Wazazi wananilazimisha nimuoe mwanamke niliyezaa nae
Nina mpenzi tunayependana ambaye tulianza kudunduliza fedha kwa ajili ya kutimiza malengo ya baadaye tuliyojiwekea. Lakini wazazi wangu wananilazimisha nimuoe mwanamke mwingine ambaye nilizaa naye.
Wazazi wako wana nia nzuri ambapo wanataka mjukuu wao alelewe na baba na mama, wakiamini hiyo ndiyo njia salama ya malezi na huo ndio ukweli. Shida iliyopo ni kuwa inawezekana wewe na mzazi mwenzako hampendani kama ilivyo awali (ingawa hujalieleza hili). Naamini hakuna ndoa ya kulazimishwa, familia yako ikifanya hivyo mnaweza kuoana lakini hata huyo mtoto msilee vema kwa sababu mtakuwa na migogoro. Kama bado unampenda mzazi mwenzako na mliachana labda kwa sababu ya ujana wasikilize wazazi wako na ujiridhishe kuwa naye anakupenda, utafute mbinu ya kumueleza huyo mpenzi wako kwa faida ya mwanao pia.
Kama humpendi tena na yeye ameshakata tamaa ya kuwa na wewe usikubali kufunga naye ndoa kwa shinikizo la wazazi kwa sababu hamtadumu katika ndoa.
Nafasi unayo bado, kaa chini tafakari kwa kina kama unaweza kufanya haya niliyokuambia, kisha wakabili wazazi uwaeleze msimamo wako ukiwa na hoja za msingi. Naamini watakuelewa.
Mume wangu anampenda anamuheshimu na kumsikiliza mwanamke wake wa zamani
Habari Anti!
Kuna mwanaume nimefunga naye ndoa mwaka juzi, tatizo akiwa na mwanamke wake wa zamani na ndiye anamuheshimu, akiwa naye hapokei simu zangu.
Nataka aniache nashindwa kumwambia nifanyeje?
Ndoa ni jambo la kheri na lina heshima yake, usikurupuke kudai talaka kwa sababu ya mtu asiyekuwa na haki na mumeo. Kwanza washirikishe wazazi kama wapo au watu wenye hekima ili mkutanishwe mlijadili katika ngazi ya kifamilia, maana kama hali ni hiyo na umesema hakuheshimu nyinyi wawili hamuwezi kuelewana. Angekuwa anakuheshimu japo kidogo ningesema mjadili na mlimalize wenyewe kwa sababu hakimu wa ndoa ni wanandoa wenyewe.
Sasa utaangalia matokeo baada ya kikao cha familia, kama amebadilika au laa. Ukiona hajabadilika ujue hana nia na wewe hapo uanze kufikiria cha kufanya kwa kuwasilisha hali halisi kwa wakubwa wa familia. Kitendo anachokifanya mumeo ni dharau na hupaswi kukifumbia macho, washirikishe wazazi wako na wake kila hatua, ukiwa na lengo la kulinda ndoa yako na si kuivunja.
Kwa sababu huyo mwanamke anafanya mambo hayo ili akukatishe tamaa, ukishindwa anakuwa amefanikiwa lengo lake.
No comments: