupe pole kwa msiba uliowapata,pole sana maana mmeondokewa na mtu mhimu maishani".Alisema mama huyo Imma akanyamaza kama dakika mbili hivi baadae akazungumza......kwa muda wote huo kale kasichana ka Jack bado kalikuwa kamesimama mbele yao na hakakuwa na mpango wowote wa kuondoka hapo."Mama mimi nimeshapoa kitambo sana kwani hapa duniani sote tu wapitaji tunapita.....Baba yeye ametangulia na sisi tutamfuata baadae".Maneno hayo,Imma aliyaongea kwa sauti ya huruma sana kiasi kwamba kale kasichana kalijikuta kakianza kulengwa lengwa na machozi."Pole sana mwanangu,ila yote ni maisha tu cha msingi nakuomba upambane mwanangu najua wanaokudharau ni wengi sana ila ipo siku watakusalimia kwa heshima,We Jack bado unangoja nini hapa? Si uende ukacheze huko maana muda sasa nakuona upo tu hapa unakodoa kodoa mimacho yako hiyo". Aliongea mama huyo lakini kasichana kakagoma kuondoka."Mama niondoke niende wapi sasa? Mimi mama siwezi kuondoka hapa maana sina pa kwenda".Kaliongea mama wa kenyewe akashindwa cha kukafanya akaishia kucheka tu huku akitikisa kichwa chake."Sasa Imma kuna kiasi kidogo nilikiandaa ili nije niwaletee pale nyumbani ila kwa vile umefika hapa ngoja nikifuate nikupe".Alisema mama Rachel kisha akaondoka pale na kuingia ndani.Alipoingia tu ndani,ka Jack kalikuja haraka hadi nyuma ya kijana Imma....Kumbe kalikuwa kameficha chanuo,haraka kalilitoa hilo chanuo kakaanza kuzichana nywele za Imma zilizokuwa zimevurugika muda huo kakizichezea chezea.Kalipomuona mama wa kenyewe akija kaliacha hima kufanya hivyo kakarudi na kusimama eneo lile kalilokuwa kamesimamia."Im
ma naomba uipokee hii bahasha,kilichomo humo ndani ndicho kitakuwa zawadi yangu kwako". Aliongea mama Rachel akamkabidhi ile bahasha Imma."Asante sana mama Mungu akubariki kwa moyo wako huu wa upendo".Sasa wakati Imma akimalizia kuyazungumza hayo....
**********************
Mara nje ya geti ikasikika gari ikipakiwa na hazikupita hata dakika tano akaonekana baba mmoja wa makamo akija akawafikia akawa anamtazama Imma kuanzia juu ya kichwa hadi chini ya miguu yake ."Baba shikamoo?" Alisalimia Imma lakini yule baba hakuitikia,aliyageuza macho yake akawa anamtazama mkewe mara hii kwa macho ya hasira alipojiridhisha aliongea "Mama Rachel hii takataka wewe ndo umeileta humu ndani? Huoni kwamba inatoa harufu ya kinyesi?" Kwa dharau huku baba huyo akijiona yeye ndiyo yeye aliyauliza hayo maswali.Mama Rachel hakumjibu moja kwa moja mumewe alibaki kimya akawa anamtazama tu,kwa upande wa Imma yeye alikuwa amejiinamia na kujiona kama hafai kuwepo pale.Mama Rachel aliendelea kubakia kimya baadae akaamua kumjibu tu mumewe."Baba Rachel siyo vizuri kumuita binadamu mwenzako takataka unakuwa unakosea sana kuyaongea maneno kama hayo".Alisema mama Rachel,yule baba akakasirika mno."We kijana sitaki nikuone humu ndani simama uanze kuondoka,kwanza unatoa harufu mbaya ya ajabu".Alisema baba Rachel na kumfanya Imma asimame ili aanze kuondoka,kabla hajaondoka Ka Jack kalimsogelea haraka kakamrudishia pale alipokuwa amekaa."We mtoto sitaki upumbavu acha hiyo takataka itoke".
ITAENDELEA...............................

No comments: